Sehemu ya 27
ILIKUWA mnyonge asubuhi, mchana, na jioni. Zilikuwa ni nyakati mbaya mno katika maisha yangu ya ujana. Nilikuwa nikijifungia ndani na kulia kama mtoto.
Wadogo zangu Peter na Daudi, ambao kama nilivyosema awali, kwa nyakati hizo kila mmoja alikuwa na maisha yake.
Walipobaini dada yao nilikuwa nikijihusisha na kazi ya ukahaba mitandaoni, kwa kweli ndugu zangu wale, walichukizwa mno.
Kila mmoja alikuwa akinilaumu kwa kumwaibisha maishani mwake. Hakuna aliye kumbuka msaada wangu kwao ulitokana na kazi hiyo hiyo ya ukahaba, ambayo wao waliona nimewadhalilisha.
Kila mmoja, katika maisha yake alikuwa katika mafanikio, kwani walikuwa na miradi yao mbalimbali ambayo niliwafungulia kupitia pesa niliyoipata kwenye shughuli ya ukahaba.
“Heri tungebakia na umasikini, kuliko aibu hii?”alisema Peter, uso wake ulikuwa na hasira kali.
“Umetuabisha sana Sofia, kama ningalijua msaada wako unatokana na kazi ya kujiuza mitandaoni, kamwe nisingekubali kusaidiwa na wewe,” Daudi naye alishadadia.
Nilisemwa na ndugu zangu wale kiasi cha kushikwa na aibu kubwa.
Waliondoka na kunitenga. Tukio la kukimbiwa na mchumba masaa machache kabala ya ndoa kwa sababu ya kuvuja kwa picha zangu, ilikuwa ni mwiba mkali moyoni.
Habari hiyo ilisambaa kila mahali. Kila nilipopita nilisindikizwa na minong’ono, watu walinisonta vidole wakisimuliana kisanga cha kukimbiwa na mwanaume kisa umalaya.
Nilikonda na kubakia mifupa, dunia ilikuwa sehemu moja ngumu sana. Katika nyakati hizo ndipo nilipojiingiza kwenye tabia ya ulevi.
Niliingia kwenye ulevi wa pombe kwa mantiki moja tu. Kupunguza mawazo, niliamini pombe inaweza kuniondolea msongo wa mawazo na kuweza kumsahau kabisa Alex.
nikawa nakwenda viwanja mbalimbali, huko nikawa nabwia ulabu. Nilipolewa chakari nikawa nacheza muziki, naimba imba kama mwendawazimu, wakati mwingine nikawa naongea kilevi peke yangu.
Ulevi ulikuwa unaniondolewa mawazo nyakati nilipolewa tu, pombe ilipokwisha, tatizo lile lilinirudia upya akilini mwangu. Moyo wangu ukawa mzito kumsahau Alex.