Sehemu ya 38
Wakaanza kuzungumza. Lengo kubwa la kumpigia simu msichana huyo lilikuwa ni kumzoea, kabla ya mambo mengine kuendelea kwanza ilibidi wawe karibu kwa kipindi fulani ili hata kama kitakuja kipindi cha kumwambia kwamba alimpenda kusiwe na tatizo lolote lile.
Alikuwa mcheshi, alimchekesha msichana huyo, hakumpa pumzi ya kuongea sana kwa sababu watu wengi walipenda kuwasikia watu wa Dar es Salaam kwa jinsi walivyokuwa wakiongea kwa mapozi, kama cherehani.
“Umenifurahisha sana!” alisema Deborah.
“Ni wajibu wangu kukufurahisha!” alisema.
“Na Dar ulikuwa unaishi sehemu gani?” aliuliza.
“Tandale!”
“Tandale?”
“Ndiyo! Ushawahi kufika?”
“Hapana! Huwa nikienda nafikiaga Mwenge kwa baba mdogo!” alijibu.
“Oh! Basi ninaishi huko! Kwa wajanja!”
“Kwa akina Diamond?”
“Yeah! Alikuwa jirani yangu, yaani nyumba yao ile kule, yetu hii,” akajiongeza kidogo.
Wakazungumza kwa dakika kadhaa na walipomaliza, simu ikakatwa na kuendelea kufanya mambo yake. Hapo kidogo moyo wake ukatulia, akawa na furaha, alijiona kuwa mshindi na pia ua ilikuwa ni lazima msichana huyo aingie mikononi mwake.
Wakati akijifikiria hayo, mara simu yake ikaanza kuita, haraka sana akahisi ni Jumanne, akaichukua, kuangalia jina, akashangaa kuona ni Deborah. Moyo ukaanza kudunda tena.
“Niambie bosi wangu!” alisema.
“Eti bosi wangu! Sasa nina ubosi gani?” aliuliza msichana huyo huku akicheka.
“Wewe ni bosi tu! Nimewaona wanawake wengi Kigoma, ila kwako, daah! Mungu kakubariki sana,” alisema.
“Hahaha! Aya ahsante! Nimekupigia kutaka kukuuliza kitu!” alisema.
“Kitu gani?”
“Kuhusu kampuni yetu!”
“Oh! Husahau! Sasa hatuwezi kuongea kwenye simu!”
“Mpaka?”
“Tuonane!”
“Basi nitakutafuta baadaye! Ama utakuwa bize?” aliuliza msichana huyo.
“Hapana! Nitakuwa na muda!”
“Sawa!” alisema na kukata simu.
Furaha aliyokuwanayo haikuweza kuelezeka hata kidogo. Moyo wake ulichanganyikiwa, hakuamini kama kweli Deborah alihitaji kuzungumza na yeye.
Haraka sana akakurupuka kutoka kwenye godoro lake na kuufungua mfuko wake wa nailoni na kuanza kuangalia nguo zake, alihitaji kuvaa nguo fulani maridadi kwa lengo la kumvutia msichana huyo.