: THE HOUSE OF THE DEVIL (Nyumba
ya kishetani)
MSIMULIAJI: HUMULI SAMAKI
MWANDISHI: METECK DERTHOD
Sehemu ya 09
Endelea...
Niliteremka na kusimama nje kabisa, ghafla
kwenye dirisha la chumbani kwangu nikaona
kama mtu anachungulia nje, nilikaza macho ili
kumwangalia vizuri, akapotea.
"Mh! ni kweli?" nilijiuliza mwenyewe. Ukweli ni
kwamba alikuwepo mtu, tena mweusi au niseme
Mwafrika kama mimi.
Nilikwenda pale dirishani, nikapanda ili
kuchungulia, nikaona mlango unafunguka
kuashiria kuna mtu alitoka maana mlango ule
ulikuwa hauwezi kukaa wazi, ni lazima ujifunge
wenyewe na mbaya zaidi mimi nilikuwa
sijaufungua zaidi ya ule wa sebuleni.
Kuna jamaa mmoja alikuwa anakuja kutokea
upande ninaoondokea kwenda kazini, simfahamu
lakini nilimsimamisha.
"Bro kuna ishu hapa inatisha kidogo, naomba
msaada wako."
"Kuna nini?" aliniuliza.
Nilimsimulia kila kitu cha siku ile tu lakini,
sikugusia mambo ya nyuma.
"Du! Kwa hiyo mimi nikusaidieje?"
"Naomba tuingie wote ndani, nataka nikachukue
simu yangu tu nimpigie huyo jamaa."
"Da! Itakuwa ngumu kidogo, unajua mimi nina
haraka sana leo," alijitetea yule mtu ambaye kwa
umbo ni bonge la mtu.
Nilijua ni uoga tu, hakuwa na kuwahi wala
kuchelewa.
Alipopita, akatokea mwingine, mzee mmoja,
kichwa chote kilichafuka kwa mvi. Nilimsalimia
huku nikimwonesha ishara kwamba nataka
kuzungumza naye.
"Mzee samahani sana."
"Bila samahani kijana."
Naye nikamsimulia tukio la siku ile, lakini wakati
ananisikiliza, mara nilimwona anatupia macho
dirishani na mimi nikageuka kuangalia, sikuona
mtu.
"Umeona nini mzee wangu?"
"Nimeona msichana ananizomea."
"Kweli?"
"Ee. Ndiyo hayo mambo unayosema?"
"Ndiyo hayo mzee."
"Twende," alisema, nikaanza kutangulia mbele,
mzee akanifuatia kwa nyuma. Hatukuwa
tukiongea chochote, najua sababu. Kila mmoja
alikuwa anaiwaza hatari ya mbele.
Tuliingia ndani, tukafika sebuleni, lakini sikuiona
simu kwenye kochi.
"Ona sasa mzee, simu niliitupia hapa, lakini
haipo."
"Au unayo mfukoni kijana?"
"Hapana, nina uhakika," nilisema huku
nikijipapasa mifukoni, hakukuwa na simu.
"Nitajie namba nijaribu kuibipu," yule mzee
aliniambia huku akitoa simu yake mfukoni.
Nilimtajia namba zote, akawa anaziandika, kisha
akapiga huku simu akiwa ameiweka kwenye sikio
lake la kulia. Nilishtuka sana kusikia simu yangu
inaita kutokea kwenye chumba cha wale
wapangaji wenzangu.
"Si hiyo?" yule mzee aliniambia akiniangalia kwa
mshangao.
Mzee alikata kisha akapiga tena, ikaita tena
kutokea kulekule, nilizidi kuogopa, nikamwambia
tutoke lakini uzee kweli
dawa, aliniambia hakuna haja ya kutoka dawa ni
kupambana tu.
Alinisogelea na kuniambia kwa sauti ya chini:
"Niwagongee mlango?"
"Si watakasirika?"
"Sasa kama unaogopa watakasirika, unadhani
simu yako utaipataje?"
"Haya wagongee. Lakini subiri, kwa nini tusiende
kwanza chumbani tukajua nani alikuwa
anachungulia nje?"
"Kijana unaonekana muogamuoga sana, we
mwanaume bwana, jifunze kukabiliana na hali
kama hii, sawa?"
"Sawa mzee."
"Haya twende huko chumbani kwako unakotaka
tukaone huyo msichana."
Tulifungua mlango wa chumbani, hakukuwa na
mtu, ila shuka nililoliacha kitandani asubuhi silo,
lilitandikwa jingine pia la kwangu.
"Khaa!" nilishangaa.
"Nini?"
"Hili shuka."
"Limefanyaje?"
"Silo nililolitandika asubuhi."
"Lakini la kwako?"
"Ndiyo langu."
Niliangalia mazingira mengine ya mle ndani na
kubaini kwamba, kuna vitu vingi sana vilikuwa
ndivyo sivyo.
"Si umeona hayupo?" yule mzee aliniuliza,
nikamjibu ndiyo, akasema twende tukachukue
simu yetu kwenye kile chumba ambacho ilikuwa
inaita.
Moyo wangu ulikuwa mzito sana, nilihisi
kizunguzungu, nilitamani kukaa chini na
kumwomba yule mzee asichukue uamuzi wa
kuifuata ile simu, lakini ningeipataje simu yangu
wakati ina namba kibao?
"Kijana, ngoja nikuoneshe dawa moja ya hao
viumbe wasiotaka kuonekana," alisema yule
mzee, nikamuuliza ni ipi hiyo.
"Tulia wewe," alisema huku akiingiza mkono
mfukoni na kutoa kimfuko kidogo, akakifungua
akatoa kitu. Nilipomuuliza ni nini akajibu:
"Ni bangi."
"Sawa kabisa, hiyo ndiyo dawa, ngoja nikupe
kiberiti."
Katika mambo yaliyonishangaza ni hilo, tulitafuta
kiberiti chumbani hadi sebuleni lakini
hakikuonekana, mbaya zaidi mimi nilikuwa na
kawaida ya kununua viberiti bunda zima, lakini
pia sikuona popote.
"Kweli una kiberiti ndani?" yule mzee aliniuliza.
"Kiberiti kipo na uzuri ni kwamba, nina bunda
zima, pia silioni."
Nilimwona yule mzee akisimama wima na
kunyoosha mikono juu kama mtu anayeomba dua
kwa Mungu.
"Kijana nimejua sasa, ngoja kidogo," alisema
huku akitoka na mimi nikimfuata kwa nyuma.
Wakati tunapita kwenye korido jirani na vyumba
vile vya wenzangu, nikaisikia simu yangu ikiita.
"Mzee mzee, hiyo bwana," nilisema, mzee
akasimama na mimi nikasimama nyuma yake,
tukasikia sauti ya mwanaume ikipokea simu
yangu:
"Haloo, Juma,Juma gani wewe? Nakuuliza Juma
gani maana mimi ndiyo mwenye simu hii, huyo
unayemsema simjui na wala hajawahi kumiliki
simu hii," sauti ya kiume ilisema, ukapita ukimya
kidogo kisha sauti hiyohiyo ikasema:
"Kama unabisha siyo simu yangu ongea na mke
wangu huyu hapa."
Mara nikasikia:
"Haloo ni kwa nini mnapenda sana kumfuatafuata
mume wangu, mara mzungumzie bangi, mara
mtusemee kwa watu."
Nilitamani sana kumwambia asiniache katika
safari yake maana kwangu kwa muda ule
palishaharibika, ningeuawa na watu
wasioonekana.
"Wewe nisubiri kijana," mzee aliniambia
akiendelea kwenda nje sikukubali.
"Mzee humu ndani mimi sikai, nimeshajua sasa."
"Umejua nini?"
"Huyo Juma anayetajwa hapo nafanya naye kazi
na ilikuwa aje na bangi kwa ajili ya hawahawa
watu wa humu ndani."
Mzee aliniangalia, akaniuliza:
"Wewe kijana unaye Mungu?"
"Ninaye."
"Huwa unakwenda kusali?"
"Sana."
"Lini umekwenda mara ya mwisho?"
"Ungeniambia tatizo ni kusali au?"
"Si hilo tu, ila una matatizo mengi. Hivi hapa
tumesimama, nyuma yako nimemuona yule
msichana amekuinamia akikung'ong'a kama mara
tatu kwa harakaharaka."
Nilitimua mbio kuelekea kusikojulikana, nikaenda
kufunga breki kwenye mtaa mmoja ambao
ukienda kushoto kwangu
unakwenda kutokea kwenye barabara ya kwenda
Kigogo Mbuyuni.
Baadhi ya watu walioniona nilivyo walitambua
nina tatizo zito kichwani, mzee mmoja aliniuliza
kama nakimbizwa nimefumaniwa.
"Sijafumaniwa mzee, lakini kwa tatizo langu
afadhali ningefumaniwa."
Huyu mzee alikuwa amebeba kibegi kidogo
mgongoni, alivaa suti nyeusi huku akionekana ni
mzee mwenye heshima kubwa katika jamii
inayomzunguka.
"Tatizo nini, hebu nisimulie kidogo tu," alisema
huku akinivutia pembeni. Nilimsimulia kila kitu,
alichokuwa akinishangaza sasa, kila hatua ya
maelezo yangu alikuwa akiachia tabasamu hata
pale nilipoamini kwamba ninachokisema kwa
wakati huo asingetabasamu na uso wake
ungeonesha kushtuka.
Nilipomaliza nikanyamaza na kumwangalia kwa
woga, nilitaka kuamini ni yule mwanaume
aliyepokea simu yangu kule nyumbani
amenibadilikia ili nisiweze kumtambua.
Moyoni nilisema kuwa, kama kweli ni yeye
atakapojidhihirisha tu kwangu nitoke mbio na
kwenda kuingia kwenye nyumba
ya mtu yeyote mbele yangu.
"Tatizo ni hilo dogo tu?" aliniuliza.
"Ni hilo tu mzee wangu. Ukiweza kunisaidia
nitashukuru sana."
"Nyumba yenyewe iko wapi?"
"Kule nyuma nyuma."
Nilimwona akiingiza mkono mfukoni na kuchomoa
simu nyeusi ndogo, wengi wanaziita za tochi
kisha akabonyezabonyeza na kuiweka sikioni.
Moyoni nilisema yaleyale.
"Si ajabu anawasiliana na yule mwanamke wa
kule nyumbani."
Nikamsikia akiuliza:
"Isdory, bado mpo hapo?"
Nadhani huyo jamaa alisema yupoyupo maana
nilimsikia huyo mzee akisema: "Unaweza kuja na
akina Tino hapa kwenye kibanda tulichotuma
pesa asubuhi ya leo? Haya njooni."
Niligeuzageuza kichwa na kukiona kibanda cha
kutuma pesa kwa kupitia mitandao mbalimbali ya
simu. Nikajua amewaita watu waje pale.
Baada ya dakika kama tatu, wakafika watu kama
saba, wanne wanawake, watatu wanaume
akiwemo Isdory na Tino.
"Huyu bwana anaitwa," alianza kusema yule
mzee akiniangalia nikajua anataka nijitambulishe
jina mimi mwenyewe, nikafanya hivyo.
Nilipomaliza, ndipo yule mzee akawaambia
wenzake kisa chote cha kwangu, mwanzo hadi
mwisho kama nilivyomsimulia awali.
"Ndugu, sisi wote walokole, kazi hiyo tunaimudu
kwa vile mara nyingi huwa tunatumia jina la
Bwana na Mwokozi wetu kufukuza uchafu kama
huo, sasa itabidi utupeleke kwenye hiyo nyumba,"
alisema yule mzee.
Nilianza kutembea mimi na wao wakawa
wananifuata kwa nyuma. Wale wanawake
niliwasikia wakizungumzia mwanamke mmoja
aliyeangushwa chini na mapepo akawa anataka
kupigana na wale waliokuwa wakimwombea.
Moyoni nikasema:
"Leo huko sijui."
Tulifika nje ya nyumba, kitendo cha kwanza
ambacho si cha kawaida, nilimwona yule kijana
muuza maji akitoka ndani. Alivaa kama siku
alivyokuja nikamwingiza ndani."
Nilishtuka sana, yeye hakushtuka, ila aliponiona
akaniambia:
"Bro nashukuru sana wamenilipa pesa zangu."
Sijui ni nini kilinipata nilijikuta nikisema sawa,
sikuongeza neno jingine lolote lile.
"Ni humu waheshimiwa," niliwakaribisha wale
watu nikiwa nimeshapishana na yule kijana.
Waliingia wote ndani, wakasimama katikati ya
korido kisha wakawa wananiangalia, yule
akaniuliza:
"Hivyo vyumba ni vipi?"
Sikumjibu kwa sauti, nilinyoosha mkono kuelekea
kwenye vyumba vyote viwili. Vilioneshwa
kufungwa kwa ndani lakini hakukuwa na sauti ya
muziki wala maongezi yao.
"Baba katika jina la Yesu," yule mzee alianza
ghafla.
"Amiiiin," walijibu wote aliofuatana nao, tena
walijibu kwa sauti ya juu kisha wakatulia kimya.
Akaanza kusali akitaja maneno ya kutisha,
nilimsikia akisema, choma moto roho mtakatifu,
mara Malaika Michael shuka na panga likatalo
kuwili.
Kifupi yule mzee alisema maneno ya ki-Mungu
kwa jinsi nilivyoelewa mimi. Ikafika mahali
akasema:
"Paaza sauti yako."
Ndipo wengine nao wakapokea kwa kila mmoja
kuomba kivyake. Wengine walisikika wakisema
wanaangusha na kuvunja ngome za ibilisi,
wengine wanachoma moto makazi ya shetani,
wengine wanamwagia damu ya Yesu pale ndani.
Nilianza kuhisi amani iliyoje, niliamini ukombozi
umefika tayari kwani sauti tu niliisikia ikipenya
hadi kwenye mbavu zangu.
Waliomba sana, kuna wakati mimi nilihisi kuchoka
lakini wao waliendelea tu hadi moyoni nikasema
kweli ni watu wa Mungu.
Ghafla nilianza kuona moshi mweusi ukitoka chini
ya milango yote ya wale ndugu, mlango wa
sebuleni kama sikikosei na mlango wa chumbani.
Moshi ulikuwa mzito kiasi kwamba, kuna wakati
nilihisi kupaliwa na kukohoa kwa nguvu lakini
wao hawakuonesha dalili ya kusumbuliwa na
moshi huo.
Mara, milango yote miwili ikaanza kufunguka
yenyewe polepole huku maombi yakiendelea kwa
kasi na nguvu ya ajabu. Milango hiyo ilifunguka
hadi ikafika mahali ndani kukaonekana.
Cha ajabu sasa, vyumba vilikuwa vyeupe, ndani
yake hakukuwa na kitu chochote, hata karatasi.
Ilikuwa kama chumba kilichopigwa deki au
kufagiliwa kwa ajili ya maandalizi ya kuingia
mkaaji mpya.
"Ha! Oneni jamani," nilijikuta nikisema hivyo.
Nilibaini kwamba, wale watu hawakuona wakati
milango inafunguka kwa vile walipokuwa
wakiomba walifumba macho na walikuwa
wakijipigapiga kwenye viganja kwa kutumia
ngumi.
Yule mzee alipoona vile akasema:
"Katika jina la Yesu."
"Amiiin."
"Sasa tushushe uwepo wa Bwana mahali hapa,
kwamba akapafanye pawe mahali salama, penye
amani na utulivu wa hali ya juu, kila mmoja sasa
amwombe Bwana hivyo."
Wakaanza kuomba tena, safari hii si kwa
kukemea kama mwanzoni, ilikuwa sauti yenye
upole na utii, mara nikasikia mlango mkubwa
ukigongwa kwa nguvu.
"Ngo ngo ngo ngoo."
"Ingia," nilisema lakini huku nikienda mlangoni,
nikaufungua! Mbele yangu alisimama yule dalali.
"Karibu bwana."
"Ee bwana nini umefanya sasa?" ndilo swali lake
hata kabla ya salamu.
"Kwa nini?"
"We hujui umefanya nini? Si wako watu humo
ndani, wamekuja kufanya nini hapa? Hujui kama
kuna watu umewaumiza? Wewe ungefanyiwa
hivyo ungekubali kweli?"
"Kaka unajua ukija kwangu njoo kwa heshima
zako zote na hoja zenye msingi, usije kama
mwendawazimu mpya, wewe unachokisema mimi
sijakisema kwako? Ulichukua hatua gani wakati
naumia mimi?" ITAENDELEA..!