Simulizi: Mke Wangu Juliana

Sehemu ya 43

Akawa na uhakika wa kumuona kila siku, moyo wake ulikuwa na furaha tele, alijisogeza kwa msichana huyo kiasi kwamba wakawa karibu mno na kila siku muda wa kwenda nyumbani, ilikuwa ni lazima amchukue John na kumpeleka mpaka Mwanga na kurudi zake nyumbani kwani hapakuwa mbali na mahali alipokuwa akiishi.

“Ulifanyaje mpaka kufanikiwa hivi?” aliuliza John.
“Ni kufanya kazi kwa bidii tu ila nitahitaji kufanya biashara zangu pia,” alijibu msichana huyo.

“Biashara gani? Inamaanisha mshahara hautoshi?” aliuliza John.
“Mshahara hauwezi kutosha! Na huwezi kufanikiwa kwa kutegemea pesa ya mshahara tu!” alijibu msichana huyo.

“Unamaanisha nini?”
“Ushasikia mtu amekuwa tajiri kwa kulipwa mshahara tu?”
“Hapana!”
“Basi ni lazima tuwe na biashara zetu, yaani lazima uwe na vyanzo vingi vya kuingiza mapato!” alisema msichana huyo.

“Oh!”
“Ndiyo hivyo!”
“Nashukuru kwa kunifumbua macho!”
“Na kwa nini umeacha biashara yako?”
“Ni kwa sababu ninahitaji kuajiriwa!”
“Unahisi utaingiza pesa nyingi kuliko kuuza samaki?”

“Hapana! Ila sitokuwa nazurura sana, inachosha, mwisho nigongwe na gari nife!” alisema John, wote wakaanza kucheka.
“Ila ungebaki kwenye biashara ingekuwa safi sana!” alisema Deborah.

“Najua ila kuna jingine kubwa!”
“Lipi?”
“Nilihitaji kuwa karibu na wewe!”
“Kuwa karibu na mimi?” aliuliza Deborah huku akionekana kushtuka.

“Ndiyo!”
“Kwa sababu gani?”
“Nakupenda!”
“Umesemaje?” aliuliza Deborah huku akipunguza mwendo wa gari!

“Ninakupenda!”
“Mimi?”
“Ndiyo!” alijibu msichana huyo, akasimamisha gari kabisa na kumwangalia John.
 
Sehemu ya 44

Deborah akabaki akimwangalia John, hakuelewa alichokuwa amekizungumza, wakati mwingine alihisi kama mwanaume huyo alikuwa akimtania.

Alimwangalia usoni, alionekana kumaanisha kile alichomwamia. Haikumuingia akilini mwake, ilikuwaje amwambie alikuwa akimpenda? Alimchukulia kama mfanyakazi mwenzake lakini pia kwa muonekano wa mwanaume huyo, hakustahili hata nusu kuwa naye.

“John!” aliita Deborah huku akimwangalia usoni, kwa kiasi fulani John akaonyesha kutokujiamini.

“Naam!” akaitikia.
“Umesemaje?” aliuliza.
John akabaki kimya, si kwamba Deborah hakusikia alichoambiwa, alikisikia sana ila alihitaji kuona ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa akijiamini kumwambia neno lile lile tena na tena.

John akavuta pumzi, alimwangalia Deborah, uzuri wa msichana huyo uliendelea kumchanganya zaidi. Kubaki kimya pasipo kurudia neno lile ungeonekana kuwa udhaifu mkubwa, kama kweli alikuwa akijiamini ilikuwa ni lazima amwambie tena.
“Ninakupenda!” alisema.
“Unamaanisha ama?” aliuliza.

“Deborah! Najua unahisi ni utani kwa sababu tu muonekano wangu na wako ni vitu viwili tofauti. Nimetamani nikwambie hiili kwa kipindi kirefu mno, nimetokea kukupenda tangu siku ya kwanza nilipokutia machoni mwangu, hicho ni kitu ambacho siwezi kukaa kimya huku kikinifurukuta moyoni mwangu,” alisema John huku akimkazia macho msichana huyo.

“Hapana!”
“Unamaanisha nini? Kwamba hunitaki?”
“Simaanishi hivyo!”
“Unamaanisha nini?”
“Natakiwa kupata muda wa kufikiria sana kuhusu hilo, si unajua mambo ya uhusiano si ya kukurupuka,” alisema Deborah.

John akashusha pumzi, siku zote aliamini kwa mwanamke yeyote ambaye alimpa muda mwanaume wa kujifikiria, asilimia tisini na tisa walikuwa wakikubaliana na kilichosemwa ila hawakutaka kuwajibu haohapo.

Moyo wa John ukaburudika, akajisikia amani moyoni mwake, mapenzi aliyokuwanayo kwa msichana huyo yalizidi kuongezeka hivyo baada ya kumaliza wakaendelea na safari.
Wakafika nyumbani kwao, akateremka na kuagana naye kisha kuingia ndani.

Akajilaza kwenye godoro lake, moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida, kila kitu kilichotokea kilionekana kama ndoto fulani ambapo baada ya muda angeamka na kujikuta akiwa kitandani.
 
Sehemu ya 45

Huo ndiyo ulikuwa mendelezo wa ukaribu wao, kila walipokuwa wakikutana maneno ya John yalikuwa yaleyale kwamba alimpenda sana Deborah.

Alimsifia kwa mambo mengi, uzuri na mambo mengine ambayo yalimfanya msichana huyo kuwa na furaha tele. Ni kweli kwenye maisha yake aliwahi kukutana na wanaume wengi wa tofauti lakini hakuwahi kukutana na mwanaume aliyekuwa na maneno matamu kama huyo.

“Una macho mazuri sana, Mungu amekupendelea kwa kila kitu,” alisema John huku akimwangalia Deborah aliyekuwa akitabasamu tu.

“Kuna mambo mengi ambayo Mungu akitupa uhuru wa kuchagua tunaweza kuyachagua, ila kwangu, hakika nitakuchagua wewe maisha yangu yote,” alisema John.

“Kwa nini?”
“Kwa sababu u mzuri, umekamilika, msichana uliyeufanya moyo wangu kukamilika kabisa. Nitakapokuwa na wewe sitohitaji kitu kingine zaidi ya mapenzi yako.

Kama nitahitaji mwanamke mwenye sura nzuri, basi ni wewe, mwanamke mwenye umbo zuri, basi ni wewe na kama nitahitaji mwanamke mwenye tabasamu pana la kutibu magonjwa yote, basi sitosita kukuchagua wewe,” alisema John, hapohapo akaushika mkono wa Deborah.
“Ninakupenda!” alisema.

“Naelewa John.”
“Natamani uingie moyoni mwangu uone ni kwa jinsi gani ninakupenda. Unanifanya nijione kuwa mwanaume niliyekamilika kuwa na wewe,” alisema John.

Wakati huo waliokuwa wakiongea walikuwa kwenye mgahawa wa ofisini kwao. Kila mmoja aliyekuwa akiingia humo walikuwa wakiwaangalia.

Hawakuamini kama msichana mrembo kama alivyokuwa Deborah alikuwa akizingumza na John kwa ukaribu ule, yaani kijana yule ambaye ni mfagiaji tu hapo, masikini, choka mbaya ndiye aliyekuwa akimfanya Deborah kutabasamu namna ile.

Walishangaa lakini hawakujua ni maneno matamu kiasi gani aliyokuwa akiambiwa mahali hapo. Walikaa mpaka baada ya kumaliza kula chakula ndipo wakaondoka kuendelea na kazi zao kama kawaida.

Deborah hakuwa na presha ya kumwambia John kama alikubaliana naye ama la! Moyo wake ulikuwa na maswali mengi juu ya kijana huyo.
 
Sehemu ya 46

Ni kweli alihisi kabisa kuwa na hisia naye za kimapenzi lakini hakujua kama alitakiwa kuwa naye ama la. Kwa muonekano wa harakaharaka John alikuwa na kila sifa ya kuwa naye lakini katika maisha halisi hakustahili hata kuwa naye.

Walikuwa watu wawili tofauti, hawakufanana, alikuwa na pesa, alipendeza, alipenda maisha mazuri lakini kila alipomwangalia John alikuwa mwanaume tofauti kabisa, masikini, asiyekuwa na kitu.

Japokuwa alikuwa na pesa lakini yeye kama mwanamke alihitaji kutumia pesa za mwanaume wake.

Huyo John mshahara aliokuwa akilipwa ulikuwa chini mara nne ya alivyokuwa akilipwa, hata kama siku angemwambia nitoe mtoko wa usiku, basi asingeweza kugharamia kitu chochote kile.

“Lakini mapenzi si pesa,” alisema Deborah huku akionekana kujifikiria sana chumbani kwake.

“Mwanaume anaweza kuwa na pesa, akakupa na ukatumia maisha yako yote lakini bado ukakosa mapenzi,” alijisemea.
Siku hiyo hakuwa na uamuzi wa moja kwa moja kwamba ni kitu gani alitakiwa kufanya. Moyo wake ulimpenda mno John pasipo kujali hali aliyokuwepo nayo.

Ni kweli hakuwa na pesa, alichokigundua kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa na pesa nyingi lakini hawakuwa na mapenzi hata kidogo.
 
Sehemu ya 47

Kwa kipindi hicho alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni mapenzi na si pesa. Kulikuwa na wanaume wengi waliokuja, waliomchukua na kufanya naye ngono lakini mwisho wa siku walimuacha na kuendelea na maisha yao.

Kwa maana hiyo walikuwa na pesa lakini walikosa mapenzi mioyoni mwao. Huyu wa kipindi hiki aliyekuja katika maisha yake hakuwa na pesa kama hao wengine lakini alibarikiwa kuwa na mapenzi.

Alimpenda, alimuonyesha mapenzi na kuufanya moyo wake kuwa na furaha mno na mwisho wa siku akajisemea basi acha awe naye, kama Mungu hakumbariki pesa basi angembariki siku zijazo, ila yeye alitakiwa kuutekeleza wajibu wake wa kumpenda kama alivyotakiwa kufanya.

Siku mbili mbele akaamua kumwambia John kwamba alikubaliana naye na hivyo kuwa wapenzi.

“Nimekukubalia, ila naomba unisaidie kwa kitu kimoja,” alisema Deborah huku akimwangalia John.

“Lolote utakalo mpenzi wangu!”
“Utanipenda maisha yako yote!”
“Huo ni wajibu wangu, nitakupenda zaidi ya ninavyokupenda sasa hivi!” alisema John.
“Kweli unaniahidi?”

“Bila shaka mpenzi! Nitakupenda hata kama sitokuwa na kitu!” alisema John na kutoa tabasamu, hakuishia hapo, akambusu msichana huyo shavuni, ukurasa mpya wa mapenzi ukafunguliwa baina ya watu hao wawili.
.
.
Je, nini kitaendelea?

Tukutane week ijayo.....
 
Shunie,
Werawera, mtandale kashinda, maskini Juliana, anyway ngoja tuone itakuwaje manake Juliana halili usingizi sababu ya John
 
Miaka kama miwili Hivi iliopita nilikua napenda sana hizi simulizi lakini saivi sijui hamu imenitokaje kwa kweli yaaan sina hamu kabisaa.

😢😢
 
Back
Top Bottom