Simulizi: Mpaka Kieleweke

117823629_219072996304959_5786223668629821241_n.jpg
 
SEHEMU YA 24

Mnaro nami nikakimbia mbio zangu zote, nikiwa nimebakiz hatua chache nikaona kama sitoiwahi kasi ile hivyo nikaamua kujirusha kupenya kwenye mlango ule kabla haujafunga....







Nikafanikiwa kuwahi, nikatua na kugeuka nyuma lakini sikumuona Mnaro, hata mazingira yalikuwa ni tofauti na ambayo nilikuwemo kabla, moja kwa moja nikagundua kuwa nilikuwa nimeingia Muifufu tayari. Kitu cha kushangaza ni kuwa sikuwa na nguo yoyote mwilini mwangu. Ikanibidi kuzunguka hovyo ndani ya pori lile kutafuta chochote cha kuvaa lakini sikupata kitu zaidi ya majani ya mgomba ambayo niliyaunganisha kwa kamba nilizotengeneza kutoka mgomba pia, kisha nikavaa kujisitiri halafu nikatembea kufuata maelekezo ya Mnaro ndani ya pori lile.

Ilinichukua kama saa zima mpaka kuanza kuona mji kwa mbali nikiwa ndani ya pori lile, nikawa makini zaidi na kugundua kuwa nilikuwa katikati ya miti ile iliyojipanga kwa mstari, nikatembea kuelekea nnje ya pori mpaka nilipoifikia mti ule wa mwisho upande wa kulia na kwenda kuweka mkufu ule ambao nilielekezwa kuuacha kwaajili ya Sauda ili atambue uwepo wangu ndani ya Muifufu, kisha nikaingia ndani ya mji ule bila hata ya kujua pa kuanzia.

Nilitembea nikirandaranda bila kuwa na pakwenda mwisho nikakuta gogo kubwa nyuma ya jumba lililojengwa kwa mawe, nikaamua kukaa hapo nikisubiri kupambazuke vizuri kwa maana kulikuwa na kagiza bado, tofauti na siku ambayo niliingia Muifufu kupitia nyumbani kwa Mnaro ambapo niliondoka kule ikiwa usiku lakini Muifufu kulikuwa mchana, leo kote palikuwa na giza.

Nikakaa pale mpaka nikajikuta nimepitiwa na usingizi.



Nilishituliwa na mlio wa mkali kama honi ya meli, nikaamka na kuona watu wakikimbia kuelekea huko ambako sauti hiyo ilitokea. Kulikuwa kumepambazuka tayari hivyo niliweza kuona kila kitu kwa ufasaha kabisa. Nikatamani kujua nini kilikuwa kinaendelea huko hivyo na mimi nikaungana na wakimbiaji wale kufuata mlio ule ambao nadhani ulikuwa ukilizwa kwa makusudi ya kuita watu.

Jambo ambalo nililugundua nikiwa katika kuwahi huko ni kuwa mimi nilikuwa tofauti na watu wote kutokana na kuvaa kwangu majani ya migomba, wenyeji wa eneo lile wangi walijifunga kaniki huku juu wakiwa hawakuvaa kitu, wengine walijifunga ngozi za wanyama mbalimbali lakini wengine ambao walikuwa na wachache tu walikuwa uchi.. uchi kabisa wa mnyama.

Nikaamua kuwa ni bora kufanana na wenyeji, vinginevyo ningeonekana mara moja kuwa mimi nilikuwa mgeni na sikujua madhara yangekuwa yapi kama ningeonekana mgeni.

Njia pekee ambayo ilikuwa rahisi kwenye kujifananisha na wenyeji wale ilikuwa kuwa uchi.. kuwa uchi hakuhitaji kuwa na chochote, ni suala la kuvua tu majani yale ya mgomba, niliwaza na kujiweka kujitoa polepole miongoni mwa wakimbiaji wale ambao bila shaka hakuna hata mmoja ambaye aliutambua uwepo wangu pale kwani hakuna ambaye alikuwa makini kwa mwingine.

Nikasimama na kuvua majani yale kisha safari ya ikaendelea nikijichanganya na ambao walitokea nyuma yangu, baadhi yao walikuwa uchi kama mimi hivyo kuniongeze ujasiri wa kuwa katika hali ile ya uchi hadharani jambo ambalo halikuwahi kutokea kabla maishani mwangu.

Tulikwenda mpka kufika kwenye uwanja mkubwa sana mbele ya jumba kubwa mno na la kifahari, jumba lile bado lingekuwa la thamani hata kama lingekuwa ndani ya dunia yetu hii yenye kila aina ya majengo. Katikati ya uwanja ule kulikuwa na mzee akiwa amekaa kwenye kiti akizungukwa na wasichana warembo kama nane hivi, pembeni yake alikuwa amesimama mwanaume wa kama miaka 40 hivi ambaye alikuwa mkubwa sana wa umbo na alikuwa na misuli ya ukakamavu hasa, mtu yule alikuwa mweusi tiii! Ngozi yake ambayo ilionekana kama ambayo imepakwa mafuta mengi sana ilikuwa ikin`gaa sana.

Watu wakaendelea kimiminika pale mpaka kukawa na kundi kubwa sana ambalo ilikuwa ngumu kuamini kuwa lote lilitokea ndani ya kamji kale kadogo.

Baada ya utulivu wa hekaheka za watu kupatikana, bwana yule mweusi sana akasimama na kuanza kuzungumza "wakazi wote wa Muifufu naomba mnisikilize kwa makini sana! Alfajiri ya leo kuna mtu kutola duniani ameingia Muifufu, mtu huyo ambaye mpaka sasa hatujamjua ameingia bila ruhusa wala taarifa kwa uongozi wetu na hatujui amewezaje kuingia wala hatujui ana lengo gani! Sasa tunataka kumpata mtu huyo ili kujua kilichomleta pamoja na kumuadhibu kwa kuingia kwake bila ruhusa, hivyo tunataka watu wote muwepo hapa! Kama kuna mtu kabaki nyumbani, awe mzee ama mtoto, mzima ama mgonjwa lazima aje hapa!. Tunatoa dakika kumi tu wote waliobaki nyumbani waje hapa". Mara baada ya kusema maneno yale minong`ono ya hapa na pale ikasikika huku baadhi ya watu wakikimbia, nadhani kurudi makwao kuwaleta ambao wamebakia nyumbani.
 
SEHEMU YA 25

"Itakuwa ni msaliti Mnaro amerudi" aliongea mzee mmoja ambaye alikuwa karibu na mimi akijaribu kukisia juu ya hali ambayo ilikuwa inaendelea.. "hapana, Mnaro hawezi kurudi hapa kwa maana anajua fika kama akikanyaga tu ndani ya Muifufu basi mkuu Magugi atajua" alijibu mzee mwingine ambaye ndiye aliekuwa akiambiwa jambo ambalo mzee yule wa awali aliliafiki.

Baada ya dakika zile kumi kuisha bwana yule aliamuru watu wote wasimame na kuwataka kila mtu kuhakikisha mkono wake wa kushoto unashikana na mtu ambaye anamjua na ni mkazi wa Muifufu huku mkono wa kulia pia ukishikwa na mtu mwingine mwenye sifa kama hizo na zoezi hilo likaanza mara moja!.

Namimi nikawa katika harakati kujaribu kushikana mkono na mtu yeyote lakini hakuna ambaye alikuwa akiukubali mkono wangu, nikaona kundi lile likiendelea kuungana kwa kushikana mikono kutoka mtu mmoja kwenda mwingine lakini mimi niliendelea kuwa mpingwaji kwa kila ambaye nilijaribu kumpa mkono wangu, hapo nikaelewa nini hasa lilikuwa lengo la mchezo ule, nimimi nilikuwa natafutwa hapa, baada ya kubaki pekeyangu kundi lote likiwa limeungana basi moja kwa moja watajua kuwa mimi ndiye ambaye sina ambaye ananijua hivyo ndiye ambaye nimeingi kutokea duniani alfajiri ya siku hiyo.

Niliingiwa na uoga wa hali ya juu nikikimbia huku na huko kujaribu kupata wa kiushika mkono wangu lakini hakuwepo mtu wa aina hiyo na sasa nikona tayari nn likuwa nimeumbuka na kukamatwa masaa machache tu baada ya kufanikiwa kuingia Muifufu nikiwa hata sijamuona mke wangu, roho iliniuma sana.

Wazo ambalo lilinijia ghafla ni kukimbia kuondoka eneo lile ili nisikutwe na ambacho kinaelekea kunikuta, lakini lilikuwa ni jambo la kutisha vilevile kwa maana nilijua watu walikuwa makini kuangalia nani anabaki akiwa hakushikwa mikono na kama nitakimbia bila shaka nitaonekana na kukimbizwa ndani ya eneo lile ambalo wao walilijua zaidi mimi nikiwa mgeni tu, lakini hakukuwa na namna nyingine hivyo nikavuta pumzi nyingi na kujiandaa nikiangalia ambapo palikuwa na nafasi nzuri ya kutorokea ili nitimue mbio, lakini nikahisi mkono wangu wa kulia ukishikwa na mkono mlaini wa mtu ambaye alikuwa nyuma yangu nilishtuka nikiona kama ilikuwa ndoto, no kageuka na kukutana na sura ya mwanamke mrembo sana akawa ameachia tabasamu zuri sana!.

Mwanamke yule ambaye alikuwa ni chotara wa Muafrika na Muarabu akakunjua kiganja chake cha mkono wa kulia na kunionesha kitu...

Ulikuwa ni ule mkufu ambao nilielekezwa na Mnaro kuuacha kwaajili ya Sauda. Ahsante Mungu, Sauda wakati muafaka! Bila uwepo wake hapa kila kitu kilikuwa kinaharibikia hapa!, Niliwaza nikiwa na furaha ya hali ya juu moyoni mwangu, nilitamani kumdandia mwanamke yule ambaye nilijua alikuwa Sauda wa Mnaro na kumkumbatia ila mazingira hayakuruhusu hivyo nikajikaza na kufanya kama hukukuwa na kitu ambacho kimetokea.

Baada ya kama dakika moja tu mkono ule wa kulia wa Sauda uliapata mtu akaushika nami nilipojaribu kumpa mtu mwingine mkono wangu wa kushoto nilishangaa akiupokea bila ubishi, nadhani ni kutokana na udhamini ule wa Sauda ambaye alionekana kumjua.

"Kuna mtu ambaye hajashikwa mkono?" Aliuliza bwana yule mbabe, lakini palikuwa kimya, kisha akaongea tena "bila shaka mtu huyo hajaja hapa lakini najua nyote mnajua kua lazima tutamkamata, uwezo wa Magugi sio wa kufananishwa na mtu yeyote..." kabla hajamaliza mzee yule ambaye alikuwa amekaa muda wote alisimama akaongea kwa hasira "hakuna wa kushindana na Magigi ikiwa nitaamua jambo.

Sasa nasema endeleeni na shughuli zenu lakini nawahakikishia mtu huyo nitamkamata kabla siku haijaisha, hakuna anayepajua Muifufu kuliko mimi kati ya watu wote walioko hai, familia yoyote ambayo itampokea mtu huyo nyumbani kwake basi hukumu ya mtu huyo itaihusu pia familia hiyo" alimaliza kuongea mzee yule na watu wakaanza kutawanyika kwa makundimakundi kila kundi likiwa na uelekeo wake, nikamuona pia Sauda akiondoka kufuata uelekeo ambao aliujua yeye hivyo nikaona utakuwa ujinga wa karne kama sitomfuata.

Nikaendelea kumfuata polepole Sauda ambaye alikuwa kwenye kundi la watu wengine wakiondoka eneo lile, tukaendelea kwenda mimi nikifuata polepole mpaka Sauda akawa ametengana na watu wale na kubaki pekeyake, akaendelea kwenda mpaka kwenye nyumba moja kuukuu akaingia humo, nami nikaendelea kumfuata nikiamini alitaka nimfuate kwa maana alikuwa akigeuka nyuma na kutizama kama namfuata kila baada ya hatua kadhaa.

Nikaingia ndani ya jumba lile ambamo tulikuta watu wengine wawili mmoja akiwa mwanamke mzee na mwingine alikuwa ni mwanaume wa makamo!.
 
SEHEMU YA 26

Sauda akanitbulisha kwa watu wale ambao walionekana kujua kila kitu juu ya mpango wangu kisha akamtaka bwana yule kuandaa mpango mzuri "sasa Mkude nataka uhakikishe kuwa huyu bwana anafanikiwa kuingia nyumbani kwa Magugi kisha mambo mengine yatafuata" aliongea Sauda maneno ambayo yalinishtua sana, kuingia kwa Magugi tena? mtu ambaye ameapa kuwa atanipata kabla siku haijaisha, tena nijipeleke mpaka kwake? Niliwaza..

"Hakuna shida, ingawa ili kumuingiza kwa Magugi itagharimu maisha ya mtu asiye na hatia" aliongea bwana yule ambaye kwa harakaharaka alionekana mpole sana.

"Unazungumzia mtu mmoja? Jambo hili ni lazima litimie hata kwa kuua mamilioni ya watu" alijibu Sauda kwa maneno yale ambayo hayakufanana hata kidogo na muonekano wake..









baada ya Sauda kuondoka nilibaki na bwana yule kila mmoja wetu akiwa kimya!. Ndani ya kichwa changu kulikuwa kukiendelea mawazo ya hapa na pale, huku nikiwa najaribu kupanga na kupangua mipango ya kujitoa Muifufu nikiwa na wote ambao natakiwa kuwarudisha duniani!.

"nawezaje kuingia kwa Magugi na nikawa salama?" nilivunja ukimya na kumuuliza bwana yule ambaye naye alionekana kama alikuwa na mambo mengi yakiendelea kichwani kwake..

"hiyo sio kazi rahisi hata kidogo, kuna mambo mengi ya kufanywa kabla ya kulifikia hilo, umeshajiuliza tayari Magugi amejuaje kama umeingia Muifufu?" alihojo bwana yule..

Nilitulia nikijaribu kufikiri kwa sekunde chache kisha nikajibu "ni jambo la kustaajabisha, sijui namna gani aliweza kugundua ikiwa hakuna mtu yeyote ambaye alishuhudia kuingia kwangu" bwana yule akakaa sawa akijisogeza karibu zaidi na ambapo nilikuwa nimekaa mimi kisha akaanza kunielezea.. "Magugi anafuga majini!.. majini ambayo anayategemea sana kwenye kupata taarifa za kila ambacho kinaendelea!, majini hao wapo kila sehemu na humuotesha kila ambacho wamekiona na kudhani kinaweza kuwa cha madhara kwake!, bila shaka majini hao ndio ambao walikuona na kumfikishia habari ndotoni kama ilivyo kawaida yao"

"duuh! sasa kuingia kwake si nisawa na kujinasisha mtegoni?" niliuliza nikionesha wasiwasi wa wazi juu ya habari ile mpya ambayo nilikuwa nimeipata!..

"ndo maana nikakwambia kuwa kuna mambo ya kufanywa kabla ya kufikia kwenda, kwanini haujiulizi tunawezaje kuongea hapa habari za kumletea madhara na hazipati pamoja na kwamba majini wake wako doria?" aliuliza tena bwana yule nami nikaelewa kuwa alikuwa akijaribu kunionesha kuwa kuna njia za kudhibiti uwezo wa wale majini kusafirisha taarifa kwenda kwa Magugi..

"kwani hakuna njia ya kufanya bila ya kwenda nyumbani kwa Magugi" nilizidi kuuliza masawali kama k awaida yangu, huwa sikai na swali lisilo na jibu ikiwa namuona ambaye anaweya kunipa majibu!..

"unaogopa?" aliuliza bwana yule lakini akawahi kuendelea kabla hata sijamjibu "hii ni vita, tena vita kubwa kwelikweli!.. kushinda kwenye vita hii ni ukombozi kwa watu wengi sana, lakini kushindwa kwake ni maangamizo kwa watu wote hao ambao wanautegemea mno ushindi huo! wewe ndiye kiongozi wa vita hii! nataka ulitambue hilo kuanzia sasa na mambo ya uoga uyaache kuanzia leo kwani kuna wengi nyuma yako wako tayari kufanya chochote kwa kukutegemea wewe!.. ikiwa utaonesha uoga basi wao watakata tamaa kabisaa!"

alisema kwa msisitizo bwana yule!..

"kama ni kuogopa nimeshaogopa sana juu ya jambo hili!.. mpaka nimefikia uamuzi wa kuja huku ni kutokana na kuamua kwa dhati kuwa niko tayari kukabiliana na changamoto zozote zilizopo! usichukulie kuuliza kwangu kama uoga, ila ni kutaka kujua nini cha kufanywa na kuhakikisha kinafanyika kwa usahihi" nilijieleza kwa msisitizo wa hali ya juu kujaribu kumuonesha bwana yule kuwa sikuwa mtu wa kutoaminiwa hata kidogo!.. bwana yule alionesha sura ya kutabasamu baada ya maelezo yangu yale kisha akaongea "sasa umeongea, nafurahi pia kuona kuwa unajiamini sana! jambo hili litafa nikiwa kwa hakika" bwana yule akanitaka kupumzika ili baadae anielezee juu ya mipango ambayo inatakiwa kufuatwa kukamilisha zoezi la mimi kuingia nyumbani kwa Magugi, lakini nikamtaka kuendelea tu na maelekezo kwani sikuwa nimechoka na pia jambo la kuelezewa tu halinihitaji kuwa na nguvu, bwana yule hakuwa mtu mbishi! akaanza kunielezea! "Muifufu kulikuwa na wachawi wa kila aina na wenye mbinu mbalimbali!..

baada ya kushindwa kurudi duniani na kubaki huku, Magugi ambaye alikuwa mwanafunzi mzuri wa uchawi huko duniani aliteuliwa kuwa kiongozi na wazee ambao baada ya muda mfupi wote walikufa na kuiacha jamii hii chini ya utawala wa Magugi ambaye aliaza akiwa kiongozi mzuri tu mwenye kuonesha kuijali hatma ya Wanamuifufu! akawaweka wachawi katika makundi kulingana na ujuzi waliokuwanao kisha akawatumia vizuri kujifunza mbinu ambazo walikuwanazo na baada ya hapo aliwafuta kumbukumbu na kuwafunza machache ambayo alijua angehitaji wamsaidie na akahakikisha anakuwa na uwezo wa kuwatawala!..
 
SEHEMU YA 27

miongoni mwa makundi ya wachawi ambao walikuwepo walikuwa ni wafugaji wa majini ambao aliwatumia wakamtengenezea majini ya kutosha ambayo angeweza kuyatumia kwa ulinzi na shughuli nyingine! baada ya kazi hiyo alitaka kuwafuta kumbukumbu kama ambavyo alifanya kwa makundi mengine lakini kwa kundi hili ilishindikana kwakuwa majini wale walikuwa tayari kupambana kuhakikisha hilo halitokei hivyo kundi lile kupitia kwa kiongozi wao wakaomba waachwe kama walivyo nao wakatoa ahadi ya kutoingilia mipango ya Magugi, ikabidi busara itumike na Magugi akakubaliana nao kwa sharti ya kuwaweka mbali na jamii, jambo ambalo walikubaliananalo hivyo wakapelekwa nyuma ya kilima kileee!..." aliendelea kuelezea kuku akinionesha kilima kilichokuwa kikionekana kwa mbali, kilima kile kilikuwa kikionekana kama ambacho kimegawanyiki mbele kikiwa kifupi huku nyuma kukizidi urefu kidogo! "kundi lile la wafugaji wa majini waliwekwa huko huku wakiahidiwa kupewa huduma zote nao wakaapa kutorudi kwenye jamii hii, lakini Magugi aliwageuka na kuwatelekeza huko huku akitumia uchawi kuzuia watu wa huku pia wasiende kule! kwa kutumia uwezo wa majini watu wale wangeweza kurudi ila kinachowakwamisha ni mila zao! watu wale huwa hawavunji kiapo ambacho wamekiweka hata iweje, kuna tetesi kuwa iwapo mtu wa jamii ile akivunja kiapo hufa! njia pekee ya kiapo chao kuvunjika huwa ni kifo cha ambaye walimuapia! hivyo kurudi kwao huku ni mpaka afe Magugi" Aliweka kituo bwana yule, akaniacha nikiwaza kuwa alikuwa ananitaka kumuua Magugi kwaajili ya watu hao! "maisha ambayo wanaishi watu wale ni magumu mno!, hata chakula na maji safi ya kunywa ni ngumu sana kupatikana kwao, hivyo wanatamani sana kurudi, tatizo ni kutoweza kwao kuvunja kiapo! iwapo utaenda kuwaona na kuwaahidi kumuua Magugi ili wao wame huru basi bila shaka watakusaidia namna ya kuwanyamazisha majini ambayo ni wao waliyatengeneza na ndio tegemezi pekee la Magugi" alimaliza kueleza bwana yule. Nilimuelewa vizuri bwana yule na kuamua kuwa ni lazima kufanya kama ambavyo amenielezea ili kujihakikishia uwezo wa kupam bana na Magugi, kwakuwa kwa msaada wa majini wale isingekuwa rahisi.

"nawezaje kufika huko walipo wafugaji wale wa majini?" niliuliza nikiwa tayari kwa safari hiyo, sikutaka kabisa jambo lile lichelewe! "itakupasa kungoja usiku uingie ili tuweze kukupatia dawa ambayo unatakiwa kuiogea katikati mwa saa nne na saa tano usiku ili kujikinga na majini wa Magugi kisha ndipo safari itakapoanza! kupanda mlima ule mpaka kushuka upande wa pili itakuchukua usiku wote mpaka kunakucha" alielezea bwana yule!!..

"huku hakuna wanyama ambao wanaweza kutumika kama usafiri na wakaenda kwa kasi za kunipikisha huko mapema?.. niliuliza naye akajibu "wanyama wapo ila hutumika kwa ruhusa ya Magugi, mtunzaji wa wanyama wale ni bwana mmoja katili sana ambaye ni mtiifu kwa Magugi kama walivyo watu wote wa Muifufu" alielezea bwana yule!..

nikachukua ule mkoba wangu niliopewa na Mnaro na kuchukua ule mkate ambao alinielezea kuwa endapo ningemlisha mtu yeyote basi angefanya chochote ambacho ningemwambia! nikakata kidogo na kumkabidhi yule bwana.. "hakikisha mtu huyo anakula mkate huu, kisha tunaweza kumtuma na hakuna mtu ambaye atamuelezea juu ya hilo" bwana yule akapokea kipande kile bila ubishi wala maswali, kisha akatoka akinitaka kupumzika, kwaajili ya safari ya usiku!..

nilibaki nikiwa na wasiwasi mwingi kwakuwa sikuwa nimejaribu kutumia mbinu ile ambayo alinifundisha Mnaro ambaye yeye mwenyewe hakuwa na uhakika kama bado huku Muifufu kuko kama ambavyo alipaacha.. vipi kama huyo bwana anayepelekewa mkate ule atakuwa ana nguvu ya kuzidi uchawi ule na hivyo kugundua dhamira yetu?! niliwaza na kubaki kuomba tu mambo yaende kama ambavyo tulihitaji....







nilibaki pale ndani nikifikiria mengi na katikati ya mawazo nikakumbuka adhma kuu ya kuwepo Muifufu, mke wangu kipenzi!.. sijui atakuwa wapi Samia wangu!, niliwaza na kujikuta nikitembea kutoka nnje ya eneo lile bila ya kujua nilikuwa nakwenda wapi, nikajikuta nafuata njia ileile ambayo ilinileta katika nyumba ile nikimfuatilia Sauda, nadhani ni kutokana na kutopajua pengine popote!..

nilifika mpaka kwenye uwanja ambao tulikuwepo masaa machache yaliyopita lakini kitu cha ajabu ni kuwa lile jumba la kifahari ambalo ndio makazi ya Magugi halikuwepo tena pale ambapo lilikuwepo mwanzo! uwanja ulikuwa mtupu, nilistaajabishwa kwa muda mfupi juu ya kutokuwepo kwa jumba lile, nikafikia kudhani kuwa pengine nilikuja eneo tofauti lakini nikajiridhisha kuwa sikuwa nimepotea, ni penyewe haswa ila uchawi ulikuwa umefanyika tayari bila shaka ni uchawi wa aina ileile ambao uliuficha mji wa Muifufu ukakosa kuonekana duniani ikiwa upo humohumo!.. Nikaamua kuwa ni bora nirudi tu kwenye yale makazi yangu ya muda kuliko kuwepo kwenye mazingira yale yasiyoeleweka na mwisho wake kunasa mikononi mwa Magugi kirahisi!...
 
SEHEMU YA 28

muda huu kagiza kalikuwa kameanza kuingia, hali ya Muifufu ilikuwa ni tulivu mno, hakukuwa na watu wengi kama iwavyo dunia ya kawaida hasa mida hii ya jioni kila mtu akirudi nyumbani kutoka kwenye shughuli mbalimbali!...

nilipokaribia nyumba ile ambayo ndipo nilipokuwa nimewekewa makazi ya muda niliona kundi kubwa la watu wakiwa wamekusanyika pale! lilikuwa ni kundi kubwa kama ambalo lilikuwepo pale kwa Magugi wakati wakinitafuta!. Nikasogea kwa taadhari sana na kugundua kuwa nyumba ile ambayo nilifikia ilikuwa ikiwaka moto! kwa mbali pia niliona watu wawili wakiwa wamefungwa kwenye miti ambayo bila shaka ilichimbiwa pale chini kwa shughuli ile kwani haikuwepo mwanzo!..

pembeni ya watu wale kulikuwa na jitu lenye misuli mikubwa mno likimchapa mmoja wa watu wale kwa fimbo za mfululizo kisha lilipumzika na kufanya mzungumzo kwa muda mfupi na baadae likamchapa yule mtu mwingine na kufanyanaye mazungumzo pia! sikuweza kuwatambua watu wale ambao walikuwa kwenye mateso yale makali lakini hisia ziliniambia kuwa alikuwa bwana yule ambaye Sauda aliniacha kwake, bwana Mkude!.. Nikafikiria kwenda kujumuika kwenye kundi lile ili kujiridhisha juu ya watu wale ni akina nani na kujua nini hasa chanzo cha mateso yale kwa watu wale!.

Lakini itakuwaje kama tayari wanaijua sura yangu na kufika kwangu pale ikawa kujikamatisha? je kama watu wale wanateswa ili kuonesha nilipo na hawaoneshi kwakuwa hawajui nilipo kwenda kwangu si itakuwa pona yao na matatizo kwangu?! nilijiuliza na kufikia uamuzi wa kujisogeza kwa taadhari mpaka kwenye kichaka kidogo ambacho kilikuwa karibu zaidi na umati ule!, angalau kutokea pale niliweza kushuhudia na kusikia sauti za juu ya kilichokuwa kinaendelea pale!..

"sogezeni hapa zile kuni" nilisikia akiagiza bwana yule mwenye kutoa adhabu na watu ambao walikuwa wamevaa sare wakakimbia na kusogeza mzigo mkubwa wa kuni miguuni mwa watu wale!..

"sheria za Muifufu ni lazima ziheshimiwe, na yeyote mwenye kujaribu kuzivunja adhabu yake ni kifo, nipe moto" alisema mtu yule kisha akaagiza apewe moto na akapewa ukuni uliokuwa ukiwaka moto mkubwa kiasi cha kutoa mwanga naye akakiangushia kwenye kuni zile ambazo zilianza kushika moto kwa kasi na hatimaya kufanya moto mkubwa ambao ulianza kuwaunguza watu wale ambao niliwagundua kuwa walikuwa wale wenyeji wangu huku umati ule ukishangilia tukio lile!...

kwa upande wangu roho iliniuma sana... niliumia kwakuwa sikuwahi kushuhudia ukatili kama ambao ulitendeka pale, lakini pia niliumia mno kwakuwa niliona waziwazi kuharibika kwa mambo ambayo yalikuwa yamepangwa hapo mwanzo!..

nilibaki pale nikishuhudia watu wale wakitapatapa katikati ya moto ule mkali mpaka wakatulia na miili yao kuteketea motoni "nadhani mmeshudia madhara ya kuwa adui wa Muifufu" alianza kuongea tena mtu yule na washangiliaji wakawa kimya ghafla kumsikiliza.. "mtukufu Magugi ameahidi huyo mtu ni lazima apatikane na kuanguka kwakwe kutakwenda na wafadhili wake wote ndani ya Muifufu pamoja na familia zao! tawanyikeni mkaendelee na shughuli zenu" alimaliza bwana yule na watu wakaanza kutawanyika wakionekana kufurahishwa na jambo ambalo limetokea!

nilibaki pale kichakani nikiwa na hofu kubwa, mpaka kufikia hapo sikuwa na muongozo tena, hata kutoka kwenye kichaka kile niliogopa nikihofia kuonekana na kupoteza maisha kama ambavyo imetokea kwa wenyeji wangu wale muda mfupi uliopita! lakini mara nilipata ujasiri nikasimama na kuanza kutembea kuelekea ambako sikuwa nikipajua, njiani nilipishana na watu wachache ila kila mmoja alikuwa na mambo yake nikaenda mpaka eneo ambalo lilionekana kuwa ni eneo la mashamba na kuanza kurandaranda kwenye mashamba ya watu bila mpango maalumu!..

nikiwa katikati ya shamba la mahindi nilihisi kama kulikuwa na minong'ono mbele kidogo ya ambapo nilikuwepo, nikaamua kusogea ili kujua alikuwa nani na alikuwa akifanya nini mashambani usiku ule "hakikisheni tunampata kabla yao na anavuka mlima Kalingisi kabla hakujakucha, ardhi hii sio salama kwake" alikuwa akiongea mwanamke ambaye nilimtambua kuwa alikuwa Sauda na vijana watatu ambao mavazi yao yalifanana na watu wale ambao waliagizwa kuleta kuni ili bwana Mkude na mkewe wateketezwe kwa moto!..

sikuona sababu ya kuendelea kujificha ikiwa watu wale walikuwa wakipanga kuhusu usalama wangu. Nikajitokeza mbele yao na wote wakashituka wakidhani wamefumaniwa katika mbinu zao lakini baada ya kunitambua Sauda akatabasamu "umewezaje kujua kama tuko hapa?" aliuliza swali ambalo lilinifanya na mimi kujiuliza ni kwanini sikwenda pengine popote bali pale ambapo ndipo hasa walikuwepo watu pekee ambao ni salama kwangu, tukianacha na hili, niliwezaje kuondoka pale nyumbani kwa Mkude huko nyuma watu wa Magugi wakafika na kuteketeza nyumba? bila shaka ni kazi ya Mnaro!.
 
SEHEMU YA 29

Nilikumbuka kuwa aliahidi kuniongoza akisema mimi ni silaha yake! nafikiri ulikuwa muongozo wake..

"hapa sio salama tena kwako, inakubidi kuondoka usiku huu, Mkude alikwenda kujaribu kukupatia usafiri kama ambavyo mlikuwa mmekubaliana lakini alikuta tayari wamegundua juu ya yeye kukuhifadhi nyumbani kwake ikawa chanzo cha kifo chake, afadhali hawakukukuta walipokwenda kusachi kwa Mkude sote tulijua tumekwisha" alielezea Sauda nikiwa kimya kuwasikiliza wao toka kuwasili kwangu eneo lile "sasa jamani mimi naondoka ila hakikisheni mnampa kila kitu kama ambavyo nimewaelekeza na kisha mumpeleke mpaka kwenye mlango wa mlima Kalingisi, kisha nyie mrudi"aliagiza Sauda nikaondoka nikiongozana na watu wale, tukapitia kwenye kijumba cha ajabu ambacho hakikuonekana kama kilikuwa kikitumika, tukachukua furushi fulani ambalo sikujua lilikuwa na nini kisha safari ikaendelea!..

tulikwenda mpaka tukaufikia mlima ule ambao ulikuwa mbali kidogo kutoka ambapo mji ulikuwepo, tukakaa na bwana ambaye alikuwa amebeba furushi akalifungua na kutoa mfuko na kunikabidhi "hicho ni chakula, kula upate nguvu kabla ya kuanza kazi ya kupanda mlima! ni mbali sana" alisema bwana yule huku akinipa na kibuyu ambacho kilikuwa na maziwa!..

nikala harakaharaka chakula kile ambacho kilikuwa nyama ya kuku aliyebanikwa, nikashushia na yale maziwa na kujiona kuwa nilikuwa vizuri!..

"humu kuna nguo, maji ya kunywa na nyama ya ng'ombe iliyokaushwa, itakufaa safarini na utakapokuwa nyuma ya mlima maana huko ni kukame na kuna njaa sana! alielezea bwana yule nami nikachagua nguo na kuvaa, maana muda wote huu nilikuwa uchi, kisha nikabeba furushi langu na kuanza safari nikiacha watu wale wakirudi Muifufu..



kazi ya kupanda mlima ule ilikuwa ngumu sana kama ambavyo nilitegemea, hasa kutokana na kutokuwa na njia za kupita huku kilima kile kikiwa na vichaka ambavyo nilipaswa kuvipenya mara kwa mara ili kusonga mbele. Ugumu pia ulichangiwa na giza ambapo mara kadhaa nili jikwaa na kujeruhiwa na miti ambayo ilikuwa na miba mikali sana kwenye vichaka vile vidogovidogo! nikawa nikikazana kupanda huku nikipumzika na kupata maji ya kunywa kila ambapo nilipata sehemu ambayo haikuwa na muinuko mkubwa sana..

Safari yangu ikawa hivyo huku nikijitahidi na kujiambia kuwa sikupaswa kukata tamaa! masaa yakakatika katika hali ile na hatimaye nikawa nimefika katika kilele cha mlima ule ambao ulionekana wa mbele lakini hatua kama kumi kutoka nilipokuwa niliona kilima kingine cha kupanda ambacho kilikuwa kimeungana na hiki na kuwa kama kilima kimoja!..

baada ya kunywa maji na kupumzika kidogo nikaamua kukikabili kilima kile cha mbele yangu nikiamini ilikuwa kazi ndogo tu kwani hakikuwa kirefu kama ambavyo kilikuwa kile ambacho nilikuwa nimekimaliza. Nikaianza kazi ya kupanda mlima ule wa pili kwa kasi, haikuwa kazi rahisi pia kwani ulikuwa mlima huu haukuwa hata ni vichaka ambavyo vingeniwezesha kushika kama ilivyokuwa kwa ule wa awali, hivyo mara kadhaa nilinusurika kuporomoka nikajitahidi kuongeza umakini na kusonga mbele! safari ikaendelea kwa masaa mengi sana lakini sikufika juu!..

pamoja na kutokuwa na saa nilijua fika kuwa ni masaa mengi yamepita lakini kwanini nilikuwa sifiki juu! nikageuka na kuangalia chini nilikotoka, sikuridhishwa na umbali ambao nilikuwa nimepanda!. Ilikuwa ni kama ambaye nimepoteza muda mwingi bila kufanya jambo lenye manufaa!.. nikiwa bado nimegeuka nikiangalia chini na kushangaa kazi ambayo nilikuwa nimeifanya ambayo haikufanana hata kidogo na matarajio yangu, nikashangaa nimesukumwa na kuporomoka mpaka chini nikatua na makalio huku nikipatwa na maumivu makali sana!...

ghafla nikasikia sauti za vicheko huku wenye kucheka vichoko hivyo wakisogea nilipo...





pamoja na kupata maumivu makali sana, nilivumilia na kusimama haraka kujaribu kukabiliana na huyo ambae amenisukuma!..

lakini kadri cheko zile zilivyokuja karibu yangu niligundua kuwa walikuwa zaidi ya mmoja, nikawa narudi nyuma kujaribu kuwaepuka lakini nikajikuta nimefika mwisho, tena nilinusurika kuanguka kutoka kwenye kilele kile cha mlima, nikajiweka sawa na kusimama hapohapo nikingojea hatma yangu!...



nilistaajabu kuona kuwa nilikuwa nakabiliwa na viumbe ambao hawakuwa wanadamu!. Walikuwa sokwe watatu wakinijia katika hali iliyoonesha kuwa hawakuwa na nia njema na mimi! nikabaki nikiwa nimesimama bila ujanja wa kujiokoa! sokwe wale wakazidi kunisogelia huku wakijitandaza vizuri kuhakikisha kwamba siwaponyoki na kutokea upande wa nyuma yao lakini waliacha upenyo mdogo baina ya sokwe mmoja na mwingine! nikaamua kuwa nafasi hiyo ndogo ingenitosha kupita, hivyo nikaendelea kujifanya kama ambaye nimezubaa bila mipango huku nikivizia nafasi ya kuwatoroka!, waliponikaribia zaidi nika chomoka kwa mbia za hali ya juu na kupita katikati ya sokwe wawili lakini mmoja wao akageuka kwa kasi kubwa na kunitegua mguu, nikaanguka vibaya sana kutokana na kasi niliyokuwanayo!...
 
SEHEMU YA 30

sasa sokwe wote watatu wakaja kwa kasi pale nilipokuwa huku mwili wangu ukiwa mzito kufanya chochote nikigumia maumivu makali yaliyotokana na kuanguka mara kadhaa!.. nikabaki nimefumba macho nikingoja kitokee chochote ambacho kingefanywa na sokwe wale kwani sikuwa na ujanja!...

"ACHAAAAAA" ilisikika sauti kubwa ikiamuru! nami nikafumbua macho na kutazama baada ya kuona sekunde zinakatika bila kudhuriwa na sokwe wale!!..

nilishangaa kuona sokwe wengine watatu wakiwa wameongezeka, sikujua wametoka wapi na wala sikumuona ambaye alitoa amri ya kuacha kwa sokwe wale ambao walikuwa wakinishambulia!.. inamaana sokwe hawa wanazungumza? nilijiuliza baada ya kujiridhisha kuwa hakukuwa na mwanadamu zaidi yangu pale!..

sokwe wale ambao walikuwa wakinishambulia wakarudi nyuma na kisha mmoja kati ya wale ambao waliongezeka akaja mpaka nilipo na kunitizama kwa makini huku akisogeza macho yake karibu kabisa na uso wangu!..

sura yake ilikuwa mbaya na yakuchekesha mno lakini ningeupata wapi ujasiri wa kucheka katika hali ile ya hatari?..

baada ya kumaliza ukaguzi wake akarudi walipo wenzie, wakawa kama wanajadiliana jambo, kisha akaja tena mwingine na kuanza kunichunguza kama alivyofanya mwenzie ila yeye alikwenda mbali zaidi na kuanza kuninusanusa kisha akatoa kicheko kikubwa sana kilichonishtua, kicheko kile mbali na kuwa kikubwa hakikutofautiana sana na cha mwanadamu!..

"bhebhaaa" alisema sokwe yule ambaye alionekana kuwa mzee kwa matamshi ambayo hayakusikika vizuri lakini nadhani alitaka nibebwe, kisha wakaja sokwe wawili mbele yangu halafu mmoja akanibeba na kunipandisha mgongoni mwa mwenzie kisha sokwe wale pamoja na mimi nikiwa mgongoni mwa sokwe tukaondoka aliyenibeba akitangulia huku wengine wakifuata kwa mwendo wa kukimbia kupanda kilima kile!..

sikujua safari ile ilikuwa ina lengo gani lakini nilishangaa kuingiwa na imani kwa sokwe wale na kuwaacha wafanye ambavyo walitaka!...

mwendo wa sokwe wale ulikuwa wa kutisha kiasi kwangu kwani walikuwa wakienda kwa kurukaruka huku wakipanda juu, nilikuwa nikihofia sana iwapo wangeteleza na kuanguka, nikawa najishika vizuri zaidi pale mgongoni ili nisianguke! maumivu ya kiuno na makalio pia yalizidi kwanyi sokwe yule alikuwa na vishindo vikubwa akiruka na kutua mbali hali iliyosababisha mtikisiko mkubwa wa mwili wangu pale mgongoni kwake!..

mlima ule ulikuwa wa ajabu sana, pamoja na kuonekana mfupi, kuupanda ilikuwa ni safari ndefu sana hata baada ya kupandishwa na sokwe wale ambao walikuwa wazoe fu wa kupanda mlima ule na walikuwa wakienda bila kusita!..

baada ya masaa kadhaa tulikuwa kwenye kilele cha mlima ule na sokwe yule akaniweka chini huku akionekana kuchoka sana! wenzake wakawa wamefika kisha nikabebwa na kuwekwa mgongoni mwa sokwe mwingine ambaye naye alitangulia kama ambavyo alifanya yule aliyenibeba mwanzo na safari ikaendelea!..

tulienda mbele kidogo kisha tukaanza kushuka mlimani!.

upande huu wa mlima ulikuwa mrahisi kushuka kwani kulikuwa na ngazi za kushuka kuelekea chini!.

safari ikaendelea nikiwa mgongoni mwa sokwe yule huku hali yangu ikizidi kuwa mbaya kutokana na maumivu..

Tukaendelea kushuka mpaka kukaanza kupambazuka, na kwambali nikaanza kuuona mji!..

kazi ya kushuka ikaendelea!.

mpaka tunafika chini ilikuwa tayari ni asubuhi, hata jua lilikuwa limetoka, nilikadiria kuwa ilikuwa majira ya saa mbili!.

Safari ikaendelea tukifuata njia ambayo ilikuwa ikielekea ulipo mji ambao kutokea kilimani niliona haukuwa mbali sana!..

na kweli baada ya muda mfupi tu tukawa tunakatiza kwenye nyumba za watu ambao walikuwa wakishangazwa na ujio wetu wakawa wanaitana na kukimbia wakitufuata nyuma!.

safari ikaenda kukomea kwenye nyumba kubwa kuliko nyingine zote ambazo niliziona, ikiwa imezungushiwa uzio mkubwa wa miti na kuacha eneo kubwa sana mbele ya nyumba ile!..

nikashuswa chini kwenye uwanja wa nyumba ile..

watu wote wakaja kunizingira wakinishangaa bila kusoma neno!.

watu wale walionekana kuwa na afya mbovu huku wakionekana kama ambao wamechoka sana!..

mara akatoka mzee sana ndani ya nyumba ile na kuja mpaka nilipokuwa watu wakimpisha njia! akanitizama kwa muda kisha akasema "muingizeni ndani" aliagiza mzee yule na kazi hiyo ikafanyika mara moja, nikabebwa na watu wale wasio na afya ya kuridhishwa na kupelekwa ndani ambapo nililazwa kwenye kitanda cha kamba, nikavuliwa nguo zote na kupakwa aina fulani ya mafuta ambayo yalikuwa ya moto sana kiansi kwamba nilikuwa nikitoa kelele ya maumivu wakati zoezi lile likiendelea!.

nikatokwa na jasho jingi sana, lakini baada ya muda mfupi maumivu yalinipungua, nikaachwa pale kitandani nikipumzika na hatimaye nikapitiwa na usingizi..



nilipokuja kuamka nikainuka kitandani na kuelekea pembeni ambapo niliona nguo zangu zikiwa zimetundikwa kwenye kamba kwa nia ya kuzivaa lakini nilihisi bado nilikuwa na maumivu ya kiuno!..

nikaanza kuangaza huku na huko ndani ya chumba kile kujaribu kuona kama naweza kuupata mkoba wangu na kweli nikafanikiwa kuupata, nikaufungua na kuchukua dawa ile ya majani na kuitafuna kisha kuanza kujipaka maeneo ambayo nilikuwa na maumivu!..

kama kawaida ya dawa ile nikahisi maeneo yale yakiwaka moto lakini ndani ya muda mfupi mno nikawa nimepona.

ITAENDELEA

BURE SERIES
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom