THE HOUSE OF THE DEVIL (Nyumba
ya kishetani)
MSIMULIAJI: HUMULI SAMAKI
MWANDISHI: METECK DERTHOD
Sehemu ya 08
Endelea...
Nilipokuja kushtuka
ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Ina maana
nililala kwa saa moja na nusu.
Jicho langu moja kwa moja lilitua kwenye bangi
pale mezani, sikuiona.
Nilihamaki kwa kusema ha! Nani amechukua
bangi yangu? Sikujibiwa na mtu, ukimya ulitawala
huku akili ikiniambia wale wapangaji wenzangu
watakuwa wanahusika moja kwa moja.
Baada ya muda nilitoka mle sebuleni, nikaenda
chumbani. Nilifungua mlango na kusimama
kwanza kabla ya kuzama ndani. Niliangaza kila
kona, nikabaini kitu.
Niligundua kwamba, kuna mtu alikaa kitandani
maana nilipoondoka asubuhi nilikuwa
nimekitandika, muda huo kwa pembeni upande
wa mbele kulikuwa na alama za makalio.
Alama hiyo ilinipa picha kuwa, aliyekaa alikuwa
na makalio makubwa sana! Nilipoangalia chini
kwenye kapeti nikabini kitu kingine kwamba,
aliyekaa alikuwa na mafuta kwenye miguu kwani
iliweka alama kuzunguka miguu yake.
Aidha, nilibaini jambo jingine kwamba, aliyekaa
kitandani pia alikuwa akisimama na
kutembeatembea kwani alama ya miguu yenye
mafuta ilionekana sehemu mbalimbali za
chumbani kwangu.
Mara nikasikia hodi ikigongwa mlango mkubwa.
Niliikumbuka ile sauti kwamba ilikuwa ya yule
msukuma mkokoteni wa maji.
"Nakuja," nilisema kwa sauti kupitia dirishani
kwani chumba changu na sebule yangu vilikuwa
upande wa mlango mkubwa wa kuingilia.
Nilitoka mpaka mlangoni, nikafungua na kumkuta
yule kijana.
"Bro vipi, wapo wale watu ndiyo nimekuja hivi."
Nilimshika mkono, nikamvuta kumwingiza ndani
bila kusema naye. Nilimwelekeza vyumba vya
wale wapangaji wenzangu kisha mimi nikaingia
chumbani kwangu.
Nilikaa kitandani na kutega sikio kitakachotokea
huko. Nilimsikia yule kijana akigonga mlango.
Aligonga mara tatu, kisha nikasikia mlango
ukifunguliwa, sikuamini. Nilitaka kutoka, lakini
nikasema nisubiri hadi mwisho nione.
Baada ya mlio wa kufunguliwa kwa mlango,
ukafuatia mlio wa kufungwa halafu ukapita
ukimya. Akilini nilijua wamemkaribisha na
wakafunga mlango na sasa wanaongea naye.
Cha ajabu, kila nilipofuatilia ili kujua kama
mlango utafunguliwa na yule kijana kutoka,
sikufanikiwa kugundua hali hiyo, nikaanza kupata
wasiwasi.
"Inamaana tangu wakati ule hadi sasa bado wapo
ndani? Wanaongea nini sasa? Au wanapigiana
mahesabu? Si yule kijana alisema anadai pesa
nyingi?" maswali hayo yote yalikuwa yangu lakini
majibu yake sikuyajua.
Usiku uliingia, muda ukazidi kwenda, sikusikia
ishara yoyote ya yule kijana kutoka. Zaidi sana
nilisikia wale wapangaji wenzangu wakipika kwa
kukaangiza kitu kama nyama.
Usiku nilitoka, nikaenda kutafuta chakula, nikarudi
nacho nyumbani. Nikala, nikaenda kuoga, nikarudi
kitandani na kulala, sikuona dalili ya
mawengewenge wala mang'amng'amu.
Asubuhi niliamka kwa kushtuka, lakini sijui nini
kilinishtua ila ni kama kuna mtu alinishika mguu.
Hakukuwa na kitu chochote chumbani mwangu.
Nilitoka na kwenda kusimama kwenye dirisha,
nikachungulia nje. Kulikuwa shwari.
Nilipotoka kuoga nikiwa navaa nguo ili kuondoka,
nikasikia wenzangu wakitoka. Nilisimama tena
dirishani kwani kwa mtu anayetoka kwenye
nyumba ile na kwenda popote ilikuwa lazima
apite mbele ya dirisha langu.
Baada ya muda walifungua mlango mkubwa,
nikasikia wakiufunga, lakini baada ya hapo
sikumwona mtu yeyote yule akipita mbele ya
dirisha.
Na mimi nilipomaliza kujiandaa, nilitoka,
nikafungua mlango na kutoka. Mbele kidogo
nilikutana na watu kama kumi wamesimama
wakiongea. Niliwasalimia nikawauliza kama kuna
usalama.
"Usalama ni mdogo bwana, kuna kijana mmoja
amepotea. Tangu jana usiku alipotoka kwa
mkewe akasema anafuatilia
madeni ya biashara zake hajarudi," alisema mzee
mmoja ambaye alisimama akiwa amejishika
mikono kwa nyuma.
"Ni biashara gani anafanya?" niliuliza.
"Huwa anauza maji kwenye mkokoteni."
"Ha! Ni yule muuza maji?"
"Huyohuyo," alisema yule mzee.
Akili za haraka nikasema hapa ndipo pa kujua
wale wapangaji ni akina nani, inabidi niseme
ukweli ili waende polisi, najua
polisi watakuja kukagua ndani.
"Lakini mbona jana usiku alikuja kwangu kudai
pesa yake?" nilihoji kwa uso wa wasiwasi.
"Ulipomlipa akaondoka?" mwanamke mmoja
aliniuliza.
"Siyo kwangu, ila mimi ndiye niliyemfungulia
mlango. Alipoingia akawaulizia wapangaji
wenzangu, nikawaonesha chumba, akapiga hodi,
akakaribishwa ndani."
"Hukumuona kutoka?"
"Kwa kweli sikufuatilia maana na mimi nilirudi
chumbani kwangu."
Wale watu kama naweza kuwapeleka pale
nyumbani, nikawaambia kwa muda ule hapakuwa
na mtu nyumbani, wanarudi jioni.
"Basi tunakwenda kuwaambia ndugu zake, jioni
watakuja, si nyumba ile pale?"
"Ndiyo."
Nilipofika kazini na kuanza kazi, akili zangu
zikawa zimefunguka kitu. Nilijiambia wale watu
wakijua ni mimi niliyetoa mchoro wote,
watanifanyaje?
Nilibaini nimechemsha, lakini nikasema moyoni
kwamba potelea mbali, wajue wasijue sawa tu.
Kuna wakati nilipigiwa simu, namba sikuitambua,
yaani ilikuwa ngeni kwenye kumbukumbu zangu.
Nilijiuliza mwenyewe kwamba anaweza kuwa
nani, lakini sikupata jibu.
Awali nilisita kuipokea kiasi kwamba ilikata,
mpigaji akapiga tena. Nikaamua kuipokea sasa:
"Halooo," nilivuta sauti.
"Hujambo bwana?"
"Nani mwenzangu?"
"Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua
nani, ungeitika kwanza kisha ndipo uniulize nani."
"Sijambo, nani mwenzangu?"
"Angalia sana bwana," alisema huyo mtu bila
kujitambulisha kisha akataka simu.
Nilishangaa sana, nikaanza kazi ya kuwaza
kwamba anaweza kuwa nani na ni kwa nini
aniambie angalia sana?
"Atakuwa jamaa wa nyumbani, kwa vyovyote
vile," nilisema moyoni na kuamini hivyo kwani
kwa maisha ninayoishi mimi si rahisi kuwa na
maadui. Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio
kwa wasiwasi. Nilijua nimeingia kwenye
mapambano makubwa na wale wapangaji
wenzangu.
Niliendelea kufanya kazi, lakini sikuwa na amani
tena. Mara alitokea yule mfanyakazi mwenzangu
ambaye alinipa ushauri wa kupulizia bangi ndani
ya nyumba ili kuwakimbiza majini au viumbe
wote wabaya.
"Vipi mambo yako, yamekwendaje?"
"Mambo gani?" nilimuuliza huku nikiwa
namtazama. Kisa cha kumtazama kwanza ilikuwa
kujiridhisha kama kweli ni yeye au wale
wapangaji wenzangu wameamua kunifuata laivu'.
"Si yale niliyokuelekeza kufanya."
Nilipomkazia macho sana, akasema ana kazi
nyingi, akageuza na kuondoka. Mlango
ulipojifunga tu, nikajiegemeza kwenye meza na
kuwaza mambo kibao. Ilikuwa kama nataka
kusinzia, lakini nikasikia sauti kichwani
zikisemezana hivi:
"Halooo."
"Hujambo bwana?"
"Nani mwenzangu?"
"Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua
nani, ungeitika kwanza kisha ndipo uniulize nani."
"Sijambo, nani mwenzangu?"
"Angalia sana bwana."
Mara nikasikia tena zikisemazana hivi:
"Vipi mambo yako, yamekwendaje?"
"Mambo gani?"
"Si yale niliyokuelekeza kufanya."
Nilishtuka na kusimama, nikaondoka kwenda nje.
Nilikutana na yule mfanyakazi tena, akaniuliza
kama naondoka.
"Vipi, unaondoka saa hizi?"
"Bado nipo."
"Kwanza nilisahau kukuuliza, vipi ulifanikisha ile
kitu ya kuvuta kama nilivyokwambia?"
Moyo ulishtuka, nilijua ni watu wawili kwani huyu
angekuwa yule aliyenifuata muda ule,
asingesema alisahau kuniuliza.
"Nilifanikiwa kupata bwana, lakini," nilisema
nikimshika mkono, nikamvutia pembeni kidogo.
"Kaka mambo makubwa kule. Kwanza unajua
kama nimekuona wewe mara ya pili hii leo?"
"Kivipi?" aliniuliza.
Nilianza kumsimulia kila kitu, kuanzia zile bangi
hadi nusu saa kabla sijaonana naye. Alishangaa
sana, akasema yeye ndiyo kwanza anaingia,
alikuwa Kariakoo, pia akasema kwa siku hiyo
ndiyo kwanza ameniona mimi muda ule.
"Sasa itakuwaje ndugu yangu?" aliniuliza.
"Sielewi."
"Sasa sikia, mimi ninajua nitapata wapi bangi, we
usiku saa moja niambie tukutane wapi, nitakuja
nayo halafu nitaiwasha na kuivuta mimi."
"Wewe huogopi?"
"Niogope nini?"
"Kufa."
"Nani ataniua?"
"Si hao watu wabaya."
"Hamna, hawawezi."
Nilimkubalia, nikamwambia nitampigia saa moja
ili tukutane akiwa na hiyo bangi yake.
Akili zangu hazikukaa sawa, niliondoka kwenda
kutafuta maji ya kunywa, kisha nikaenda
kupumzika kwenye kibanda cha kuuza vocha za
simu.
Pale, mtu yeyote anayenijua angeniona angebaini
nina matatizo mazito kichwani mwangu, kwani
sikuwa sawa hata usoni. Muda mwingi niliwaza
maisha ya kwenye ile nyumba, hasa usiku wa
siku hiyo ambapo najua wale watu wakija ndiyo
balaa litakuwa kubwa zaidi.
"Halafu usiku wa leo lazima watakuja kunifanyia
maajabu yao, lakini dawa yao nisilale. Oke,
kumbe bangi itapulizwa leo, kidogo itakuwa
nafuu," nilisema moyoni, nikashtuliwa na sauti ya
kike nyuma yangu iliyoita jina langu.
NILIPOGEUKA nyuma, nikamwona dada mmoja
aitwaye Mwantumu Seleman nilikuwa naishi naye
Mwananyamala. Akaniuliza habari za siku.
Niliamua kumsimulia janga langu, lakini ghafla
likaja gari, akaingia huku akiniambia atanitafuta
siku nyingine.
Baadaye nilirudi kazini huku nikiwa na hali ya
wasiwasi, hata kazi zangu zikuzifanya sawasawa
kama ilivyo kawaida yangu. Iliniuma sana!
Muda wa kazi ulipokwisha, niliondoka moja kwa
moja hadi nyumbani. Sikutaka kupitia mahali siku
hiyo, lakini nilishakubaliana na yule mfanyakazi
mwenzangu aliyesema atakuja na bangi yake.
Wakati nafungua mlango mkubwa nilibaini
wenzangu walisharudi maana mlango
haukufungwa na funguo, nikaingia ndani.
Nilipofika kwenye mlango wangu wa kuingilia
sebuleni, wakati naufungua nikasikia mlango wa
chooni unafunguliwa, yaani kumaanisha kwamba
kuna mtu anatoka.
Ukisimama mlangoni pangu, mtu akitoka chooni
unamuona bila kificho, hususan kama anakuja
vyumbani. Lakini pia hata akiwa anatoka kwenda
uani, utamuona kwa mgongoni. Nilisita kuingia
nikiamini nitamwona mtu huyo. Nilianza kuona
miguu ikitoka, moyo wangu ukashtuka, mara
nikamwona mtu mwenyewe.
Nilijikuta nikisisimka mwili, niliamini naona kivuli
chake na si yeye. Ni mtu mweusi, wakati
nilitarajia angekuwa mweupe.
Alivyozidi kunisogelea, nikabaini kuwa, ni yule
kijana muuza maji kwenye mkokoteni.
"Ha! Wewe vipi, unatafutwa sana unajua?"
nilimwambia.
Badala ya kunijibu, alikata kona kuufuata mlango
mkubwa. Na mimi nikamfuata kwa nyuma,
nilimkuta akiwa anamalizikia
kutoka nje. Niliitupa simu kwenye kochi kisha
nikatoka kumfuata, na mimi nilifungua mlango
ambao ulishaanza kurudi baada ya yule kijana
kutoka.
Nilishangaa kutomuona popote kule nje. Wazee
wawili walikuwa wanapita, nikawauliza kama
wamemuona mtu ametokea mlangoni pale,
wakasema hapana, ila kuna mbwa alitokea ndani
kazunguka nyumba.
"Mh! Mbwa tena?" niliwauliza wale wazee, nao
wakasisitiza kuwa ni mbwa, tena mweusi.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio, wasiwasi
uliongezeka kiasi cha kunifanya niishiwe nguvu.
Wakati huo wale wazee walikuwa wakimalizikia
kwa mbali. Niliogopa kurudi ndani, nikawa
nimesimama mlangoni.
Wazo lilinijia kwamba, nimpigie simu yule
mfanyakazi mwenzangu kumuomba aje mapema
maana hali ni mbaya sana. Lakini simu nayo
ilikuwa sebuleni kwenye kochi, nitaipataje, yaani
nitaifuataje kule ndani wakati niliamini tayari
kumeshakuwa ukanda wa kifo?
Niliteremka na kusimama nje kabisa, ghafla
kwenye dirisha la chumbani kwangu nikaona
kama mtu anachungulia nje, nilikaza macho ili
kumwangalia vizuri, akapotea.
"Mh! ni kweli?" nilijiuliza mwenyewe. Ukweli ni
kwamba alikuwepo mtu, tena mweusi au niseme
Mwafrika kama mimi.
Nini kitaendelea