Simulizi:Death Of Innocent

Hili zao la belinda lipo kweli.?
Au ndo wa mwisho kuzaliwa,?sio kwa mahaba hayo[emoji36]
Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kabla sijaendelea nahuu utamu naoana mtoto anamiaka5 lakini baba yake yupo jela miaka 8.Kwahiyo mama alikuwa anapeleka utamu jela?au alimtiaje?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
*Sehemu ya 09*


Belinda alipofikiria pesa aliyokuwa nayo mfukoni ilikuwa ni shilingi elfu kumi peke yake, hiyo ndiyo ilikuwa maisha yake hakuwa na tegemeo la kupata pesa mahali pengine mpaka wakati wa kujifungua! Hakuwa na jinsi ilikuwa ni lazima asaidie, alichukua pochi yake na kuifungua akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi Nyamizi ambaye naye aliwakabidhi wazee wa kijiji ili waende kununua sanda.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa Belinda kuwa na pesa, alielewa mbele kulikuwa na shida kubwa kwa sababu nyumbani kwao na prosper asingeweza kupata msaada wowote!
Pamoja na hayo yote hakuwa tayari kumuua mtoto wake.

Belinda alishindwa kuelewa 
maisha yangeendeleaje bila 
pesa, pesa pekee aliyokuwa amebaki nayo ilikuwa shilingi elfu kumi ambayo aliitumia kununua sanda ya mama yake Prosper! Hakuwa na jibu la jinsi gani angeitunza mimba yake mpaka kujifungua, aliielewa hali ya uchumi kijijini Tutuo, alijua dada zake na prosper waliobaki wangehitaji msaada kutoka kwake.

Aliona giza kubwa mbele yake lakini yote alimwachia Mungu, alikuwa tayari kwa lolote lakini si kurudi tena Dar es Salaam kwa baba yake, aliamini maisha yalikuwa yamembadilikia na hayo ndiyo yalikuwa maisha yake! Kulikuwa ni kuporomoka kwa aina yake lakini hakuwa na jinsi ya kuubadilisha ukweli huo hiyo ndiyo ilikuwa hali halisi.

Mwezi mmoja baadaye:
Maisha yalikuwa magumu sana kwa Belinda na familia nzima ya akina Prosper iliyotegemea yeye angetoa msaada, mara nyingi walilala na kushinda na njaa sababu ya kukosa chakula!Afya ya Belinda ilizidi kudhoofika, akakonda na alionyesha dhahiri dalili za kupungukiwa damu jambo alilokabiliana nalo kwa kula mboga za majani chukuchuku ambazo gharama yake ilikuwa ni kuzichuma tu na kuzipika.
Mara nyingi alikumbuka maisha ya starehe aliyoishi nyumbani kwao, maisha hayo hayakuwepo tena ilimlazimu azoee hali aliyokuwa nayo.

Chakula chao kikuu kilikuwa mihogo na karanga, ambacho walikila mara moja kwa siku! Mihogo hiyo ilipatikana baada ya kufanya vibarua katika mashamba ya watu ya mihogo na ujira wao ulikuwa ni hiyohiyo mihogo waliyoitumia kula, Belinda alikuwa na mimba lakini alilazimika kwenda kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu asubuhi mpaka saa kumi jioni.

Kwa mwanamke mjamzito ilikuwa ni kazi ngumu lakini alilazimika kuifanya ili aishi, ili kupata pesa ya kumwezesha kwenda kumwona Prosper gerezani kila jumapili,Belinda alilazimika kutafuta kazi ya kusomba maji na kupasua kuni nyumbani kwa mwarabu mmoja tajiri kijijini hapo! Kwa pipa moja la ndoo kumi na mbili Belinda alilipwa shilingi mia tatu, ilikuwa ni pesa kidogo sana lakini alilazimika kuikubali! Alitunza shilingi mia mbili na kutumia shilingi mia.

Akiba aliyojiwekea kwa kufanya kazi hiyo ndiyo ilimwezesha kuwalipia nauli wifi zake pamoja na yeye mwenyewe kwenda gerezani kumwona Prosper! Yalikuwa ni maisha ya huzuni kubwa kwa Belinda aliyekulia katika familia ya kitajiri na yenye fahari kubwa lakini alilazimika kuyakubali.

Belinda alikonda na kukondeana, akabaki mifupa tupu ni mimba tu iliyoonekana mbele yake, nywele zilizotiwa dawa kichwani mwake zilichakaa na kulazimika kuzikata, pamoja na shida zote hizo bado Belinda hakuwaza kurudi kwa baba yake ambako alijua baba yake angemtoa roho.

“Nitafia hukuhuku Tutuo kamwe sitathubutu kurudi kwa baba nina uhakika atanichinja! Ninajua ameshaambiwa mambo mengi ya ajabu na mama na ndugu zangu wa kambo ili anichukie!” Aliwaza Belinda.

**************
Belinda aliendelea kuishi na kuitunza mimba yake katika mazingira hayo magumu! Akipasua kuni na kusomba maji nyumbani kwa mzee Mohamed, zilikuwa ni kazi ngumu sana kwa mama mjamzito lakini hakuwa na chaguo jingine ilibidi azifanye hivyohiyo vinginevyo asingepata pesa ya kumpa mahitaji muhimu pamoja na nauli ya kumpeleka gerezani kila mwisho wa wiki.

Belinda alikuwa na uwezo wa kuamua kurudi Dar es Salaam na kuanguka miguuni mwa baba yake akiomba msamaha, aliamini pengine angeweza kusamehewa ingawa hakuwa na uhakika sana, alishindwa kufikia uamuzi huo kwa sababu alimpenda mno Prosper na hakuwa tayari kumwacha peke yake.

Alifanya kazi ngumu za kupasua kuni na kusomba maji kwa muda wa miezi minane ya mimba yake, hakukumbuka hata siku moja kwenda kliniki kupimwa maendeleo ya mimba yake, alichofanya ni kununua vifaa muhimu alivyoambiwa na akinamama wazoefu wa mambo ya uzazi kijijini kama vile mipira ya kuvaa mikononi,khanga za kutosha, wembe na nepi za mtoto wake.

Watu wote kijijini walimshangaa kwa jinsi alivyofanya kazi ngumu akiwa na mimba kubwa ya kujifungua wakati wowote, mwezi wa tisa wa mimba yake ulipoingia Belinda alizidiwa na kuishiwa na nguvu kabisa, alianguka siku moja wakati akipasua kuni chini ya jua kali na kuzimia, walimtoa juani na kummwagia maji akazinduka.

Mzee Mohamed mwarabu tajiri aliyekuwa akifanya kazi kwake alipopata taarifa hizo alimfukuza kazi sababu ya kuogopa angeweza kufia nyumbani kwake.
“Belinda iko wewe acha kazi sababu wewe uko na mimba kuba sasa!”

Mzee Mohamed alimwita Belinda na kumwambia
“Hapana mzee ninaweza tu ile ilikuwa ni bahati mbaya kwani nilikanyaga mti nikaanguka chini, tafadhali niache nifanye kazi sina pesa ya chakula wala nauli ya kwenda kumwona mume wangu gerezani!” Belinda alimbembeleza mzee Mohamed lakini haikusaidia kitu amri ilishatolewa afukuzwe kazi na hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Belinda aliondoka nyumbani kwa mzee Mohamed akilia machozi kwani pesa aliyokuwa nayo ilikuwa haitoshi kumkamilishia kila kitu wakati wa kujifungua, alijua wangeitumia kwa chakula kabla miezi tisa kamili haijakamilika.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani mpaka Belinda anapatwa uchungu saa moja na nusu ya jioni siku ya Ijumaa ya mwezi huo wa tisa hakuwa na pesa yoyote kama akiba yake, pesa yote alishaitumia kuwatunza dada zake na Prosper, Nyamizi na Kasanda ambao hawakujishughulisha na kazi yoyote pamoja na kuwa afya zao zilikuwa njema.

*Je,nini kitaendelea?*
 
*Sehemu ya 10*


Hapakuwa na pesa ya kumpeleka hospitalini usiku ule ilibidi ateseke na uchungu mpaka asubuhi lakini bado hakujifungua, aliendelea mpaka saa tano asubuhi hali ilikuwa bado ileile mtoto hakuwa tayari kutoka, Belinda aliishiwa na nguvu sababu ya kusukuma mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio na mguu wake mmoja ulipoteza kabisa hisia.

Saa sita mchana Kasanda na Nyamizi walishtukia badala ya kichwa kutokeza katika njia ya uzazi mkono wa mtoto ulichungulia!

Wote waliogopa na kulazimika kutafuta baiskeli na kukimbia hadi kijiji cha jirani kuchukua mkunga wa Jadi, naye alipokuja na kuiona hali aliyokuwa nayo Belinda alishtuka.
“Huyu alikuwa anakwenda Kliniki kweli?”
“Hapana!”

“Mh!” Mkunga aliguna.
“Tusaidie mama!”
“Sina uwezo wa kuwasaidia kama mna pesa tukodisheni gari tumpeleke hospitali!”

“Hatuna hata senti tano!”
“Sasa tutafanya nini?”
“Labda niende kwa mzee Mohamed nikaombe msaada!” Kasanda alisema kwa sauti ya upole.

“Wifi nisaidieni nitakufa!” Belinda alisema akiwa katika maumivu makali.
“Ngoja niende!” Alisema Kasanda na kutoka mbio kwenda kwa mzee Mohamed kuomba msaada wa gari. Aliporudi alikuwa na trekta lenye tela na Belinda alipakiwa mara moja ndani ya tela na safari ya kwenda hospitali ya mkoa, Kitete ilianza.
***************

Njia nzima Belinda aliendelea kusukuma lakini mtoto hakutoka, damu peke yake ndiyo zilivuja kwa wingi na kulichafua tela la trekta, hakuna mtu aliyekuwa na uhakika kuwa Belinda angepona katika tatizo hilo, walipofika hospitali walipokelewa na daktari alipopima alithibitisha kuwa mtoto aliyekuwepo tumboni alikuwa bado yuko hai ila mapigo yake yalikuwa yakiendelea kufifia.
“Daktari huyu mama ana tatizo gani sasa?”

“Ah! Ana Malpresentation, nafikiri alikuwa haendi kliniki kupimwa mlalo wa mtoto!” Alisema daktari Kaniki bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Kitete akimaanisha mtoto wa Belinda alikuwa amelala vibaya na kutanguliza mkono.
“Sasa tutafanya nini?”

“Hakuna la kufanya zaidi ya kumpeleka chumba cha upasuaji tukamfanyie Ceasserian section, tujaribu kuokoa maisha yake pamoja na ya mtoto!” Alijibu daktari akimaanisha ilikuwa ni lazima Belinda apelekwe chumba cha upasuaji kufanyiwa operesheni ya uzazi.
“Amekula kitu chochote tangu jana?”
“Hapana!” Kasanda na Nyamizi waliitikia.
“Safi sana!”

Kwa haraka bila kuchelewa Belinda alibebwa kwenye machela na kukimbizwa chumba cha upasuaji ambako aliandaliwa na operesheni kufanyika, madaktari walifanikiwa kumtoa mtoto katika dakika zake za mwisho, rangi yake ya ngozi ilikuwa bluu sababu ya kukosa hewa ya oksijeni na alionekana kutohema na ikalazimika afungiwe mashine ya oksijeni ili mapafu yake yafanye kazi.

“Amepata Cynosis!” Alisema daktari akiiongelea rangi ya bluu iliyokuwa katika mwili wa mtoto.
******************

Baada ya operesheni hiyo Belinda akiwa hajitambui alirudishwa moja kwa moja wodini ambako aliendelea kupata matibabu, mtoto wake alitunzwa katika chumba maalum ambako aliendelea kupewa matunzo ya kumsaidia apumue vizuri.

“Daktari mgonjwa wetu atapona kweli?” Nyamizi alimuuliza daktari Kaniki.
“Atapona ila atakuwa na matatizo kidogo yaliyosababishwa na kuchelewa kufika hospitali!”
“Matatizo gani daktari?”

“Belinda ametoboka tundu kati ya mfuko wa mkojo na njia ya uzazi! Hali hii sisi kitaalamu tunaiita Vaginal vesco fistula au kwa kifupi VVF kwa hiyo mkojo utakuwa unatoka tu wenyewe na wakati mwingine utatokea ukeni! Ni hali ngumu kidogo kuishughulikia itabidi Belinda abaki hapa hospitali kwa muda mrefu kidogo!”

“Matibabu yake ni nini?”
“Matibabu yake ni mpaka operesheni tu na hii itafanyika baada ya miezi mitatu hadi sita katika muda huu wote mkojo utakuwa unatoka peke yake!”
“Kuna tatizo jingine lililojitokeza daktari?”

“Ndiyo mguu wake wa kushoto umepoteza hisia kwa sababu mshipa wa fahamu unaoshughulika na mguu huo uligandamizwa na mtoto! Lakini hili si tatizo kubwa sana baada ya muda akifanya mazoezi hali yake itakuwa nzuri!” Alimaliza daktari na kuwaaga Nyamizi na Kasanda.

Walibaki katika masikitiko makubwa na hawakujua nini wangefanya kumsaidia Belinda katika tatizo alilokuwa nalo na hawakuwa na uhakika kama mtoto angepona.

 Miezi miwili baadaye:
Belinda alikuwa bado yuko hospitali akisubiri siku tisini zitimie ili afanyiwe operesheni, muda wote huo alimkumbuka Prosper gerezani, hakuna siku hata moja iliyopita bila kumfikiria na alitamani atoke hospitalini na kwenda gerezani Isanga kumwona lakini haikuwezekana.

Hali aliyoambiwa na daktari ilikuwepo! Mkojo ulivuja wenyewe na kulowanisha nguo zake, alitoa harufu mbaya kiasi kwamba wagonjwa wenzake hawakupenda kabisa kukaa naye!

Alishangaa mpaka muda huo baba yake alikuwa bado hajamtafuta, hilo lilimuumiza sana moyo wake na zaidi ya hilo wifi zake walikomea siku moja aliishi kwa kutegemea misaada ya ndugu wa wagonjwa wengine waliomhurumia walipokuja wodini kusalimia ndugu zao na kusikia habari yake.

Ilikuwa ni siku ya Jumamosi asubuhi daktari Kaniki alipokuwa akipita raundi wodini, alipokifikia kitanda cha Belinda alianza kutabasamu na kumwita Belinda kwa jina.

“Naam daktari!”
“Nafikiri sasa hivi hali yako ni nzuri kidogo inabidi urudi nyumbani uje baada ya mwezi mmoja ili tuone kama tutaweza kukufanyia operesheni!”
“Sawa daktari lakini......!”
“Kwani vipi Belinda?”

“Wifi zangu hawajaja kuniangalia tena, nina wasiwasi wanaweza wakawa hawataki niende tena kwao!”
“Sasa tufanye nini?”
“Daktari ungeniacha tu nikae hapa wodini!”

“Belinda haiwezekani kukaa wodini siku zote hatuna vitanda kabisa! Nakuomba tu uende nyumbani na urudi baada ya muda huo, hali yako inaendelea vizuri!” Alimaliza daktari na kuhamia kitanda cha mgonjwa mwingine.

Belinda alijikunja kitandani na kumkumbatia mtoto wake Alikuwa ni mtoto mzuri aliyefanana na baba yake Prosper kwa kila kitu.

Belinda alishindwa kuelewa angepokelewa vipi nyumbani na watu ambao walimfikisha tu hospitali na kuondoka zao! Lakini hakuwa na mahali pengine kwa kwenda mkoani Tabora zaidi ya kurudi Tutuo, siku ya Jumatatu asubuhi alimbeba mtoto wake mgongoni na kuondoka hospitali.

Alikuwa akichechemea kwa sababu mguu wake bado ulikuwa hauna fahamu vizuri pamoja na kufanya mazoezi kwa muda mrefu, hakuwa na nauli alichechemea hadi kituo cha mabasi ambako badala ya kupanda basi la kwenda Tutuo aliomba msaada katika basi la kwenda Isanga gerezani, hakuwa mvumilivu siku hiyo ipite bila kumwona Prosper! Alikuwa amemkumbuka mno na alitaka Prosper amwone mtoto wao.

“Mh! Jamani humu ndani kuna mtu amebeba samaki waliooza nini?” Mmoja wa abiria aliuliza, hali ya hewa ndani ya basi alilopanda ilikuwa nzito sababu ya harufu.

Belinda alijua harufu hiyo ilitokanana na nini lakini hakutaka kuwaeleza ukweli, swali hilo la abiria lilimuumiza sana moyo wake akajikuta akilia! Nguo zake zote zililowa mkojo uliotoka bila fahamu zake sababu ya tundu alilotoboka wakati wa kujifungua.

*Je, nini kitaendelea?*
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…