Sehemu ya 15
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda niliondoka kwa kumpitia msichana wangu wa kazi na kuondoka naye hadi kwangu Tabata Savana. Nilipofika nilimweleza kuwa nitaishi naye kama ndugu yangu japokuwa nitamlipa msahahara kama kawaida. Alinishukuru kwa kumtoa kwenye mateso.
****
Niliyaanza maisha mapya ya kuishi kwangu nikiwa na mzee Sambi ambaye wakati huo alikuwa akinitafutia eneo kwa ajili ya kunifungulia Min super market maeneo ya karibu na aliponipangia kati ya Tabata Mawenzi na Shiba.
Niliendelea kumshukuru Mungu kwa kuyabadili maisha yangu huku bado nikiwa siishi kumkumbuka mume wangu Beka juu ya kunipa talaka bila sababu.
Kila nilipokuwa peke yangu nilimkumbuka sana Beka mwanaume ambaye niliamini ndiye wa maisha yangu.
Nilikuwa na mzee Sambi ambaye nilimpenda kutokana na kujitoa kwa ajili yangu huku akijitahidi kuona naishi maisha ya furaha muda wote. Lakini mapenzi ya kweli yalikuwa kwa Beka.
Lakini lazima niseme ukweli mzee Sambi sikumpenda kwa asilimia zote. Niliapa kumsamehe Beka kama atagundua makosa yake na kuja kuniomba msamaha.
Unaweza kunishangaa, lakini nilikuwa radhi kuishi maisha yoyote na Beka na kuwa tayari kuachana na kila kitu nilichoahidiwa na mzee Sambi.
Beka nilimpenda naye alinipenda hilo nililitambua, lakini kilichovunja mapenzi yetu sikukielewa mpaka siku ile alipokuja na kunipa talaka iliyokosa maelezo ya kina.
Mara nyingi nilipokuwa peke yangu nilijisahau na kuweka mkono shavuni na machozi kunitoka kukumbuka. Pamoja na raha nilizopewa na mzee Sambi huku ujenzi wa jumba langu la kisasa ukiendelea.
Bado nilikuwa na jereha kubwa moyoni mwangu ambalo siku zote donda lilikuwa bichi kwa vile sikujua sababu ya kupewa talaka bila kuelezwa kisa hasa.
Siku zote mtu akihukumiwa kwa kosa analolijua hata kama ni dogo na hukumu kuwa kubwa hujua kosa lake.
Lakini kwangu hata nilipokuwa katikati ya furaha kila nilipokumbuka mazingira tata ya talaka yangu furaha ilinipotea na kujikuta nikitokwa machozi na mkono shavuni.
Mara nyingi msichana wangu wa kazi alikuwa akinishtua na kutaka kujua sababu ya mimi kuwa vile.
Siku moja uvumilivu ulimshinda na kuamua kuniuliza:
“Dada una tatizo gani?”
“Nipo sawa.”
“Hapana dada si mara ya kwanza kukuona hivi, mara nyingi ukiwa peke yako unakuwa umeshika tama machozi yanakutoka kisha unatikisa kichwana na kufuta machozi."
“Mmh! Mdogo wangu ya dunia.”
“Yapi dada, mbona mimi yangu nimemwachia Mungu.”
“Ni kweli mdogo wangu, lakini langu linanitesa kila nikilikumbuka, kwa akili ya kawaida unaweza kulidharau lakini langu ni donda ninalo litonesha kila mara.”
“Kwani dada una tatizo gani?” Mariamu aliniuliza akiwa ananitazama kwa jicho la huruma.
Kwa vile alikuwa msichana aliyepevuka nilimweleza yote. Baada ya kunisikiliza alinipa pole..
“Duh! Dada unataka kuniambia mpaka leo hujajua sababu ya talaka yako?”
“Sijajua, na kibaya dua na maombi yangu yote yalikuwa kwa mume wangu. Hata katika maisha yetu hatukuwahi kugombana.”
“Basi si angekuambia kuliko kukupa mtihani usioujua?”
“Wee acha, kila nikikumbuka moyo unaniuma sana.”
“Lakini dada mbona Mungu kasikia kilio chako.”
“Mungu hajasikia kilio changu bali kanipandisha toka chini. Lakini jibu la swali langu bado sijalipata.”
“Ungeachana nalo tu.”
“Najitahidi kufanya hivyo, lakini moyo wangu umekataa kupinduka.”
“Na mama anasemaje?”
“Mama ajue nini ikiwa talaka kanipa Beka kwani mama yangu ni familia ya mtalaka wangu?”
“Mmh! Lakini Mungu mkubwa ipo siku utasahau.”
“Ndicho ninachokiomba usiku na mchana mawazo juu ya mtalaka wangu yafutike kichwani mwangu.”
Maisha yaliendelea huku nikiwa sina pingamizi ya kumpa mwili wangu mzee Sambi kwa vile sikuona sababu ya kunyima mwili wangu kwa vile tuliishi kama mke na mume.
Siku moja tukiwa kitandani tumejilaza, ilikuwa siku ya mapumziko, ambazo mzee Sambi alizitumia kuja kwangu kushinda mpaka jioni.
“Mwaija,” aliniita kwa sauti ya chini.
“Abee.”
“Unayaonaje maisha?”
“Namshukuru Mungu mazuri.”
“Kuna kitu umepungukiwa?”
“Kinaweza kuwepo, lakini kwa sasa nina imani hakuna.”
“Vipi kuhusu ombi langu?”
“Lipi?” nilimuuliza huku nikijigeuza na kumtazama.
“Kuhusu mtoto.”
“Hakuna tatizo.”
“Upo tayari kuzaa na mimi?”
“Ndiyo.”
“Asante sana mpenzi wangu.”
“Ni wajibu wangu kukufurahisha mpenzi wangu kwa vile nawe amenifurahisha. Mungu akijalia nitakuzalia watoto hata kumi.”
“Usiniambie!”
“Tatizo lipo wapi baba anauwezo malezi si tatizo.”
“Mi nataka wawili kwanza.”
“Basi baba jitahidi kuwatafuta hao watoto.”
“Kwa furaha hata kabla ya kuwapata nitakupa leo hundi ya milioni kumi kama asante ya kuonesha una mapenzi ya dhati na mimi.”
Siku ile alinipa hundi la milioni kumi, nami mara moja nikaanza kuitega mimba kwa kutumia kalenda ya kupata mtoto.
Sikuwa mvivu siku zote za hatari nilijitahidi kukutana na mapenzi wangu.
Siku zilikatika bila kuonekana dalili za kushika ujauzito kitu kilichonishtua sana.
Mwezi wa tatu ulipokatika nilijikuta nikipata wazo labda mzee Sambi ndiye mwenye tatizo na kumsingizia mkewe ndiye hazai.
Siku moja tukiwa tumejilaza kitandani, nilimdodosa mzee Sambi juu ya mkewe kushindwa kumzalia mtoto.
“Samahani mpenzi.”
“Bila samahani.”
“Eti tatizo la mke mwenzangu lilikuwa nini?”
“Tatizo gani?”
“La kusindwa kubeba mimba?”
“Ni historia ndefu haina muhimu kwa sasa.”
“Hapana, nina sababu zangu.”
“Sababu ipi?”
“Naomba kwanza uniambie.”
“Sababu kubwa mke wangu hana mfuko wa uzazi.”
“He! Tatizo nini?” nilishtuka kusikia vile.
“Alipata matatizo kwenye mfuko wa uzazi uliopelekea kuondolewa.”
“Wakati huo mmo ndani ya ndoa?”
“Hapana.”
“Ina maana tatizo alilipata kabla ya ndoa?”
“Ndiyo.”
“Sasa kipi kilichokufanya umuoe ukijua kabisa hazai na kukufanya sasa hivi uhangaike nje ya ndoa kutafuta mwanamke akuzalie mtoto?”
“Ni historia ya muda mrefu, mke wangu kabla ya tatizo hilo alikuwa mpenzi wangu wakati huo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha sita. Wakati anajiandaa na mtihani alijigundua ana ujauzito.”
“Sasa wewe unajua mwanafunzi kwa nini hamkutumia kinga au kalenda ya mzunguko wa hedhi?”
“Wee acha huwezi kuamini mke wangu nimeanza naye mapenzi toka yupo kidato cha tatu. Muda wote tulikuwa makini, hata sikumbuki tulikosea wapi.”
“Ehe!”
“Kwa vile alikuwa amebakiza miezi mitano afanye mtihani na ujauzito ulikuwa wa miezi mitatu ilibidi tufanye mpango wa kutoa.”
“Mmh! Ikawaje?”
“Kumbe aliyemtoa hakumsafisha vizuri, baada ya muda alianza kusumbuliwa na tumbo.
Hata mtihani wa kidato cha sita aliufanya kwa shida. Hatukujua tatizo mapema kutokana na yeye kusafiri kwenda kwa bibi yake kwa miezi mitatu.
“Huko alipokwenda hali ilizidi kuwa mbaya na kulazwa hospitali moja. Alinieleza alisafishwa tena na kupata nafuu. Lakini ugonjwa wa tumbo ndiyo ukawa tatizo lake.
“Aliporudi Dar nilimchukua na kumpeleka kwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake. Vipimo nilionesha mfuko wa uzazi umeharibika na hakukuwa na njia yoyote ya kunusuru hali yake zaidi ya kutolewa mfuko ule.
“Mke wangu alilia sana huku akinilaumu nimemuharibia maisha yake. Sikuwa na jinsi zaidi ya kumuahidi kumuoa na kuishi naye mpaka Mungu atakapomchukua mmoja wetu.
“Basi nilibidi ‘nijicommit’ nijifunge kwa maandishi.
“Baada ya miaka saba alitaka tuasili mtoto, lakini nilimshauri kwa nini nisitafute mtoto wa nje ya ndoa. Mwanzo alikataa katakata kwa kuamini mwanamke nitakayezaa naye atamdharau kwa vile hawezi kuzaa.
“Nimbembeleza na kumweleza siri ile itabakia kati yake na mimi na nusu ya mali yangu nitampa yeye ila niwe na mtoto wa damu yangu kutoka kwa mwanamke wa nje atakaye nizalia kwa mkataba.
“Ilibidi tukubaliane atakayeingia ndani ya nyumba yetu ni mtoto na si kitu kingine. Hapo ilibidi nianze kusaka mtu wa kuzaa naye.
Kwa kweli kila niliyemgusia kuzaa naye alitaka ndoa.
“Kwangu ilikuwa ngumu kutokana na masharti ya mke wangu. Ndipo nilipokutana na dada yako ambaye nilimuahidi kama atakubali kunizalia mtoto ningempa zawadi mkubwa.
Tatizo lingine ambalo lilimtibua dada yako na ndiyo chanzo ya kunifukuza lilikuwa kumwambia kama atakuwa tayari tukapime. Hicho ndicho kilichosababisha mi na dada yako tukosane.
“Lakini nashukuru sasa hivi nimeangukia kwenye mikono salama.”
“Kama mlikubaliana na mkeo kupata mtoto, kwa nini unatumia fedha nyingi kunijengea nyumba na kuninunulia gari wakati ningekuzalia mtoto tu na kuachana?”
“Pamoja na yote niliyokueleza, mke wangu mkorofi sana kiasi cha kunifanya nyumba niichukie jambo dogo anaomba talaka.”
“Labda unamnyanyasa kutokana na hali yake.”
“Haijatokea hata siku moja, basi siku hizi kabadilika amekuwa mtu wa kukasirika bila sababu.”
“Sasa akijua umenifanyia vitu hivi tofauti na makubaliano yenu unafikiri itakuwaje, si ndiyo kuuana!” nilijikuta nikiingia woga.
“Hawezi kufahamu hata siku moja.”
“Sababu ya kuuliza hivyo inatokana na mimi kukutega siku zangu za hatari bila mafanikio.”
“Kwa hiyo ulitaka tufanyeje?”
“Tukacheki afya zetu tujue sababu ya kuchelewa kupata mimba ni nini.”
“Hakuna tatizo.”
Tulikubaliana siku ya pili kwenda hospitali kuangalia tatizo la kuchelewa kupata mimba linatokana na nini au kati yetu kuna mwenye tatizo linalosababisha nisishike ujauzito.
***