SEHEMU YA 52
“Kijana! Acha porojo, nenda katafute pesa. Huwezi kuwa na binti yangu halafu ukaenda kumchakaza na umasikini wako. Ninampenda binti yangu, sitopenda kuona siku moja akiwa kwenye maisha ya chini, nitahitaji aolewe na mtu mwenye pesa, muonekano mzuri na si wewe,” alisema mzee huyo.
Alikuwa Mkristo ambaye kila Jumapili alikuwa akienda kanisani, alikubalika lakini yeye huyohuyo leo hii alikuwa akimwambia John kwamba hakutakiwa kuwa na binti yake kwa kuwa tu hakuwa na pesa.
Hilo likamliza John, mbele ya wazazi wa Deborah na msichana huyo akaanza kutokwa na machozi. Hilo halikusaidia, msimamo wa wazazi hao ulikuwa uleule kwamba Deborah hakutakiwa kuolewa na mtu masikini kama alivyokuwa.
Deborah hakuvumilia kukaa sebuleni, akasimama na kwenda chumbani kwake, akajifungia na kuanza kulia mfululizo.
Moyo wake uliuma kwa kiwango cha juu kabisa. Ni kweli alimpenda mno John, hakutaka kuona akiondoka na kumuoa msichana mwingine, ndoto yake ilikuwa ni kuolewa na mwanaume huyo kwa kuwa tu alimuonyesha mapenzi ya dhati.
John alikaa sebuleni, mwili wake ulipigwa ganzi, alitamani kusikia wazazi hao wakibadilisha uamuzi wao na kumwambia walikubaliana naye lakini haikuwa hivyo.
Akainuka na kuondoka zake, akatoka nje huku akilia, aliuchukia umasikini aliokuwanao, alichukia maisha aliyokuwa akiishi kipindi hicho.
“Hivi kweli ninakataliwa kuoa kwa sababu ya umasikini wangu?” alijiuliza, alikosa jibu, akaanza kupiga hatua kuelekea nyumbani kwao.
Wazazi wa Deborah walikaa sebuleni, walikuwa wakizungumza kuhusu uamuzi waliokuwa wameamua siku hiyo. Walifurahi kuona hilo likitokea, walipongezana lakini wakiwa hapo, ghafla mlango ukafunguliwa, Deborah akatoka akiwa na begi lake la nguo na kuanza kwenda nje.
Wote wakashtuka, hawakuamini kile walichokiona, walimuita, hakuitikia, ni kama hakuwasikia vile, akafungua mlango na kuondoka zake.
Wazazi wake walikataa kuolewa na John lakini moyo wake ulimwambia ni lazima akaishi na mwanaume huyo.