Sehemu ya 45
Niliondoka nikiwa na hasira, nilitambua hata majina yake alikuwa akibadili badili kila wakati, hili la Victor kama utakumbuka vizuri hakuniambia yeye, ila nilisikia akiitwa na mwanamke mmoja huko msasani loung beez Hotel jina.
“Victor mbwa wewe, ulaniwe milele huko uliko.” Nilinong’ona.
Niliondoka na kurudi nyumbani, kwa mara nyingine mapenzi yakanichapa.
Tukio la kufanya mapenzi kwenye gari langu lilikuwa likijirudia kila siku, kuna wakati niliumia kila kumbukumbu hiyo ilipojitengeneza akilini mwangu, na kuna wakati nilifurahia na kumisi mno Victor.
Hata hivyo kuna jambo nilijifunza, kitendo cha mwanamke kutoa mwili wake sadakalawe kwa mwanaume unaye kutana naye ndani ya muda mchache sio jambo zuri.
Kwa muda mfupi nilikuwa nimetokea kumpenda mno Victor, moyo wangu ulikuwa umekufa umeoza kwake, lakini mpumbavu yule hakuliona hilo. Naye kwa muda mfupi akaniumiza na kwenda zake.
Siku zilikwenda, miezi ikakatika, Victor sikumwona tena machoni mwangu, nikabakia na kidonda moyoni mwangu, kila wakati sura yake nzuri ilijitengeneza kichwani.
Niliishi kwa machungu nikiwa nimezingirwa na picha ya mwanaume huyo kichwani mwangu, ilikuwa hivyo kwa mwaka mzima, hadi siku moja ulipoibuka mkasa mwingine uliozifutuilia mbali kumbukumbu zote za Victor, mbwa yule.
****
Ilikuwa ni asubuhi Moja, nilikuwa katika kumalizia usingizi wangu wa asubuhi, usingizi ulioambatana na uchovu. Hii ni kutokana na usiku wa kuamkia siku hiyo, nilichelewa sana kulala baada ya kukesha katika harusi ya mfanya kazi wangu mmoja aliyekuwa anaoa.
Nikiwa katika ‘hang over’ kutokana na konyagi nilizozifakamia usiku huo, kiasi cha kunifanya nilale kama mfu, ghafla, nilistushwa na sauti kali ya kengele ya getini.
Nafsi ilitaka nisimame, lakini mwili iligoma, kengele ikazidi kugongwa. “Nanii aaagh!!” nilimaka. Sikupenda kabisa mgongaji aendelee kunivurugia pumziko langu asubuhi ile.
Na kwa mara ya kwanza nikaona umuhimu wa kuishi na dada wa kazi ambaye angeweza kunisaidia kuikabiliana na ile kadhia.
Kengele ikalia tena.