Sehemu ya 10
“Mwaija nataka uwe mpenzi wangu, nakuhakikishia kwa jina la Mungu kukufanyia mambo yote niliyokuahidi hata kabla ya kukutana nawe kimwili ili uniamini.”
“Na dada?”
“Mwaija, dada yako hajitambui pia hajui hatima ya maisha yake na kusahau uzuri una mwisho.”
“Lakini kumbuka kufahamiana na wewe ni kupitia kwa dada huyohuyo ambaye amekuwa waluwalu.”
“Mwaija nina malengo mazuri na wewe, ukikubali nitahakikisha nakuachisha hii kazi na kukufungulia mini super market utakayoimiliki mwenyewe.”
“Yote umesema mazuri ambayo kila mwanamke anayatafuta kuyapata kwa mpenzi wake. Lakini tatizo siwezi kushea mwanaume na dada yangu, ni matusi kwetu.”
“Mwaija, dada yako si mke wangu ni mpenzi wangu, hata nikimuacha bado ana wanaume wengine. Naomba usiipoteze nafasi hii.”
“Samahani kwa hili siwezi,” pamoja na ahadi nono sikuwa tayari kujidhalilisha.
“Inawezekana nimekushtua ila nakuomba nenda nyumbani jifikirie taratibu kisha utapata jibu. Ila naomba usinifikirie vibaya kwa vile nimekutafutia kazi ndiyo sababu ya kukutaka.”
“Walaa, ila tu siwezi kushea penzi na dada yangu.”
“Najua utasema hivyo lakini kama utamwambia mtu yeyote nilichokuahidi atakushangaa kama utakataa.”
“Ni kweli atanishangaa, lakini heshima ya mtu haibebwi na mtu mwingine bali yeye mwenyewe.”
“Najua Mwaija, ila naomba nilichokuambia kipe muda akilini mwako ili uweze kunipa jibu ambalo najua litakuwa zuri kwako na kwangu.”
“Sidhani kama nitakuwa na jibu tofauti na nililokueleza.”
“Najua una msimamo, naomba utafute mawazo hata kwa rafiki zako wa karibu nina imani utabadilika.”
“Sawa, lakini siamini kama kuna mabadiliko zaidi ya hili nililokueleza. Japokuwa sikuwa tayari kuufungua moyo wangu kwa sasa lakini kwa ukarimu wako na kuonesha kunijali kama ungekuwa huna uhusiano na dada ningeweza kukupa nafasi ya kukufikiria.”
“Sawa Mwaija, bado nasisitiza sitakuwa na wewe kwa ajili ya kukuumiza. Najua umeumizwa hivyo nitajitahidi kuwa mfariji wako.”
“Halafu kuna kitu kingine ambacho nakiogopa, kama usingekuwa na uhusiano na dada bado suala la kutembea na mume wa mtu linanitisha.”
“Mwaija, mke wangu hana kizazi nami nina pesa leo hii nikifariki nani atakuwa mrithi wangu? Nilitaka kuzaa na dada yako lakini alikataa hawezi kuzaa.
“Hebu fikiria nitabadili wanawake wangapi wakati kipindi hiki hali ni mbaya kama usipokuwa makini?”
“Ni kweli, lakini umenipa mtihani mzito.”
“Wala si mzito, upe muda moyo wako kwa vile kitu nitakachokifanya kina manufaa makubwa sana kwako. Mwaija fedha sina sana ila nina uhakika wa kukufanya uishi maisha ya ndotoni.”
“Mmh! Bado mtihani kwangu.”
“Mwaija kama hilo huwezi naomba unisaidie kitu kimoja.”
“Kitu gani?”
“Basi nizalie mtoto mmoja akiwa wa kiume nitakupa milioni 20 akiwa wa kike milioni 10.”
“Tatizo si kukuzalia bali kushea penzi na dada yangu.”
“Mwaija naomba katika hayo mawili moja lifanyie kazi.”
Wakati huo tulikuwa tumefika nyumbani, kabla ya kuteremka bwana wa dada alinipa bahasha.
“Ya nini?”
“Kaifungulie ndani.”
Sikutaka kuhoji, nilipokea. Kabla ya kuondoka alinishika mkono mmoja kwenye bega na kuniangalia kwa muda mpaka machozi yakamtoka.
“Shemu unalilia nini?” nilimuuliza.
“Basi, naomba tulilozungumza usimwambie mtu.”
“Hata siku moja sina tabia hiyo.”
“Nimefurahi kusikia hivyo, naomba uyafanyie yote kazi niliyokueleza.”
“Sawa.”
Tuliagana na mimi kuteremka kwenye gari na kuelekea ndani. Bwana wa dada naye alipaki gari pembeni na kuingia ndani kuonana na dada. Mimi nilikwenda moja kwa moja kuoga ili nipate muda wa kupumzika.
Baada ya kuoga na kula nilijilaza kitandani na kuifungua bahasha ambayo ilikuwa na fedha mpya, nilipohesabu nilikuta laki saba taslimu. Niliziweka kwenye kabati langu na kurudi kitandani kujilaza. Nilijikuta nawaza vitu vingi kuhusiana na maneno ya bwana wa dada. Machoni kwake alionesha hafanyi mzaha lakini bado sikutakiwa kumkubalia kwa vile ingeonesha jinsi gani familia yetu isivyojiheshimu.
Nilikuwa na wazo la kulitupilia mbali lakini niliamini mama anaweza kunisaidia hata kuweza kulimaliza bila kumuudhi bwana wa dada pia kutogombanisha na dada yangu japokuwa niliamini kabisa katika tabia yake hata kama yule bwana angeamua kuachana naye hakuna chochote kingemgusa moyoni mwake.
Wazo lile sikutaka kuliacha lipite vilevile japokuwa moyoni nilikuwa na uamuzi wangu ambao niliamini utabakia kama ulivyo.
Wazo la kwenda kumueleza mama nililisitisha kidogo na kupanga kwanza kwenda kumwambia da Suzy ili nijue atanipa mawazo gani. Da Suzy toka nianze kazi pale alikuwa mtu wangu wa karibu ambaye tulifikia hatua kila mtu kumweleza mwenzake mambo ya ndani, japokuwa kuna baadhi ya tabia za familia yangu nilimficha.
Siku ya pili nilipokwenda kazini wakati wa chakula cha mchana nilimweleza da Suzy kuwa nina mazungumzo naye baada ya kazi, naye alinieleza atanisikiliza.
Baada ya muda wa kazi tulikwenda kwenye mgahawa ulilokuwa karibu na kazini kwetu.
Kwa vile nilijua mazungumzo yetu yatachukua muda kidogo, nilimpigia simu bwana wa dada kuwa asije kunichukua nitachelewa kidogo. Lakini mwenzangu alipokea tofauti na kujua ninataka kumkimbia kutokana na kauli yake ya kunitaka kimapenzi.
“Mwaija, usifike huko nililofikisha kwako ni ombi tu si lazima. Ulitakiwa kulifanyia kazi na kuliangalia lina uzito gani kama halina mashiko ungeachana nalo na si kukimbiana.”
“Hapana shemu, kuna kitu kitanichelewesha kwa leo, lakini kesho utanichukua kama kawaida,” nilijaribu kumtoa wasiwasi.
“Mwaija mi nipo tayari kukusubiri kwa muda wowote lakini leo nikurudishe nyumbani kama kawaida.”
Mmh! Shem bado alikuwa king’ang’anizi.
“Hapana shemu leo naomba nisikusumbue.”
“Mwaija najua umekasirika, bado nasisitiza ni ombi wala si lazima. Wewe ni mtu mzima mwenye kujua zuri na baya kama ulishawahi kuolewa hakuna kigeni tena kwako.”
“Shemu umeenda mbali sana, kama kungekuwa na mabadiko yoyote ningekueleza. Unavyonifahamu ndivyo nilivyo.”
“Basi naomba ukubali nikusubiri,” shemu alikuwa king’ng’anizi. Ilibidi nimkubalie anipitie ili niondoe wasiwasi wake.
“Basi hakuna tatizo nikimaliza mambo yangu nitakutaarifu.”
“Hapo sawa,” kauli ya bwana wa dada ilinishtua na kujiuliza nini mwisho wa yote kama sitakubaliana na yeye kitu ambacho kilikuwa kwenye mawazo yangu.
Baada ya kukubaliana na bwana wa dada, nilimgeukia da Suzy ambaye alionekana kunishangaa muda wote niliokuwa nikibishana.
“Vipi Mwaija?” aliniuliza baada ya kukata simu.
“Ndiyo yaliyonifanya niombe ushauri wako.”
“Yepi hayo?”
“Ndiyo maana tupo hapa.”
“Mmh! Haya.”
Vinywaji tulivyoagiza vililetwa, wote tuliagiza juisi ya embe mchanganyiko na parachichi. Kila mtu alichukua glasi yake na kunywa kidogo kisha da Suzy alikaa mkao wa kusikiliza.
Baada ya kutulia kwa muda nilimwita da Suzy.
“Da Suzy.”
“Abee mdogo wangu,” aliniitikia huku akinitazama usoni.
“Kuna jambo moja nimekutana nalo jana limenipa wakati mgumu. Japokuwa nilikuwa na uamuzi wangu lakini sikutaka kuamua peke yangu kwa vile naliona jambo lenyewe zito.”
"Jambo gani mdogo wangu?" Niliamua kumpa historia fupi ya maisha yetu na nilichoelezwa na bwana wa dada jana yake. Da Suzy alionesha kunishangaa, baada ya kunitazama aliniuliza swali.
“Mwaija unataka kuniambia Mzee Sambi si mpenzi wako?”
“Ni shemeji yangu bwana wa dada yangu.”
“Basi sote tunajua yule ni mtu wako.”
“Walaa, ni shemeji yangu.”
“Basi Emma hajui lolote, ingekuwa wewe si mtu wa mzee Sambi lazima angekutongoza. Yule mwanaume mchafu sana, ameishatembea na robotatu ya wafanyakazi pale.”
“Lakini wewe naona anakuheshimu sana.”
Kauli yangu ilimfanya da Suzy kucheka kitu kilichonifanya nishtuke.
“Dada mbona unacheka?”
“Mwaija we mtu wangu wa karibu siwezi kukuficha kitu. Emma alipokuja kazini mimi ndiye nilikuwa mtu wake wa kwanza.”
Nilijikuta nikishtuka lakini nilificha mshtuko wangu. Da Suzy aliendelea kunipasha nisivyovijua.
“ Kwa kweli nilimpenda toka siku ya kwanza kuanza kazi. Kwa vile nilitaka kumvuta karibu yangu, nilitumia muda mwingi kumfundisha kazi.
“Lakini baada ya muda alipanda cheo kwa vile alikuja na elimu yake. Hapo ndipo aligeuka mchafu sana kwa kutembea ovyo na kila msichana mzuri anayekuja kufanya kazi.
“Si kazini hata huko anapokaa simu yake kila siku nilikuwa nakamata ujumbe wa mapenzi wa wanawake tofauti. Nilijaribu kumshauri na nia yetu ilikuwa tuoane lakini hakuonesha kubadilika, niliona kuchangia mwanaume ni kujidhalilisha.
Mwisho wa siku nilibwaga manyaga.” Da Suzy alijikuta akinipa historia ya uhusiano wake na bosi wetu Mr Emma.
“Mmh! Pole sana, sasa kazi mlifanyaje?”
“Kwa vile maisha nayajua nilijielekeza kwenye kazi na kumpa uhuru.”
“Lakini wewe si umeolewa?”
“Ndiyo, tena na rafiki wa karibu wa Emma.”
“Mmh! Ilikuwaje?”
“Huwezi kuamini yule mkaka alikuwa akinipenda muda mrefu lakini nilimtolea nje. Baada ya kutendwa na Emma nilimfungulia milango ili kumkomesha Emma.”
“Mmh! Baada ya kuoana nini kilifuata?”
“Hakuna kitu zaidi ya kuheshimiana tu.”
“Ninavyowajua wanaume lazima kuna siku huwa anataka kukumbushia, inakuwaje akiomba?”
“Huwa namueleza tuheshimane, mwanzo alikuwa mbishi lakini sasa amenielewa.”
“Mmh! Wanaume ukiwachekea wanaweza kukuharibia ndoa bure,”
“Umeona eeh, mdogo wangu.”
“Lakini naona kama umri ulikuwa umemzidi?”
“Ni kweli, Emma nimemzidi miaka mitano, lakini nilimpenda sana huwa sipendi kukumbuka penzi langu lililopeperushwa kama vumbi kwenye upepo makali.”
“Mmh! Pole sana dada.”
“Asante.”
Da Suzy alitulia kwa muda akiwa ameinama kuonesha jinsi gani mapenzi yalivyomuumiza kumpenda mtu asiye muaminifu. Baada ya muda alinyanyua uso wake na kuchukua glasi ya juisi na kunywa kidogo na kunitazama kisha alisema:
“Mdogo wangu una mtihani mzito ambao ni sawa na kuitumia turufu moja iliyokuwa mkononi, ikutoe mrithi au ikutoe kapa.”
“Una maana gani da Suzy?”
“Mpaka mzee anakueleza jambo kama hilo ujue basi kakufuatilia muda mrefu. Malengo yake ni makubwa sana kwako.”
“Lakini kumbuka tayari ameishatembea na dada yangu.”
“Ni kweli, lakini kwa tabia ya dada yako ya kutokuwa na bwana mmoja, hiyo ni nafasi ambayo naamini unaweza usiipate mpaka unakufa.
Mtu akujengee nyumba na akununulie gari kwa ajili ya mapenzi ni wachache katika dunia ya leo ambayo wanaume wengi ni matapeli.
“Kama huwezi kukubali kuwa nyumba ndogo basi mbebee ujauzito ili upate hayo mamilioni. Nina imani Mzee Sambi alivyo na hamu ya mtoto lazima ahadi zote tatu atatimiza ukimzalia mtoto.”
“Mmh! Dada unanipa mtihani.”
“Hakuna mtihani, yupo wapi Beka uliyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua. Mdogo wangu Waswahili wanasema bahati haiji mara mbili na mchuzi wa mbwa unywe ungali moto ukipoa haunyweki.”
“Kwa hiyo unanishauri nimkubalie?”
“Mwaija mkubalie, nafasi kama hiyo mdogo wangu wenzako tunaiendea kwa waganga wewe inakujia miguuni unataka kuipiga teke?”
“Lakini naogopa kugombana na dada.”
“Fanyeni hata penzi la siri nina imani litakusaidia katika maisha yako.”
“Mmh! Nitajaribu kwa vile umeivunja ngome ya moyo wangu sina budi kukubaliana na wewe,” nilijikuta nikilegeza msimamo