Simulizi: Mke Wangu Juliana

Sehemu ya 21.

John hakuwa mzoefu wa mitaa mingi ya Kigoma Mjini hivyo rafiki yake, Jumanne ndiye aliyekuwa akimchukua na kwenda naye huko mitaani kufanya biashara ya kuuza samaki na kurudi nyumbani.

Maisha hayakuwa ya kawaida hata kidogo, kulikuwa na ugumu mkubwa mbele yake, hakukata tamaa, aliamini kuna siku moja angefanikiwa kama watu wengine, na inawezekana kabisa angeweza hata kuagiza gari kutoka Japan na kuliendesha katika mitaa hiyo.

Alipenda kujifunza kwa watu waliokuwa wamefanikiwa zaidi yake, aliamini kwa kufanya hivyo kungemfanya kuwa tofauti na watu ambao hawakuwa wamefanikiwa au hata kutokuwa na ndoto zozote zile za kufanikiwa mbele ya safari.

Alikuwa akitoka nyumbani alfajiri sana na alipokuwa akichukua samaki na kwenda kuwauza, mpaka majira ya saa sita mchana alimaliza na hivyo kutafuta sehemu zilizokuwa na watu waliokuwa wakiweka mijadala mbalimbali na kuanza kusikiliza.

Moyo wake ulikuwa na kiu kubwa ya kufanikiwa, hakutaka kujiona akibaki hapo alipokuwa miaka yote na ndiyo maana alijaribu kuwafuata watu waliokuwa wamepiga hatua na kuwasikiliza kile walichokuwa wamekifanya mpaka kuwa hapo walipokuwa.

Hapo Mwanga, kulikuwa na mzee aliyeitwa Miraji, huyu alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiishi maisha mazuri. Alikuwa na nyumba nzuri, magari ya kifahari na alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiishi kama wafalme katika mtaa huo wa uswahilini.

Nyumbani kwa mzee huyo kulikuwa na bomba la maji, watu ambao hawakuwa na mabomba nyumbani kwao walipendelea kwenda hapo na kuchota maji hayo.

Kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa, mara nyingi alikuwa akikaa yeye na wakati mwingine walikuwa watoto wake.
Kila alipomwangalia mzee huyo, alipata picha ya mtu aliyekuwa amefanikiwa.

Kwa muonekano tu aliokuwanao hakuwa kama watu wengine, alionekana kuridhika na kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake.

Alihitaji kumsikia akizungumza naye kuhusu mafanikio, alitamani kuweka nae ukaribu ili apate kile alichokuwa akikihitaji wakati huo.
 
Sehemu ya 22.

Alikwenda kuchota maji siku ya kwanza, ya pili na ya tatu ndipo alipoanza kuzungumza na mzee huyo. Mara ya kwanza aliposikia lafudhi yake, mzee huyo akagundua John alitoka jijini Dar es Salaam, alimwangalia vizuri kama mtu aliyehitaji kusikia mengi kutoka kwake.

John akakohoa, aliamua siku hiyo kuzungumza na mzee huyo kwani kila siku alikuwa akichota maji na kuondoka, ila kwa siku hiyo alihitaji kujua mengi kuhusu maisha yake kwa ujumla, alivyofanikiwa mpaka kuwa hivyo alivyokuwa.
“Kwa nini unaniuliza hivyo?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia John kwa macho ya kumdadisi.

“Kwa sababu ninataka kujua! Kwa nini umeniuliza kwa kushangaa sana?” alilijibu swali lake, na akauliza swali.
“Ni vigumu sana vijana kuniuliza kuhusu maisha yangu, yaani jinsi nilivyofanya mpaka kufanikiwa!” alijibu mzee huyo.

“Vijana wengi wanakuuliza kuhusu nini?”
“Mabinti zangu tu! Wengi huniambia wanataka kuwaoa!” alijibu mzee huyo na kutoa tabasamu lililomaanisha kwamba vijana hao walimuulizia kuhusu mabinti zake katika hali ya utani tu.

“Hahaha! Mimi ninahitaji kujua zaidi kuhusu njia ulizozitumia mpaka kufanikiwa!” alisema John.
“Zipo nyingi tu! Ila kabla ya yote naomba nikuulize swali?”

“Uliza tu!”
“Umetoka Dar es Salaam mpaka Kigoma kwa sababu gani?”
“Kufanikiwa!”
“Yaani utoke Dar halafu uje Kigoma kisa kufanikiwa tu?”

“Ndiyo! Kwani ni vigumu?”
“Inategemea!”
“Na nini?”
“Malengo yako! Kama kweli umedhamiria, utafanikiwa japo kwa ugumu sana!”
“Kwa sababu gani? Mbona wewe umefanikiwa ukiwa Kigoma?”

“Nilikuwa na akili ya ziada, nilijitoa kwa kufanya kazi kama mbwa!”
“Na mimi ndicho ninachotaka kufanya!” alisema John.

Walikuwa wakizungumza kuhusu mafanikio, muda mwingi John aliuliza maswali yaliyomfanya mzee huyo kugundua alikuwa akizungumza na mtu aliyekuwa na akili ya ziada.

Waliongea mambo mengi, alimfundisha mambo mbalimbali lakini kwenye hayo yote yalibebwa na kitu kimoja kilichosema ili afanikiwe ilikuwa ni lazima afanye kazi kwa bidii.
 
Sehemu ya 23.

Mafanikio haikuwa bahati, hakuna mtu aliyefanikiwa kwa bahati. Kufanikiwa si kama kucheza bahati nasibu, ili ufanikiwe ilikuwa ni lazima upambane, ujinyime kwa kufanya mambo mengi ya anasa na mwisho wa siku kupata kile ulichokuwa ukikihitaji.

Ukimuona mtu amefanikiwa, haimaanishi alibahatika, hapana, kufanikiwa ilikuwa ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii, yaani ni sawa na kufaulu mitihani ilikuwa ni lazima usome, huwezi kusema husomi halafu mtihani wa mwisho ufaulu, hakuna kitu kama hicho.

Hiyo ndiyo ilikuwa ni sawa na mafanikio. Wakati mzee huyo akisema hayo yote John alikuwa kimya akimsikiliza kwa makini kana kwamba mwisho wa siku kulikuwa na maswali angeulizwa.

Mzee huyo aliongea kwa dakika zaidi ya arobaini na baada ya hapo, akajiinua kutoka kwenye kiti na kuanza kuelekea ndani pasipo kuaga.

“Umeongea mengi sana, mwisho kabisa unaondoka bila kuniaga!” alisema John huku akitabasamu kwa mshangao.

“Nakuja! Unajua kusoma?”
“Ndiyo!”
“Kiingereza unakijua?”
“Hapana!”

“Hata kidogo?”
“Ndiyo! Sijui hata kidogo!”
Mzee Miraji akatoa tabasamu na kuingia ndani.

John akabaki mahali hapo huku akiangalia jinsi watu walivyokuwa wakiendelea kuchota maji. Aliona namna wengi wao walivyovaa, walionekana kutokuwa na maisha mazuri kabisa, inawezekana yeye alikuwa na maisha mabovu lakini kulikuwa na wengine walikuwa na maisha mabovu kushinda yeye.

Baada ya dakika kadhaa mzee Miraji akarudi akiwa na kitabu mkononi mwake, akamsogelea John na kumkabidhi, kitabu hicho kiliandikwa Rich Dad Poor Dad kilichoandikwa na mwandishi aitwaye Robert Kiyosaki.
“Kiingereza sifahamu!” alisema John haraka sana baada ya kuona kava.

“Umeniambia! Ila hicho kimeandikwa kwa Kiswahili. Unajua hapa Tanzania tuna wahuni wengi sana, wanavichapisha hivyo kwa lugha ya huku na kuuza kisiri,” alisema mzee Miraji, John akakifungua, kweli kiliandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Kinahusu nini?” aliuliza.
 
Sehemu ya 24.

“Ni maisha ya kijana aliyekuwa na baba wa aina mbili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine masikini. Hao watu walikuwa na mawazo mawili tofauti waliyokuwa wakimpa kijana huyo. Kakisome, mwisho wa siku utaibuka na kitu kikubwa sana,” alisema mzee Miraji.
“Nashukuru sana!” alisema John, akasimama na kuaga.

“Ila kumbuka kitu kimoja!”
“Kipi?”
“Kufanya kazi kwa bidii! Usipende kulala, kumbuka usingizi rafiki yake umasikini!” alisema mzee huyo. John akatoa tabasamu na kuondoka zake.

Akafika chumbani kwake, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufungua kitabu kile na kuanza kukisoma, alivutiwa nacho, kwenye kila mstari ambao aliupitia ulikuwa ukimgusa mno.

Alikaa na hicho kitabu kwa siku mbili, alikisoma kwa ufasaha mpaka Jumamosi ambapo akamrudishia mzee huyo, akamwambia alichojifunza na kumuahidi angeyafanyia kazi mambo yote na mwisho kufanikiwa kama watu wengine.

Hilo lilikuwa jambo zuri hivyo akaondoka zake. Siku ziliendelea kukatika na ilipofika Jumapili, asubuhi na mapema akajiandaa na kwenda kanisani, katika Kanisa la TAG Mwanga Msufini ambalo alikwenda siku kadhaa zilizopita.

Aliingia kanisani hapo akiwa mgeni kabisa, kila mtu aliyekuwa akimwangalia, hakumfahamu hata mmoja. Alivalia kawaida, vijana wengi waliokuwa humo walipendeza, walivalia nadhifu na walionekana kuwa na mafanikio makubwa.

Alikaribishwa na mwanamke mtu mzima aliyekuwa mlangoni mwenye cheo cha shemasi na kuonyeshwa kiti alichotakiwa kukaa, akakisogelea na kutulia hapo.

Moyo wake ulifarijika, ilipita miaka mingi hakuwa ameingia kanisa kiasi kwamba aliamini hakuwa akifanikiwa kwa sababu alijiweka mbali na Mungu.

Alitulia kitini hapo, alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, na hata ibada ilipoanza, alitumia muda mwingi kuwa kimya na kuangalia huku na kule.

Ilipofika majira ya saa 3:35 asubuhi, akaanza kusikia watu wakiongea kwa nyuma, akageuka na alipopitisha macho yake, yakatua kwa msichana mmoja mrembo mno, aliyevalia vizuri na kuzibana nywele zake vilivyo.
 
Sehemu ya 25.

Alimwangalia msichana huyo, alishtuka, hakutegemea kumuona ndani ya kanisa hilo. Akaachana na ibada kwanza, aliyagandisha macho yake kwa sekunde kadhaa huku akionekana kama kupigwa butwaa.
Alikuwa Deborah!

Msichana huyo baada ya kuongea na kusalimiana na mwanamke aliyekuwa mlangoni, akaingia ndani.

Uzuri wake ulikuwa tishio, wanaume wakageuka na kumwangalia.
Kila alipokuwa akipita, hapakuwa na utulivu wa macho, watu wengi walikuwa wakimwangalia yeye, alionekana kutokujali, akatafuta kiti na kukaa, kitu cha kwanza kilikuwa ni kusali kwa kumshuruku Mungu kufika salama kanisani hapo.

Muda wote huo John hakuacha kumwangalia msichana huyo. Alikuwa mzuri, aliyevutia lakini alionekana kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu, hakuringia uzuri wake, inawezekana aliringia huko nje lakini ndani ya kanisa, alionekana kuwa mnyenyekevu kupita kawaida.

“Mwanamke mzuri halafu mnyenyekevu kwa Mungu! Sijawahi kuona,” alijisemea John wakati Deborah akisimama na kwenda mbele kabisa na kuanza kucheza pamoja na waimbaji, alicheza bila kujali uzuri wake, mavazi yake, alipokuwa mbele za Mungu, alicheza kadiri awezavyo kama Mfalme Daudi.

Ibada iliendelea, wageni walijitambulisha na watu walipomsikia John ametoka jijini Dar es Salaam, wakahitaji kufahamu mengi kuhusu sehemu hiyo kwani wengi walikuwa wakipasikia tu.

Ibada ilipomaliza, vijana wakamfuata na kumsalimia kwa shangwe, walimkaribisha kwani alisema kuwa amehamia kwenye kanisa hilo, maisha yake yote yangekuwa mkoani Kigoma.

Wakati akisalimiana na washirika wengine, akili yake ilikuwa kwa Deborah, msichana huyo aliuteka moyo wake ghafla sana, alichanganyikiwa, alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kuwa na Deborah.

Labda amuoe! Akaona kuwa jambo gumu kwa sababu kwa jinsi alivyovaa tu ilionyesha kutoka kwenye familia ya kitajiri tofauti na alivyokuwa.

Alimwangalia msichana huyo aliyekuwa akiongea na watu, moyo wake ulivurugika kabisa, alisubiri kufuatwa na Deborah ili aende kumsalimia na kumkaribisha lakini hakupata nafasi hiyo, akaamua kwenda yeye mwenyewe.
 
Sehemu ya 26.

Alipomfikia, akaonyesha tabasamu, naye msichana huyo akafanya hivyohivyo na kumpa mkono kwa lengo la kumsalimia. Walipogusana, John akahisi kama akipigwa shoti moja ya hatari!

“Karibu sana mgeni! Nilisikia umetoka Dar es Salaam!” alisema msichana huyo huku akiachia tabasamu pana.
“Ndiyo! Nimetoka huko!”
“Na umekuja huku kufanya nini? Kutembea?”

“Hapana! Nimekuja kutafuta maisha!”
“Kigoma?”
“Ndiyo! Nimebarikiwa sana na huduma yenu, hakika sijawahi kuiona kwenye makanisa mengi!” alisema John.

“Usijali! Tunapokuwa mbele za Mungu huwa hatutakiwi kujiona kitu, hatutakiwi kuyaangalia mavazi yetu, ni kama ilivyokuwa kwa Mfalme Daudi, mbele za Mungu alicheza mpaka nguo zikamvuta, hakuangalia ufalme wake,” alisema msichana huyo.

“Nimebarikiwa kwa kweli!”
“Oh! Utukufu kwa Mungu!” alisema Deborah, wakapiga stori mbili tatu, msichana huyo akamuaga.

“Ila hujaniambia unaitwa nani!” alisema John.
“Naitwa Deborah!”

“Oh! Asante kwa kukufahamu!”
“Karibu!”
Deborah akasalimiana na watu wengine na kuwachukua wadogo zake, wakaingia ndani ya gari na wazazi wao kisha kuondoka kanisani hapo.

John alibaki akiwa amesimama, aliliangalia gari lilivyokuwa likiondoka machoni mwake. Alitamani kulisimamisha , azungumze tena na Deborah kwani alivurugwa mno.

Huku akiwa kwenye hali hiyo, mara akashikwa bega kwa nyuma, haraka sana akageuka, macho yake yakagongana na ya msichana mmoja aliyekuwa kwenye tabasamu pana, mavazi yake yalikuwa ya kawaida, si kama Deborah.

“Karibu sana mgeni!” alisema msichana huyo huku akimpa mkono.

“Nashukuru sana!”
“Naitwa Juliana!” alisema.
“Oh! Naitwa John!”
“Karibu mpendwa!” alisema msichana huyo huku akiwa na tabasamu.

“Asante sana!” aliitikia na msichana huyo kuondoka, haraka sana akageuka ili aliangalie tena lile gari, lilipotea machoni mwake.
“Deborah! Deborah! Deborah! Nitapambana kwa ajili yako, nifanikiwe na kukutolea mahari!” alijisemea kwa sauti ndogo, moyo wake ukatekwa vilivyo na msichana huyo.

.
.
Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 27

John alichanganyikiwa, akili yake iliruka, hakuamini kama angekutana na msichana aliyekuwa mrembo wa sura kama alivyokuwa Deborah.

Moyo wake ni kama ulipigwa ganzi, sura ya msichana yule iliendelea kukisumbua kichwa chake. Alibaki kanisani akiongea na watu wengine lakini akili yake haikuwa hapo kabisa.

Alitamani kuuliza kuhusu msichana huyo zaidi, alihitaji kufahamu mahali alipokuwa akiishi, aende kuzungumza naye na kumwambia alikuwa mzuri lakini alishindwa kufanya hivyo.
Alikaa kanisani kwa dakika kadhaa kisha kurudi nyumbani.

Sura ya Deborah iliendelea kuwa kichwani mwake, alipaangalia Kigoma, alimkumbuka msichana yule, moyoni alijiambia kabisa hakustahili kuishi huko, alitakiwa kwenda kuishi jijini Dar es Salaam katika mtaa wa watu wenye pesa, Osterbay.

Njia nzima ya kwenda nyumbani aliendelea kumfikiria msichana huyo, alikuwa na mawazo mengi mno mpaka alipofika nyumbani ambapo akajifungia chumbani kwake.

Alitulia humo kwa dakika kadhaa, akachukua kitabu chake ambacho alikuwa na kazi ya kuandika kila kitu kilichokuwa kikiendelea (diary) na kuandika kuhusu msichana huyo.

Jumapili, 14/08/2016: Nilimuona msichana mrembo wa sura, nikampenda, ni msichana wa aina yake ambaye ninaamini ni lazima siku moja atakuja na kuwa mke wangu wa ndoa. Kwa jina anaitwa Deborah.

Baada ya kuandika hivyo, akatulia chumbani hapo mpaka jioni ambapo akatembeatembea na usiku ulipoingia akaingia chumbani na kulala.

Asubuhi ilipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumkumbuka Deborah, hakuacha kuchanganyikiwa, alitamani siku hiyo amuone tena lakini hakujua ni mahali gani alipokuwa akiishi.

Alfajiri hiyo akaondoka na kuelekea Kibirizi kuchukua samaki na rafiki yake, Jumanne. Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu maisha huku kwenye kila neno alilokuwa akizungumza Jumanne alimsisitizia ni lazima awekeze sana na kuachana na wanawake.

“Mimi sipendi wanawake!” alisema John.
“Ni vizuri sana kama ndiyo hivyo, utafanikiwa!”

“Ila nampenda mwanamke mmoja tu!” alisema.
“Mwanamke gani?”
“Anaitwa Deborah!”
“Yupo Dar?”
 
Sehemu ya 28

“Hapana! Nilimuona jana kanisani!” Jumanne akasimama na kumwangalia rafiki yake, ni kama alimshangaa sana, hapohapo akaanza kutoa kicheko kikubwa na kumpigapiga begani mwake.

“Rafiki yangu! Hawa mademu wasikuchanganye sana,” alisema Jumanne huku akimwangalia John na kuendelea kucheka.

“Ila ninataka kumuoa!”
“Kwani yupo vipi?”
“Ni mrembo! Halafu anaonekana ana pesa sana,” alijibu.
“Ana pesa?”
“Ndiyo!”

“Sasa atakukubali muuza samaki?”
“Ushaanza kunishusha sasa!”
“Si hivyo! Unajua hawa mademu wa sasa hivi wanapenda sana pesa!” alisema Jumanne.
“Ila yule ameokoka!”

“Nani kakwambia waliookoka hawapendi pesa? Kuna wachungaji matapeli kichizi,” alisema Jumanne.

“Kwa hiyo nifanyeje?”
“Umempenda kweli?”
“Sana tu!”
“Basi mwambie!”
“Mh!”

“Usigune! Mfuate na umwambie ukweli! Au unaogopa?”
“Sikuwahi kuzungumza naye ujue, yaani tulisalimiana tu!” alisema John huku akimwangalia rafiki yake huyo.

“Haijalishi! Mfuate na uzungumze naye!”
Wakafika Kibirizi, wakachukua samaki na kwenda kutembeza kama kawaida yao. Siku nzima kichwa cha John kiliendelea kumfikiria Deborah, alitamani kumtafuta na kumwambia kama alivyoambiwa na Jumanne lakini alishindwa kufanya hivyo.

Alijipa moyo kwamba inawezekana Jumatano msichana huyo angekuwepo ibadani hivyo siku hiyo ilipofika, akaelekea kanisani jioni. Muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule, kila aliposikia mtu akiingia kanisani, aligeuka na kuangalia.

Deborah hakufika kanisani, alichanganyikiwa lakini alijipa moyo kwamba ilikuwa ni lazima ajue mahali msichana huyo alipokuwa akiishi ama kufanya kazi.

Ibada ilipokwisha, akasalimiana na washirika wenzake, akamfuata kijana mmoja ambaye kidogo alizoeana nae na kuanza kumuuliza kuhusu Deborah.

“Yupo vipi?”
“Ni mweupe kidogo, anapendeza, alikuja na familia yake na kuondoka nayo kwa gari,” alijibu John.

“Unamzungumzia Deborah!”
“Yeah! Halafu ndiye yeye bwana! Sijui kwa nini sikukutajia jina lake!” alisema John na kuanza kucheka.
“Amefanya nini?”
“Kwani anaishi wapi?”
“Mji Mwema!”

“Mji Mwema! Kule ushuani?”
“Yeah! Anafanya kazi kwenye kampuni ya kusindika samaki!” alijibu kijana huyo.
“Oh! Sawa! Mji Mwema sehemu gani?”
“Unazijua kota za Posta?”
 
Sehemu ya 29

“Ndiyo!” alijibu japokuwa hakuwa akizijua.
“Basi kwenye kota zile, nyumba ya juu! Zamani walikuwa wakiishi Wakongoman, hapo ndipo anapoishi!” alisema kijana huyo.
“Kumbe ni pale?”

“Yeah!”
Alielekezwa, akaridhika na siku iliyofuata huku akiwa na kapu lake la samaki akaanza kwenda huko Mji Mwema. Alipitia njia ya makaburi ya Mwanga, akatokea Mtaa wa Game ambapo akaunganisha mpaka kwenye barabara iliyokuwa ikielekea Mji Mwema na kuanza kupandisha kilima kidogo.

Majumba yaliyojengwa huko yalimdatisha kupita kawaida, alibaki akiyaangalia, yalivutia machoni mwake. Alipandisha na nyia hiyo mpaka kwenye kota tatu za Posta ambazo zilikuwa zimezungushiwa fensi ya seng’enge na kuziangalia.

“Niliambiwa kwa juu! Kwa hiyo ili kufika upande wa pili inabidi nipitie na hii barabara mpaka huko!” alijisema na kuanza kuifuata narabara ya upande wa kulia, mbele kidogo akapandisha ya upande wa kushoto na kuachana na ile iliyokuwa ikielekea jeshini na kuunganisha mpaka Bangwe kulipokuwa na nyumba ya mkuu wa mkoa.

Akapandisha juu mpaka alipokutana na njia panda ambapo akakata kushoto na kukutana na nyumba kadhaa zilizoonyesha kumilikiwa na watu wenye pesa.

Aliifuata nyumba ya kwanza, alipofika getini, akaanza kugonga, wala hazikupita sekunde nyingi, mlango ukafunguliwa na mlinzi mmoja aliyekuwa na bunduki yake kubwa.
“Samahani!” alisema mara baada ya salamu.
“Bila samahani!”

“Hapana ni kwa akina Deborah?” aliuliza huku akimwangalia mlinzi huyo.
“Hapana! Ni nyumba hiyo inayofuata!” “Sawa.”

Akatoka na kwenda katika nyumba hiyo, alipofika, akagonga hodi, geti likafunguliwa na mlinzi na kuanza kuzungumza naye. Alimuulizia Deborah, akaambiwa hakuwepo.
“Yupo nani?” aliuliza.

“Mfanyakazi na mama yake!”
“Sawa! Aliniambia nilete samaki hapa!”
“Nani?”

“Deborah! Nimetoka kazini kwake akasema nilete hapa,” alisema John.
“Sawa! Ngoja nimuite dada wa kazi!” alisema mlinzi na kuondoka.

Baada ya dakika mbili, akarudi akiwa na mfanyakazi aliyekuwa na sufuria ndogo, akamwambia kama alivyomwambia mlinzi na kisha kumpa samaki wadogo na kisha kuondoka zake.
 
Sehemu ya 30

Alijihesabia hasara lakini hilo hakutaka kulitia akilini kabisa, alichokuwa akihitaji ni kuwa na huyo Deborah tu. Aliendelea na biashara zake na alipomaliza, akarudi zake nyumbani na kuendelea na ratiba zake nyingine.

*** Deborah alikuwa kazini kwake akiendelea na kazi yake kama kawaida. Alikuwa na furaha tele kwa sababu barua za kuongezwa mishahara zilifika ofisini na hivyo kusaini mkataba mwingine.

Muda wote moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli dau lake lilipanda na hivyo kuyafanya maisha yake kuwa mazuri zaidi.

Alifikiria mambo mengi lakini kubwa zaidi lilikuwa ni kujenga nyumba yake mwenyewe. Baba yake alimpa zawadi ya kiwanja kilichokuwa hukohuko Mji Mwema na kitu ambacho alitakiwa kufanya ni kujenga nyumba yake tu.

Huku akiendelea na kazi yake, akaona simu yake ikiita, haraka sana akaichukua na kuangalia kioo, alikuwa mama yake, akaachia tabasamu na kuipokea.

“Mama huwezi kuamini!” alisema Deborah hata kabla ya salamu.
“Kuna nini tena?”
“Eti tumeongezewa mishahara!” alisema huku akionekana kuwa na furaha.

“Ndiyo maana ukatuagizia samaki, tule tujidai?” aliuliza mama yake.
“Kuwaagizia samaki?”
“Ndiyo! Si umemwambia muuza samaki alete samaki hapa nyumbani?” aliuliza mama yake.
“Mimi?”

“Ndiyo!”
“Hapana mama!”
“Ila muuzaji alisema umemuagiza, na kawaacha hapa ndiyo tunawatengeneza!” alisema mama yake.
“Oh! Samaki? Yeah! Nilimwambia awalete, kumbe aliwaleta?”

“Ndiyo!”
“Sawa mama! Kesho nitaagiza wengine,” alisema na kisha kukata simu.
Akaanza kujifikiria, alimwambia mama yake kwamba kweli alimwagiza mtu apeleke samaki lakini ukweli ni kwamba hakufanya hivyo.
 
Sehemu ya 31

Alijifikiria ni mtu gani alimwambia muuzaji apeleke samaki nyumbani kwao lakini akashindwa kupata jibu.
Alikaa kwa dakika nyingi akiwa na mawazo ndipo akahisi inawezekana mtu aliyemtuma muuza samaki apeleke samaki nyumbani kwao alikuwa akimtaka.
“Huu uzuri huu! Yesu nisaidie!” alisema Deborah.

Alifanya kazi mpaka jioni, akarudi nyumbani na kuendelea na mambo yake. Bado suala la muuza samaki lilimsumbua moyo wake, alijifikiria sana na kusubiri kama angeona namba ikimpigia na kumwambia kuhusu suala la samaki lakini hapakuwa na simu yoyote iliyoingia.

“Sasa atakuwa nani? Mh! Hawa wanaume wana shida sana,” alijisemea na kuanza kucheka, jambo la samaki akaamua kulipuuzia.

*** Juliana alikuwa na shida nyingi, matatizo mngi ya kifamilia, yalimsononesha na kumkata maini lakini hayo yote hayakumfanya kuacha kumfikiria mwanaume ambaye alimuona kanisani, John aliyetoka jijini Dar es Salaam.

Moyo wake ulimpenda mara ya kwanza tu alipomuona, alisalimiana naye na alipogusana naye mikono, alihisi hali ya ajabu ikiwa imepita mwilini mwake.

Alihisi huyo ndiye ambaye angekuja kuwa mume wake wa baadaye, alikuwa na hisia hizo lakini hakujua ni kwa namna gani angezibadilisha hisia hizo na kuwa kweli.

Alitoka jijini Dar es Salaam, bila shaka alikuwa na pesa za kutosha. Hakutaka kuangalia pesa, alichokuwa akikiangalia ni penzi lake moyoni mwake, amuoe na hatimaye kuishi naye mpaka kifo chake.

Hakujua alikuwa akiishi wapi lakini aliamini angezidi kumuona zaidi kwa kuwa alisema hapo Kigoma alihamia na angeishi maisha yake yote.

Alitamani kumwambia mama yake juu ya mwanaume huyo lakini alishindwa, kwanza angeanzia wapi, angemwambiaje ili apate kueleweka na kuonekana mtu aliyekuwa akijielewa.

Ikambidi anyamaze tu, hivyo kuendelea na maisha yake. Hali ilikuwa mbaya nyumbani kwao, hawakuwa na nafuu hata kidogo, kila siku kupata ilikuwa majaliwa lakini kukosa ilikuwa ni kawaida sana.
 
Sehemu ya 32

Waliteseka, hawakuwa na kimbilio jingine lakini kila siku mama yake aliamini kuna siku wangefanikiwa, wangekuwa na maisha mazuri kama waliyokuwanayo watu wengine.

Hakuacha kuwaambia hivyo watoto wake, Juliana alimuunga mkono lakini kila alipoangalia mbele, hakuona dalili za kuwa na maisha hayo hata kidogo.

Alikubaliana na mama yake kwa sababu tu hakutaka kumkatisha tamaa lakini ukweli ni kwamba moyo wake haukuamini hata kidogo.
Siku ziliendelea kukatika, maisha yaliendelea kuwa mabovu kiasi kwamba hata ada ya mtoto ilikosekana na hivyo kurudishwa nyumbani kwanza.

Hilo lilionekana kuwa pigo kwa familia nzima, walikuwa na mawazo lakini hawakutaka kukata tamaa, waliendelea kufanya biashara ndogondogo ya mboga za majani sokoni kwani ndicho kitu walichokuwanacho kipindi hicho.

“Juliana! Unajua nakupenda sana,” alisikika mwanaume mmoja, alikuwa mwanaume mwenye umri wa miaka thelathini, aliyekuwa akijiheshimu, maisha mazuri, alikuwa na kila kitu kilichomfanya kuonekana mwanaume mwenye mafanikio.

Alikuwa na pikipiki tatu alizowapa vijana ambao kazi yao ilikuwa ni kumpelekea pesa ya hesabu kila Jumapili. Hakuwa na shida hata kidogo, alikuwa na kila kitu alichokihitaji.

Mwanaume huyo aliitwa Sangiwa Machebe. Alikuwa kijana mtanashati ambaye alipendwa na wasichana wengi kwa kuwa maisha yake yalikuwa ni ya mafanikio makubwa.

Alipapatikiwa na kila mtu lakini kwake mtu aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote alikuwa huyo Juliana. Alijitahidi kumnunulia zawadi nyingi, kumwambia kwamba alikuwa akimpenda lakini msichana huyo hakutaka kuelewa kabisa.

Hilo lilimuumiza Sangiwa, alihitaji kuyabadilisha maisha ya msichana huyo lakini yeye mwenyewe alionekana kutokuwa radhi kukubaliana naye.

Kila siku aliambiwa kwamba moyo wake haukuwa kwake, ni kweli alikuwa na mafanikio makubwa lakini kwa msichana huyo alionekana kuwa si lolote lile.

“Juliana! Kwani tatizo nini?” aliuliza Sangiwa huku akimwangalia msichana huyo.
“Ni kwamba moyo wangu haupo kwako!” alijibu kwa sauti ya upole.

“Upo wapi sasa?”
“Sijajua kabisa.”
“Kwa mwanaume mwenye pesa kuliko mimi?” aliuliza.
“Hapana!”
“Mwenye elimu kuliko mimi?”
 
Sehemu ya 33

“Hapana Sangiwa!”
“Au mwenye kazi nzuri kuliko mimi?” aliuliza tena.

“Sangiwa! Naomba unielewe tu kaka yangu, nitaendelea kukuheshimu kama kaka yangu!”
“Kaka yako?”

“Ndiyo! Sangiwa naomba unielewe! Kuwa na wewe halafu moyo wangu ukawa haupo kwako, unahisi ni kitu kizuri?” aliuliza msichana huyo.
“Ila si unaweza hata kunipenda mbele ya safari! Ninahitaji kuwa nawe,” alisema Sangiwa, kwa jinsi alivyokuwa akionekana usoni, alimaanisha alichokuwa akikisema.

Hilo halikukubalika kwa Juliana, ni kweli Sangiwa alikuwa na maisha mazuri, kila kitu ambacho kilihitajika kwa mwanamke yeyote yule lakini jambo la ajabu kabisa, kwa msichana huyo hakuwa moyoni mwake hata kidogo.

Wanawake wengi walijua ni kwa namna gani Sangiwa alimpenda Juliana, waliona wivu, walimshangaa msichana huyo, walitamani kumshawishi akubaliane naye lakini kwa Juliana lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo.

Mama yake alifahamu hilo lakini hakutaka kumuingilia binti yake, aliamini msichana huyo alikuwa na uhuru wa kumchagua mwanaume yeyote wa maisha yake lakini si kumlazimisha awe na mtu fulani kwa kuwa alikuwa na pesa.

Alimsisitizia kila siku Juliana kwamba mwanaume ambaye angekubali kuwa naye basi awe amempenda kwa moyo wake, na si kumpenda kwa sababu ana kitu fulani katika maisha yake.

“Kama si chaguo lako, achana naye,” alisema mama yake, alikuwa akimzungumzia Sangiwa.
“Najua mama! Ila ananing’ang’ania sana!”
“Hata akisema nini, hutakiwi kwenda kinyume na moyo wako! Binti yangu hebu sogea hapa,” alisema mama yake na kumtaka asogee. Akaendelea:

“Mungu amekuandaliwa mume mwema maishani mwako, ni lazima ujue moyo wako unahitaji nini, kama mtu hayupo, usiyalazimishe mapenzi kwani kuna wengi wanajuta mpaka leo hii.

“Kuna wanawake wanalia kwenye ndoa, waliangalia pesa, umaarufu, vikawadanganya, hawakufuata mioyo yao, tamaa iliwaingia na wakati mwingine wanajuta kwa nini wapo kwenye ndoa,” alisema mama yake na kuendelea.
 
Sehemu ya 34

“Ni lazima ujue kila mwanamke unayemuona hapa duniani, Mungu amemuandalia mume mzuri ambaye utaishi naye kwa upendo na amani maisha yako yote, hata mkigombana, mtakuwa wepesi mno kusameheana na kusahau mliyotendeana, ila ukijilazimisha kumfuata fulani kisa pesa, kuna siku utalia na kujuta maisha yako yote,” alisema mwanamke huyo.

Maneno ya mama yake yakaingia moyoni mwake, yakamjenga na kurudi nyuma kutoka kwa Sangiwa. Yalimfungua na kumshukuru kwani alihisi endapo angemkubali mwanaume huyo, kuna siku isiyokuwa na jina angekuja kuumia mno moyoni mwake, na inawezekana matatizo yakawa makubwa mpaka kujimaliza, hivyo hakutakiwa kuwa na haraka.

Hapo, alitamani kumwambia mama yake kuhusu huyo John ila hakujua ni kwa namna gani angemuanza. Alihisi mama yake angemwambia kwamba kwa sababu alitoka jijini Dar es Salaam ndiyo maana alimpenda kumbe haikuwa hivyo.

Hakutaka kumwambia kwa wakati huo lakini alijiahidi kwamba siku moja ilikuwa ni lazima kumwambia kuhusu moyo wake, jinsi ulivyompenda mwanaume huyo ambaye hakujua aliishi wapi, alichokijua ni kwamba alikuwa akisali naye kanisa, hilo tu.

.
.
.
Je, nini kitaendelea?
 
Asante sana shunie. Hadithi nyingi unazozileta humu huwa ni nzuri. Na pia huwa unatueleza kabisa kama kutakuwa na arosto ili tukiona kimya tuelewe. Asante sana
 
Sehemu ya 34

“Ni lazima ujue kila mwanamke unayemuona hapa duniani, Mungu amemuandalia mume mzuri ambaye utaishi naye kwa upendo na amani maisha yako yote, hata mkigombana, mtakuwa wepesi mno kusameheana na kusahau mliyotendeana, ila ukijilazimisha kumfuata fulani kisa pesa, kuna siku utalia na kujuta maisha yako yote,” alisema mwanamke huyo.

Maneno ya mama yake yakaingia moyoni mwake, yakamjenga na kurudi nyuma kutoka kwa Sangiwa. Yalimfungua na kumshukuru kwani alihisi endapo angemkubali mwanaume huyo, kuna siku isiyokuwa na jina angekuja kuumia mno moyoni mwake, na inawezekana matatizo yakawa makubwa mpaka kujimaliza, hivyo hakutakiwa kuwa na haraka.

Hapo, alitamani kumwambia mama yake kuhusu huyo John ila hakujua ni kwa namna gani angemuanza. Alihisi mama yake angemwambia kwamba kwa sababu alitoka jijini Dar es Salaam ndiyo maana alimpenda kumbe haikuwa hivyo.

Hakutaka kumwambia kwa wakati huo lakini alijiahidi kwamba siku moja ilikuwa ni lazima kumwambia kuhusu moyo wake, jinsi ulivyompenda mwanaume huyo ambaye hakujua aliishi wapi, alichokijua ni kwamba alikuwa akisali naye kanisa, hilo tu.

.
.
.
Je, nini kitaendelea?
Mapenzi bana....huyu moyo wake uko huku, yule moyo wake uko kule, yaani ni shida

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom