Sehemu ya 123
Deborah akashtuka, hakuamini alichokisikia, ni kama alikuwa akiota vile, yaani mfanyakazi yeye wa kawaida kuchukua nafasi ya kuwa meneja badala ya mzee Masako, hakika ilikuwa ndoto ambayo hakuwahi kuiota hata siku moja.
“Najua elimu yako si kubwa sana kama mzee Masako, ila utatakiwa kuwa meneja na mzee huyo nitamfukuza kazi ama kumshusha chini, huwezi kuwa na kiongozi ambaye anawasikiliza watu wengine wampangie maamuzi ya kuwafukuza watu kazi,” alisema John na kuendelea:
“Baada ya kuwa meneja, utatakiwa kusoma, nitahakikisha unakwenda nchini Sweden kusomea japo kwa mwaka mmoja, kama utakwenda peke yako ama na mume wako, hakuna tatizo, nitahakikisha nasimamia kila kitu. Kama familia mtaamua nyie wenyewe,” alisema John na kuendelea:
“Sifanyi haya kwa sababu una akili sana, au mfanyakazi mkubwa, ninafanya haya kwa sababu ya wema wako, kama ubaya hulipwa hapahapa duniani basi hata wema nao hulipwa hapahapa!” alisema na kumgeukia mzee Abraham.
“Najua ni kwa namna gani umeghafirika sana, umechanganyikiwa, umekonda kupita kawaida. Ni maisha, huwa tunapita katika matatizo mengi sana. Na katika hili ninaamini utakuwa umejifunza sana. Unadaiwa bilioni mbili na TRA, nakuahidi nitazilipa.
Ni kiasi kikubwa lakini nitajitahidi hata kulipa kidogokidogo na mwisho upate kila kitu chako kilichochukuliwa!” alisema John na kuendelea:
“Sifanyi haya kwa kuwa umestahili sana, ninafanya kwa sababu ninataka kuwaonyesha watu kwamba tunaweza kulipa ubaya kwa wema, lakini pia ninafanya hivi kwa ajili ya binti yako.
Ninahitaji kumuona akifurahia, yeye kuwa meneja huku baba yake akiwa kwenye hali mbaya, umeneja hauwezi kumpa furaha maishani mwake. Ninahitaji afurahie kila kitu na ndiyo maana nimeamua kufanya hayo yote,” alisema John.
Mzee Abraham alikuwa kimya, kile alichoambiwa hakikuaminika masikioni mwake, macho yake yakaanza kuwa mekundu na baada ya sekunde kadhaa machozi yakaanza kumtitirika.
Maneno aliyoongea John yalikuwa makubwa, yenye faraja lakini kwa msaada aliokuwa ameutoa kwake na kwa binti yake hakika hakuwa na uwezo wa kulipa wema huo hata siku moja.