Sehemu ya 121
“Kwa nini Kigoma?” aliuliza John.
“Kwa sababu ni vigumu kuonana na mtu anayekufahamu lakini pia unakumbuka biashara ya samaki, kampuni niliyokupa huko?” aliuliza baba yake.
“Ndiyo!”
“Nataka uende ukaiangalie, uone ni kitu gani kinaendelea huko, ila kwanza zungumza na mzee Kayore na umwambie kuhusu hilo,” alisema baba yake.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akawasiliana na mzee huyo na kuomba kuonana naye ofisini kwake. Mzee huyo alifika muda muafaka na hivyo kuanza kuzungumza naye.
Alimwambia alitaka kwenda mkoani Kigoma kwa lengo la kuangalia biashara yao ilivyokuwa ikiendelea huko, alimwambia angekuwa huko kwa muda wa miezi kadhaa lakini aliloliomba hakutaka mtu yeyote afahamu kama alikwenda huko.
Alihitaji majina ya watu waliokuwa wameajiriwa katika kampuni hiyo mkoani Kigoma, akapewa na kuanza kuipitia, akaangalia mishahara yao na mambo mengine.
Alizungumza naye mambo mengi, kikubwa alichomuhusia ni usiri, hata kama kuna siku lingetokea kitu gani, ilikuwa ni lazima kuwe na usiri, asiufumbue mdomo wake na kumwambia kama alikuwa akimfahamu.
Baada ya kuzungumza naye kwa marefu, akaagana naye, akarudi nyumbani na kumwambia baba yake kwamba alikuwa tayari kuanza maisha mengine, ya upande wa pili ili ampate mwanamke aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hivyo kuelekea safari ya huko Kigoma ambapo yalimkuta yote yaliyokuwa yamemkuta.
|
|
Je, nini kitaendelea?
Tukutane tena week ijayo