Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Simulizi: Namchukia Mama Yangu

Sehemu ya 11

“Fanyeni hata penzi la siri nina imani litakusaidia katika maisha yako.”
“Mmh! Nitajaribu kwa vile umeivunja ngome ya moyo wangu sina budi kukubaliana na wewe,” nilijikuta nikilegeza msimamo.

“Tena nakuomba mdogo wangu usiipoteze bahati hii. Hebu angalia jinsi Mungu alivyosikia kilio chako baada ya kukimbiwa na Beka.

“Tena amekwambia humpi mwili wako mpaka akamilishe alichokuahidi, Mungu akupe nini? Waache dada zako watakuja kuuanika wakati jua limekuchwa na kuutwanga mbichi.”

“Nilikuwa nawazo la kumshirikisha mama suala hili,” nilimweleza wazo langu la awali.

“Mwaija utaharibu kila kitu, kama una wasiwasi wa kugombana na ndugu zako mbebee mimba ule maisha. Tena mtoto anazaliwa akiwa na uhakika wa maisha yake tayari.

“Mwaija mizee kama hii ndiyo inatafutwa mjini, hela zao hazina chenji. Mdogo wangu kwangu mimi hata angekuwa mpenzi wa mama yangu mzazi, kama angenitangazia bingo kama hiyo nisingelaza damu.”
“Naweza kumkubalia lakini sijui kama yupo sawa?”

“Kivipi?”
“Kiafya, si unajua dada yangu mwingi wa habari, tusije chuma janga tulile wenyewe.”
“Mmh! Kweli hilo umenena mdogo wangu.”
“Kwa hilo utanisaidiaje?”
“Usimpe mwili wako labda mtumie kondomu.”

“Tukitumia kondomu mtoto tutampaje?”
“Sikiliza mdogo wangu hilo kwa sasa achana nalo, akiisha kutimizia kila kitu kwa jina lako. Sharti lako kubwa ili umpe mwili wako mwende kwanza mkapime.”
“Mmh! Dada nimekueleza itabidi nifanye hivyo.”

“Na majibu yake usiyacheleweshe ili asibadili uamuzi, si unajua wanawake tupo wengi wote tunataka hichohicho.”
“Nashukuru dada yangu kwa ushauri wako.”

Baada ya mazungumzo nilimpigia simu bwana wa dada kuwa nimemaliza kilichonichelewesha naye alinieleza atafika muda si mrefu.

Baada ya robo saa alifika kunichukua, kwa vile da Suzy alikuwa akikaa njiani kwenda kwetu, tuliondoka naye na kumteremshia njiani.
Baada ya kumteremsha da Suzy, tulibakia wawili kwenye gari, tulikwenda mwendo mfupi bwana wa dada alinisemesha akiwa ameangalia mbele.

“Mwaija za kazi?”
“Nzuri shemeji, shikamoo.”
“Marahaba, sasa wewe wasiwasi wako nini?” aliniuliza swali bila kunitazama.
“Wasiwasi! Wa nini?”
“Naona umeishaanza kuniogopa, nimekueleza lile ni ombi wala haliingiliani na mambo mengine.”

“Nikuogope kivipi?” sikumuelewa.
“Najua huniamini na kuona natumia turufu ya kukusaidia ili niweze kufanikisha mambo yangu. Lakini sivyo hivyo sina nia mbaya na wewe. Ningeweza kumpa mtu yoyote fedha niliyonayo lakini naamini kwako haitapotea.”

“Uliyosema nimekuelewa lakini sikuwa na maana hiyo. Nilikuwa na mazungumzo kidogo na da Suzy, nikaona nitakuchelewesha.”
“Niliyeamua kukuleta kazini na kukurudisha ni mimi wala sikulazimishwa na mtu.”

“Sawa, lakini kunipitia si adhabu, kama kuna dharura lazima tuambiane.”
“Nimekuelewa, ila nilipata wasiwasi, jana kuzungumza leo upatwe na dharura.”
“Walaa, wasiwasi wako siku zote wanadamu si wapangaji bali kila kitu hupanga wenyewe.”

“Ni kweli, vipi mzigo uliuona?”
“Ooh! Samahani kwa kuchelewa kushukuru, asante sana shemeji yangu,” nilijikuta nikiona aibu ya kuchelewa kutanguliza shukurani mapema.

“Usihofu ni kawaida, nia yangu siku moja uishi maisha kulingana na heshima yako.”
Nilijikuta nikipata kugugumizi cha kumpa jibu kuwa nimekubali, nilitaka mwenyewe kwanza aniulize kuliko kukurupuka.

Kwa vile tulikuwa tumekaribia maeneo ya nyumbani, nilishangaa siku ile kusimamisha gari mbali kidogo na nyumbani na kunigeukia kisha aliniita jina langu.

“Mwaija?”
“Abee.”
“Vipi, nina imani umepata muda wa kufikiria.”
“Nini?” nilijifanya sijui.
“Au basi,” shemeji naye alipindisha swali lake.
“Shemeji,” nilimwita huku nikimtazama usoni.

“Naam.”
”Wewe na dada mpoje?” nilimtupia swali.
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Jibu swali si sikuuliza swali.”
“Mwaija mbona hilo tulishalizungumza toka jana?”
“Sina maana ya unayofikiria ila jibu nililokuuliza.”

“Tulikuwa wapenzi.”
” Mlikuwa wapenzi, sasa hivi?”
“Si wapenzi tena.”
“Hilo halinihusu.”
“Ulikuwa unasemaje?”
“Nina imani tabia za dada unazijua vizuri?”

“Tabia zipi?”
“Za kutokuwa na mwanaume mmoja.”
“Ndiyo.”
“Nina imani katika starehe zenu kuna kipindi hamkutumia kinga.”
“Sina kumbukumbu hiyo, lakini sijawahi kukutana naye bila kinga.”
“Basi kupata uhakika tukapime.”
“Ili?”

“We si unataka kuzaa na mimi.”
“Mwaija mi nipo sawa mbona!”
“Sijakataa, ila muhimu tukapime, hata mimi najijua nipo sawa. Lakini kwa uhakika zaidi tukapime pamoja,” nilimwambia nami nipo tayari ili kumtoa hofu.

“Mmh! Sawa.”
“Mbona kama nakulazimisha?”
“Walaa nipo tayari.”
“Kwa hiyo tutakwenda lini?” nilimuuliza kumsikiliza.
“Siku yoyote utakayotaka.”
“Kesho ukinipitia wakati wa kutoka kazini.”

“Hakuna tatizo, Mwaija ila leo nitakushushia hapa sifiki kwenu.”
Ajabu siku ile mzee Sambi hakutaka kufika nyumbani kitu kilichonishtua sana.

“Vipi mbona leo hufiki nyumbani?”
“Sitakiwi.”
“Na nani?”
“Na dada yako.”
“Hutakiwi una maanisha nini?”
“Dada yako hataki nifike kwenu.”
“Kwa sababu gani?”

“Anasema yeye si mke wangu hivyo anahitaji uhuru.”
“Mmh! Sasa itakuwaje?”
“Kila kitu nimekihamishia kwako." "Tokea lini umekatazwa na dada kufika nyumbani?" "Leo inatimia wiki?" "Wiki! Muongo!”

“Kweli kabisa.”
“Mbona kila siku ulikuwa ukifika nyumbani?" "Sababu nilikuwa nakurudisha nyumbani pia nilizungumza na mama na dada yako mdogo." "Kwa hiyo itakuwaje?" "Basi tena, kama utakuwa tayari kuwa na mimi sitafika tena kwenu, tutajua tukutane wapi?”
“Tukutane wapi ili iweje?” nilishindwa kumuelewa tukutane ili iwe nini.

“Si kama unavyofikiri, nia kubwa kukutana baada ya kazi na kuzungumza kisha unarudi nyumbani kwenu.”
“Makubaliano yetu mpaka unipatie tulivyokubaliana na pia kwenda kupima, sasa habari hiyo inakuwaje?” pamoja na kuonesha dalili za kukubali lakini sikutaka kujirahisi.

“Kupima tunakwenda kesho, kwa vile nimekuahidi lazima nitafute kiwanja nikununulie na kuanzisha ujenzi.”
“Mmh! Hiyo si itakuwa kazi ya mwaka mzima?”

“Hapana ni ya miezi miwili, nilichokuwa nasubiri jibu lako tu.”
“Mi nimekubali.”
“Basi kila kitu niachie mimi, ungependa wiki hii uanze kuendesha gari lako?”
“Hapana nimalizie kwanza nyumba.”
“Basi Mwaija ndani ya miezi miwili utakuwa ndani ya nyumba yako.”
“Basi nikuache uwahi nyumbani.”

Niliagana na mzee Sambi aliyenipa elfu hamsini ya kupandia Bajaj japokuwa nyumbani hapakuwa mbali. Sikutaka kukodi Bajaj nilichepua kwa mguu hadi nyumbani.
Nilipofika dada alishtuka na kuniuliza:
“Vipi shemeji yako ndiyo kasusa?”
“Kwani vipi?”

“Achana naye kapewa lifti anataka kupiga mpaka honi.”
“Una maana gani?”
“Kumpa penzi mara moja kanigeuza mkewe, ooh! Nataka kukuoa ooh, nataka kuzaa na wewe nani kamwambia mi kiwanda cha kutotolea watoto.”
“Lakini dada yule jamaa ana fedha zake kwa nini usimkubalie.”

“Mwaija nawe msichana kama mimi hujapungukiwa kitu. We si mtu wa kuolewa mkubalie.”
“Dada nikimkubalia si utakasirika.”
“Mwaija nikasirike ili iweje?”
“Si tutakuwa tumechangia mwanaume mmoja.”

“Angekuwa mume wangu hapo kidogo afadhali, lakini mpita njia, wee kama katuma maombi mkubalie maisha yenyewe yapo wapi,” dada alisema kama alikuwa akijua nini kinaendelea.
“Mmh! Basi acha nikapumzike.”
“Haya mdogo wangu, kama katia timu kazi kwako hela zinamuwasha.”

“Dada baadaye basi.”
“Haya mdogo wangu.”
Niliagana na dada na kwenda chumbani kwangu kubadili nguo ili niende nikaoge. Baada ya kuoga na kula nilijilaza chali kama kawaida yangu mikono niliweka kichwani. Nilijikuta nikipata wazo la kumweleza dada kuwa mzee Sambi ananitaka kimapenzi.

Niliamini kutokana na maneno yake hawezi kushtuka lakini kwa upande wangu niliona ni mapema sana kumwambia jambo lile ambalo bado lilikuwa halijakamilika. Nilijiuliza nini hatima ya maisha yangu kama nitakuwa na mzee Sambi mwanaume mwenye mke.

Niliamua kufanya kwanza siri mpaka kila kitu kitakapokuwa wazi, kwa vile nilikuwa nimechoka na kazi usingizi haukuchelewa kunichukua.
***
 
Kwa hapo anakosea. Mtu ameshatembea na sister wako. Na wewe uangukie hapo hapo hapana. Halafu jamaa mwenyewe ana mke. Angejipa muda yeye mwenyewe aka focus na kazi yake
 
Sehemu ya 12

Niliamua kufanya kwanza siri mpaka kila kitu kitakapokuwa wazi, kwa vile nilikuwa nimechoka na kazi usingizi haukuchelewa kunichukua.
***
Siku ya pili baada ya muda wa kazi mzee Sambi alinipitia, kutokana na makubaliano yetu ya kwenda kuangalia afya zetu, alipofika tu nilimueleza tuliyokubaliana jana yake.

Naye hakuwa na pingamizi alikubali twende tukapime.
Tulikwenda kwenye hospitali moja iliyopo Keko Maduka mawili. Kama kawaida tulifika na kupokelewa na dada mmoja aliyekuwa mapokezi .

Baada kuandika kadi alituelekeza kwa daktari chumba kilichokuwa mbele kidogo.

Tulielekea moja kwa moja kwa vile muda ule hakukuwa na wagonjwa wengi, wengi walionekana wamekuja kupata huduma ya sindano za masaa.
Baada ya kuingia ndani chumba cha daktari tulipokelewa na kaka mmoja mtanashati..

“Karibuni.”
“Asante,” tulijibu kwa pamoja.
“Ndiyo niwasaidie nini?”
“Tulikuwa tunataka kuangalia afya zetu.”

“Kuangalia kivipi?”
“Kupima Virusi vya Ukimwi.”
“Mmh!” daktari aliguna kidogo na kututazama wote kwa zamu kisha aliuliza.

“Mpo vipi?”
“Ni marafiki.”
“Wa kimapenzi?”
“Ndiyo,” alijibu mzee Sambi.
“Mna muda gani katika uhusiano wenu?”
“Mwezi sasa,” alijibu mzee Sambi.

“Sasa katika huo mwezi mlipokutana mlitumia kinga?”
“Hatujawahi kukutana, tumekuja hapa kupima ili tujue afya zetu kabla ya kuanza uhusiano rasmi.”
“Kwa mfano mmoja amekutwa na tatizo mtafanyaje?”

“Kwa upande wangu hakuna kitakachopungua kwa vile nina mapenzi ya dhati na mpenzi wangu,” alijibu mzee Sambi huku akiushika mkono wangu na kuupapasa.

“Na dada yangu kama utamkuta mzee ana matatizo?”
“Kwa upande wangu naamini mapenzi ndiyo yataishia hapa.”

“Kwa nini?”
“Kumbuka mi bado msichana mdogo nahitaji kuwa na familia halafu leo mwenzangu awe hivyo unafikiri raha ya ndoa ipo wapi?”
“Lakini kuna njia ya kuweza kupata mtoto bila tatizo.”
“Hiyo njia ndiyo siitaki kabisa kwa vile haipo salama asilimia mia.”

“Mzee umemsikia mama?” daktari alimuuliza mzee Sambi huku akimtazama.
“Kwangu hakuna tatizo, ikiwa hivyo namruhusu aamue chochote anachotaka lakini kama tatizo litakuwa kwake bado nitaendelea kumpenda na kumpa huduma zote muhimu kama nilivyomuahidi.”
“Sawa, basi nitawapa kalatasi mtangia chumba cha kwanza mkono wa kushoto mkapime damu.”

“Hakuna tatizo.”
Daktari aliinama na kuandika karatasi ya vipimo na kutupa, tulizipokea na kufuata maelekezo. Tulitoka na kuingia chumba cha pili, kwa upande wangu sikuwa na wasiwasi kwa vile sikuwa na tabia za kurukaruka pia hata mtalaka wangu naye hakuwa na tabia mbaya japokuwa sikutembea naye muda wote tulipokuwa pamoja.

Mzee Sambi naye hakuonesha wasiwasi wowote, baada ya kuingia chumba cha maabara tulikaribishwa kwenye kiti. Tulikaa na kumpa vyeti vyetu baada ya kusoma alichukua vifaa na kutuchukua damu mtu mmoja mmoja. Baada ya kumaliza zoezi lile alituomba tukakae sehemu ya mapumziko kusubiri majibu yetu.

Tulitoka hadi kwenye makochi na kukaa kusubiri majibu, muda wote tulikuwa kimya hakuna aliyeanzisha mazungumzo. Baada ya robo saa tuliitwa kwa daktari nilijua majibu yameishatoka.
Tuliingia kwa daktari na kukaa kimya kusubiri majibu yetu.

Baada ya kukaa kwenye viti ndani cha chumba palikuwa kimya, daktari alikuwa akipitia karatasi ya majibu yetu. Muda ule niliutumia kumsoma anachokisoma kina nini kwa kuangalia usoni kwake kwa kuamini atakacho kisoma kitaonekana kwenye uso wake.

Nilimuona akisoma akiwa ametuliza macho, muda wote aliosoma karatasi ya kwanza alikuwa ametuliza macho. Aliiweka pembeni ya kuchukua nyingine ambayo ndiyo iliyokuwa na jina langu. Aliisoma taratibu kama ya kwanza lakini kuna kipindi niliona kama amekodoa macho. Baadaye aliyarudisha katika hali ya kawaida.

Aliichukua karatasi ya kwanza na kuisoma upya na kuirudia yangu harakaharaka kisha alitutazama. Macho yake yalionesha kuna kitu amekiona kwenye karatasi sikujua karatasi yangu au ya mzee Sambi.
Alikohoa kidogo na kutuita majina yetu kupitia kwenye vyeti vyetu.

“Mwaija.”
“Abee.”
“Mzee Sambi.”
“Naam.”
“Majibu yenu yametoka, sasa sijui niyatoe kwa kila mmoja au kwa wote pamoja?”
“Kwa wote, sababu ya kuja pamoja kila mtu anataka kujua afya ya mwenzake.”
“Vizuri, je, mpo tayari kupokea majibu yenu?”

“Daktari acha mbwembwe we tupe jibu tujue tunasuka au tunanyoa,” mzee Sambi ilibidi amweleza daktari aliyeoneka jambo dogo anataka kulikuza kitu ambacho humuongezea mtu hofu moyoni.

“Sawa nimekuelewa mzee, majibu yenu yapo kama ifuatavyo wote wawili kwa vipimo vya awali vinaonesha mpo sawa.”
“Una maanisha?” nilimsikia lakini sikumuelewa.

“Damu yenu wote inaonesha ipo safi.”
“Ooh! Alhamdulilah,” japokuwa nilikuwa na uhakika na afya yangu lakini nilimshukuru Mungu kwa vile sikuwa na uhakika wa uaminifu kwa mtalaka mwenzangu kwa asilimia mia.

Lakini upande wa mzee Sambi yeye alikuwa yupo katika hali ya kawaida zaidi ya kutabasamu na kuninyanyua na kunikumbatia kwa furaha.

“Hongera mpenzi wangu.”
“Asante.”
“Jamani kama nilivyosema vipimo vya awali ndivyo vinavyoonesha mpo salama.”
“Ina maana kuna majibu mengine?”nilijikuta nikiuliza kwa sauti huku nikijitoa kifuani kwa mzee Sambi.
“Hapana ila mnatakiwa msikutane bila kinga mpaka mchukue vipimo vya pili ambavyo ni baada ya miezi mitatu.”
“Kwani mimi sihitaji kurudia kwani nina zaidi ya miaka miwili, simjui mwanaume.”
”Mmh! Hongera.”

“Hata mimi nilikuwa najijua nipo salama, lakini kwa vile nilitaka kumtoa hofu mpenzi wangu. Lakini ili kuzidi kumtoa hofu nitafikisha miezi mitatu nitapima tena ndipo tuanze uhusiano rasmi,” Mzee Sambi alinitoa hofu.

“Basi mi niwapeni hongera kwa kutunza afya zenu, majibu yasiwape kiburi bali yaongeze uaminifu katika uhusiano wenu,” daktari alituasa.

“Asante daktari.”
Baada ya kuchukua majibu na kupata nasaha za daktari tuliondoka kurudi nyumbani. Njiani moyo wangu ulijikuta ukijaa furaha na kuanza kumuamini mzee Sambi ambaye tokea mwanzo alionesha nia njema kwangu.
 
Sasa dada Mwaija kashapima tuone kitakachofuata, na mama akijua sijui ataanza figisu tena?
 
Sehemu ya 13

Baada ya kuchukua majibu na kupata nasaha za daktari tuliondoka kurudi nyumbani. Njiani moyo wangu ulijikuta ukijaa furaha na kuanza kumuamini mzee Sambi ambaye tokea mwanzo alionesha nia njema kwangu.
****
Mzee Sambi aliendelea kunipeleka na kunirudisha nyumbani kwa mtindo wa kunicha njiani na kunipa fedha ya nauli ya teksi. Wiki mbili baadaye alinijulisha kiwanja kimepatikana na mwisho wa wiki alinipeleka kwenda kukiona.

Kiwanja kilikuwa kizuri sana kilichokuwa maeneo ya Boko hakikuwa mbali na Barabara ya Bagamoyo. Kilikuwa kikubwa cha kutosha kujenga nyumba kubwa na kubakia eneo la kupumzikia.

Kwa kweli siku ile kwa mara ya kwanza nilifurahi sana na kumkumbatia mzee Sambi kwa furaha ya kweli toka moyoni.
“Asante mpenzi wangu.”

“Huu ni mwanzo tu, nataka uamini sipo na wewe kukupotezea muda wako bali kuhakikisha nayabadili maisha yako.”
“Asante mpenzi naanza kuamini.”
“Utaamini siku moja, najuta kuchelewa kufahamu mapema.”

“Hayo achana nayo tugange yaliyopo.”
“Basi mpenzi tukirudi kwenye gari nitakuonesha ramani ya nyumba yako inatakiwa kuwa vipi?”

“Ramani yake ipo wapi?” nilijikuta nimepata kimuhemuhe mtoto wa kike.
“Ipo kwenye gari.”
“Twende nikaione,” mtoto wa kike shauku ikanipanda.

“Ataiona tu wala usiwe na wasi.”
“Lakini mpenzi huku mbali sana na mji?”
“Si utakuwa na usafiri wako ili kukurahisishia kwenda popote bila tatizo.”

“Mmh! Hapo sawa.”
Baada ya kuzunguka eneo la uwanja wangu tulirudi kwenye gari. Kabla ya kuondoka alinionesha ramani ya nyumba yangu pia picha ya nyumba iliyokuwa imeishajengwa tayari ambayo ilionekana nzuri pembeni kuna gari la kifahari na bustani ya nguvu.
“Basi nyumba yako ikiisha itakuwa kama hivi.”

“Muongo!” nilishtuka kuiona nyumba nzuri sana kuwa yangu.
“Ikiwa tofauti na hii picha ikatae.”
“Na hili gari la kifahari lililopo pembeni ya nyumba nitakuwa nalo?”
“Lazima kila kitu kiwe kama kwenye picha.”

“Wawooo! Jamani asante mpenzi wangu.”
“Hizi ni rasharasha mambo mazuri yanakuja.”

Tulitoka kwenye kiwanja changu na kunirudisha nyumbani kama kawaida aliniteremshia mbali na nyumbani.

Nilipofika nyumbani nilijikuta kila dakika nikitabasamu baada ya kukumbuka picha ya jumba la kifahari nililooneshwa na mpenzi wangu na kunihakikishia nyumba yangu ndivyo utakavyokuwa vile.
Nilijikuta nikiyaona maisha yangu yakibadilika na kunifanya niwe mtu mbele ya watu.

Nilikumbuka baadhi ya wanawake wengi waliokuwa wakija kazini na kuwatetemekea kwa vile walikuwa na magari au wake wa watu wenye fedha nami nilijua tayari nimewafikia.

Moyo uliniuma baada ya kujua sina haki ya asilimia mia hata nikiwa naye. Nilijiuliza kwa upendo alionionesha angekuwa wangu peke yangu sijui ingekuwaje.
Naamini ningekuwa juu zaidi ya mawingu.
Siku iliyofuata ilikuwa Jumatatu nilikwenda kazini kama kawaida. Da Suzy aliniuliza mchakato wangu na mzee Sambi. Nilimweleza yote sikumficha hata moja.

“Unaona mdogo wangu ulitaka kuupiga teke mfuko wa fedha.”
“Lakini kumbuka si wangu wa kufa na kuzikana, lakini ndiyo hivyo cha kuazima hakisitiri matako.”

“Mdogo wangu usifikirie visivyo kuhusu, ridhika na unachokipata. Amekuahidi mambo mengi na moja ameanza kulitekeleza. Ningekuwa ndiyo mimi mbona ningemzalia huyu mtoto kwa vile mmepima na kuzijua afya zenu.”

“Mmh! Sawa, huwezi kuamini nimeanza kumpenda hata bila kujijua.”
“Chezea faranga wewe,” da Suzy alitania.

“Walaa, si kwa ajili hiyo bali ameonesha upendo wa dhati kwangu, ni mtu mwenye huruma mkweli pia mwenye dhamira njema kwangu.”

“Basi mdogo wangu usiipoteze nafasi hiyo.”
“Dada sasa hivi mimi na mzee Sambi kama chanda na pete.”

“Hongera mdogo wangu, la muhimu mzalie mtoto ndicho kilio chake.”
“Atampata tu muda si mrefu tukianza kujirusha.”

“Ina maana hujampa?” da Suzy alishtuka kusikia siku zote hizo sikuwa nimempa mwili wangu mzee Sambi.

“Dada sikutaka kuwa naye kibiashara bali kujua hatma ya maisha yangu.”
“Kweli mdogo wangu una msimamo.”

Tuliendelea na kazi, jioni kama kawaida mpenzi wangu alinipitia kunirudisha nyumbani. Gari lilipofika makutano ya Barabara ya Chang’ombe na Nyerere nilishangaa kuona likinyooka kufuata Barabara ya Nyerere badala ya kukata kushoto.

Sikutaka kumuuliza kwa kujua labda ameamua kupitia Barabara ya Mandela na kuingilia barabara ya kuelekea maghorofa ya Tazara. Lakini tulipofika njia panda ya Nyerere na Mandela alikata kulia badala ya kushoto kitu kilichonishtua.

Vilevile sikuhoji nilitaka nione mwisho wake utakuwa vipi. Gari lilielekea Buguruni, lakini tuliongoza hadi Tabata Dampo. Tulipinda kulia kufuata barabara ya kuelekea Tabata.

Tulipofika Bima alikata kulia kuelekea Tabata Kimanga nami nilikuwa kimya nimetulia nione ananipeleka wapi.

Tulipofika Savana alikata kulia na kusimamisha gari nje ya nyumba moja yenye geti na kuteremka kufungua geti.
Aliporudi kwenye gari nilimuuliza.
“Mpenzi wewe si una mke?”
“Ndiyo.”

“Sasa unanipeleka wapi?”
“Ondoa wasiwasi mpenzi.”
“Kama kwako naomba unishushe.”
“Hapana mpenzi, kwani nilikuambia nakaa wapi?”

“Sasa huku wapi tunakwenda wapi?”
“Bebi mbona wasiwasi, siku zote nayajali sana maisha yako kuliko kawaida.”

“Najua lakini naomba uniambie huku unanipeleka wapi?”
“Unaniamini?”
“Nakuamini.”
“Basi niachie mimi kila kitu.”

“Haya baba.”
Mzee Sambi aliliingiza gari ndani ya geti na kulisimamisha mbele ya nyumba nzuri.
“Tumefika,” alisema huku akinitazama usoni.
Sikumjibu nilitulia nikimuangalia, baada ya kuzima gari alinieleza:

“Tushuke.”
Bila kuhoji kitu niliteremka na kufunga mlango wa gari na kusimama nje ya gari kusubiri kujua pale nimeletwa wapi. Wazo langu la kwanza labda nyumba ya wageni.

Lakini katika makubaliano yetu ilikuwa mpaka akamilishe kila kitu ndipo na mimi nimpe mwili wangu. Lakini moyoni nilijikuta nikiwa tayari kumsikiliza atakachokitaka na kuusihi moyo wangu kutokuwa na swali kwa lolote litakalo kuja mbele yangu.

Mzee Sambi baada ya kufunga mlango wa gari alikwenda hadi kwenye mlango wa nyumba ile na nilishangaa kuona akitoa ufunguo mfukoni na kufungua mlangoni. Baada ya kuzungusha funguo alinyonga kitasa na kuusukuma mlango kwa ndani.
Baada ya mlango kufunguka aliingia ndani na kutoka kisha aliniita.
“Bebi njoo.”

Nilimfuata bila kusema kitu nikijua siku ile sikuwa na ujanja wa kukataa kufanya chochote na mzee Sambi, kutokana na kila alichokuwa akifanya mbele yangu kilianza kuivunja ngome ya moyo wangu.

Nilipofika mlangoni alinishika mkono na kuniingiza ndani ya nyumba ile, ambayo sebule yake ilikuwa imekamilika na kuwa na kila kitu kwa mtu mwenye maisha ya juu.
“Karibu mpenzi.”
“Asante,” nilijibu huku nikipepesa macho.
“Unapaonaje hapa?”

”Mmh! Pazuri.”
Alinishika mkono na kunipeleka mpaka chumbani nikajua shughuli imefika kwa vile sikuwa na uwezo wa kupinga, kwa vile mpaka kukubali kuingia mule ndani nilikubali kwa hiyari yangu sikulazimishwa na mtu.

“Karibu bebi.”
“A..a..sante.”
“Mbona una wasiwasi?”
“Walaa,” nilikataa tu lakini mazingira yale yalinifanya nipoteze kujiamini.

“Unakionaje chumba?”
“Kizuri,” nilijibu kwa mkato.
“Bebi naomba nikuambie kitu.”
Nilijua hana cha kuniambia zaidi ya kuniomba kufanya mapenzi kutokana na kunionesha vitu vya kunijali. Lakini bado nilikuwa na maswali kujiuliza pale ni kwa nani?

“Niambie tu bebi.”
“Naomba nikuambie toka moyoni mwangu, Mwaija nakupenda.”
“Hata mimi nakupenda,” nilijibu nikiwa bado sijiamini.

“Nimefurahi kusikia hivyo.”
“Hata mimi nafurahi kwa yote unayonifanyia na mengine utakayonifanyia.”
“Naomba kwanza tutoke nje.”
“Hakuna tatizo.”

Tulitoka hadi nje ya nyumba na kunizunguka kuiangalia ile nyumba iliyokuwa kwenye hali nzuri sana. Bado sikumuelewa alinitoa nje kufanya nini.
“Mwaija.”
“Abee.”
“Hii nyumba unaionaje?”
“Mmh! Nzuri.”

“Basi mpenzi kuanzia sasa utakaa hapa.”
“Na ile nyumba unayonijengea Boko?”
“Hapa nimekupangia kwa muda wakati unasubiri nyumba yako kuisha ili nami nipate muda wa kuwa na wewe baada ya kazi kwa nafasi.”
“Mmh! Asante mpenzi,” nilimshukuru kwa kumkumbatia.

“Basi vitu vyote unavyoviona ndani vimenunuliwa juzi na kupangwa jana. Baada ya kuridhika ndiyo nikakuleta ujionee nyumba yako.”

“Asante sana,” nilijikuta nikiwa na furaha ya ajabu moyoni na kuona kama Mungu kaamua kunifanyia muujiza.

“Haya ni matunda ya msimamo na tabia zako, sijawahi kuona msichana kama wewe katika kipindi hiki.”

“Mbona tupo wengi tu basi mmekuwa wavivu kuchagua vinavyong’aa barabarani mkadhani vyote ni dhahabu.”
“Nimekubali na kauli yako.”

Tulirudi ndani, kwa vile muda ulikuwa umekwenda nilimuomba aniwahishe nyumbani.
“Bebi kwa nini silale leo hapa?”
“Mmh! Peke yangu jumba lote hili?”
“Tutalala wote.”

“Hapana siku nyingine, si unajua mimi mtoto wa mama lazima nikaage nyumbani kuwa naanza kujitegemea.”
“Hakuna tatizo nakusikiliza wewe.”
“Basi kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.”

“Hakuna tatizo.”
Tulikubaliana kuondoka tulizima taa na kufunga mlango wa nyumba na geti na kunirudisha nyumbani. Tulipofika maeneo ya Mwembe Yanga alinikodia teksi hadi nyumbani.

Nilijifika nyumbani na kuwa na mawazo mengi juu ya mzee Sambi. Baada ya kuoga na kupata chakula cha usiku nilimfuta mama chumbani kwake na kumweleza siri yangu.
 
Sehemu ya 14

Nilijifika nyumbani na kuwa na mawazo mengi juu ya mzee Sambi. Baada ya kuoga na kupata chakula cha usiku nilimfuta mama chumbani kwake na kumweleza siri yangu.

Aliposikia namgongea chumbani alitoka na kuniuliza, kwa vile sikuwa na kawaida ya kumfuata muda ule.

Toka nilipoanza kazi baada ya kazi nilikuwa chumbani kwangu na kuangalia mikanda ya filamu.
Sikutaka kukaa nje kwa kuhofia kujiingiza kwenye vishawishi vibaya. Mama aliponiona aliniuliza:

“Vipi mama?”
“Nilikuwa na mazungumzo na wewe kidogo.”
“Sawa, nisubiri sebuleni nakuja.”
“Hapana mama nataka tuzungumzie chumbani kwako.”

“Mmh! Makubwa mazungumzo ya chumbani kwangu?”
“Ndiyo mama.”
“Haya karibu.”
Niliingia chumbani kwa mama na kukaa kitandani kwake karibu yake. Mama alimaliza kuweka vitu vyake vizuri kisha aliunigeukia.

“Haya mama niambie.”
“Mama kuna kitu ninacho muda mrefu, ilikuwa vigumu kukueleza mwanzo kwa vile sikuwa na uhakika nacho.”

“Kitu gani hicho?”
“Mama nimepata rafiki wa kiume ambaye amejitolea kila kitu katika maisha yangu.”

“Nilijua, nilisubiri kuambiwa ningekuuliza ningeonekana muongo.”
“Inawezekana lakini mwanzo ilikuwa ngumu kulisema.”

“Haya mwanangu ulikuwa unasemaje?”
“Mama mtu mwenyewe unamfahamu.”
“Mwanangu nimfahamu vipi bila kunifahamisha.”
“Mzee Sambi.”
“Mzee Sambi aliyekuwa mpenzi wa dada yako?”

“Ndiyo.”
“Mmh! Makubwa, kwa nini umekubali kushea mapenzi na dada yako?” nilimshangaa mama kuniambia swali kama lile.

“Hata mimi mwanzo sikutaka kukubali, lakini mzee yule alinieleza mambo mengi kuhusiana na dada kumfukuza na alivyotaka kumfanyia ambavyo vyote dada alivipiga teke.”

“Vitu gani?”
“Alitaka awe nyumba yake ndogo na kumuahidi kumjengea nyumba na kumnunulia gari.”

“Muongo wanaume wa mjini utawaweza, wanataka wakutumie wakitimiza haja zao wanaondoka bila kwa heri. Dada yako aliniambia nikamkatalia.”

“Mama makubaliano yetu ni kuwa naye baada ya kunikamilishia kila alichoniahidi.”

“Atawahi muongo mkubwa, atakuletea nyaraka za uongo ili uamini lakini mwisho wa siku kila kitu atakichukua.”

“Kwangu tofauti, hivi ninavyo kwambia ameisha ninunulia kiwanja na ujenzi utaanza mara moja.”

“Muongo?” mama alishtuka.
“Tena mama nyumba ikiisha litakuwa bonge la jumba pia amesema ataninunulia gari la kifahari.”

“Mmh! Hongera.”
“Asante na sasa hivi amenipangia nyumba nzima hivi ndiyo nimetoka kuiona yenye kila kitu ndani.”
“Dada yako akijua itakuwaje si unaujua ukorofi wake.”
“Yeye ndiye aliyeniambia kama namtaka nimchukue.”

“Basi mimi sina tatizo, kwa hiyo nyumba aliyokupangia itakuwaje?”
“Nitahamia wakati wowote.”
“Kwa hiyo utakuwa unakaa naye?”
“Hapana, hatujakubaliana hilo bali ametaka niwe huru na kuweza kuonana naye na kupanga mambo yetu kwa uhuru mkubwa.”

“Sawa, umeona ulijifanya mlokole yote haya ungeyapatia wapi?”
“Mama nilitaka kusahau, amesema eti nikimzalia mtoto wa kike atanipa milioni kumi na kiume ishirini.”

“Masuala ya nyumba na gari yanakufa?”
“Walaa hiyo ni bonasi ya furaha ya kupata mtoto.”
“Mmh! Makubwa.”
“Mama mbona unaguna.”
“Ndiyo nasikia kwako kumzalia mtu mtoto akulipe fedha.”

“Mama amesema mkewe hana kizazi hivyo anategemea kwangu.”
“Wewe ndiyo unacho?”
“Mama maneno gani hayo?” maneno ya mama yalinivunja nguvu.
“Sio maneno gani, kwani huyo mkewe alilokosa kwa Mungu nini?”
“Sasa mama yeye kukosa kizazi na mimi kunaingiaje?”

“Siyo kuingiaje bali nenda na mawili, usije ahadi ya milioni kumi na ishirini ikayeyukia hewani ukachanganyikiwa bure. Mtoto ni majaliwa ya Mungu na si kwa ahadi ya fedha ingekuwa hivyo mkewe angemzalia.”

“Sawa mama nimekuelewa, nilikuja kukufahamisha tu.”
“Hicho kiwanja chenu kipo wapi?”
“Boko.”
“Utanipeleka lini nikakione?”
“Mwisho wa wiki.”

“Basi mwanangu nakutakia kila la heri.”
“Asante mama yangu.”
Niliagana na mama na kwenda kulala japokuwa nilichelewa kulala kwa kauli ya mama labda sina kizazi kwa kweli iliniumiza sana.

Nilijikuta nikiyadharau yote kwa kuamini kila kitu chini ya jua muwezeshaji wa yote ni Mungu pekee si mwanadamu.

Niliamini hakukuwa na haja ya kuendelea kuwa nyumbani kwa vile sifa ya nyumbani kwetu sikuipenda siku zote. Ilionekana Mungu alisikia kilio changu cha kuishi kwenye nyumba yenye sifa mbaya kilipokelewa.

Pamoja na furaha ya kutoka nyumbani lakini suala ya kuanza kuishi na mzee Sambi kama mke na mume sikuliafiki kwa vile ilikuwa mapema sana.

Kukaa peke yangu jumba lile niliona haifai lazima nilitakiwa kuwa na mtu wa karibu. Nilikumbuka kuna msichana mmoja aliyekuwa akifanya kazi za ndani kwa jirani yetu niliye kuwa nimezoeana naye. Kuna siku alinifuata kabla ya kuanza kazi super market kuniomba aje pale kwetu au nimtafutie kazi kutokana na manyanyaso na ugumu wa kazi aliokuwa akikutana nao pale.

Niliamini nikiwa naye angenisaidia kazi pia kunichangamsha nikiwa nyumbani peke yangu. Nilijikuta nikipata tumaini la kuwa na mtu wa kukaa naye. Baada ya kuwaza sana usingizi ulinichukua.
***
Siku ya pili kabla ya kwenda kazini nilibahatika kumuona yule msichana ambaye alikuwa na umri wa miaka kumi na saba.

Kwa kweli alifurahi sana kumpa habari ambazo ilionekana alikuwa akizisubiri kama wokovu. Nilimweleza nitapitia jioni ya siku ile nikitoka kazini na kwenda naye kwangu. Nilikwenda kazini na kumweleza da Suzy ambaye alizidi kuusifia uamuzi wangu wa kukubali kuwa na mzee Sambi.

Jioni mzee alinipitia na kumweleza kuanzia siku ile nitahamia kwangu. Alifurahi sana kwa kitendo changu cha kukubaliana na yeye bila masharti magumu.

“Lakini mpenzi nitakuwa na msichana wa kazi.”
“Walaa usiwe na wasiwasi, nilikuwa na wazo hilo maana jumba ni kubwa unatakiwa kuwa na mtu kama mimi sipo,” mzee Sambi alinifurahisha sana hakuwa mtu wa kunipinga jambo.
“Basi sasa hivi nakwenda kumpitia na kwenda naye kwangu.”

“Hakuna tatizo.”
Tulikwenda hadi Temeke na kumpitia msichana wa kazi ambaye nilimkuta amejiandaa. Kabla ya kuondoka niliwaaga ndugu zangu ambao walishtuka.

“Vipi tena?”
“Nawakimbia kidogo.”
“Wapi?”
“Tabata.”
“Mmh! Vipi Beka karudi nini?” dada mdogo aliuliza.

“Walaa, yupo mwingine, dada anamjua.”
“Siku hizi yupo na Mzee Super.”
“Mzee Sambi?” dada mdogo alishtuka.
“Ndiyo, mdogo wetu kaamua kujimilikisha mzee mzima.”

“Ha! Wee Mwaija umekosa wanaume wote mpaka umchukue mpenzi wa dada yako, we si ulikuwa mlokole imekuwaje leo kuchangia bwana na dada yako?” dada alizidi kushangaa.
“Kila kitu dada anajua.”
“Mwache kwa raha zake, mzee yule mshamba nilimtimua. Eti ataninunulia gari, ooha atanijengea nyumba utongozaji wa kizamani .

Nilimpa penzi la muda sio kung’ang’aniana kama ruba.
Alichonichefua zaidi eti tukapime ili nimzalie eti atanipa milioni kumi, nilimwambia mimi nina shida ya mtoto? Aliambiwa mi kiwanda cha kuzalisha watoto. Mdogo wangu kamzalie mtoto upate hiyo nyumba, gari na milioni kumi.”
“Mmh! Kumbe nimekuwa bwege kati mambo yanapita juu yangu bila kujua.

Kwa hiyo umemruhusu mdogo wako atembee na bwana yako?”
“Kipi cha ajabu si afadhali Mwaija aliniuliza kuliko wewe uliyekuwa ukitembea na bwana yangu mpaka ukaniwekea fitina nikaachwa,” dada mkubwa alimjia juu dada mdogo.

Niliona mjadala wangu utavumbua yasiyonihusu. Niliona dawa ni kuwaaga.
“Jamani dada zangu mi nawahi nina imani tutaonana mwisho wa wiki.”
“Hakuja tatizo ukitulia uje utuchukue.”
“Hakuna tatizo.”

Kwa vile muda ulikuwa umekwenda niliondoka kwa kumpitia msichana wangu wa kazi na kuondoka naye hadi kwangu Tabata Savana. Nilipofika nilimweleza kuwa nitaishi naye kama ndugu yangu japokuwa nitamlipa msahahara kama kawaida. Alinishukuru kwa kumtoa kwenye mateso.
****
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom