Sehemu ya 50
Nilipanga baada msiba kwisha nisafiri kuchunguza kifo cha baba ambacho kwa upande wangu sikukubaliana nacho.
****
Siku ya pili tulimzika baba, msiba ulioudhuliwa na watu wengi sana, wafanyakazi wenzangu walikuwa miongoni mwa watu waliokuja kumzika baba yangu na kunipa faraja kubwa.
Msibani kulikuwa na minong’ono ya chinichini ikisema, msiba ule si bure lazima kutakuwa na mkono wa mtu. Mama hakukubaliana na minong’ono ile kwa kuamini kifo cha baba pamoja na vitu vya kushangaza kutokea bado aliamini ni amri ya Mungu.
Baada ya mazishi na kukaa siku mbili nilimuomba mama niondoke naye ili tukamalizie msiba nyumbani kwangu. Lakini mama alikataa na kusema msiba ataumalizia palepale nyumbani kwake. Sikuwa na jinsi kwa vile alikuwa ameamua ilibidi niiache familia yangu ikae na mama kipindi chote cha mama kumaliza msiba wa baba.
Wiki moja ilikatika na muda wa kurudi kazini ulifika. Nilirudi zangu kwangu na kumwacha mke wangu amtunze mama kwa kipindi chote cha kumalizia msiba wa baba. Nilirudi zangu nyumbani siku ya jumapili na jumatatu asubuhi nilikwenda kazini. Nilianza kazi nikiwa bado na kitendawili kizito kichwani mwangu kutokana na kifo cha baba. Pamoja na mama kusema kifo cha baba ni amri ya Mungu sikutaka kukubaliana naye japokuwa nilimkubalia ili kumlizisha.
Nilipanga siku ya Ijumaa niondoke na gari la kampuni kwenda Malalo. Niliamini hata kama nitalala Tewe siku ile na kesho yake lakini siku ya jumapili. Lazima niwe nimerudi kwa muda wowote ili mradi jumatatu inikute kazini.
Wiki nzima niliyokuwa kazini nilikuwa katika dimbwi la mawazo kuhusiana na mazingira ya kifo cha baba yangu. Wengi walijua kukosa kwangu raha kazini kulitokana na maumivu ya kifo cha baba yangu, ambaye siku zote alikuwa mtu wangu wa karibu. Japokuwa kifo cha baba kiliniuma sana kutokana na kipindi kile ndicho nilikuwa nikiwahitaji sana wazazi wangu kula jasho langu.
Kilichonichanganya zaidi na kuupa moyo wangu wasiwasi kilikuwa mazingira ya kifo cha baba. Niliamini utatuzi wake ningeupata kwa mtoto wa mzee Kidereko. Bado safari yangu ilibakia siri yangu sikutaka kumshirikisha mtu yeyote.
Mwisho wa wiki niliomba gari kama nakwenda kumuona mama. Kwa vile nilikuwa naivana na bosi, alinikubalia niondoke na gari. Siku ya ijumaa niliondoka kazini saa tano asubuhi, watu wote walijua nimekwenda kumuona mama.
Niliondoka kazini saa tano na nusu, nilitumia saa mbili na nusu kufika Chalinze kutoka na mwendo kasi niliokuwa nikitembea nao. Niliunganisha moja kwa moja kuelekea Lushoto. Kwa mwendo niliokuwa nakwenda nilifika Tewe saa kumi na mbili jioni. Nilikuta bado mwanga wa jua bado haujazama vizuri na kuamini mambo yangu kama yatafanikiwa yatakwenda vizuri ningeweza kurudi siku ileile na kuelekea kwa mama kisha ningerudi kazini.
Ugeni wangu wa ghafla uliwashtua, baada ya kunipokea walitaka kujua ujaji wangu wa siku ile.
Kwa vile muda ulikuwa bado nilipata muda wa kuzungumza na mtoto wa mzee Kidereko. Palepale nje chini ya mti, wote walitupisha kutuacha tuzungumze wawili.
“Ndiyo ndugu zangu za siku?” mtoto wa mzee Kidereko aliniuliza.
“Nzuri kiasi,” nilimjibu huku nikimtaza na kukutanisha macho yalionesha anashauku ya kujua kilichonipeleka pale.
“Hata mimi ujaji wako umenionesha kuna kitu, ehe, ndugu yangu tatizo nini?”
Nilimuelezea utata wa mazingira ya kifo cha baba yangu. Baada ya kunisikiliza alimwita msaidizi wake, alimwita kijana mmoja kati ya wasaidizi wa baba yake mzee Kidereko.
“Hamis njoo.”
“Naam.”
“Niletee unga wa kutazamia mbali.”
Juma alikwenda ndani na kurudi na chupa ndogo aliyomkabidhi. Baada ya kumkabidhi alifungua chupa na kujimiminia unga mweupe mkononi. Kisha aliumwaga kwa kuusambaza na kutulia kuutazama ule unga aliopeperuka kwa upepo.
Aliutazama ule unga uliokuwa ukipepea kwa upepo kama anaangalia kitu ambacho mimi sikukiona. Baada ya kutulia kwa muda alishusha pumzi ndefu na kusema:
“Kuna vita nzito sana.”
“Vita?” nilishtuka kusikia vile.
“Tena nzito, mmh! Kuna kazi!”
“Kazi?” nilizidi kushtuka na maneno ya mganga.
“Tena nzito, hii kwangu.mmh, sijui!” mganga alinikatisha tamaa bila kujua hiyo ni vita gani na uzito wake ni upi.
“Mbona unanitisha?”
“Sikutishi, ndiyo ukweli wenyewe, vita hii ingenoga mzee angekuwepo.”
“Una maana gani?”
“Kifo cha baba yako kina siri nzito.”
“Mganga hebu nieleze tatizo kuliko kunizungusha na kunitisha.”
“Inaonesha hapa kifo cha baba yako kimetokana kisasi.”
“Kisasi?” nilishtuka.
“Ndiyo.”
“Kisasi kipi tena?”
“Baada ya kifo cha mgoni wako wa pili, ndugu zake hawakukubali kama kile kifo cha amri ya Mungu. Kutokana na mazingira ya kifo chake, aliamua kukifanyia uchuguzi ndipo walipo kukuta. Hawakukubali kumpoteza ndugu yao, waliamua kulipa kisasi.
“Inavyoonekana waganga wengi wa nchini wamechemsha hivyo wakaamua kutoka nje ya nchi kuhakikisha wanakulambisha mchanga. Inaonesha uchawi waliotumia kukuroga umetoka mbali sana.
“Naweza kusema mshukuru sana mzee Kidereko kwa kinga aliyokupa. Uchawi waliotumia tungekuwa tumekwisha kukuzika muda mrefu. Unakumbuka siku moja ukiwa kazini uliumwa sana kichwa kisha ulitoka damu puani?”
“Ndiyo nakumbuka.”
Nilikumbuka siku moja ambayo nina imani katika kusimulia sikulisema hili. Ni kweli siku moja nikiwa kazini baada ya kazi ya kutoa vifaa ambayo vilikuwa vingi na kunifanya nisimame kwa muda mrefu.
“Nilipokaa kichwa kilianza kuniuma kama kinapasuka kikifuatiwa na kutokwa damu nyingi puani.
Nilikimbizwa hospitali ambako nilikutwa na maralia. Baada ya matibabu nilijisikia vizuri na kuruhusiwa kutoka hospitali. Hali ile haikujirudia tena na kuamini yale yalikuwa maralia tu.
“Basi yale hayakuwa maralia ilikuwa ndiyo safari, shukuru kupelekwa kwenye mizimu, uchawi uliofanyiwa mbaya sana. Kutoka damu puani ilikuwa safari isiyo na kwaheri. Lile lilikuwa jini la kutumwa, jini Makata lilikuwa likukate palepale.
“Baada ya kuona kwako ngoma nzito walibadilisha mashambulizi na kuyaelekeza kwenye familia yako.
Wameanza na baba yako baada ya hapo atatafutwa mtu mwingine.”
“He! Ina maana wamepanga kuiteketeza familia yangu yote?” nilishtuka kusikia vile.
“Ndiyo.”
“Wanatumia uchawi wa ndizi, wanaroga kwenye mkungu wa ndizi wenye ndizi mbichi, ikiiva ndizi moja na kundoka, basi katika familia yako anaondoka mtu mmoja.”
“Mungu wangu!” nilishika kichwa kwa mshtuko.
“Mtego wao haukuwasumbua kukunasa kwa vile kilikuwa kisasi cha kuuawa ndugu yao, hivyo ilikuwa rahisi kukupata.”
“Sasa utanisaidiaje?”
“Kazi hii kwa uwezo wangu nzito sana, ila nitakuelekeza kwa mzee mmoja ambaye alikuwa swahiba wa baba ambaye naye yupo vizuri kama mzee Kidereko.”
“Anakaa wapi?”
“Maeneo ya mbele kidogo japo kuna kamwendo kadogo.”
“Tunaweza kwenda leo?”
“Tunaweza kwa vile muda bado.”