HADITHI YA KUSISIMUWA NCHI YA WACHAWI-2
ILIPOISHIA:
Kabla sijaenda mbele zaidi nataka kusema kuwa, kama kuna shughuli mbalimbali za binadamu zinazoonekana kwa macho ya kawaida duniani, pia kuna shuguli kama hizo hizo zisizoonekana kwa macho ya kawaida, lakini zinashirikisha wachawi na mambo yao.
SASA ENDELEA&[HASHTAG]#8230[/HASHTAG];
Wachawi wana kila kitu, wana mikutano ya nchi, mikutano ya kimataifa, ya kanda ya mabara na pia wana mabenki, japokuwa kwa macho tunazungumzia mabenki ya pesa, wao wana mabenki ya damu, nyama na dawa za kienyeji.
Huwa wanakopeshana, wanalipana na wapo wasiotaka kulipa ambapo huchukuliwa adhabu mbalimbali kulingana na makosa. Zipo nchi ambazo wachawi wake wanafukuzwa katika uanachama, zipo zinazoingizwa, wapo wakuu wa wachawi wa nchi wanaopinduliwa wengine hata kuuawa na pia kunakuwa na uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano kuchagua viongozi wa kichawi wa nchi husika ambapo wapiga kura huandikisha majina yao na kuwa na vitambulisho vya kupigia kura.
Pia kuna bendara ya umoja wa wachawi barani Afrika, Ulaya na duniani kote. Aidha, kila nchi ina bendera yake inayoonesha utambulisho wa kitaifa. Mfano, bendera ya kichawi ya Tanzania ni rangi nyekundu, nyeusi na kahawia, katikati ina picha ya mnyama Twiga.
Nchi ya Nigeria, bendera yake ya kichawi ina rangi nyekundu bila mchanganyiko, katikati ina picha ya mkono mweusi umeshika kibuyu chenye shanga.
Kuna wachawi wanaofanya biashara za kimataifa, mfano kutoa dawa za kienyeji Tanzania kupeleka India kwa njia za kichawi na kule mchawi anaweza kununua ngozi za wanyama akaja kuuza Tanzania, Kenya au Uganda kwa wachawi wengine ambao hawana mitaji mikubwa.
Ilikuwa mwaka 1980 nikiwa na umri wa miaka thelathini tu, ndipo niliposhawishiwa na mzee mmoja, sasa marehemu kujiunga na wachawi. Huyu mzee namtaja kwa jina moja la Madume, tulikutana kwenye shughuli ya uvuvi samaki ziwani Victoria, alitokea kunipenda sana kutokana na tabia yangu njema na kuwa kama kijana wake.
Usiku mmoja nikiwa nimelala alinijia katika ndoto, lakini baadaye niligundua ilikuwa 'laivu'.
"Kijana wangu Israeli, unaoenekana unaweza kukifanya kile ambacho mimi ninacho, nitafurahi sana kama utakipenda ili nikupe," aliniambia kwa sauti ya utu uzima.
"Kwa wewe baba nitapenda, na ikibidi naomba unipe sasa," nilimjibu.
Mzee Madume akanishika mkono na kunivuta, nikasimama. Tulisimama sanjari, akanisogezea uso wake kwenye uso wangu, kwa hiyo pua yake ikagusa pua yangu, midomo yake ikawa kwenye midomo yangu, paji lake la uso halikadhalika, kuna wakati alitembeza uso wake mpaka kidevu chake kikagusana na changu.
Kufumba na kufumbua, tukawa kwenye nyumba ya udongo, dhaifu kwa kila hali, katika chumba ambacho koroboi ndiyo ilikuwa ikitoa mwanga hafifu uliofanya tuonane kwa tabu. Tulikuwa watatu, mimi, mzee Madume na mtu tuliyemkuta ndani ya chumba kile.
"Kaa chini kijana wangu," mzee Madume aliniambia kwa sauti ileile niliyoizoea.
Nilikaa chini kwenye ngozi nyeusi, kila nilipokuwa nikimkamata sura yule mtu tuliyemkuta mle ndani, kibatari kilipoteza nuru na kumfanya aonekane kwa tabu kidogo, hivyo kuna wakati nililazimika kufumbua macho mpaka mwisho ili nipate nafasi ya kuona sawasawa.
"Fumba macho," mzee Madume aliniambia, lakini si kwa amri.
Nilifumba macho na kusubiri tamko jingine kutoka kwa mzee huyo au yule mwenyeji wetu. Nilihisi hali ya kama maji yakinigusa mwilini, kuanzia shingoni kuteremka na uti wa mgongo hadi kiunoni. Yalikuwa ya baridi mfano wake hakuna, nikasema siiiii.
"Sii nini kijana wangu? Wewe sasa ni mtu kama mimi, utaishi kama mimi na wala hakuna binadamu yeyote atakayekuweza," mzee Madume aliniambia lakini tukiwa palepale kwenye kitanda alichonikuta.
"Ha!" Nilisema na kushtuka.
Je, nini kitatokea? Usikose Itaendelea Kesho