RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 38
MTUNZI:Enea Faidy
.....Mr Aloyce bado hakumuelewa vizuri mkewe kwa kauli aliyoisema. Kauli ile iliibua utata mkubwa kichwani mwake na kumtaka mkewe amueleze ukweli.
"Niambie mke wangu... Nini kinaendelea? Maana Mimi sielewi!" Alisema Mr Aloyce kwa sauti ya upole ili mkewe amweleze ukweli wote. Lakini kwa bahati mbaya sana Maimuna alisita kueleza ukweli ambao alitaka kumwambia Mr Aloyce.
Viboko mfululizo vilivyosikika kwa sauti kubwa vilimshukia Maimuna na kumfanya ahangaike kupita kupita kiasi. Aligalagala pale chini kama nyoka aliyepondwapondwa kichwa chake. Sauti na yowe la kilio viliibuka kwa Maimuna kwani alishindwa kuvumilia maumivi ya viboko alivyochapwa na MTU asimfahamu.
"Nasemaaa!nasemaaa!" Alisema Maimuna huku akilia.
Mr Aloyce na Mlinzi wake walibaki na mshangao kwani kila walichokiona walihisi ni muujiza tu. Walibaki kimya huku wakimshangaa mwanamke yule.
"Aloyce... Mimi ni mchawiiii.." Alisikika Maimuna na kwa bahati mbaya sana alishindwa kuongea kwa sauti ndogo hivyo sauti ilipaa sana na kuwafanya wapita njia na majirani kujazana sana nje ya geti kwa Mr Aloyce. Kwa uzito wa adhabu alioipata Maimuna ilimbidi tu aseme ukweli wote uliomwacha mdomo wazi Mr Aloyce.
"Naitwa Maimuna.. Sio mama yake Eddy kama ulivyodhani..." Alisema Maimuna na kumfanya Aloyce ahamaki. Alichanganyikiwa sana na kushindwa kuzungumza.
"Nisamehe Aloyce... Nilikuja kuiteketeza familia yako.... Mkeo alishaliwa nyama ... Mimi nilikuja kumlinda Eddy ili sehemu zake za siri zibaki mikononi mwa Doreen"
"What? Ati nini? Kwanza Doreen ni nani?" Mr Aloyce alijikuta anauliza maswali matatu mfululizo huku hasira zikiwa zimempanda kupita kiasi. Alitamani achukue jiwe zito na kumponda nalo mwanamke yule.
"Ni mchawi... Alikuwa anasoma na Eddy..." Alisema Maimuna huku akilia kwa sauti kubwa.
"Oh! Shit!" Alisikika baba Eddy.
Watu waliokuwa pale nje walizidi kutafuta upenyo wa kuingia mle ndani. Lakini geti lilikuwa limefungwa, kelele nyingi kutoka nje zilizidi kusikika.
"Mchawiiiiii! Mchawiii! Tufungulie tumwadhibu huyo mchawiiii!! Funguaa! Mwanamke mchawi hafai kuishi!!" Sauti zile kutoka nje zilimhamasisha mlinzi kufungua geti na kuwaruhusu watu waingie. Cha ajabu watu wale waliingia wakiwa wameshikilia silaha za aina mbalimbali. Wengine mawe wengine visu huku wengine wakiwa wameshikilia fimbo na mapanga. Hali ilichafuka sana pale ndani.
Umati wa watu ulikuwa uvamia uwanja wa Mr Aloyce tayari kwa kumwadhibu mchawi aliyesababisha kilio na majonzi katika familia ya ile iliyokuwa imejaa upendo na amani hapo awali."Tuue tu... Afe Huyo" walisema. Ghafla Maimuna akabadilika na kuwa kiumbe tofauti na vile anavyofahamika wote wakashtuka.
*****
Doreen aliendelea kushangaa kwa hofu sana ndani ya chumba kile. Upepo mkali uliovuma chumbani mle na kuangusha baadhi ya vitu vilivyokuwa vimewekwa vizuri ulimfanya Doreen ajione mdogo kama sisimizi juu ya janga lile.
Akiwa bado haelewi la kufanya ghafla sura ya MTU aliyemfahamu ikatokea mbele yake na kumfanya Doreen apigwe na mshangao wa hali ya juu.
"Haa! Dorice!" Alisikika Doreen akiita kwa mshangao.
"Mimi hapa! Sema nikusikie!" Alisema Dorice kwa sauti iliyojaa dharau kupita kiasi. Kisha kabla hajaendelea na lolote akanyoosha kidole chake ukutani na ghafla kikatokea kama runinga pana iliyoonesha siku ambayo Doreen alimpaka kamasi usoni kiuchawi ili asipendwe na Eddy. Kisha akaonekana Doreen akimkata Eddy sehemu zake za siri.
"Ulikuwa mjanja sana sio?" Alisema Dorice. Doreen hakuamini macho yake alitetemeka kwa hofu kupita maelezo.
"Do..Dor...Dorice... Umepata wapi huo ujasiri wa kunitisha kiasi hicho?" Aliongea Doreen kwa kigugumizi sana. Dorice alimtazama Doreen na kucheka kidogo huku akitembeatembea ndani ya chumba kile.
"Ulininyang'anya penzi langu kinguvu kwa mtu nimpendae sana.. Cha ajabu ulitaka kumharibia yeye na familia yake... Kwanini wewe in katili na mbaya kitabia kuliko sura yako?" Aliuliza Dorice.
"Tafa..Tafadhali Dorice
nisamehe.."
"Nimekusamehe tangu zamani... Ila nataka kukufunza adabu. Umeua wengi sana wasiokuwa na hatia umewaharibu wengi sana bila kosa." Alisema Dorice na kutoweka machoni mwa Doreen.
Doreen alichanganyikiwa mno, lakini kilia alipotaka kupotea na kumtoroka Dorice hakuwa na nguvu, kwani Dorice alikuwa na nguvu nyingi mno ambazo zilimsaidia kufanya kila alichokitaka. Na hakuna mchawi ambaye angeweza kumshinda Dorice kwa wakati ule.
Ghafla bin vuu! Kichapo kikali kikamshukia Doreen. Alihisi mawe mazito yanamshukia kichwani mwake na kumpiga kwa nguvu. Alihisi maumivu makali mno. Akapiga ukunga mkali baada ya kushindwa kuvumilia maumivu Yale. Hakuona sababu ya yeye kuendelea kukaa ndani ya chumba kile huku akitaabika akaamua kufungua mlango na kutoka nje ya chumba huku akilia kwa sauti kali . kilio chake kiliwashtua wengi na kuwafanya watoke njee kutazama kulikoni.
Umati wa watu ulifurika kumtazama Doreen pale nje. Alikuwa uchi wa mnyama huku akipiga kelele sana.
"Naacha uchawiii... Mimi si mchawi...uwiiiii... Nisaidieni" alilalama huku akipiga mbio bila kujali kuwa hajavaa nguo yoyote.
Watu walianza kumfuata huku wakipiga kelele "mchawii! Mchawiiii" "masikini we! Binti mzuri hivi kumbe ana mambo ya uchawi?" Walisikika watu wakiongea vikundi vikundi.
Watu walikazana kupiga picha huku wengine wakiokotw mawe na kumfukuza Doreen huku wakimtupia mawe.
Doreen alikimbia sana huku akipiga kelele sana.
Ghafla mama mmoja alipiga kelele sana
"Huyu mtoto aliinibia pesa zangu mgahawani kumbe ni mchawi! Alaaniwe!"
"Mimi alikuja dukani kwangu akataka aniwangie Leo ameumbuka" walizungumza yule mama wa mgahawa ambaye alitapeliwa na Doreen kwa mazingira ya kutatanisha sana ndipo alipojibiwa na mwanaume mwingine ambaye Doreen alijaribu kumuwangia ili aibe pesa.
Doreen alizidi kupiga mbio sana huku umati ule wa watu mjini Iringa ukizidi kumfata kwa kasi wakiwa wameshika mawe na wengine viboko.
*****
Baba Pamela alikuwa ametulia kidogo huku akimtazama binti yake kwa masikitiko makubwa.
"Daddy najisikia hasira hata kumtazama mama" alisema Pamela huku akilia.
"Hutakiwi kuwa hivyo... Nataka tufanye jambo hapa!"
"Jambo gani mume wangu?" Aliuliza mama Pamela.
"Nataka tumwombe Mungu mpaka atujibu juu ya binti yetu"
"Hakuna tatizo mume wangu.." Alisema mama Pamela kwani tayari maneno ya mumewe yalimpa nguvu hata ya kuzungumza.
"Pamela una amini kama Mungu anaweza kutenda mambo ambayo sisi hatuwezi?"
"Ndio naamini... Lakini..."alisema pamela
"Lakini nini? Ukiwa na imani hutakiwi kutilia shaka.."
"Sawa baba niombee tu.."
Baba Pamela aliwataka wote wapige magoti kisha wakaanza na nyimbo na baada ya hapo akaanza kufanya maombi. Aliomba sana akiwa anataka Mungu amrudushie mwanae titi lake.
Radi Kali zikaanza kupiga katika nyumba zilipiga radi nyingi wakati baba Pamela akiendelea kusali kwa bidii na imani sana. Ghafla akawaambia watoke nje wote.
"Roho wa Mungu ananiambia kuna kitu kimefukiwa pale nje ili kutuangamiza" alisema baba Pamela kisha wote wakatoka nje. Baba Pamela aliongoza njia mpaka Pale ambapo Mama Pamela alifukia sahani iliyokuwa na kinyesi. Wakafukua.
Cha ajabu akatokea nyoka mkubwa sana ambaye hakuna aliyetarijia kama angekuwa pale.
"Mungu wangu!" Alisikika Mama Pamela akizungumza kwa woga. Baba Pamela alizidi kumwomba Mungu mpaka yule nyoka alipobadilika na kuwa na sura ya Doreen lakini mkiani akabaki kuwa nyoka. Wote walistaajabu sana huku wakitetemeka kwa woga...