Sehemu ya 22
Niliuma meno na kusukuma kwa nguvu zote. Mara kitu kilifyatuka kwa mbele na kufuatiwa na damu nyingi nyeusi. Niliendelea kujikema, damu iliendelea kutoka ikiwa mabongemabonge na kufika robo ya sinki la choo.
Ilikuwa damu nyeusi iliyokuwa ikinuka kama kitu kimeoza. Wakati huo nilianza kuharisha mfululizo kitu kilichonifanya niishiwe na nguvu na kuanguka msalani.
***
Niliposhtuka nilijikuta nipo hospitali, niliponyanyua machoni niliwaona watu kwa shida macho yalikuwa kama yana ukungu wakiwa wamejazana kitandani kwangu huku nikiongezewa damu.
Uwezo wa kuona vizuri sikuwa nao kwa vile nilipojitahidi kutazama vizuri niliona kitanda kikizunguka na kunifanya nifumbe macho na kizunguzungu kikali kilinishika.
Niliisikia sauti ya mama ikiniita:
“Mwaij...Mwaija.”
Nilimsikia lakini sikuwa na uwezo wa kufumbua mdomo japokuwa nilijitahidi kuitikia. Nilikuwa najisikia vibaya sana kizunguzungu kilikuwa kikali sana.
Nilitulia nimefumba macho, kizunguzungu nacho kilipungua taratibu na usingizi ulinipitia.
Niliposhtuka nilijikuta bado nipo kitandani na mama na dada zangu walikuwa wapo pembeni wakionesha wapo kwenye nyuso za huzuni. Mara aliingia daktari na kusogea kitandani kwangu.
“Mwaija,” aliniita kwa sauti ya upole.
“Abee,” safari hii sauti ilitoka.
“Unajisikiaje?”
“Kizunguzungu.”
“Kitaisha tu, damu uliyopoteza ilikuwa nyingi.”
“Damu!?” Nilishtuka.
“Ndiyo, ulikuja kwenye hali mbaya sana, mpaka sasa hivi unazungumza Mungu mkubwa.”
“Mimba yangu ipo salama?” lilikuwa swali lililonitoka mdomoni, kwani haikuwa tofauti na tukio la awali la kuharibika mimba yangu.
“Bado tunaangalia kwanza hali yako mengine yatafuata baadaye.”
“Mama,” nilimwita mama aliyekuwa amesimama pembeni ya kitandani.
“Abee mwanangu unaendeleaje?”
“Kizungumzungu, lakini kwa sasa afadhali kidogo.”
“Pole.”
“Asante mama.”
“Pole Mwaija,” dada zangu nao walinipa pole.
“Asante.”
Kuna kitu kimoja nilikigundua katika nyuso za mama na dada zangu. Walionekana wamevimba macho kuonesha kama walikuwa wakilia.
“Mama,” nilimwita kwa kujilazimisha.
“Abee mama.”
“Mbona kama wote mlikuwa mkilia?” nilimuuliza mama.
“Mmh! Wee acha tu kweli Mungu mkubwa.”
“Kwa nini mama?”
“Sikuamini kama ungeweza kuzungumza hivi.”
“Kwa nini?”
“Hali tuliyokukuta nayo tulichanganyikiwa, mimi ndiye kidogo niliyejitahidi lakini dada zako walipokuona waliangua kilio. Hatukuamini kama utapona.”
“Kwani ilikuwaje?”
“Tumepigiwa simu na bwana yako akilia huwezi kuamini tulivyondoka nyumbani ndivyo tulivyo hakuna aliyekumbuka viatu wala kanga ya kujifunga juu.
“Tulikukuta amelazwa sebuleni damu chapachapa huko msalani ndiyo usiombe utafikiri kumechinjwa ng’ombe na harufu kali kama kuna kitu kimeoza.”
“Mungu wangu, ujauzito wangu upo salama?”
“Hatujajua, huwezi kuamini mimi na dada yako mkubwa tuna siku ya pili tupo hospitali hatujarudi nyumbani.”
“Kwa nini mama?” nilishtuka kwani niliamini tukio lile lilikuwa la siku ileile.
“Kwa hali uliyokuwa nayo tulijua umefariki kwani hata mapigo ya moyo yalionesha kusimama. Pamoja na kuelezwa turudi nyumbani hatukukubali. Tulilala nje ya hospitali kwa siku mbili mpaka ulipofumbua macho lakini hukuweza kuzungumza.
“ Lakini tulielezwa damu waliyokuwekea unaweza kurudi katika hali ya kawaida.
Damu uliyopoteza ni nyingi sana. Yaani tungechelewa kidogo tungekupoteza damu ilikuwa imekwisha kabisa mwilini, kwani tatizo nini mwanangu?” mama aliniuliza akiwa ameniinamia.
Nilijitahidi kuelezea hali yangu tokea damu ya siku ya kwanza na ya siku ile nilipotokewa na tatizo lile.
“Mmh!” waliguna wote.
“Kwa nini ulikaa kimya?” dada mkubwa aliniuliza.
“Nilijua labda ya kawaida kwa vile sikuwa na maumivu yoyote.”
Kuguna kwao kulinishtua na kujiuliza kulikoni kuguna wote kwa mpigo. Nilichowaeleza mbona kilionekana kuwashtua na kutazamana wote.
“Jamani kuna nini?” niliuliza baada ya kuingiwa na hali ya woga.
“Mwaija hebu kwanza tuangalie tiba za hospitali.”
“Kwa nini unasema hivyo mama?”
“Kauli zako zimenitisha mtu kupatwa na tatizo kila ukikutana na mwenzio. Pia hata yule mwanamke nina imani hakuwa mwema kwako.”
Kauli ya mama ulinishtua na kujiuliza inamaana aliyekuja alikuwa mke wa mzee Sambi na kama ni yeye mbona hakuniambia kweli. Nilikubaliana na kauli ya mama kutokana na mshtuko alioupata mzee Sambi juu ya ugeni ule pia hata kumfahamu kwa wajihi wake.
“Kwani mama aliyekuja si mwenye nyumba?”
“Tutajua tu kama amri ya Mungu au mkono wa mtu.”
Jioni alipokuja mzee Sambi kuniona alionesha uso wa furaha baada ya kunikuta nipo katika hali nzuri. Niliamini siku mbili nilizokuwa sina fahamu zilimchanganya sana.
“Karibu mpenzi,” nilimkaribisha.
“Asante, pole sana.”
“Asante.”
“Vipi unaendeleaje?”
“Sijambo.”
“Vipi umekula?”
“Ndiyo.”
Baada ya muda mama na dada zangu walitoka nje na kuniacha na mzee Sambi. Niliamini ile ndiyo ilikuwa nafasi yangu ya kupata ukweli aliyekuja siku ile kwangu alikuwa nani.
“Eti mpenzi aliyekuja siku ile alikuwa mkeo?”
“Mbona unauliza hivyo?”
“Nijibu swali langu,” nilikuwa mkali kidogo.
“Ndiyo.”
“Ndiyo nini?”
“Ni mke wangu kweli.”
“Mzee Sambi, mkeo alikuja kwangu kufanya nini?”
“Sijui.”
“Amepajuaje?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Na kwa nini ulinificha ukanidanganya?”
“Nilihofia kukushtua kwa vile nilikwenda nyumbani tukayamaliza.”
“Huu ugonjwa wangu nina wasiwasi na mkeo.”
“Kafanya nini?”
“Nitajua tu, ila kama ni yeye nitakufa naye.”
“Hawezi kufanya mchezo wowote mchafu.”
“We mtetee labda nife.”
“Mpenzi usiwe na mawazo potofu, kwa vile upo hospitali ngoja tuone kitakachoendelea.”
Siku ya pili niliamka nikiwa na nguvu na chupa za damu nilizoongezwa ziliisha na kujiona nipo sawa. Nilichotaka kujua kuhusu ujauzito wangu.
Majibu ya vipimo vyangu yalipatikana jioni ya siku ile baada ya mzee Sambi kuja. Vipimo vilionesha ujauzito wangu umetoka. Baada ya kupewa taarifa ile nilipata mshtuko uliosababisha nipoteze fahamu.
Baada ya kurudiwa fahamu na kukumbuka kilichonitolea nililia sana. Niliamini siku ile kama ningekuwa ghorofani basi ningejitupa au kama kungekuwa na sumu karibu yangu ningekunywa.
Roho iliniuma kama kidonga na kujiuliza hali ile itaendelea mpaka lini.
Nilijiuliza ule ndiyo utakuwa mchezo wa kushika ujauzito na kutoka katika maisha yangu. Taarifa za kupoteza uhauzito wangu ilimliza mzee Sambi kama mtoto.
Kwa kweli lilikuwa pigo lingine kubwa maishani mwangu. Toka siku niliyopewa taarifa ya kuharibika kwa ujauzito wangu mwingine, chakula kilikataa kupita mdomoni japokuwa mama na dada zangu walinilazimisha nile angalau kidogo.
Siku nne kwangu zilikuwa sawa na mwezi mzima kwa mawazo na kushindwa kula, kila nilipofikiria mateso yanayonipata na kupoteza ujauzito wangu kula mara.
Nilikonda kama niliugua kwa muda mrefu. Mama na dada zangu walitumia muda mwingi kuwa karibu yangu huku wakibembeleza angalau nile kidogo, lakini wapi chakula kilikataa kupita mdomoni, muda mwingi nilikuwa nikilia tu.
Kingine kilichoniumiza akili kilikuwa maumivu ya tumbo na kuendelea kutoka damu kama ya hedhi kwa muda mrefu. Nilikuwa nashinda na pedi ili nisijichafue.
Mgonjwa wa tumbo wasiwasi ulikuwa labda sikusafishwa vizuri. Ilibidi nifanyiwe usafi upya. Nilimshukuru Mungu kidogo hali ya maumivu ya tumbo ilitulia na kuamini maumivu yale yalisababishwa na uchafu uliobaki.
Kuendelea kutoka kwa damu kulinichanganya sana japokuwa haikutoka nyingi sana. Lakini bado nilipakia na swali kwa nini iendelee kutoka.
Nilifanya vipimo vyote lakini haukuonekana ugonjwa wowote. Nilianza kuingia na wasiwasi yale ni mambo ya kiswahili ‘kishirikina’.
Kila kukicha hali yangu ilizidi kubadilika nikawa siwezi kunyanyuka.
Nikawa mtu wa kulala kitandani miguu ilikuwa kama imepooza. Kutokana kukosa ufumbuzi wa ugonjwa wangu daktari mmoja alimshauri mama tuhangaike upande wa pili.
Ilibidi nitolewa hospitali, ungeniona siku ile ungelia machozi. Nilikuwa nimekwisha kama mgonjwa wa kifua. Mama alinichukua na kunipeleka kwa mtaalamu Temeke Yombo.
Mwaija miye nilikuwa wa kubebwa kama mtoto mdogo sura yangu kwa muda mfupi ilibadilika kama mzee kila aliyeniona alitokwa na machozi.
Nilipelekwa kwa mganga wa kiume ambaye aliponiona kabla ya kunitibu alishauri kwanza nikapimwe damu kwani nilikuwa na dalili zote za ugonjwa wa kisasi kama kukonda na nywele kubadilika rangi.
Nilipelekwa hospitali kupima na majibu yalikuwa sina tatizo lolote. Mganga baada ya kupata majibu alianza kunitibu kwanza kwa kuangalia tatizo langu nini.
Japokuwa nilikuwa siwezi kukaa lakini alichokuwa akikisema nilikisikia:
“Mgonjwa wenu amechezewa na mwanamke.”
“Kivipi?”
“Ametupiwa jini.”
“Na nani?” mama aliuliza.
“Na mwanamke mmoja alimtembelea kwake.”
Kauli yake ilifanya mama na dada zangu waangaliane na kushusha pumzi ndefu.
“Ni nani?”
“Mwenyewe anamjua, kuna siku alitembelewa na mgeni saa tano asubuhi akiwa amevaa vitenge kuanzia juu mpaka chini. ni kweli?”
“Ni kweli kabisa,” nilijibu.
“Basi yule ndiye mbaya wenu japokuwa siku ile hakuja kwa shari.”
“Ni nani?”
“Huyu ana mwanaume ambaye ana mke na yule ndiye mkewe. Bahati mbaya alikuwa hajulikani ila alitaka kupata ukweli baada ya kuujua ukweli ndipo alipokwenda kufanya mambo yake.
“Alitumia uchawi wa jini kupitia mumewe, jini lile lilikuwa likitembea naye bila kujua na muda wa kukutana jini lilitangulia mbele ili kuuharibu ujauzito wako.
Baada ya kukutana na mwenzako ndipo lilipopata nafasi ya kutangulia na kusababisha utokwe na damu ukiwa mwanzo wa kuuharibu ujauzito wako.
“Kwa vile ulitoka damu hukufahamu tatizo, ulikwenda hospitali na kufanikiwa kuzuia damu isitoke. Kwa vile ulikuwa hujui kilichokuwa kikiendelea uliamini tatizo lako limekwisha.
Kwa vile jini lile lilitumia njia ya wewe kukutana na mwenzako, lilisubiri mtakapokutana tena. Siku mliyokutana lilitumia nafasi ile kuuharibu ujauzito wako ulioambatana na kutoka damu nyingi sana.”
“Sasa mbona baada ya ujauzito kutoka kila siku hali yake inazidi kuwa mbaya damu imekuwa haikomi kutoka?” mama aliuliza.
“Lile jini lililotumwa kwake lilikuwa na kazi mbili kubwa, kazi ya kwanza limeifanya vizuri na sasa linafanya kazi ya pili.”
“Kazi gani?” mama aliuliza.
“Kwanza kuiharibu mimba ambayo limefanikiwa, pili kummaliza taratibu mpaka azimike kabisa.”
“Mungu wangu! Kwa hiyo bado jini hilo lipo?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo utatusaidia vipi?”
“Kumtibu tu.”
“Na aliyemfanyia?”
“Ngoja kwanza tumtibu kisha mambo mengine yatafuata.”
Nilianza kupata tiba kwa kupewa dawa ya majani mabichi kunywa ambayo ilisababisha nitapike na kuharisha. Baada ya muda nilipewa uji uliochanganywa na dawa.
Baada ya kunywa nilipitiwa usingizi, kwa muda mrefu toka nianze kuumwa nilipitiwa na usingizi mzito.
Nilipoamka nilikuta tayari imeandaliwa nyungu ambayo nilifushwa kwa kufunikwa na shuka. Kwa vile sikuwa na uwezo wa kukaa peke yangu nilishikiliwa mpaka huduma ilipokwisha.
Nilirudishwa na kulazwa kwenye mkeka huku nikiwa navuja jaho kama maji mwili mzima kutokana na joto kali la nyungu. Baada ya mapumziko nilipatiwa chakula ajabu nilikuwa chakula vizuri.
Siku ile nililala pale na kubaki na dada kwa ajili ya kunisaidia kwa vile miguu haikuwa na nguvu. Nilikaa kwa mganga kwa wiki mbili nikiendelea kupata tiba.
Tiba ile ilinisaidia niliweza kusimama na kutembea lakini kwa shida, Lakini nilikuwa na mbadiliko makubwa katika afya yangu ilikuwa tofauti na nilivyokwenda nilikuwa mtu wa kubebwa tu.
Lakini mpaka naondoka kwa mganga damu ilikuwa imekata hata hamu ya kula nilikuwa nayo. Tatizo lilikuwa kwenye nguvu za miguu nilikuwa siwezi kusimama au kutembea kwa muda mrefu.
Pia alikatazwa nisirudi kwangu mpaka mganga atakapokwenda kupatengeneza. Kipindi chote nilichokuwa kwa mganga sikumuona mzee Sambi.
Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa hospitali siku nilipomuuliza kuhusu mkewe kuja nyumbani kwangu.Tangu siku ile alipoondoka sikumuona tena.
Nilijikuta najawa na mawazo kuhusu kupotea kwa mzee Sambi kwa sababu niliamini matatizo yote yanatokana na yeye.
Nilijiuliza kuna nini kimemsibu mpaka kunikimbia.
Lakini muda ule sikumfikiria sana yeye zaidi ya afya yangu, niliendelea kutumia dawa nilizopewa na mganga ili kuimalisha afya yangu. Nilitumia zile dawa kwa wiki lakini miguu ilikuwa bado haijapata nguvu.
Nilirudishwa tena kwa mganga baada ya miguu kuanza kupasua na kuwaka moto. Usiku nilikuwa silali kutokana na ukali wa maumivu nilikuwa nakesha nikilia mbona niliteseka vitu vingine visikie kwa mtu siyo vikukute.