SEHEMU YA THELATHINI NA SITA
...Mama Eddy alitazama juu ili kuona kama kuna chochote lakini hakuona kitu. Ilimbidi atumie nguvu zake za uchawi alizokuwa Nazo ili kujilinda kwani aliziona dalili za kuvamiwa katika mazingira ya kutatanisha.
Mama Eddy ambaye jina lake halisi alijulikana kama Maimuna hakuwa Mtu wa kawaida Bali alitumwa na uongozi mkuu wa himaya aliyotokea Doreen ili kumsaidia kupata vitu alivyovihitaji.
Alitumia mbinu ya kujifanya mke wa Mr Aloyce ili kuweza kumteka vizuri na kumfanya asihangaike sana kuhusu mwanae kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa kuharibu kazi. Maimuna alikuwa ni kijakazi mkongwe wa Bi Tatile na alikuwa akiaminika sana katika himaya ya Wanatatile kwani ni mtu pekee aliyewahi kufanikisha ajali kubwa ya mabasi mawili iliyoua abiria wote kisha wakafanywa kitoweo katika sikukuu ya kumpongeza Bi Tatile kama kiongozi bora wa wachawi wote Afrika Mashariki. Bi Maimuna alikuwa akiaminika sana kwa kila kazi anayoagizwa kwani hakuwahi kufanya makosa zaidi ya tukio moja tu la kuanguka kanisani akiwa katika harakati za kuwanga mchana.
"Maimuna! Maimuna! Hapa sio kwako na Leo ndio mwisho wa ubaya wako kwenye familia hii" ilisikika sauti nyororo isiyo na mkwaruzo hata kidogo huku ikijirudia rudia. Maimuna alibaki na mshangao wa ajabu sana, akataharuki huku akihema kwa nguvu. Akaaangaza macho kila upande pasipo kumuona mtu yeyote.
Akazidi kuchanganyikiwa sana. Ghafla wazo likamjia akilini mwake, bila kuchelewa akaamua kulifanyia kazi. Akanyoosha mkono wake wake wa kulia kisha nguvu nyingi zikamjia kama radi mkononi mwake. Bi Maimuna akaachia tabasamu mwanana akiamini hakuna kitakachomdhuru kwa wakati ule wala wakati mwingine wowote. akatulia kimya akimsubiri adui yake, lakini hakuona chochote zaidi ya ukimya mzito uliokuwa umetawala.
"Kumbe unaniogopa eeeh!" Alisema Maimuna.
"Ha ha ha! Sikuogopi Maimuna... Nakuvutia pumzi tu maana sina papara" sauti ile iliyojaa dharau ilisikika. Bi Maimuna hakutushika hata kidogo kwani alikuwa anajiamini kupita kiasi. Ghafla sura yake ikabadilika sana na kuwa sura ya kutisha sana.
Meno yakawa marefu kama mnyama mkali, kucha zikawa ndefu na Kali kama za chui anayemvamia swala, macho yake yakawa meusi huku mboni yake ikiwa nyekundu kama moto. Lengo lake lilikuwa ni kuonesha nguvu zake mbele ya adui yake ambaye hakujua ni nani. Ghafla kicheko kikali cha kutisha kilichojaa dhauri na jeuri kikasikika na kumfanya Maimuna ajione mdogo kama simimizi ilihali hamjui nana aliyemcheka.
Wakati huo huo Mlango ulifunguliwa na Mr Aloyce aliingia sebuleni pale.
"Mamaaaa" Mr Aloyce alipiga ukunga wa nguvu baada ya kumkuta mkewe akiwa na umbile la kutisha sana. Uvumilivu ulimshinda alijikuta anakimbia nje kama chizi huku akihema kwa nguvu. Mlinzi alimshangaa Mr Aloyce bila kuelewa kinachoendelea.
"Vipi bosi?" Aliuliza mlinzi huku akicheka sana. Mr Aloyce alianguka chini kama mzigo huku akihema kama Mtu aliyepanda mlima mrefu kwa kasi. Mlinzi alimsogelea na kumuuliza kilichojiri.
"Kuna maajabu humo ndani"
"Maajabu gani?"
"Mke.. Mke wangu...Ame..."
"Amefanyaje tena?" Aliuliza mlinzi kwa woga kwani alishapewa onto Kali na mwanamke yule kuwa asimfatilie kwa lolote. Lakini kabla hajasema chochote kuna kitu kiliwashtua Mr Aloyce na mlinzi wakabaki wameduwaa kwa mshangao.
******
Mama Pamela hakuwa na la kufanya zaidi ya kulia tu. Muda wote ule hakujua Doreen anaendeleaje ila kilichomshangaza ni kwanini Doreen hakwenda sebuleni kujumuika nao? Alinyanyuka kitini na kwenda chumbani kwake. Lakini ghafla mshangao wa ghafla ulimvaa mwanamama yule baada ya kukuta hali ya chumba ni mbaya sana kila kitu kilikuwa shaghalabaghala tu, ndipo machale yakamcheza, akasogelea droo anayohifadhia pesa.
"Mungu wangu!" Alishtuka mama Pamela baada yakukuta droo IPO wazi lakini haina pesa yoyote zaidi ya stakabadhi ambazo hakuwa na shida nazo wakati ule. Macho yalimtoka kwa mshangao huku akitoatoa vitu ndani ya droo ile bila kuona chochote. Akasimama wima akiwa ameshika mkono kiunoni kwa hasira
"Doreen!" Aliita kwa jazba bila kujua Doreen alikwishaondoka muda mrefu uliopita. Mama Pamela akakugua tena ili kujiridisha kama kweli pesa hazikuwamo lakini bado hakukuta pesa ndani ya droo ile wala eneo lingine chumbani mle.
Mama Pamela alichanganyikiwa sana akatoka ndani ya chumba kile na kupiga hatua za harakaharaka koridoni kuelekea chumbani kwa Doreen.
Alifika mlangoni na kufungua mlango kwa jazba kubwa. Lakini cha ajabu chumba kilikuwa kitupu na hakukuwa na mtu yeyote wala dalili za uwepo wa mtu. Mama Pamela akahamaki, akamwita Doreen kwa sauti kali lakini hakuitikia.
"Mungu wangu ina maana Doreen ametoroka na pesa au?" Alijiuliza Mama Pamela akiwa ameishiwa nguvu kabisa. Hakutaka kuamini kama binti anayemuamini kiasi kile angetenda tukio lililotokea.
Mama Pamela alitoka nje ya nyumba yake ili kumtazama vizuri Doreen. Alimtafuta pale uani na kila upande wa nyumba lakini Doreen hakuwepo. Moyo wa mama Pamela ukatawaliwa na lawama nyingi sana. Akajilaumu ni kwanini hakumsikiliza mumewe mpaka yote hayo yametokea.
Akakaa chini kibarazani huku machozi yakimchuruzika. Kila akikumbuka maneno ya mwanae roho ilimuuma zaidi, hakuwa na hamu hata ya kula. Alikuwa na simanzi nzito iliyopelekea mafuriko ya machozi usoni mwake. Alilia mpaka machozi yakamkauka akiwa pale pale kibarazani kwake. Hakutaka hata kumwona binti yake kwani uchungu ungemzidia. Kwa jinsi alivyokuwa akimpenda na kumjali Pamela hakuamini kirahisi kuwa Leo amekuwa adui yake mkubwa na kumpa lawama za uchawi.
"Mungu tu Anajua" aliwaza Mama Pamela.
Majira ya saa kumi na moja jioni, Baba Pamela aliwasili jijini Mbeya na kufika nyumbani kwake akiwa na mawazo tele juu ya familia yake. Alipofika ndani tu alikutana na mkewe ambaye uso wake ulivimba sana kwa machozi ya siku nzima. Baba Pamela hakushangaa sana kwani alihisi mkewe anamlilia binti yao Pamela kumbe si hivyo tu, Bali alikuwa na jambo zito lililomtatiza sana moyoni mwake.
****
Familia ya akina Dorice ikiwa bado imekaa kikao babu yake Dorice aliyefahamika kama Mganga Tawi La Mtawile alikuwa tayari ametoa wazo kuwa atafanya jambo.
Familia nzima ikaondoka kwenye nyumba ya mama Dorice na kwenda moja kwa moja kwa Mganga Tawi la Mtawile ili kujua Dorice yupo wapi na katika hali gani.
Na kwakuwa hapakuwa mbali sana, walitumia mwendo wa dakika tano tu mpaka kufika kwenye nyumba ta Tawi La Mtawile.
Mganga yule maarufu mkoani singida, alikuwa ametenga eneo maalum nyumbani kwake kwaajili ya shughuli za uganga. Alipanga vyema vibuyu na dawa zake pembeni alizungushia kaniki nyeusi na nyekundu. Akavua viatu, kisha akawaamrisha wote waliombatana nae wavue viatu ndipo wakae kwenye zulia alilotandika chini. Wote wakafata kama walivyoamriwa.
Mganga Tawi alianza kuimba nyimbo za kuita mizimu na kuongea maneno ambayo wengine hawakuyaelewa . alitumia dakika kumi nzima kisha akachukua kioo kikubwa, akanyunyiza dawa na kuipakaza vizuri kwa kutumia mkia kama wa ng'ombe. Akaita jina la Dorice Mara tatu. Baada ya muda mfupi ardhi ikatetemeka sana radi zikapiga mfulululizo na kuwafanya wote waogope. Na kila mmoja alitamani kukimbia kwani palikuwa na utisho wa ajabu....
ITAENDELEA..........