Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Simulizi: Namchukia Mama Yangu

nzuri sana
Sehemu ya 09

Nilijilazimisha kuinywa mpaka nikamaliza bia moja. Dada aliniongezea nyingine ambayo niliendelea kunywa bila kujua kipi kitafuata.

Nilijikuta nikihisi kizunguzungu, dada aliendelea kunilazimisha nimalize bia nyingine, kitu kilichonifanya nilewe na kulala pale nilipokuwa nimekaa.

Nilishtuka siku ya pili na kujikuta nimelala kitandani kwangu nikiwa nimejisaidia haja ndogo bila kujua huku nikisikia njaa kali. Nilinyanyuka na kwenda kuoga na kufanya usafi kisha nikaanza kutafuta supu.
***
Nilijikuta nikijiingiza katika ulevi ili kupunguza mawazo, pamoja na kufanya yote bado sikuwa tayari kuutoa mwili wangu kama asusa kwa wanaume kwa kuhofia maradhi.

Japokuwa dada zangu walinikuwadia kwa wanaume ikiwa ni pamoja na kuniletea fedha walizopewa, lakini sikuwa tayari kujiingiza kwenye ukahaba.

Niliamua kujiingiza kwenye ulevi kama mfariji wangu kwa kipindi kile kilichokuwa kigumu sana kwangu, kwa vile mpaka muda ule bado sikujua sababu ya kupewa talaka ambayo ilionekana kuwa na siri nzito ambayo sikuwa nikiijua.

Lakini kulikuwa na tatizo lililokuwa likinisumbua mpaka mama akanikataza kunywa pombe kwa kuwa ilikuwa ikinishinda. Kila nilipokuwa nikinywa pombe na kuanza kulewa, niliangua kilio kumlilia mume wangu.

Kwa wenzangu ilikuwa ni karaha na kuonekana kama nilikuwa nikiwapigia makelele wakati awali tulilizungumza na kukubaliana. Nilijitahidi kumsahau mume wangu, mtu ambaye nilimzoea na kuamini kifo ndicho kingetutenganisha lakini talaka ilikuwa pigo na kovu kubwa maishani mwangu.

Kila nilipolia na kukemewa niliwaahidi dada zangu kuwa sitalia tena, pia niliahidi nitaachana na mawazo ya mtalaka wangu aliyeniacha bila sababu za kueleweka.

Lakini kila nilipokunywa pombe na kulewa yote yalijirudia na kuanza kulia huku nikitawaliwa na mawazo mabaya ya kunitaka ninywe sumu ili niepukane na aibu ya kuachwa.

Wakati kwangu likiwa pigo mujarabu moyoni mwangu, dada zangu waliotangulia kuachika hawakutetereka waliendelea na maisha kwa kutumia miili yao kama mitaji ya kuwaweka mjini bila kuhofia hali ya hatari.

Niliamini njia ya kumuondoa mume wangu akilini ni kuwa bize kuliko kuendelea kukaa nyumbani na kujilazimisha kunywa pombe ambayo kila nilipolewa nilimlilia mtalaka wangu.

Niliamini ubize pekee ndiyo ungeweza kunisaidia kuchosha mwili na nikirudi nyumbani mchovu, nitafikia kuoga kula na kulala kuliko kushinda nyumbani kusubiri wanaume.

Mwanaume mmoja wa dada mkubwa alikuwa anafanya kazi serikalini, niliamini anaweza kunisaidia kupata kazi.

Nilimweleza dada amweleze anitafutie kazi popote.
Baada ya kumweleza dada amwambie alinihakikishia kunipa jibu ndani ya wiki.
****
Baada ya siku nne dada aliniletea taarifa kuwa kazi imepatikana kwenye super market iliyopo katikati ya jiji. Kwa kweli nilifurahi sana kupata kazi nikiamini kuwa bize kutanifanya niwe mbali na vishawishi vibaya.

Nilielezwa Jumatatu nilitakiwa nianze kazi, bwana wa dada alisema atanipitia asubuhi ya siku hiyo, hivyo nilitakiwa niamke mapema kujiandaa kabla hajafika.

Kwa vile taarifa niliipata siku tatu kabla, nilijiandaa kwa kutafuta nguo itakayoendana na maeneo yale, japokuwa siku zote sikupenda kuvaa nguo fupi kwani zilininyima uhuru na kujiona nakuwa mtupu.

Siku ya Jumatatu niliamka alfajiri, nikajiandaa na kuelekea kwenye kazi hiyo. Saa moja kasoro bwana wa dada Sauda alifika na gari lake na kunichukua kunipeleka kwenye hiyo super market.
Tulikwenda mpaka kwenye super market iliyokuwa katikati ya jiji. Tulipofika alipiga simu na kumsikia akizungumza.

“Haloo...eeh...nimefika...haya nakuja.”
Baada ya kukata simu aliniambia:
“Twende.”
Sikumjibu, nilimfuata, tukaingia naye ndani na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi moja iliyokuwa ya vioo vitupu na kuingia ndani.

Ndani tulimkuta kaka mmoja mtanashati, baada ya kuingia nilikaribishwa kwenye kiti. Nilikaa na kutulia huku bwana wa dada akisalimiana na yule kaka kisha alisema:
“Sasa bibie mi acha niwahi, kila kitu atamalizia huyu mwenyeji wako.”

“Hakuna tatizo.”
Bwana wa dada alitoka na kuniacha na yule kaka ambaye aliniomba radhi na kutoka. Baada ya muda alirudi na fomu ambazo zilikuwa za kuajiriwa. Baada ya kukaa aliniuliza maswali mawili matatu kisha alinipeleka sehemu, nikapigwa picha.

Baada ya zoezi lile nilirudi ofisini kwa yule kaka aliyekuwa meneja wa duka lile kubwa sana. Alinyanyua simu na kuagiza chai, baada ya muda ililetwa na kunywa kisha alimwita dada mmoja.

Alipofika alimweleza:
“Suzy huyu ni mfanyakazi mpya, naomba umpe ushirikiano wa hali ya juu.”
“Hakuna tatizo bosi.”
“Kampatie sare na aanze kazi.”
“Hakuna tatizo, atakuwa sehemu gani bosi?”

“Mweke kwa keshia.”
“Hakuna tatizo, kitambulisho?”
“Muone Sam nina imani kitakuwa tayari.”
“Haya shem, nina imani Suzy atakusaidia, kazi njema.”

“Asante.”
Nilitoka na Suzy mpaka kwenye chumba kimoja kilichokuwa na sare na kunichagulia inayonitosha kisha tuliongozana mpaka kwenye chumba kingine na kukuta kitambulisho changu kipo tayari.

Nilipewa na kukivaa kisha nilipelekwa sehemu na kuelekezwa kama mtu akishalipia bidhaa aliyonunua namuwekea kwenye mfuko na kuwakaribisha tena.
Haikuwa kazi kubwa sana lakini nilichoka sana kwa vile sikuwa nimezoea kusimama muda mrefu.

Jioni bwana wa dada alinipitia. Kabla ya kuondoka da Suzy niliyekuwa nimemzoea kwa haraka, alinieleza muda wa kuingia kazini na umuhimu wa kuwahi.

Nilimshukuru na kumuahidi kuwahi siku ya pili. Niliingia ndani ya gari la shemeji na kurudishwa nyumbani. Njiani shemeji aliniuliza mambo mengi kuhusiana na kazi.
Sikusita kumshukuru kwa msaada wake ambao ulikuwa muhimu kuliko kitu chochote kwa wakati ule.

Tokea siku ile nilianza kazi ya kuuza kwenye super market na jioni shemeji alinipitia kama kawaida. Siku zote nilirudi nimechoka baada ya kuoga na kula muda mwingi niliutumia kitandani kwangu kupumzika.

Taratibu nilianza kumsahau mtalaka wangu Beka na kuamini kuna maisha mengine baada yake kwa kujua kila linalomtokea mwanadamu lina makusudio yake.

Kazi niliizoea na kuwa maarufu kutokana na ucheshi wangu. Lakini nilikuwa na wakati mgumu kazini kutokana na wanaume wengi wakware kunitaka kimapenzi.

Pamoja na ahadi nyingi nilizopewa kama nitakubali kujitoa kwao kimapenzi, sikuwa tayari kujiingiza katika dunia iliyoniumiza na kufikia hatua ya kuwachukia wanaume, japokuwa sikutakiwa kumhukumu mtu kwa kosa la mwingine.
Moyoni nilipanga baada ya miaka miwili ndipo niufungue moyo wangu.

Najua unaweza kushangaa uamuzi wangu lakini kila aliyekumbwa na mkasa wa mapenzi hawezi kunishangaa kwa vile mapenzi yanaumiza sana hasa uachwe na mtu unayempenda tena bila kujua kosa lako.

Siku zilikatika huku nikizidi kuifurahia kazi yangu na maisha yangu mapya ya kuishi kama mdudu wa sikio bila kuwa na mshirika. Mwanzo niliamini maisha yale yangekuwa magumu ya kuishi bila mwanaume, lakini kila kitu ukiamua unaweza nami niliweza kabisa.

Nakumbuka siku moja wakati natoka kazini nikiwa ndani ya gari la shemeji bwana wa dada, baada ya kutoka kazini tulikwenda mwendo wa dakika tano, akanigeukia na kuniuliza:
“Mwaija una mpango gani?”
“Kuhusu nini shemeji?”
“Si nilisikia umeachana na mumeo?”

“Ndiyo.”
“Sasa una mpango gani baada ya kuachana naye?”
“Mmh! Bado sina mpango wowote nimeamua kupumzika kwanza.”
“Mwaija wewe bado msichana mdogo kwa nini ujifuje?”

“Sijifuji bali nimeamua kupumzika, kilichonikuta Mungu anajua.”
“Mwaija siyo Mungu anajua, mwanaume uliyekuwa naye hakuwa sahihi kwako.”
“Ukisema hivyo sikubaliani na wewe, Beka namjua vizuri kuliko mtu yeyote, kuna kitu tu ambacho kimesababisha aniache.”
“Kitu gani?”

“Wee shemu, tuyaache tu yalishapita hayo,” kwa kweli sikupenda kuzikumbuka habari za mtalaka wangu.
“Kama anatokea leo na kutaka kukurudia utakubali?”

“Naweza kukubali kama atanieleza sababu ya kuniacha na mimi kuikubali.”
“Sasa Mwaija tuachane na hayo kuna kitu nataka kukuambia japokuwa ninacho muda mrefu, lakini naamini leo ni siku muafaka.”
“Kitu gani hicho shemeji yangu?”
“Kuhusu wewe.”

“Mimi! Nimefanya nini?”
“Siyo kwamba umefanya kitu ila kuna jambo nimejifunza kwako kwa muda mrefu.”
“Kipi?”
“Mwaija una tabia tofauti na dada zako.”

“Kivipi?”
“Unajiheshimu pia unajitambua.”
“Nashukuru kwa kulifahamu hilo.”
“Baada ya kuligundua hilo nilikuwa na ombi moja ambalo nina imani litakuwa na faida kubwa kwako.”
“Ombi gani?”
“Nataka nibadili maisha yako uweze kumiliki nyumba na gari.”

“Kivipi?”
“Nafikiri unajua mimi na dada yako tukoje?”
“Ndiyo najua.”
“Basi nimeshamfumania na wanaume zaidi ya watatu.”

Shemeji alitulia kuzungumza akasimamisha gari kuwaruhusu watu waliokuwa wakivuka barabara eneo la Chang’ombe Maduka Mawili wavuke. Baada ya watu kuvuka alibadili gea na kukanyaga mafuta kisha alinigeukia na kusema:
“Unajua nilikuwa nina mipango mikubwa na dada yako.”

“Mipango gani?”
“Nimjengee nyumba na kumnunulia gari.”
“Tatizo nini?”
“Hataki nimuoe zaidi ya kupenda maisha anayoishi, wewe ni mdogo lakini una akili sana.”

“Shem, si nasikia umeoa?”
“Ndiyo, lakini angekuwa nyumba yangu ndogo.”
“Mmh! Na mimi unataka kuyabadilisha maisha yangu kivipi?”

“Mwaija nataka uwe mpenzi wangu, nakuhakikishia kwa jina la Mungu kukufanyia mambo yote niliyokuahidi hata kabla ya kukutana nawe kimwili ili uniamini.”


ITAENDELEA LEO SAA NNE USIKU

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Sehemu ya 23

Nilitumia zile dawa kwa wiki lakini miguu ilikuwa bado haijapata nguvu.
Nilirudishwa tena kwa mganga baada ya miguu kuanza kupasua na kuwaka moto. Usiku nilikuwa silali kutokana na ukali wa maumivu nilikuwa nakesha nikilia mbona niliteseka vitu vingine visikie kwa mtu siyo vikukute.

Kutokana na kusikia maumivu makali hata kutembea nilishindwa kwani kulikuwa kama kwenye nyayo kuna vidonda. Nilipofika nilianzishiwa dozi nyingine .

Dawa niliyopewa hukuwepo malaika wako alikuwepo, baada ya kunywa siku ya pili mwili ulianza kukoboka ngozi kama nyoka kitu kilichonitisha sana.

Mganga alisema ile ni sumu iliyokuwa mwilini hivyo ilikuwa inatoka. Nilitakiwa kujipaka mafuta mazito mwili mzima usiku kabla ya kulala ili asubuhi nikiamka nikute ngozi iliyokoboka imebanduka usiku.

Kopo kubwa la mafuta nilikuwa najipaka lote mwili ulikuwa kama nimetumbukia kwenye tope la mafuta. Ngozi iliyotoka ilibanduka tararibu ilichukuwa zaidi ya wiki kumalizika.
Baada ya kukoboka mwili kazi ikabakia nguvu kwenye miguu ambayo haikuonesha mabadiliko. Ila maumivu ya miguu yaliisha tatizo likabaki kwenye nguvu.

Kuwaka miguu kuliisha na kubadilika kuwa ya baridi na kuonesha dalili zote za kupooza.
Hali ile ilizidi kunichanganya akili, kila kukicha nilikonda mtoto wa kike na kubakia kichwa kama guruguja.

Dunia watu wanateseka, nilikuwa namaliza mwezi kwa mganga kazi yangu ilikuwa kukaa kwa muda kwani hata mgongo ulianza kunisumbua. Muda mwingi nikawa nalala kama nyoka.

Ilionesha wazi mganga alichemsha kuniponyesha japokuwa hakutaka kusema. Miguu iliyokuwa imeanza kukonda na kuwa midogo. Nami nilijikatia tamaa na kuanza kukataa dawa kwa kuamini nilikuwa nakunywa kama maji kwa vile hakukuwa na mabadiliko yoyote ya dawa nilizokunywa.

Niliwaomba wanirudishe nikafie nyumbani, lakini mama na dada zangu waliniomba niendelee kuvumilia kwa vile mganga alisema hajakata tamaa.

“Jamani kama mmenichoka naomba mnirudishe nikafie kwangu.”

“Mwaija mwanangu sisi wote tunaumiza vichwa juu yako. Hakuna mwenye furaha kila mmoja anateseka kwa ugonjwa wako.”

“Sasa kama siponi kuna faida gani kuendelea kuwa kwa mganga, mi najua nakufa kwa nini msinirudishe nikafie nyumbani.”

“Mwaija usiseme hivyo kuugua siyo kufa.”
“Jamani mimi nimeishakufa nasubiri kuzikwa.”

“Hapana mwanangu, basi tufanye mpango wa kukupeleka kwa mganga mwingine.”
“Sitaki kwenda kwa mganga yoyote niacheni nife.”

Ilibidi nirudishwe nyumbani baada ya kushindikana kutibika. Nilirudishwa nyumbani kumalizia siku zangu za kuishi zilizobakia. Kila kukicha hali yangu ilikuwa mbaya.
Nilikonda mpaka uti wa mgongo ulitoka nilipolala nilihisi naumia kwa vile nilikuwa nalalia mifupa.

Kula nilishindwa, chakula changu kikuu kilikuwa uji tena nusu kikombe.
Jamani maradhi mengine yasikie kwa watu si ya kuugua, nikawa kila siku lazima nipoteze fahamu. Kuna siku kutokana na maelezo ya mama walidhani nimekufa, kilio cha dada zangu kilikusanya watu nje.

Ilikuwa baada ya kupoteza fahamu kwa siku mbili, kilichositisha kuzikwa kwangu ni joto la mwili ambalo wazee walisema wanaweza kunizika ningali hai.

Baada ya hapo sikuelewa kinachoendelea mpaka niliposhtuka baada ya kupiga chafya mfuliulizo. Nilipofumbua macho nilijikuta sehemu ambayo haikuwa ngeni lakini bado sikuwa na uhakika nayo.

Nilipojaribu kunyanyuka nilishindwa, nilipojipapasa bado nilikuwa kwenye mifupa mitupu. Kutokana na harufu niliyokuwa naisikia nilijua pale ni kwa mganga.

Nilijiuliza pale ni wapi na kwa nini wamenipeleka tena kwa mganga ikiwa tulikubaliana nisubiri mauti yangu. Nikiwa bado nipo katikati ya mawazo kwa nje ya chumba nilichokuwa nimelala, nilisikia sauti ya watu wakizungumza nje ya chumba.

Nilisikia sauti ya mama akizungumza na sauti nyingine ambayo ilinishtua. Ilikuwa ya mtu ninayemfahamu lakini nilijua labda zinafanana na nyingine ilinishtua zaidi ilikuwa kama ya mama Amina mganga aliyenitibu mwanzo.

Nilimsikia akizungumza:
“Mmesikia chafya atakuwa amerudiwa fahamu.”

“Hata mimi nimesikia.”
“Mmh! Akipona nitashukuru,” nilimsikia mama akisema.

“Tumuombe Mungu, lakini mwanao yote kayataka mwenyewe, nilimueleza arudi akadharau. Wagonjwa wengi wakipata nafuu huwa hawajali kumalizia tiba na kujiona wapo sawa matokeo yake ugonjwa unamrudia tena kwa kazi kubwa kwa vile vita inakuwa mara mbili.”

“Hakuniambia, kama angenieleza haya mapema ningemleta pengine hata ujauzito wake usingetoka.”

“Nilimwambia arudi niufunge lakini kadharau matokeo yake ni haya. Lakini nakuhakikishia Mwaija atatembea na kurudia katika hali yake ya kawaida.”

“Kweli?” mama aliuliza.
“Tatizo alilonalo likitoka mbona mwanao mzima, hilo nina uhakika wa kulitoa.”
Nilishangaa kusikia mganga akijiamini kupita kiasi, kwani hata mganga wa Yombo alisema hivyo lakini mwisho wa siku alichemka.
“Ngoja nikamuangalie.”

Baada ya kunyamaza sauti ile, niliyosikia nyayo za miguu zikija ndani. Nilitulia nilitizama juu kwa vile sikuwa na nguvu ya kujigeuza nilivyolazwa ndivyo nilivyolala.
Baada ya muda nilisikia nikiitwa.

“Mwaija.”
“Abee,” niliitikia.
Baada ya kuitikia aliyeniita alisogea karibu yangu ndipo nilipomtambua vizuri kuwa ni mama Amina.
“Pole.”
Badala ya kuitikia nilianza kulia, mama Amina alinibembeleza:

“Mwaija utapona japo umechelewa sana.”
Lakini kumbe sikuwa nalia kwa maumivu bali aibu ya kumkimbia baada ya kupata ujauzito na kuondoka bila kurudi pia kuwa muongo kwa niliyomuahidi.

“Silii hilo dada.”
“Unalia nini?”
“Nimekuwa muongo na hii ndiyo adhabu yangu.”

“Hebu achana na hayo, naomba nikupe uji wa dawa kwa vile sasa hivi huwezi kula chakula kigumu ili niendelee na tiba yako.”

“Sawa.”
Mama Amina alitoka na kuniacha na maswali nani aliyenipeleka kule. Baada ya muda alirudi na bakuli la uji akiwa ameongozana na mama pamoja na da Suzy hapo nipo nilipojua aliyenileta kwa mama Amina ni da’ Suzy.

Nilijikuta nikisahau ugonjwa wangu na kutabasamu baada ya kumuona da’ Suzy japokuwa niliamini sura yangu ilikuwa kama ya mzee kutokana na kukonda kwa ugonjwa.
“Mwaija,” da Suzy akiniita
“Abee.”

“Pole mdogo wangu.”
“Sijapoa.”
“Utapona tu dada.”
“Mmh! Nitashukuru japokuwa imani yangu imekuwa ndogo sana.”

“Mwaija kwa uwezo wa Mungu utapona tu mdogo wangu.” Mama Amina alinipa moyo.
Walisaidiana kunikalisha kisha nilipewa uji uliochanganywa na dawa. Japokuwa nilikuwa mgonjwa niliweza kuunywa wote uliokuwa kwenye bakuli.

Baada ya kunywa waliniacha nipumzike kwa muda. Baada ya muda nilifuatwa na kutolewa nje ilionesha ni majira ya jioni inayokimbilia usiku kutokana na kigiza kuanza kuimeza nuru ya mchana.

Kama kawaida nilitolewa kwa kubebwa, ilikuwa yataka moyo kwani kila aliyenishika alishika mifupa. Nilitolewa uani na kulazwa kwenye mkeka.

Nilielezwa natolewa mdudu (jini) niliyetupiwa kazi ya kumtoa ilianza mara moja. Nilipewa dawa ya maji ambayo nilielezwa ni miti zaidi ya nane ilikuwa imechangwanywa.

Baada ya kunywa nilianza kujisikia vibaya tumbo likaanza kunichanganya na kusikia kichefuchefu. Nilianza kutapika lakini hakuna kilichotoka nilipoanza kujigogoa.

Mama Amina alikuja na kuingiza vidole mdomoni kwangu kama anatafuta kitu na kukitoa kwa kukwangua.

Aliingiza vidole mpaka mwenye koromeo na kukwangua na kutoa vitu kama malenda na kusema anatoka. Sikuelewa anatoka nani, aliendelea kufanya vile na kutupa nje yale malenda.

Alifanya vile zaidi ya mara tano kisha alisema:
“Lilikuwa limeanza kukomaa lakini bahati nzuri limetoka lote.”

Bado sikuelewa lilikuwa limekomaa nini. Baada ya muda nilipewa uji wa dawa ambao ulinifanya niharishe mpaka nguvu ziliniishia. Mauti niliyaona mbele yangu, baada ya zoezi lile nilirudishwa ndani.

Kutokana na mshikemshike nilipitiwa na usingizi mzito. Niliamshwa usiku sana na kupewa ndizi zilizopondwa na kulazimishwa kula japo mwili haukuwa na nguvu hata kidogo.

Baada ya kula nilirudi kitandani kulala.
Siku ya pili niliamshwa na kupewa uji wa dawa na kupumzika. Majira ya saa nne nilipata kifungua kinywa cha nguvu. Nilishangaa siku ile nilikula vizuri.

Mama Amina aliniambia mdudu aliyekuwa akinisumbua ametoka. Japokuwa nilikuwa naumwa lakini nilikuwa na uwezo wa kuzungumza.

“Mdudu ndiyo nini?”
“Jini ulilotupiwa.”
“Unamaanisha limetoka?” sikuamini.
“Ndiyo.”

“Mbona yule mganga wa mwanzo alisema ametoka na kupata nafuu lakini matatizo yalizidi?”

“Hakumtoa.”
“Alifanya nini?”
“Alimpoza, waganga wengi huwapoza tu lakini hawawatoi.”

“Kwa hiyo wewe umemtoa?”
“Ndiyo.”
“Hata rudi tena?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo nimepona.”
“Kwa vile kilichokuwa kikikumaliza tumekitoa nina imani sasa hivi afya yako itaimarika.”
Kauli ya mama Amina niliiamini kwa asilimia ndogo sana kwa kuamini aliyosema ilikuwa kunipa moyo.

Ajabu mwili wangu ulikuwa mwepesi tofauti na siku za nyuma ambao niliusikia mzito kama nimebebeshwa mzigo kizito hata kuhema kwangu kulikuwa kwa shida lakini baada ya zoezi lile nilihema vizuri.

Nilikaa kwa mama Amina kwa siku kadhaa huku nikiendelea kutimia dawa zake.Alinieleza jini nililotupiwa lilitaka kufanya viungo vyangu kupooza kama ningechelewa mwili mzima ungekufa ganzi na kupooza kabisa.

Nilijiuliza hata kama ndiyo mke wa mzee Sambi kanifanya hivi kosa langu nini ikiwa alikubaliana na mumewe. Kama alikuwa akimtaka mumewe angenieleza kama ningekataa ndiyo angenitenda.

Moyoni niliwaza mengi baada ya kupina nami lazima nilipe kisasi kama alivyonifanyia.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom