Simulizi: Mke Wangu Juliana

Simulizi: Mke Wangu Juliana

Sehemu ya 114

Hilo halikuwa tatizo, akampitia na hatimaye kumchukua, kwanza alitaka kwenda naye huko hotelini, lakini akaahirisha na kumpeleka nyumbani kwao.

Huko akakutana na wazazi wake, akamtambulisha rasmi kwamba alikuwa mchumba wake, mwanamke ambaye alitaka kumuoa na kuishi naye maisha yake yote.

Kwa Amanda ilikuwa ni furaha tele, hakuamini kama kweli alipata nafasi kama hiyo, kutambulishwa kwa wazazi wa mpenzi wake kilikuwa kitu kikubwa kuliko vyote alivyowahi kufanyiwa.

“Mnapendana kweli?” aliuliza baba yake John.
“Ndiyo! Tunapendana na tunachokipanga ni kuoana na kuwa pamoja,” alijibu John huku akiwa na tabasamu pana.

Wazazi hao wakawapa baraka zote na kisha kuondoka zao. Ilikuwa ni majira ya saa mbili usiku. Ndani ya gari walikuwa wakiongea mambo mengi, Amanda alimwambia John jinsi alivyokuwa akijisikia muda huo, hakuamini kama kweli alimtambulisha kwa wazazi wake.

Walitumia dakika kadhaa wakafika katika Hoteli ya Kilimanjaro na kuteremka, wakaenda kwenye meza moja mgahawani na kutulia hapo. Haraka sana John akampigia simu Christina ambaye alimwambia yupo njiani.

Waliagiza chakula na kuanza kula, walikuwa wakizungumza mambo mengi tu, baada kama ya nusu saa, tayari Christina alifika mahali hapo na hivyo kumpigia simu John
“Njoo huku kwenye mgahawa!” alisema John.
“Sawa love!”

Ni ndani ya sekunde chache, Christina akatokea mahali hapo. Alipowaona watu hao, akashtuka, akabaki akimwangalia Amanda kwa mshtuko, hakuamini kile alichokuwa akikiangalia wakati huo.

Amanda alibaki akiwa amekodoa macho, hakuamini kumuona rafiki yake huyo mahali hapo, alichanganyikiwa. Alikumbuka namna alivyozungumza naye na kumwambia alikuwa na miadi ya kuonana na mpenzi wake, kitendo cha kuwa hapo kilimfanya kuhisi mwanaume aliyekuwa akimzungumzia alikuwa John.

John hakugundua kama wawili hao walikuwa wakishangaana, alichokifanya ni kusimama na kumkaribisha Christina mahali hapo, msichana huyo akakaa huku akiwa haelewi ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani aliamini John angekuwa peke, asingekuwa na Amanda mahali hapo.
“Si alisema anakwenda kwa Martin?” alijiuliza.
 
Sehemu ya 115

Mtoko ukabadilika, ni kama roho zao zikaingiwa nyongo. Amanda alimwangalia Christina kwa hasira, akahisi kabisa rafiki yake huyo alikuwa akimuibia mpenzi wake bila kujua kitu kilichomuumiza mno.

“Christina! Huyu ndiye huyo mwanaume uliyeniambia?” aliuliza Amanda huku akimwangalia Christina.

John alishangaa, kitendo cha msichana huyo kutajwa jina na mpenzi wake kilimshtua kupita kawaida. Hapo akahisi wawili hao walikuwa wakifahamiana.

“Mnafahamiana?” aliuliza John kwa mshtuko.
“Ndiyo! Ni rafiki yangu! Aliniambia kwamba leo anakwenda kuonana na mwanaume anayempenda, kumbe ndiye wewe!” alisema Amanda, hata sahani ya chakula akaisogeza pembeni kabisa.

“Kwani wewe si uliniambia utakwenda kulala kwa Martin, kwa nini upo hapa?” aliuliza Christina, sasa aliamua, rafiki yake alimwaga ugali, yeye akaamua kumwaga mboga.

John alinyamaza, kile alichokisema Christina kilimuumiza mno, hakuamini kama mpenzi wake huyo alikuwa na ratiba nyingine ya kwenda kulala na mwanaume mwingine.

Akashusha pumzi, Amanda akanyamaza, akaangalia chini, alihisi rafiki yake suala hilo angelifanya siri lakini kwenye hali ya kushangaza, akalimwaga mbele ya John.

“Kulala kwa Martin? Martin ndiye nani?” aliuliza John huku akimwangalia Christina.
“Ndiyo umuulize huyo! Nashangaa ananilaumu na wakati hakuwahi kuniambia kuhusu wewe,” alisema Christina, akajiweka upande mwingine kimaongezi kuonyesha hakuwa na kosa.

“Amanda! Martin ndiye nani?” aliuliza John, hakutaka kuonyesha kukasirika, kwa mbali tabasamu lilionekana usoni mwake.

“I was about to talk to you, so sorry!” (samahani, ndiyo nilipanga kuongea nawe) alijibu msichana huyo.
“Really? What is it about?” (Kweli? Kuhusu nini?) aliuliza John.

“Martin...”
“Who the hell is he?” (ndiye nani?) aliuliza John.

Amanda akanyamaza, kujibu lilikuwa jambo gumu mno. Rafiki yake huyo alimuharibia, hakutaka kumpoteza John kwani tayari mwanaume huyo alionyesha mapenzi ya wazi juu yake na kubwa zaidi ni kuwa alikwenda kumtambulisha mpaka kwa wazazi wake.

Amanda hakuwa na ujanja, akaanza kumwamboa John kuhusu Martin, ni kweli alikuwa mpenzi wake na alipanga kuachana naye kwa kuwa alionyesha nia naye.
“Kuachana naye?” “Ndiyo!”
 
Sehemu ya 116

“Kivipi na wakati uliniambia huna mwanaume yeyote yule?” aliuliza John.
“Naomba unisamehe!”

“Amanda! Kama kweli uliweza kunidanganya kwa jambo hili, utaweza kuniambia ukweli kwa mengine? Leo ulipanga kwenda kulala kwa huyo Martin, hivi kuna kuachana hapa kweli? Amanda! Hapana kwa kweli!” alisema John, hapohapo akasimama, akamuita mhudumu na kuomba bili yake mezani.

Muda huo Amanda alikuwa akilia tu, hakuamini kama kweli rafiki yake huyo alimpotezea mpenzi wake aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwake.

Christina hakujali, kwake kila kitu kilikuwa poa kabisa. Hakujiona kuwa na kosa kwani hata kama angeulizwa, angesema tu kuwa alikutana na mwanaume njiani, akamtongoza na ikawa hivyo, kosa la Amanda ni kwamba hakuwahi kumuonyesha mpenzi wake, hivyo hakujua.

John alikuwa kimya, alijizuia kutokupiga kelele, hoteli hiyo ilikuwa na watu wenye heshima zao, hivyo hataka kama angetiwa hasira kwa namna yoyote ile asingethubutu kupayuka.

Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini mwanamke aliyekuwa akimuonyesha mapenzi yote, kumbe usiku huo alipanga kwenda kulala na mwanaume mwingine, moyo ulichoma kupita kawaida. Mhudumu akaleta bili yake, akaichukua, akaisoma na kumlipa.

“Twende nikurudishe nyumbani!” alisema John huku akisimama na kuelekea ndani ya gari lake, Amanda akafuata.

John hakuzungumza kitu, japokuwa msichana huyo alikuwa akiomba sana msamaha ndani ya gari lakini hakuongea chochote kile.

Alichokigundua msichana huyo hakumpenda, alikuwa na mwanaume mwingine, kama kweli alipanga kwenda kulala naye, basi mapenzi hayakuwa kwake kabisa.

Walitumia dakika kadhaa mpaka kufika kwao, akasimamisha gari na kumtaka ateremke.
“Naomba unisamehe John mpenzi! Najua nimeko....”
“Naomba uteremke garini! Tutaongea kesho!” alisema John, tayari macho yake yalikuwa mekundu mno.

Kwa upole, Amanda akateremka ndani ya gari! John hakutaka kubaki, akaondoka zake mahali hapo, Amanda akaanza kulia kama mtoto, hakuamini kama John aliamua kumuacha, lawama zake zote zikawa kwa rafiki yake, hata urafiki wenyewe ukawa na dalili ya kufa.
 
Sehemu ya 117

Moyo wa John ni kama ulipigwa, ganzi, kile kilichotokea kilimuumiza kupita kawaida. Hakuamini kama msichana aliyekuwa akimpenda, aliyeamua kumpa moyo wake aliamua kumficha kwamba alikuwa na mwanaume mwingine.

Kama alimpa akiwa na mwanaume huyo, inamaanisha angeendelea kuwa naye hata kama angemuoa. Hakuwa radhi kumuacha na ndiyo maana usiku wa siku hiyo alitaka kwenda kulala naye. Ilimuuma mno.

Aliendesha gari mpaka alipofika nyumbani, akateremka na kuanza kuelekea ndani. Majira yalikuwa ni saa nne kasoro, aliwakuta wazazi wake wakiwa sebuleni, alipoingia tu na kumwangalia, waligundua kulikuwa na tatizo, walihitaji kujua kilichotokea.

Macho yake yalikuwa mekundu, ilionyesha kulia sana kabla ya kufika nyumbani hapo. Hawakujua lolote lile, mama yake akasimama, akamsogelea na kumkumbatia.
“Kuna nini kijana wangu?” aliuliza mama yake.

John hakujibu kitu, alibaki kimya huku akimwangalia mama yake ambaye ni kama alimuongezea maumivu ya moyo wake zaidi.
“Kuna nini John?” aliuliza baba yake ambaye naye akainuka kwenye kochi na kumsogelea.
“Amanda...” alijibu.
“Amanda? Huyu mchumba wako?”
“Ndiyo!”

“Amefanya nini tena?” aliuliza mama yake.
John hakujibu, akaanza kulia mbele yao, kitendo cha kuulizwa swali lile kikaanza kumkumbusha kilichokuwa kimetokea dakika chache nyuma. Baada ya kutulia, akaanza kuwasimulia kila kitu.

Wote walikuwa makini kumsikiliza, alisimulia kwa uchungu tangu siku ya kwanza alipokutana na msichana huyo, walivyotongozana na hatimaye kuwa wapenzi mpaka siku hiyo.
“Kwa maana hiyo hakuwa mkweli kwako?” aliuliza mama yake.

“Ndiyo mama!”
Baba yake akamsogelea, alimpomfikia, akamkalisha kwenye kochi kwa lengo la kutaka kuzungumza naye, kwani alimwangalia kijana wake, alihisi kulikuwa na sehemu aliyokuwa akikosea.

“Mwanangu John!” aliita baba yake, John akageuza macho na kumwangalia.
“Hakuna mwanamke yeyote atakayekukataa kwa sasa...” alisema baba yake, John akamkazia macho zaidi, alishtushwa na kile alichoambiwa.

“Kwa nini?” alijikuta akiuliza.
“Kwa sababu una pesa! Kila mwanamke unayemuona mjini ana mtu wake, na anapotokea mwanaume mwingine mwenye pesa, ni lazima tu awe naye,” alisema baba yake. John akanyamaza.
 
Sehemu ya 118

“Wanawake wanapenda pesa! Ipo hivyo! Anapotokea mwanaume mwenye nazo, anakuwa tayari kufanya lolote lile. Wanaume wengi wenye pesa hawapendwi kwa mapenzi ya dhati, wanapendwa kwa sababu ya pesa zao,” alisema baba yake, John alikuwa makini kumsikiliza.
“Kwa hiyo sitokuja kupendwa kwa sababu nina pesa?” aliliza.

“Ni vigumu! Wengi watapenda pesa zako lakini si kwa mapenzi ya dhati. Leo hii mwanamke anampenda mwanamuziki Diamond Platnumz lakini hampendi Nassibu Abdul...Umaarufu, pesa na elimu ni vitu vinavyomfanya mwanamke akupende hata kama moyo wake haupo kwako!” alisema baba yake.

“Oops! Nifanye nini ili nipendwe?”
“Kuwa masikini tu!”
“Niwe masikini?”
“Ndiyo! Ukitaka kupata penzi la dhati, ishi kwenye umasikini, msichana atakayekupenda kwenye hali hiyo, huyo ndiye mtu sahihi wa kuwa nawe,” alijibu baba yake.

Alichokiongea ni kweli kabisa lakini hakujua ni kwa namna gani angekuwa masikini. Alizoea kuishi maisha ya kitajiri, kitendo cha kuambiwa kuishi kwenye maisha ya upande mwingine kwake kilionekana kama kitu kisichowezekana kabisa.

Alimwambia baba yake ukweli kwamba isingewezekana hata kidogo, kuishi maisha hayo, ajinyime lilikuwa jambo gumu kuliko mambo yote hayo.

Baba yake hakumlazimisha zaidi ya kuonyesha tabasamu tu na kumwacha kijana wake afanye yale ambayo aliyaona sahihi kufanya kipindi hicho.

Muda mwingi Amanda alikuwa akimpigia simu John kwa lengo la kutaka kumwambia aonane naye lakini John hakuwa akipokea simu.
Hakutaka kuwa na mwanamke huyo tena, ni kweli alimpenda, alimthamini lakini kitendo cha kuwa na mwanaume mwingine aliamini hata kama angekuwa naye, bado angeendelea kuwa na mwanaume huyo hivyo kuzidi kumuumiza.

Amanda hakukoma, alikuwa akituma meseji mbalimbali za kuomba msamaha na kuahidi kutokuendelea na Martin lakini bado meseji hazikujibiwa, japokuwa John alimwambia kwamba wangeongea, hakutaka kufanya hivyo tena.

Baada ya siku kadhaa za kumsumbua, hatimaye John akaamua kubadilisha namba yake ya simu, hakutaka kuwasiliana na mtu huyo maisha yake yote, kama aliamua kumdanganya, ilitosha ilikuwa ni lazima atafute mwanamke mwingine lakini si Amanda.
 
Sehemu ya 119

Msichana huyo alipoona John amebadilisha namba, akaamua kumfuata ofisini kwake, aliamini kwa kitendo hicho John angeweza kumsamehe na hatimaye kuwa kama zamani.
Alipofika huko, akaongea na sekretari kwamba alitaka kuonana na John.

Mara kwa mara msichana huyo alikuwa akifika hapo, alikwenda moja kwa moja ofisini, na kipindi ambacho waliachana, John hakutaka mtu yeyote yule afahamu.

Hivyo alivyofika na kuongea na sekretari ambaye alimwambia yupo, moja kwa moja akanyoosha mpaka ofisini, akaufungua mlango na kuingia ndani.

Macho yake yakagongana na ya John aliyekuwa nyuma ya meza ya kioo, kumuona msichana huyo moyo wake ukashtuka, hakutegemea kumtia machoni siku hiyo, hakuwa na miadi naye na mbaya zaidi aliachana naye.

“John! Please usinifukuze, naomba niongee nawe,” alisema Amanda, John akanyamaza, hakuongea kitu chochote kile, alibaki akimwangalia tu.

Amanda akaanza kumwambia kuhusu huyo Martin, alieeleza mambo mengi kwamba baada ya kufikiria kwa muda mrefu aliamua kuachana na mwanaume huyo.

Martin alimuomba akalale kwake lakini alikataa kwa kuwa aliamua kuwa naye. Lilikuwa ni jambo gumu kumwambia moja kwa moja na ndiyo maana aliamua kumuacha taratibu.

Alizungumza maneno mengi sana, zaidi ya elfu tano lakini John hakuzungumza lolote lile zaidi ya kumwangalia tu. Kwa kipindi hicho hakutakiwa kuwa na huruma hata kidogo, kama ingekuwa hivyo, hatari ingekuja mbele yake, yaani kumuonea mtu huruma na kuwa naye, siku ya kuamua kukuumiza asingekuonea huruma.

Baada ya nusu saa kuzungumza mfululizo, Amanda akanyamaza, sasa akabaki kimya kusikiliza maamuzi ya John, angemwambia nini baada ya kumwambia mambo mengi.
“Toka nje...” alisema John huku akimwangalia msichana huyo aliyeonakana kushtuka.
“John....”

“Amanda...nimesema toka nje...” alisema John kwa sauti ya chini, ya taratibu sana.
Amanda alishindwa kuelewa haraka kama John alikuwa akimaanisha ama la! Alimwambia kirahisi sana atoke nje baada ya kumwambia mengi kuhusu yeye na huyo Martin.
“John! Naomba unisikilize...” alisema.
 
Sehemu ya 120

John akanyanyua mkonga wa simu na kupiga sehemu, baada ya dakika moja tu, wanaume wawili waliokuwa na miili iliyojazia wakaingia ndani, wakamchukua Amanda na kumwambia alitakiwa kuondoka ndani ya ofisi hiyo.

Msichana huyo alibaki akilia kwa maumivu makali, hakuamini kwamba yeye ndiye aliyekuwa akifanyiwa vile na mwanaume aliyekuwa akimpenda.

Kwa muda huo John alionekana kubadilika, alikuwa mwanaume aliyekuwa na msimamo wake, hakutaka kuyumbishwa na mwanamke yeyote yule kwa kuwa alikuwa na kila kitu ambacho mwanamke mrembo alitamani sana kuviona kwa mwanaume aliyekuwa akimuhitaji.

Wanaume wale wakamshika Amanda na kuanza kutoka naye mule ndani. Alikuwa akilia kama mtoto lakini watu hao hawakutaka kujali, walichotaka kuona ni kumuona akiwa nje ya geti tu.

Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa John kuonana na msichana Amanda. Hakutaka kumfikiria kwa lolote lile. Kutokana na kuwa na pesa, John alipata wasichana wengine wawili, Rose na Lilian lakini wote hao walikuwa kama Amanda, walimpenda kwa kuwa alikuwa na pesa tu.
Kila siku baba yake alimwambia ni lazima abadilishe aina ya maisha aliyotaka kuishi, kama kweli alihitaji kumpa msichana aliyekuwa akimpenda basi alitakiwa kubadilisha maisha yake.

“Lakini nitaanzia wapi?” alijiuliza.
Hakutaka kubaki na swali hilo moyoni mwake, akamshirikisha baba yake, akazungumza naye, alichomwambia ni kwamba alitakiwa kwenda hata mkoani Kigoma kwa lengo la kwenda kuishi kimasikini huko.
 
Sehemu ya 121

“Kwa nini Kigoma?” aliuliza John.
“Kwa sababu ni vigumu kuonana na mtu anayekufahamu lakini pia unakumbuka biashara ya samaki, kampuni niliyokupa huko?” aliuliza baba yake.

“Ndiyo!”
“Nataka uende ukaiangalie, uone ni kitu gani kinaendelea huko, ila kwanza zungumza na mzee Kayore na umwambie kuhusu hilo,” alisema baba yake.

Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akawasiliana na mzee huyo na kuomba kuonana naye ofisini kwake. Mzee huyo alifika muda muafaka na hivyo kuanza kuzungumza naye.

Alimwambia alitaka kwenda mkoani Kigoma kwa lengo la kuangalia biashara yao ilivyokuwa ikiendelea huko, alimwambia angekuwa huko kwa muda wa miezi kadhaa lakini aliloliomba hakutaka mtu yeyote afahamu kama alikwenda huko.

Alihitaji majina ya watu waliokuwa wameajiriwa katika kampuni hiyo mkoani Kigoma, akapewa na kuanza kuipitia, akaangalia mishahara yao na mambo mengine.

Alizungumza naye mambo mengi, kikubwa alichomuhusia ni usiri, hata kama kuna siku lingetokea kitu gani, ilikuwa ni lazima kuwe na usiri, asiufumbue mdomo wake na kumwambia kama alikuwa akimfahamu.

Baada ya kuzungumza naye kwa marefu, akaagana naye, akarudi nyumbani na kumwambia baba yake kwamba alikuwa tayari kuanza maisha mengine, ya upande wa pili ili ampate mwanamke aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hivyo kuelekea safari ya huko Kigoma ambapo yalimkuta yote yaliyokuwa yamemkuta.
|
|

Je, nini kitaendelea?

Tukutane tena week ijayo
 
Safi sana... Ngoja tuone...

Ila John... mkuki kwa nguruwe... yeye anarukaruka, ila kurukwa kidogo ana mind...


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom