Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Sehemu ya 05

Japokuwa sikupenda kurudi nyumbani, ilibidi nikubaliane na mama kwa shingo upande kwa kuamini aliyonieleza yalikuwa yana umuhimu kukubaliana nayo.

“Kwa hiyo mama kwa kipindi hiki mume wangu utamsaidiaje?”
“Mwaija unachekesha, nimsaidiaje wakati ana ndugu zake?”

“Mama yule ni sawa na mwanao mpaka nakuomba msaada nina sababu zangu.”
“Mwanangu nawe king’ang’anizi haya unataka shilingi ngapi ukampe mumeo?”
“Hata laki mbili kwa ajili ya kujikimu kimaisha wakati anatafuta kazi.”

“Nitakupa laki,” mama alisema huku akinyanyuka na kuelekea chumbani kwake.
Baada ya muda alitoka na shilingi laki moja mkononi na kunikabidhi huku akisema:

“Mwanangu we ndiyo mwanamke wa kwanza kumhonga mwanaume badala ya kuhongwa wewe.”
“Mama simhongi, kumbuka yule ni mume wangu.”

“Kwa hiyo unarudi lini kwa mumeo?”
“Atakaponieleza nirudi.”
“Umeshakula?”
”Ndiyo mama.”
“Mumeo umemwacha wapi?”
“Nyumbani.”
“Basi muwahi.”

Niliagana na mama na kurudi nyumbani kwangu, njiani niliwaza mambo mengi kuhusiana na kushindwa kumshawishi mama kunipa kodi ya kulipia pango.
Kitu kilichokuwa kigumu moyoni mwangu ni kutengana na mume wangu kipenzi.

Lakini hali iliyotokea ilinifanya nisiwe na jinsi na kukubaliana na kilichoamriwa.
Nilipofika nyumbani nilimkuta mume wangu kajilaza mikono ikiwa bado kichwani kuonesha jinsi gani kichwa kipo katika wakati mgumu. Nilimwangalia mume wangu ambaye sikuwahi kumuona kwenye hali ile siku za nyuma.

Moyo uliniuma na kujiuliza upepo gani mbaya uliotukuta kufikia hatua ile. Kila kitu tulichokifanya kilikuwa kibaya, afya yetu ilidhoofu kwa mawazo na chakula cha kulambalamba ili kuipitisha siku, japokuwa nyumbani walikuwa na uwezo lakini nilichoka kuomba kila siku.

Nilisimama mlangoni kabla ya kuingia chumbani na kumuangalia mume wangu kwa uchungu huku moyo ukiniuma, bila kujielewa nami machozi yalianza kunitoka na kuweka michirizi mashavuni.

Maumivu yalikuwa makubwa kuliko kawaida, niliwaza mengi. Nilikiangalia chumba chetu, nilimwangalia mume wangu ambaye bado alikuwa kwenye dimbwi la mawazo hata nilipoingia hakushtuka.

Moyo uliniuma na kuamini hakuna kitu kibaya baada ya kifo kama umaskini kwani niliona ulivyokuwa ukiyatenganisha maisha yetu ya mume na mke kwa muda bila kujua itachukua muda gani kuwa tena pamoja na mume wangu.
Nilijikuta nikipata wazo la ghafla na kunifanya nimwite mume wangu kwa sauti.

“Bekaa,” sauti yangu ya juu ilimfanya ashtuke na kunitazama.
Uso wake ulikuwa umetanda na machozi macho yalikuwa mekundu mishipa ya kichwa ilimsimama. Mume wangu alikuwa akitia huruma, nami nilijikuta nikitokwa machozi zaidi.
“Unasemaje?” aliniuliza huku akinitazama.

“Mume wangu kwa nini tusiuze baadhi ya vitu vyetu vya ndani ili tulipe deni la nyumba na kulipia kodi wakati tukisubiri mambo yawe mazuri?”
“Wazo zuri mke wangu, lakini tukiuza vitu vyote na bado mambo yasiwe mazuri itakuwaje?”

“Ina maana mpaka muda wa kudaiwa tena utakuwa hujapata gari?”
“Mke wangu lazima nikuambie ukweli, si kwamba gari nimenyang’anywa wiki mbili zilizopita bali nina mwezi wa tatu sasa.”
“Mume wangu,uongo huo!” kauli ile ilinishtua na kuona mume wangu ananidanganya.

“Kweli mke wangu, muda wote nimeishi kwa kuungaunga, kila kukicha maisha yanazidi kuwa magumu. Ndiyo maana nikaona kwa nini nikutese wakati familia yako ina uwezo nikuache ukapumzike kwenu ili nijipange upya kuliko kuendelea kukutesa.”

“Mmh! Yaani una miezi mitatu huna kazi, kwa nini hukuniambia?” nilimlalamikia mume wangu.

“Nilikuwa najipanga, kama mambo yangekwenda vizuri usingejua kitu, lakini kila kukicha mambo yamezidi kuwa magumu.”

“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Kwani ulipokwenda imekuwaje?” mume wangu aliniuliza kwa shauku majibu ya safari yangu.

“Mama kasema nirudi nyumbani, hawezi kutukopesha fedha kwa vile hajui tutarudisha lini.”
“Hakuna tatizo basi fanya mpango uhamishe vitu.”

“Tuvipeleke wapi?”
“Kwenu.”
“Kwetu?” nilishtuka.
“Ndiyo.”
”Na wewe?”
“Mwaija naomba uchukue vitu vyote nina imani vitakuwa salama kuliko kukaa navyo mimi. Naweza kuvipoteza.”

“Kwani unataka kwenda wapi mume wangu?”
“Sijajua lakini baada ya wiki utajua kila kitu.”
“Nimekuletea hela ya kutumia wakati ukijipanga kwa ajili ya kuyaanza maisha mapya.”

“Umezitoa wapi?”
”Kanipa mama.”
“Ulimwambia nini?”
“Baada ya kusema hawezi kunisaidia, nilimuomba fedha itakayokusaidia wakati wa kuhangaikia kazi.”

“Shilingi ngapi?”
“Laki moja.”
“Asante mke wangu.”
Baada ya kumkabidhi fedha tulikubaliana kuhama siku inayofuata.

***
Siku iliyofuata nilihamishia vyombo kwenye chumba changu na kuagana na mume wangu ambaye mwanzo alikuwa akija kunitembelea usiku baada ya mihangaiko yake ambayo haikuwa na matumaini yoyote.

Kwangu kukosa haikuniuma sana, nilizidi kumuombea kwa Mungu apate kazi. Kuja kwake jioni kulinifanya nifarijike sana. Lakini ghafla mume wangu alipotea na kukosa mawasiliano kabisa.

Sikuwa na wasiwasi sana kwa kuamini huenda amepata kazi na muda anaorudi ni mbaya, nikaamini siku akipata mapumziko ya mwisho wa wiki atakuja kuniona.

Ilipokatika wiki bila mawasiliano nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi. Nilipokwenda kwao kumuulizia niliambiwa nao hawajamuona kama mimi.

Nilikwenda mpaka kwa madereva wenzake wa maeneo ya Vetenari na Mwembe Yanga. Wote walisema hawana taarifa zake, majibu yale yalinichanganya sana. Nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganyikiwa.

Mama hakuwepo ila niliwakuta dada zangu ambao walishangazwa na hali yangu ilivyokuwa.
“Mwaija mdogo wetu mbona upo hivyo?”
“Beka ana wiki na nusu haonekani.”
“Kaenda wapi?”

“Hata najua?”
“Kwao?”
“Nao wanasema wana muda kama wangu hawajamuona.”
“Kijiweni kwake?”
“Nao pia wanasema hawana taarifa zake.”
“Mmh! Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Hata najua!”

“Kama hajakuaga basi hakuona umuhimu wa kukuaga we tulia akirudi utamuona.”
“Sasa nitajua amekwenda wapi?”
“Kama ndiyo mimi angekuta nimeolewa kabisa,” dada alisema bila aibu.

“Dadaa yaani sijui amekwenda wapi mie nikimbilie kuolewa, akirudi?”
“Atajiju kwa vile hakuona umuhimu wa kukuaga wewe, dawa ya jeuri ni kiburi.”
“Hapana dada siwezi kufanya hivyo.”
“Basi vumilia usitulilie kama mtoto anayenyonya, maana ndoa yako kama ya mbinguni. Wote hapa dada zako tuliolewa kipi kigeni?”

Sikutaka kubishana na dada zangu kwani walikuwa tayari wamekunywa, maisha ambayo kwani siku zote niliyapiga vita. Ilibidi nijilazimishe kuzoea ile hali ya kutoonana na mume wangu.
***

Siku zilizidi kukatika bila kupata taarifa za mume wangu yupo wapi.
Mama alinieleza niendelee na maisha yangu ikibidi hata kutafuta mwanaume kwa wakati ule wa kuniliwaza wakati namsubiri mume wangu.

Japokuwa kulikuwa na wanaume wengi walionimezea mate lakini sikuwa tayari kujidhalilisha. Niliiheshimu ndoa yangu pia mwenyewe nilijiheshimu, sikutaka kuwa na sifa mbaya kama dada zangu. Siku nazo zilikatika bila kupata taarifa za mume wangu.

Sikuchoka kwenda kuuliza kwao na kijiweni kwake labda kulikuwa kuna mtu ana taarifa zake. Kila nilipouliza majibu yalikuwa yaleyale, hawakuwa na taarifa zozote.

Nilijikuta nikianza kuzoea taratibu maisha ya peke yangu na kuamua kujichanganya kama zamani huku moyoni nikiwa na swali lisilo na jibu, mume wangu amekwenda wapi?
 
Hii ngoja ifike mbali mbali nianze isoma nayo
 
Sehemu ya 06

Nilijikuta nikianza kuzoea taratibu maisha ya peke yangu na kuamua kujichanganya kama zamani huku moyoni nikiwa na swali lisilo na jibu, mume wangu amekwenda wapi?

Hata kama angekuwa amekwenda kutafuta maisha bado alitakiwa kuniaga kwa vile mimi ndiye nilikuwa mkewe na mtu wake wa karibu.

Miezi minane ilikatika bila kujua mume wangu yupo wapi huku nikizidi kuwa katika mtihani wa wanaume walionitaka kimapenzi huku mama na dada zangu wakitumika kunikuwadia.

Kuna mwanaume mmoja aliahidi kama nikimkubali basi angeninunulia gari. Najua angekuwa mtu mwingine angekubali kwa vile hakuwa na mawasiliano na mumewe aliyeondoka bila kuaga.

Lakini kwangu sikuwa hivyo labda ningepata taarifa ya kifo cha mume wangu tena niwe na kithibitisho, hapo ndipo naweza kubadili mawazo na kwa mwanaume muoaji si wa kunichezea kwa vile ana fedha zake mwisho kila mwenye fedha kuugeuza mwili wangu kama dekio.
Baada ya kukaa muda mrefu nilipata wazo la kutafuta kazi.

Wazo langu nilimueleza dada ambaye alinieleza atamwambia bwana yake mmoja aliyekuwa na cheo kwenye kampuni moja mjini.
Baada ya kumweleza, alimwuliza nilikuwa nina ujuzi gani, kwa kweli sikuwa na ujuzi wowote zaidi ya elimu ya kidato cha nne tena niliyefeli.

Lakini alikubali kunipatia kazi katika supermarket moja ambayo aliniahidi kunipa jibu baada ya wiki.
Nilimuomba Mungu nipate kazi ili niwe bize nisiwe na wazo baya la kujiingiza katika umalaya wa kuugawa mwili wangu kama pipi.

Siku moja tukiwa sebuleni na mama pamoja na dada zangu tukiangalia na kusikiliza muziki wa taarab kwenye video, zikiwa siku nne kabla ya kupata jibu la kuanza kazi, tulisikia sauti ya gari likisimama nje ya nyumba.

Hakuna aliyekuwa na mawazo nalo kwa kujua kama mgeni wetu atapiga honi au kugonga mlango kwa vile marafiki za dada zangu wengi walikuwa wenyeji pale.

Niliwaona kina dada wakitazamana, nilijua kila mmoja alikuwa akijiuliza labda ni mgeni wake, kwa vile hawakuwa na bwana wa siku zote, aliyewahi ndiye aliyepata nafasi ya kuwa na mmoja wa dada zangu.
Mara mlango uligongwa, wote tuliondoa macho kwenye video na kuangalia mlangoni.

“Karibu,” dada mkubwa alikaribisha.
Tukiwa tunaangalia mlangoni, sikuamini kumuona mume wangu Beka akiingia. Jamani hata nilivyoamka sijui, nilijikuta nikimkumbatia kwa nguvu na kufanya wote tuanguke chini.

“Yoyooo mume wangu.”
Ajabu nyingine baada ya mume wangu kuingia, mama alipata mshtuko na kudondoka toka juu ya kochi mpaka chini. Kwa kweli sikuelewa ule ulikuwa mshtuko wa nini.

Niliamini kabisa huenda mama naye hakutegemea kumuona mkwewe ambaye alikuwa amempoteza zaidi ya miezi minane ameonekana tena akiwa katika hali nzuri. Ilibidi tuingie kwenye kazi ya kumhudumia mama aliyekuwa amepoteza fahamu.

Baada ya kuzinduka aliomba tumuingize chumbani kwake, tulifanya vile mara moja. Baada ya dakika chache, niliwaacha dada zangu nikatoka kwenda kwa mume wangu aliyerudi kama maji jangwani.

Kabla sijazungumza lolote dada zangu nao walitoka, tulijikuta mimi na dada zangu tukiwa na hamu ya kuzungumza na mume wangu.
“Jamani shemeji za siku?” dada yangu alimuuliza.

“Nzuri tu.”
“Mmh! Naona mambo si mabaya.”
“Kiasi.”
“Jamani basi niacheni nizungumze kwanza na mume wangu,” niliingilia kati baada ya kuona wananizuia hamu yangu kwa mume wangu.

Dada zangu walinipisha, lakini kabla ya kuondoka walimpiga mzinga shemeji yao.
“Shem makoo makavu,” wakimaanisha wanataka kunywa.

Mume wangu bila kusema kitu aliingiza mkono kwenye mfuko wa juu wa shati na kutoa elfu kumi na kuwapatia.

“Mambo si hayo,” walishukuru na kuondoka na kuniacha nikiwa na shauku ya kuzungumza na mume wangu. Nilimwangalia kama ndiyo siku ya kwanza ya ndoa yetu.

“Jamani mume wangu karibu,” nilimkaribisha na kumshika kwa kumuogopa.
“Asante,” alijibu kwa sauti ya chini.
“Jamani Beka mbona sauti ya chini unaumwa?”

“Hapana.”
“Uchovu wa safari?”
“Wala, nipo sawa.”
“Sasa tatizo nini?”
“Basi tu, sasa Mwaija naomba tuzungumze nje kwa vile mi si mkaaji.”
“Kwa nini tusizungumzie chumbani kwetu.”

“Hakuna tatizo.”
Tulitoka hadi nje ya nyumba kubwa na kuelekea kwenye chumba changu kilichokuwa banda la uani. Tuliingia chumbani kwetu ambako nilikuwa nimepatengeneza kama nilikuwa naishi na mtu, muda wote chumba changu kilikuwa kwenye hali ya usafi.

“Karibu mume wangu,” nilimkaribisha kwa heshima zote.
“Asante,” bado asante yake haikuwa na uchangamfu.

“Mume wangu mbona huoneshi furaha kuwa karibu yangu, au hujanikumbuka?”
“Kwa kweli najitahidi lakini inashindikana.”

“Nini?”
“Najua hata nikikueleza huwezi kunielewa, lakini ipo siku Mungu akijalia tukionana nitakueleza na utanielewa.”
“Kitu gani mume wangu?”
“Nina mambo mengi lakini siwezi kukueleza ila naomba nitakachokifanya ukipokee.”

“Kitu gani mume wangu.”
“Mwaija nakupenda sana na naamini mpaka nakufa sitampata mwanamke aliyenipenda kama wewe.”
“Mume wangu mbona unasema aliyekupenda kwani mi nimekufa si nipo?” kauli yake ilinishtua.

“Ndiyo maana nikasema kila nitakachokisema itakuwa vigumu kunielewa.”
“Beka mbona leo sikuelewi?”
“Najua hutanielewa ila elewa sina jinsi lazima iwe hivyo.”

“Beka! Una nini?”
“Narudia tena katika maisha yangu mpaka naingia kaburini sitapata tena mwanamke kama wewe.”

“Beka au umesikia nimeolewa?”
“Hapana, sijasikia chochote kibaya kwako ndiyo maana nasema sitapata mwanamke mzuri na mwenye heshima kama wewe katika maisha yangu.”

“Kwa hiyo unarudi ulipokuwa na kuniacha nyumbani?”
“Hapana, nina imani unayajua maisha yetu yalivyokuwa?”

“Ndiyo mume wangu.”
“Kilichotokea mpaka kutengana unakijua?”
“Ndiyo mume wangu, baada ya maisha yetu kubadilika na kuwa magumu.”

“Unajua baada ya miezi sita mimi ningekuwa wapi?”
“Mume wangu mi nitajuaje wewe ungekuwa wapi?”
“Unajua sababu ya mama yako kuanguka nilipoingia?”

“Hata sijui.”
“Basi kama tungekuwa pamoja leo hii ningebakia jina.”
“Ungebakia jina? Una maana gani?”
“Mwaija naomba nikueleze kilichonileta kwenu.”

“Kipi mume wangu?”
“Nimeamua kuachana na wewe.”
“Sijakuelewa, kuachana kivipi?”
“Leo nimekuletea talaka yako.”
“Talaka yangu! Kivipi?” nilishtuka na kushindwa kumuelewa mume wangu alikuwa anamaanisha nini.

“Mwaija, nakuacha huku nakupenda sana tena sana, lakini talaka nitakayokupa ni usalama wa maisha yangu.”

“Beeka, nilitaka kukuua?”
“Walaa!”
“Sasa usalama upi?”
“Kwa leo hutanielewa.”
“Nieleze nitakuelewa tu mume wangu.”
“Ipo siku lakini siyo leo.”
“Sasa unaniacha ili iweje?”
“Kila kitu mama yako anajua.”
“Mama anajua nini?” jibu la mume wangu lilinishtua sana.

“Mwaija mama yako anajua kila kitu juu ya talaka hii.”
“Anaijua kivipi?”
“ We kamuulize.”

“Ndiye aliyesema unipe?”
”Nikiondoka muulize mama yako atakujibu kila kitu tena kwa kirefu.”
“Beka mbona sikuelewi, mara kujua kilichomuangusha mama, mara nimuulize mama kuhusu talaka yangu mbona sikuelewi?”

“Majibu ya maswali yote anayo mama yako, ila kila kilichopo hapa ni mali yako na sehemu ya kiwanja cha Charambe nitakiuza na kukupa haki yako. Siwezi kukudhulumu hata senti tano kwa vile ni haki yako.”

“Beka umesikia maneno gani mabaya juu yangu? Au umeambiwa na mimi nilijiunga na dada zangu kufanya mchezo mchafu?” nilijikuta nikijitahidi kubashiri sababu ya kupewa talaka.
“Wala sivyo unavyodhania, hujafanya na nina amini huwezi kufanya.”

“Umesikia nina mwanaume?”
“Hapana.”
“Sasa kosa langu nini mpaka unaniacha mume wangu?”
“Huna kosa ila mama yako anajua kila kitu.”

“Beka kwa nini aniambie mama yangu wakati wewe upo? Kama kuna kosa niweke wazi mume wangu, japokuwa naamini sina kosa kwako.”
“Nimekwambia siku yoyote tukionana nitakueleza sababu ya talaka, naamini hutakasirika na utakubaliana nami kwa uamuzi wangu huu.”

“Beka nimekaa muda gani kukusubiri? Nimejitunza kwa ajili ya ndoa yetu, nimevumilia mangapi leo hii nakuona mume wangu furaha yangu unaigeuza kilio?

Beka umepata mwanamke mwingine? Nipo tayari kuishi uke wenza lakini siyo kuniacha Beka, bado nakuhitaji katika maisha yangu,” nilimpigia magoti mume wangu ili abadili uamuzi.

“Hata mimi nakuhitaji tena sana.”
“Sasa kwa nini unaniacha mume wangu, kama kuna kosa niambie ili nami nijitetee.”

“Mwaija huna kosa.”
“Jamani! Kama sina kosa, kwa nini unaniacha? Beka ni unyama gani unaonifanyia? Nimekusubiri kwa muda mrefu huku kila siku nikikuombea kwa Mungu ufanikiwe. Leo nimekuona kicheko changu kimegeuka kilio?

“Beka mume wangu nionee huruma, nimeteseka kwa miezi minane sijui upo wapi, unatokea na kunipa talaka, hii ni haki? Beka mume wangu hebu rudisha moyo nyuma.

Naomba usijifikirie wewe peke yako, nifikirie na mimi mume wangu,” niliendelea kupiga magoti mbele ya Beka ambaye naye alikuwa akitokwa na machozi huku mishipa ya kichwa ikiwa imemsimama.

Beka aliinama na kulia kilio cha kwikwi, kitu kilichonifanya ninyamaze na kumnyamazisha mume wangu.

”Beka usilie mume wangu, niambie tatizo nini, kama kuna uwezekano tulitatue.”
“Mwaija,” aliniita huku akinitazama, macho yakiwa mekundu.
“Naam mume wangu.”
“Mwaija nakupenda zaidi ya sana, lakini lazima nikuache ili pawepo na usalama wa maisha yetu.”

“Usalama upi? Mbona sikuelewi?”
“Kwa leo hutanielewa, naomba nikuachie mzigo wako mi niondoke.”

“Mzigo gani Beka?”
“Talaka yako.”
“Beka unasema kweli au unatania?”
“Sijawahi kukutania,” Beka alisema huku akiingiza mkono kwenye mfuko wa shati na kunipa karatasi.

Niliipokea nikiwa siamini, niliifungua na kuisoma, kweli ilikuwa talaka moja. Nilipatwa na mshtuko na kuanguka chini.
 
Yaani kufuatilia fresh story shida sana, utamu unakolea na episode inakata. Ingekuwa ilipostiwa ikaisha ni mwendo Wa kusoma tu.
 
nashukuru ahsante sana, nitakutumia korosho za mama ,
 
Sehemu ya 07

“Sijawahi kukutania,” Beka alisema huku akiingiza mkono kwenye mfuko wa shati na kunipa karatasi.

Niliipokea nikiwa siamini, niliifungua na kuisoma, kweli ilikuwa talaka moja. Nilipatwa na mshtuko na kuanguka chini.

***
Nilipozinduka nilijikuta nipo chini
nimelazwa, pembeni walikuwepo dada zangu.

“Vipi Mwaija?”
“Beka yupo wapi?” niliwauliza kwanza mume wangu.

“Amekuja kutuita na kutueleza umepatwa na mshtuko, tumeingia ndani na kukuta umepoteza fahamu, baada ya huduma ya kwanza umezinduka.”
“Beka yupo wapi?” niliendelea kumuulizia mume wangu.

“Baada ya kutuita tulijua tutakuwa naye ndani, lakini kumbe yeye ameondoka. Beka ni mwanaume muuaji mkubwa sikutegemea,” alisema dada mkubwa kwa hasira.

Macho yangu yalitua kwenye mkono wa dada na kumuona ameshikilia karatasi, nilinyanyuka na kumpokonya ile karatasi na kuisoma, nilikuta kweli ni talaka yangu.

“Jamani kosa langu nini mpaka nipewe talaka?” niliuliza huku nikiangua kilio.
“Sasa unatuuliza sisi wakati mlikuwa wenyewe ndani?” dada alionesha kunishangaa.

“Dada kwani kawaambia sababu ya kunipa talaka?”
“Hajatuambia kitu zaidi ya kutuita na kutueleza kuwa umeanguka. Lazima wewe unajua sababu ya kupewa talaka.”

“Dada zangu hata sijui chochote, basi ameamua tu, yaani kujizuia siku zote kwa ajili yake, matokeo yake kunipa talaka. Kweli hii ni halali?” niliuliza kwa uchungu huku nikiendelea kulia.

“Sasa mdogo wangu sisi tutajuaje? Wewe ndiye uliyetakiwa kutuambia sababu.”
“Najua ninyi ndiyo mmeniponza na kuonekana nami nina wanaume wa nje,” niliwalaumu dada zangu.

“Koma weee, upuuzi wako na mtalaka wako usikufanye utukosee adabu,” dada zangu walinijia juu.

“Laki..” nilikatwa kauli.
“Funga domo lako, alikuja akakufumania?”
“Hapana.”
“Sasa kwa nini utulaumu, kwani wakati anakuoa na sasa, kipi kimebadilika hapa kwetu?”

Niliona hakuna msaada wowote kwa dada zangu, niliendelea kulia mpaka mama alipokuja na kunikemea.
“We mtoto mbona unaleta uchuro?”
“Mama inauma, kosa langu nini la kupewa talaka?”

“Wewe Mwaija kipi cha ajabu kwani wewe ni wa kwanza kuachwa. Kipi kimepungua kwako, toka aondoke huyo mwanaharamu wako, hukulala na njaa wala kulala nje.”

“Mama inauma mtu nimsubiri siku zote atokee na kunipa talaka, hii ni halali kweli? Si bure kuna kitu tu mama,” nilimlalamikia mama huku nikiendelea kulia.

“Kama unajua huna kosa achana naye, huenda keshaoa huko alipokwenda. Amekuja kuachana na wewe. Unajuaje pengine mwanamke aliyempata alimdanganya hajaoa.”

“Lakini mama mbona mume wangu kaniambia eti wewe ndiye unayejua sababu ya talaka yangu?”

“Nini! Mimi niijue talaka yako?” kauli yangu ilionesha kumshtua sana mama.
“Ndiyo mama.”
“Sasa haya makubwa! Yaani mimi nijue sababu ya talaka yako wakati mnapeana mimi sikuwepo?”

“Hapana, ila mume wangu kasema wewe unajua sababu ya mimi kupewa talaka.”
“Mumeo ndiyo kakwambia hivyo?”
“Ndiyo, kasema nikuulize wewe.”

“Hii ajabu! Mwenye kutoa talaka asikwambie, mimi nitajuaje? Huoni huo ni ukosaji wa adabu anaofanya mumeo? Shukuru Mungu kupewa talaka, ni wazi yule mwanaume alikuwa hakufai na pia hakuwa na mapenzi nawe.”

“Hapana mama, mume wangu namfahamu vizuri kuna kitu mama unakijua ila unanificha, yeye si mwendawazimu kusema hivyo.”

“Nikufiche ili iweje?”
“Eti, halafu nini kilichokuangusha wakati alipoingia mume wangu mpaka ukapoteza fahamu?”
“Mwaija! Swali gani hilo?” niliona mama akinibadilikia.

“Mama kuna ubaya gani kukuuliza?”
“Ulitaka nife ufurahi?”
“Mama mi nifurahie kufa kwako?” nilimshangaa mama.
“Sasa hilo ni swali gani?”

“Basi mama yamekwisha, lakini bado talaka yangu naamini kuna kitu si bure.”
“Mumeo asituchanganye, upuuzi wake usitugombanishe bure kuwa makini mwanangu.”
“Mmh! Sawa nitajua tu,” ilibidi nikubali ili yaishe kwani hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

“Hilo ndilo neno.”
Baada ya kusema vile, mama alitoka nje na kuniacha peke yangu, wakati huo dada zangu walikuwa wameshatoka kitambo na kuniacha na mama.

Chumba nilikiona kichungu, niliitazama upya talaka yangu huku nikitokwa machozi, haikuwa na mabadiliko yoyote zaidi ya kuandikwa nimeachwa kwa talaka moja.

Siku hiyo nilishinda chumbani kwangu nimejilaza kifudifudi nikiwa nimelalia mto nikiendelea kulia. Nilijitahidi kuvuta kumbukumbu katika maisha yangu ya ndoa kama kuna kosa lolote nililowahi kumkosea mume wangu hata kwa siri kufikia kuamua kunipa talaka.

Baada ya kutafuta kwa muda, sikubaini kosa nililomtendea mume wangu wala kuliwaza, maneno ya mume wangu yalinirudia kichwani kuhusu sababu ya fumbo la talaka yangu.

Maneno yalijirudia kichwani mwangu kama mtu aliyekuwa akisikiliza redio.
“Unajua baada ya miezi sita mimi ningekuwa wapi?”

“Mume wangu mi nitajuaje wewe ungekuwa wapi?”
“Unajua sababu ya mama yako kuanguka nilipoingia?”

“Hata sijui.”
“Basi kama tungekuwa pamoja mpaka leo hii ningebakia jina.”
“Ungebakia jina? Una maana gani?”
“Mwaija naomba nikueleze kilichonileta kwenu.”

“Kipi mume wangu?”
“Nimeamua kuachana na wewe.”
“Sijakuelewa, kuachana kivipi?”
“Leo nimekuletea talaka yako.”
“Talaka yangu! Kivipi?” lilikuwa neno lililonishtua sana.

“Mwaija, nakuacha huku nakupenda sana tena sana, lakini talaka nitakayokupa ni usalama wa maisha yangu.”
Nikarudia yale maneno kwa sauti ya chini kama namwambia mtu.

“Miezi sita mume wangu angekuwa wapi? Na...na sababu ya mama kudondoka! Kudondoka..mama...i..i...naashiria nini? Kwani kuna nini kati ya siri ya talaka na mama?

Mmh! Eti kunipa talaka ni usalama wa maisha yake...mmh! Amesikia nimeathirika?... Mungu wangu lazima kuna mtu amekwenda kumpa uongo mume wangu kuwa nimekuwa malaya na kutembea na mtu aliyeathirika? Mmh!

La...la...kini mbona ameuliza kuanguka kwa mama? Jamani hii talaka ina nini, sikubali lazima nimtafute Beka anieleze kiundani...aa...au mama alimtaka mume wangu kimapenzi?

Jamani mbona sipati jibu, jamani naweza kuwa kichaa bure.”
Nilijikuta nikikosa jibu na kukifanya kichwa kisitulie kwani kilikuwa kikiniuma kama kidonda kila nilipolazimisha kuwaza kitu kilichokosa jibu.

Siku ile sikutoka mpaka siku ya pili nilipofuatwa na mama ndani kunibembeleza.

“Mwaija mwanangu mbona unataka kukufuru Mungu kwa kupewa talaka, kwani wewe ndiye wa kwanza?”
“Mama heri ningefanya kosa ningekuwa tayari kuachika, lakini kumsubiri mume wangu zaidi ya miezi nane, uvumilivu wangu zawadi yake kunipa talaka? Heri angenieleza kosa langu nikajua moja, mama inauma, inaumaa.”

“Mwanangu lazima ujue kama hukumkosea mumeo basi miezi hiyo nane lazima amepata mwanamke ndiyo maana amerudi kukuacha, siku zote fimbo ya mbali haiui nyoka.”
“Lakini mbona maneno yake yamenichanganya sana.”

“Maneno gani?”
“Eti sababu ya wewe kuanguka.”
“Amekwambiaje?”
“Aniambie nini zaidi ya kuniacha njia panda, mara sijui sababu ya talaka wewe ndiye unajua mara sijui kunipa talaka ni usalama wa maisha yake, yaani hata sielewi,” nilisema huku moyo ukiniuma.
“Sasa yote hayo kakuweka wazi?”
“Wapi mama!”

“Yule mwanaume mbaya sana, amekuacha na mafumbo ili atugombanishe. Lazima amepata mwanamke mwingine. Kwa jinsi mlivyoagana mpaka unampa fedha za kuanzia maisha, hakutakiwa kukupa talaka mpaka akueleze kosa lako,” maneno ya mama yalinigusa.

“Hapo ndipo ninapozidi kuumia moyoni mama yangu.”
“Mwaija wewe bado msichana mdogo, nina imani ukitaka kuolewa huchukui hata wiki utaolewa. Kwa hivyo asikuumize akili.”

“Sawa nitaolewa lakini kwa nini nimeachwa?” hilo ndilo lililoniumiza.
“Mwanangu siku zote ukiona penzi limefika mwisho basi ujue ndiyo mwanzo wa penzi jipya.”

Mama yangu alifanya kazi ya ziada kunipoza moyo, kwa upande mwingine niliona kama kulikuwa na kosa alitakiwa anieleze hata kama la kusingiziwa kwa vile mimi nilikuwa mkewe.

Kitendo cha kunipa talaka na kuniachia maswali yasiyo na majibu kilinifanya nikubaliane na maneno ya mama.
Wazo la haraka lilikuwa kwenda nyumbani kwa wazazi wa mume wangu kuulizia sababu ya kupewa talaka nikiamini huenda aliwaeleza.
 
Sehemu ya 08

Wazo la haraka lilikuwa kwenda nyumbani kwa wazazi wa mume wangu kuulizia sababu ya kupewa talaka nikiamini huenda aliwaeleza.

***
Siku tatu zote nilikuwa kwenye mawazo mazito juu ya kupewa talaka bila kosa na kusababisha nipoteze hamu ya kula. Moyoni niliona heri mume wangu angepotea hata miaka kumi nikajua bado nipo naye kuliko kitendo kile cha kunipa talaka bila sababu.

Nilijikuta nikianza kuvikaribisha vidonda vya tumbo kutokana na kuwa na mawazo pia kukaa muda mrefu bila kula hata nilipojilazimisha nilishindwa kutokana na kuona chakula hakina ladha.

Niliamua kwenda ukweni kuuliza sababu ya kupewa talaka labda wao aliwaeleza. Wakwe zangu walikuwa wakikaa Buguruni kwa Mnyamani.

Nilipofika nilishtuka kukuta nyumba yao ya udongo wameanza kunyanyua upande kwa kujenga kwa tofali za udongo ulaya. Nilijua mambo ya mume wangu yamemnyookea.

Niliwakuta wazazi wake wote wapo nje, waliponiona walinipokea kama zamani, hakukuwa na tofauti yoyote wakati nikiwa na mtoto wao na nilipoachika. Mapokezi ya wakwe zangu yalinishtua na kuamini huenda talaka niliyopewa hawana taarifa nayo.

Baada ya kukaribishwa na kusalimiana na wazazi wa mtalaka wangu, baba mkwe aliniaga kwamba alikuwa akitoka kwenda zake Buguruni Chama. Kwa vile nilikuwa nimewafuata wao wote nilimuomba asiondoke ili nizungumze nao kwa pamoja.

“Samahani mama mi nafika Buguruni Chama,” baba mkwe aliniaga.
“Baba samahani nilikuwa na mazungumzo na ninyi wote wazazi wangu.”
“Hakuna tatizo mama.”
Baba mkwe alirudi kunisikiliza, baada ya kukaa alinisubiri mimi nieleze kilichonipeleka pale. Kwanza nilianza kwa kuwaomba msamaha.

“Kwanza samahani wazazi wangu.”
“Bila samahani mama,” alijibu mama mkwe.
“Nina imani mnajua kilichotokea karibuni kuhusu mimi na mwenzangu?”
“Ndiyo.”

Kauli yao ilinishtua kidogo kuonesha wanajua kila kitu lakini waliamua kukaa kimya. Ile ilinifanya niamini nitaweza kujua sababu ya mimi kupewa talaka.
“Wazazi wangu mpaka sasa nipo njia panda, ni kweli nimeachika talaka moja. Lakini mpaka sasa sijajua sababu ya kuachwa.”
“Hujui sababu ya kuachwa? Unamaanisha nini? Kwani ilikuwaje?”

“Amekuja na kunipa talaka bila maelezo.”
“Mmh! Sasa mwanangu amekupa talaka bila maelezo inakuja kweli, au kuna kosa ulilolifanya mwenzio kagundua?”
“Wazazi wangu, Mungu ndiye anajua lakini toka mume wangu ameondoka nimekuwa mtulivu na mstahimilivu kumsubiri yeye huku nikimuombea kwa Mungu afanikiwe.

“Lakini amerudi mume wangu kapendeza, furaha yangu ya kumuona ikageuka shubiri.”
“Wee mwana, unataka kutuambia mume wako amefika tu na kukupa talaka?” mama mkwe alionesha kushtuka.

“Ndiyo wazazi wangu.”
“Kakwambia tatizo nini?”
“Wazazi wangu kila nikimuuliza aniambie tatizo la kunipa talaka haniambii zaidi ya kusema nimuulize mama yangu ndiye anajua, mama naye kumuuliza kanijia juu kuwa mume wangu hana adabu, talaka atoe yeye sababu atoe mama yangu.”
“Mmh! Makubwa, inamaana hakuna tatizo lolote kabla ya kuondoka mumeo?”
“Hakuna wazazi wangu.“

“Amekuja na kukupa talaka bila kosa?”
“Ndiyo mama, nimemuuliza sababu ya kunipa talaka haniambii. Hata kama alikuwa na nia ya kuniacha angeniambia nikajua moja. Inauma mtu kumsubiri siku zote hizo faida ya uvumilivu ni talaka? Inauma... Inauma sana,” nilianza kulia kwani moyo ulikuwa ukiniuma.

“Basi mwanangu nyamaza kulia.”
“Mama inauma, jinsi tulivyoishi na mapenzi tuliyopeana na Beka si wa kunipa talaka kama ameniokota baa.”
“Kwa hiyo hakukueleza sababu?” walirudia swali la awali.

“Ndiyo wazazi wangu, ndiyo mana nimekuja hapa mnielezee sababu ya mimi kupewa talaka ili nijue kosa langu, huenda kweli nilimkosea mwenzangu bila mimi kujua.”

“Eti mama Beka mwanao alikueleza sababu ya kumpa talaka mkewe?” baba mkwe alimgeukia mkewe.
“Hajaniambia.”
“Wazazi wangu nawaombeni nipo chini ya miguu yenu niambieni sababu ya Beka kunipa talaka.”

“Uongo mbaya mie sijui, labda mama yako,” baba mkwe alimtupia mpira mkewe.

“Mume wangu Beka aliporudi alitueleza amempa talaka mkewe. Nina imani wote tulishtuka kwa sifa alizokuwa akikumwagia kabla ya kuondoka na aliporudi siku ile hata bila ya kupumzika alikuja kwako.

Aliporudi alitushtua kwa kutuambia kuwa amekupa talaka. Tuliingiwa wasiwasi labda amekuja huko kwa vile ni muda mrefu uko peke yako basi kakukuta na mwanaume.”

“Hapana wazazi wangu, amekuja ametukuta tupo sebuleni, alipofika alitusalimia na kuniomba tuzungumze, tukaingia chumbani kwetu, akasema ananipenda sana na hatapata mwanamke kama mimi lakini hana jinsi ameamua kunipa talaka.

“Nimembembeleza sana anieleze sababu ya kuniacha amekataa zaidi ya kuniambia kila kitu mama anajua. Basi niliamini wazazi wangu aliwaambia.”

“Kama mama yake hakumwambia sijui nani anajua sababu ya talaka, tulitegemea mzazi wako kuja lakini amekaa kimya basi tumejua sababu mnaijua wenyewe.”

“Mama haki ya Mungu sijui lolote, niliamini ninyi mnajua.”
“Mwenetu tumembembeleza lakini amesema wewe unajua.”
“Mimi?”nilisema huku nikijishika kifuani kushangaa kauli ya mume wangu.
“Ndiyo.”

“Jamani Beka mbona ananionea, mimi niijue sababu halafu nije niulize?”
“Ndiyo maana hata sisi tunashaanga wewe kusema hujui.”

“Wazazi wangu kama Beka kapata mwanamke mwingine angeniambia kuliko kunikosanisha na mama yangu. Japo nampenda lakini suala la kuachwa siwezi kulipinga japokuwa linaniuma sana.”
“Mmh! Sasa huu mtihani,” mama mkwe alisema.

“Kwani mama, Beka yupo wapi?”
“Beka aliondoka siku ya pili baada ya kutoka kwenu bila kutupa jibu lolote.”
“Amekwenda wapi?”

“Kwa kweli kama yeye hakukwambia sisi itakuwa vigumu.”
“Sawa wazazi wangu, kama mmekataa kuniambia alipokwenda Beka naamini hata sababu za kuachwa mnazijua."
“Hilo hatujui.”

“Nashukuru wazazi wangu kwa kunificha, lakini siwezi kuwalaumu, ila siku zote nitamlaumu Beka kwa kunitendea unyama.“

Baada ya kusema vile nilinyanyuka na kuondoka bila kuaga. Baada ya kutoka nilisikia nyuma wakiniita lakini sikugeuka baada ya kuona napoteza muda wangu bure.

Nilikwenda kwa mwendo wa haraka hadi Buguruni, nikachukua daladala hadi Temeke Mikoroshini kisha nikaelekea nyumbani.

Nilipofika niliingia chumbani kwangu na kujifungia nikajilaza kitandani.
Nilijikuta moyo ukiniuma kwa kuonewa bila kosa, nilijiuliza kosa langu nini, kwa nini nimekosa ushirikiano na kuwa peke yangu? Machozi yalizidi kunitoka kama maji.

Sauti nisiyoielewa niliisikia ikisema: Machozi siyo dawa ya maumivu wala ufumbuzi wa matatizo. Dawa ni kupambana, acha kulia futa machozi songa mbele.

Nilishtuka nipo peke yangu chumbani, nikagundua nipo kwenye mawazo makali yaliyonifanya nisikie sauti za watu. Lakini nilikumbuka kauli ile tulielezwa na mwanaharakati mmoja aliyekuja shuleni wakati nipo kidato cha nne na kutupa moyo wasichana tunapotokewa na matatizo ya kukatisha tamaa.

Nilinyamaza na kufuta machozi na kujikuta nikirudia mlolongo mzima wa maisha yangu mpaka kupewa talaka na yote niliyokutana nayo baada ya kupewa talaka.

Nilijikuta nikikubaliana na kauli ya mama kuwa Beka alipokwenda amepata mwanamke na aliporudi akaamua kunipa talaka akisingizia mama anajua ili kunikosanisha na mama yangu.
Nilinyanyuka na kwenda kuoga huku nikijiapiza kusahau yote. Baada ya kuoga nilitoka hadi nje nilipowakuta dada zangu wakiendelea kunywa pombe.

Nilisimama kwa muda nikiwaangalia jinsi walivyokuwa wakiyafurahia maisha. Hawakuwa na wanaume lakini kila siku mioyo yao ilijaa furaha tofauti na mimi niliyekuwa nimeolewa lakini kila kukicha maumivu yaliutawala moyo wangu.

Nilijikuta nikijilaumu kuchelewa kutoa uamuzi wa kutafuta mwanaume kwa mtu aliyenitenda. Moyoni niliamini unaweza kuishi bila mwanaume na maisha yako yakasonga.

Nilikumbuka maisha ya mama toka baba afariki ambaye sikubahatika kumuona. Aliweza kuishi maisha ya furaha japokuwa niliamini kwa umri wake baada ya kifo cha baba alikuwa na uwezo wa kuolewa.
Mama hakutaka kuolewa na alikuwa akiishi maisha yake mwenyewe.

Japokuwa mwanzo tabia yake ya kuwa na mwanaume zaidi ya mmoja na wote wakiwa waume za watu sikuipenda, baada ya maumivu niliyopewa na Beka nilikubaliana na mama na kuona hakukuwa na faida ya kuishi maisha ya ndoa au kuwa mwaminifu kwa mwanaume asiyekuwa mwaminifu.

Baada ya kuwaza sana huku nikiendelea kuwatazama dada zangu waliokuwa wakifurahia maisha, waliponiona waliniita ili nikaungane nao kupunguza mawazo.
“Njoo mdogo wangu, kunywa kidogo upunguze mawazo.”

Nilijisogeza karibu na kupewa glasi iliyokuwa na bia nusu. Niliichukua na kuipeleka mdomoni na kuinywa kama maji. Ilikuwa chungu kiasi cha kunifanya nifumbe macho na kuipitisha kooni kwa shida. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilianza kunywa bia kwani niliamini humpunguzia mtu mawazo. Nilijikuta nikipingana na mawazo yangu ya awali kuwa pombe ni uhuni.

Dada zangu walifurahia kitendo changu cha kujaribu bia. Waliniongezea kwenye glasi kila nilipomaliza, japokuwa sikuwahi kunywa lakini haikuwa mbaya sana.
Nilijilazimisha kuinywa mpaka nikamaliza bia moja. Dada aliniongezea nyingine ambayo niliendelea kunywa bila kujua kipi kitafuata.
 
Sehemu ya 09

Nilijilazimisha kuinywa mpaka nikamaliza bia moja. Dada aliniongezea nyingine ambayo niliendelea kunywa bila kujua kipi kitafuata.

Nilijikuta nikihisi kizunguzungu, dada aliendelea kunilazimisha nimalize bia nyingine, kitu kilichonifanya nilewe na kulala pale nilipokuwa nimekaa.

Nilishtuka siku ya pili na kujikuta nimelala kitandani kwangu nikiwa nimejisaidia haja ndogo bila kujua huku nikisikia njaa kali. Nilinyanyuka na kwenda kuoga na kufanya usafi kisha nikaanza kutafuta supu.
***
Nilijikuta nikijiingiza katika ulevi ili kupunguza mawazo, pamoja na kufanya yote bado sikuwa tayari kuutoa mwili wangu kama asusa kwa wanaume kwa kuhofia maradhi.

Japokuwa dada zangu walinikuwadia kwa wanaume ikiwa ni pamoja na kuniletea fedha walizopewa, lakini sikuwa tayari kujiingiza kwenye ukahaba.

Niliamua kujiingiza kwenye ulevi kama mfariji wangu kwa kipindi kile kilichokuwa kigumu sana kwangu, kwa vile mpaka muda ule bado sikujua sababu ya kupewa talaka ambayo ilionekana kuwa na siri nzito ambayo sikuwa nikiijua.

Lakini kulikuwa na tatizo lililokuwa likinisumbua mpaka mama akanikataza kunywa pombe kwa kuwa ilikuwa ikinishinda. Kila nilipokuwa nikinywa pombe na kuanza kulewa, niliangua kilio kumlilia mume wangu.

Kwa wenzangu ilikuwa ni karaha na kuonekana kama nilikuwa nikiwapigia makelele wakati awali tulilizungumza na kukubaliana. Nilijitahidi kumsahau mume wangu, mtu ambaye nilimzoea na kuamini kifo ndicho kingetutenganisha lakini talaka ilikuwa pigo na kovu kubwa maishani mwangu.

Kila nilipolia na kukemewa niliwaahidi dada zangu kuwa sitalia tena, pia niliahidi nitaachana na mawazo ya mtalaka wangu aliyeniacha bila sababu za kueleweka.

Lakini kila nilipokunywa pombe na kulewa yote yalijirudia na kuanza kulia huku nikitawaliwa na mawazo mabaya ya kunitaka ninywe sumu ili niepukane na aibu ya kuachwa.

Wakati kwangu likiwa pigo mujarabu moyoni mwangu, dada zangu waliotangulia kuachika hawakutetereka waliendelea na maisha kwa kutumia miili yao kama mitaji ya kuwaweka mjini bila kuhofia hali ya hatari.

Niliamini njia ya kumuondoa mume wangu akilini ni kuwa bize kuliko kuendelea kukaa nyumbani na kujilazimisha kunywa pombe ambayo kila nilipolewa nilimlilia mtalaka wangu.

Niliamini ubize pekee ndiyo ungeweza kunisaidia kuchosha mwili na nikirudi nyumbani mchovu, nitafikia kuoga kula na kulala kuliko kushinda nyumbani kusubiri wanaume.

Mwanaume mmoja wa dada mkubwa alikuwa anafanya kazi serikalini, niliamini anaweza kunisaidia kupata kazi.

Nilimweleza dada amweleze anitafutie kazi popote.
Baada ya kumweleza dada amwambie alinihakikishia kunipa jibu ndani ya wiki.
****
Baada ya siku nne dada aliniletea taarifa kuwa kazi imepatikana kwenye super market iliyopo katikati ya jiji. Kwa kweli nilifurahi sana kupata kazi nikiamini kuwa bize kutanifanya niwe mbali na vishawishi vibaya.

Nilielezwa Jumatatu nilitakiwa nianze kazi, bwana wa dada alisema atanipitia asubuhi ya siku hiyo, hivyo nilitakiwa niamke mapema kujiandaa kabla hajafika.

Kwa vile taarifa niliipata siku tatu kabla, nilijiandaa kwa kutafuta nguo itakayoendana na maeneo yale, japokuwa siku zote sikupenda kuvaa nguo fupi kwani zilininyima uhuru na kujiona nakuwa mtupu.

Siku ya Jumatatu niliamka alfajiri, nikajiandaa na kuelekea kwenye kazi hiyo. Saa moja kasoro bwana wa dada Sauda alifika na gari lake na kunichukua kunipeleka kwenye hiyo super market.
Tulikwenda mpaka kwenye super market iliyokuwa katikati ya jiji. Tulipofika alipiga simu na kumsikia akizungumza.

“Haloo...eeh...nimefika...haya nakuja.”
Baada ya kukata simu aliniambia:
“Twende.”
Sikumjibu, nilimfuata, tukaingia naye ndani na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi moja iliyokuwa ya vioo vitupu na kuingia ndani.

Ndani tulimkuta kaka mmoja mtanashati, baada ya kuingia nilikaribishwa kwenye kiti. Nilikaa na kutulia huku bwana wa dada akisalimiana na yule kaka kisha alisema:
“Sasa bibie mi acha niwahi, kila kitu atamalizia huyu mwenyeji wako.”

“Hakuna tatizo.”
Bwana wa dada alitoka na kuniacha na yule kaka ambaye aliniomba radhi na kutoka. Baada ya muda alirudi na fomu ambazo zilikuwa za kuajiriwa. Baada ya kukaa aliniuliza maswali mawili matatu kisha alinipeleka sehemu, nikapigwa picha.

Baada ya zoezi lile nilirudi ofisini kwa yule kaka aliyekuwa meneja wa duka lile kubwa sana. Alinyanyua simu na kuagiza chai, baada ya muda ililetwa na kunywa kisha alimwita dada mmoja.

Alipofika alimweleza:
“Suzy huyu ni mfanyakazi mpya, naomba umpe ushirikiano wa hali ya juu.”
“Hakuna tatizo bosi.”
“Kampatie sare na aanze kazi.”
“Hakuna tatizo, atakuwa sehemu gani bosi?”

“Mweke kwa keshia.”
“Hakuna tatizo, kitambulisho?”
“Muone Sam nina imani kitakuwa tayari.”
“Haya shem, nina imani Suzy atakusaidia, kazi njema.”

“Asante.”
Nilitoka na Suzy mpaka kwenye chumba kimoja kilichokuwa na sare na kunichagulia inayonitosha kisha tuliongozana mpaka kwenye chumba kingine na kukuta kitambulisho changu kipo tayari.

Nilipewa na kukivaa kisha nilipelekwa sehemu na kuelekezwa kama mtu akishalipia bidhaa aliyonunua namuwekea kwenye mfuko na kuwakaribisha tena.
Haikuwa kazi kubwa sana lakini nilichoka sana kwa vile sikuwa nimezoea kusimama muda mrefu.

Jioni bwana wa dada alinipitia. Kabla ya kuondoka da Suzy niliyekuwa nimemzoea kwa haraka, alinieleza muda wa kuingia kazini na umuhimu wa kuwahi.

Nilimshukuru na kumuahidi kuwahi siku ya pili. Niliingia ndani ya gari la shemeji na kurudishwa nyumbani. Njiani shemeji aliniuliza mambo mengi kuhusiana na kazi.
Sikusita kumshukuru kwa msaada wake ambao ulikuwa muhimu kuliko kitu chochote kwa wakati ule.

Tokea siku ile nilianza kazi ya kuuza kwenye super market na jioni shemeji alinipitia kama kawaida. Siku zote nilirudi nimechoka baada ya kuoga na kula muda mwingi niliutumia kitandani kwangu kupumzika.

Taratibu nilianza kumsahau mtalaka wangu Beka na kuamini kuna maisha mengine baada yake kwa kujua kila linalomtokea mwanadamu lina makusudio yake.

Kazi niliizoea na kuwa maarufu kutokana na ucheshi wangu. Lakini nilikuwa na wakati mgumu kazini kutokana na wanaume wengi wakware kunitaka kimapenzi.

Pamoja na ahadi nyingi nilizopewa kama nitakubali kujitoa kwao kimapenzi, sikuwa tayari kujiingiza katika dunia iliyoniumiza na kufikia hatua ya kuwachukia wanaume, japokuwa sikutakiwa kumhukumu mtu kwa kosa la mwingine.
Moyoni nilipanga baada ya miaka miwili ndipo niufungue moyo wangu.

Najua unaweza kushangaa uamuzi wangu lakini kila aliyekumbwa na mkasa wa mapenzi hawezi kunishangaa kwa vile mapenzi yanaumiza sana hasa uachwe na mtu unayempenda tena bila kujua kosa lako.

Siku zilikatika huku nikizidi kuifurahia kazi yangu na maisha yangu mapya ya kuishi kama mdudu wa sikio bila kuwa na mshirika. Mwanzo niliamini maisha yale yangekuwa magumu ya kuishi bila mwanaume, lakini kila kitu ukiamua unaweza nami niliweza kabisa.

Nakumbuka siku moja wakati natoka kazini nikiwa ndani ya gari la shemeji bwana wa dada, baada ya kutoka kazini tulikwenda mwendo wa dakika tano, akanigeukia na kuniuliza:
“Mwaija una mpango gani?”
“Kuhusu nini shemeji?”
“Si nilisikia umeachana na mumeo?”

“Ndiyo.”
“Sasa una mpango gani baada ya kuachana naye?”
“Mmh! Bado sina mpango wowote nimeamua kupumzika kwanza.”
“Mwaija wewe bado msichana mdogo kwa nini ujifuje?”

“Sijifuji bali nimeamua kupumzika, kilichonikuta Mungu anajua.”
“Mwaija siyo Mungu anajua, mwanaume uliyekuwa naye hakuwa sahihi kwako.”
“Ukisema hivyo sikubaliani na wewe, Beka namjua vizuri kuliko mtu yeyote, kuna kitu tu ambacho kimesababisha aniache.”
“Kitu gani?”

“Wee shemu, tuyaache tu yalishapita hayo,” kwa kweli sikupenda kuzikumbuka habari za mtalaka wangu.
“Kama anatokea leo na kutaka kukurudia utakubali?”

“Naweza kukubali kama atanieleza sababu ya kuniacha na mimi kuikubali.”
“Sasa Mwaija tuachane na hayo kuna kitu nataka kukuambia japokuwa ninacho muda mrefu, lakini naamini leo ni siku muafaka.”
“Kitu gani hicho shemeji yangu?”
“Kuhusu wewe.”

“Mimi! Nimefanya nini?”
“Siyo kwamba umefanya kitu ila kuna jambo nimejifunza kwako kwa muda mrefu.”
“Kipi?”
“Mwaija una tabia tofauti na dada zako.”

“Kivipi?”
“Unajiheshimu pia unajitambua.”
“Nashukuru kwa kulifahamu hilo.”
“Baada ya kuligundua hilo nilikuwa na ombi moja ambalo nina imani litakuwa na faida kubwa kwako.”
“Ombi gani?”
“Nataka nibadili maisha yako uweze kumiliki nyumba na gari.”

“Kivipi?”
“Nafikiri unajua mimi na dada yako tukoje?”
“Ndiyo najua.”
“Basi nimeshamfumania na wanaume zaidi ya watatu.”

Shemeji alitulia kuzungumza akasimamisha gari kuwaruhusu watu waliokuwa wakivuka barabara eneo la Chang’ombe Maduka Mawili wavuke. Baada ya watu kuvuka alibadili gea na kukanyaga mafuta kisha alinigeukia na kusema:
“Unajua nilikuwa nina mipango mikubwa na dada yako.”

“Mipango gani?”
“Nimjengee nyumba na kumnunulia gari.”
“Tatizo nini?”
“Hataki nimuoe zaidi ya kupenda maisha anayoishi, wewe ni mdogo lakini una akili sana.”

“Shem, si nasikia umeoa?”
“Ndiyo, lakini angekuwa nyumba yangu ndogo.”
“Mmh! Na mimi unataka kuyabadilisha maisha yangu kivipi?”

“Mwaija nataka uwe mpenzi wangu, nakuhakikishia kwa jina la Mungu kukufanyia mambo yote niliyokuahidi hata kabla ya kukutana nawe kimwili ili uniamini.”


ITAENDELEA LEO SAA NNE USIKU
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom