SEHEMU YA 20
Yaani nilivyokuwa nikiwaangalia marafiki wa Scaila niligundua walikuwa ‘malaya’ tu lakini kwa jinsi nilivyokuwa nikimpenda msichana huyo, nilimuona kama malaika vile, yaani eti malaika alikuwa kwenye kundi la mashetani.
Baada ya kuwasindikiza, akarudi na nikaanza kuongea naye mambo mengi sana. Alionekana kuwa mtu aliyechangamka sana, alinisifia kwa jinsi nilivyokuwa na mambo mengine mengi.
“Kwanza naomba namba yako,” nilimwambia.
“Tena afadhali! Jana nilitaka tuongee lakini ilishindikana!” aliniambia.
Tukabadilishana namba na mambo mengine kuendelea. Sikufichi, kipindi hicho nilijisikia furaha isiyo kifani, kuwa karibu na Scaila ilionekana kuwa bahati moja kubwa mno.
Pale kochini alipokuwa, nikamsogelea, nikamwangalia usoni na kuanza kutoa tabasamu pana ambalo lilikuwa ni kama matayarisho ya kitu fulani.
“Unataka kufanya nini? Hapana! Hapana Nye...” aliniambia huku akitoa tabasamu lakini hata kabla hajamaliza, alichokuwa akitaka kunikataza tayari nikaanza kukifanya, tukaanza kubadilishana mate kwa sekunde kadhaa, halafu tukaanza kuangaliana.
“Oh! It my fault, I’m sorry...” (Oh! Ni kosa langu, samahani...) nilimwambia huku tukiangaliana.
“Kwa nini umenifanyia hivi?” aliniuliza.
“Ndiyo maana nimesema samahani! Nilizidiwa!” nilijitetea, nikaona haitoshi, kulikuwa na kiumbe kingine nilikuwa sijakisingizia kesi, haraka sana nikakisingizia.
“Shetani alinipitia...”
Scaila akatabasamu, hapohapo haraka sana akanisogelea na kuanza tena. Niliona mtoto alidhamiria hivyo kumshika zaidi kwa dakika moja na kuachiana.
Naweza kusema huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mapenzi yetu. Nikatokea kumpenda Scaila kuliko mwanamke yeyote yule. Niliona kama malaika fulani ambaye Mungu aliamua kunishushia, kumbe sikujua kama mwanamke huyu alikuwa na roho mbaya, ya kikatilia hata zaidi ya shetani.
Nilihisi kama nimeokota embe chini ya muarobaini kumbe niliopata shubiri chini ya mkomamanga.
|
|
|
Hii hadithi itakuwa inatoka Jumatatu na Alhamisi.