SEHEMU YA 19.
Tukaachiana na kuanza kuwasalimia marafiki zake. Sikutaka kuleta macho ya tamaa. Wanaume huwa tunakuwa na matatizo, tunapokutana na marafiki wa wapenzi wetu akili zetu huwa zinaruka, yaani ni kama tunachanganyikiwa na mwisho wa siku unatamani uwe na hao wote.
“Mungu nisaidie! Huu mtihani mgumu sana,” nilijisemea kimoyomoyo huku nikiendelea kuwasalimia kwa kuwashika mikono yao laini iliyoniachia harufu mbalimbali za manukato yao.
“Jamani huyu ndiye aliyenisaidia,” alisema Scaila huku akiwaangalia wenzake.
“Jamani kumbe ni kaka mzuri hivi,” alisema msichana mmoja, alikuwa mweupe, ana mwanya na nywele zake alizinyoa kwa staili ya panki, alivalia skin tight nyeusi, japokuwa alikuwa amekaa, lakini kwa jinsi bastola zilivyoonekana, niligundua alikuwa na mzigo wa haja.
“We Janeti! Koma,” alisema Scaila huku akijifanya kukasirika, hapohapo akaanza kucheka kwa kicheko cha taratibu.
“Oh! Anaitwa Janeth! Mungu endelea kunipigania kijana wako, napata tabu sana, yaani nateseka,” niliendelea kujisemea moyoni mwangu, hakukuwa na kipindi kilichokuwa kigumu kama hicho.
Tuliongea mambo mengi mahali hapo, Scaila hakuisha kunisifia, alizungumza maneno yote mazuri kuhusu mimi kiasi kwamba marafiki zake walihisi walikutana na malaika kwa jinsi nilivyoonekana kuwa mwema.
Baada ya nusu saa, marafiki zake wakaaga, wakasimama na kuanza kuondoka. Hapo ndipo nilipomfaidi huyo Janeth. Alikuwa si mchezo, yaani kila nilipokuwa nikimwangalia kwa kuibia, nilijikuta nikimsifu Mungu kwa uumbaji wake maridhawa.
“Mungu nisaidie! Mungu nisaidie! Bila wewe mimi siwezi!” niliendelea kujisemea.
Nilikuwa nikikutana na ugumu mkubwa sana mbele yangu, kulikuwa na mapambano mazito ambayo nilitakiwa kuyashinda kwa nguvu zote.
Huyo Janeth na wale wengine walionekana kudhamiria kabisa kuniingiza kwenye matatizo na Scaila kwani hata walivyokuwa wakiondoka, walikuwa wakiondoka kimitego sana.
Kwa kawaida mpaka muda huo ilikuwa ni lazima ugundue kuwa siku zote rafiki wa mwizi lazima awe mwizi lakini kwangu sikuhisi hilo kabla.