*Sehemu ya 24*
Alicia shuleni:
St.Thomas ilikuwa ni shule maarufu ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam ni shule hiyo ndiyo Alicia alisoma, ilisifika kwa kutoa elimu bora kitu ambacho Belinda na mumewe wake walitaka kumpa mtoto wao ingawa walijua wazi alikuwa ni mgonjwa.
Siku hiyo ya Jumatatu Alicia alikuwa shuleni baada ya wiki nzima kupita bila kuingia darasani sababu ya majipu yaliyokuwa yamevimba mwilini mwake, alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo waliokuwa katika chumba cha mikutano wakimsikiliza mtaalam wa Afya akiongea na wanafunzi juu ya gonjwa hatari la Ukimwi lililotishia maisha ya Watanzania na lilimuogopesha Alicia kupita kiasi.
“Dalili zake ni nyingi lakini kubwa kabisa ni homa za mara kwa mara, kukohoa kwa muda mrefu, kuharisha, mwili kuwasha na majipu!” Alisema mtaalam huyo wanafunzi wote wakiwa kimya na kumsikiliza kwa makini.
Dalili zote ambazo mtalaam alizitaja zilikuwa mwilini mwa Alicia, mwili wake ulijaa upele, ukurutu na ulimwasha kupita kiasi, alikohoa na alikuwa na majipu mengi mwilini mwake!
Homa hazikukatika, karibu kila siku alikuwa na homa na pia alipoteza uzito wa mwili na kukonda.
Dalili zilipotajwa wanafunzi wote ndani ya ukumbi waligeuka kumwangalia yeye! Kitendo hicho kilimuumiza moyo Alicia na kumfanya alie machozi.
“Kwanini mnaniangalia hivyo? Kwani mmeambiwa mimi nina Ukimwi?” Aliuliza Alicia na hakuna mtu aliyelijibu swali lake.
Hakutaka tena kubaki shuleni alitoka nje ya ukumbi na kutembea taratibu kwenda nyumbani kwao njia nzima akilia machozi! Hakuwa tayari kukubali kuwa alikuwa na Ukimwi, aliziona dalili alizokuwa nazo ni za ugonjwa mwingine wowote lakini si Ukimwi.
Alipofika nyumbani kwao aliingia ndani na kwenda moja kwa moja hadi chumbani kwa mama yake, alimkuta amejilaza kitandani, mama alishangazwa na hali aliyokuwa nayo mtoto wake.
“Vipi Alicia?”
“Mama niambie ukweli!”
“Ukweli gani mwanangu?”
“Mama kwanini mnanificha?”
“Tunakuficha nini Alicia?”
“Daktari ametufundisha kila kitu juu ya Ukimwi! Dalili zote za Ukimwi mimi ninazo, mama niambie ukweli je, mimi nina Ukimwi?”
Badala ya kujibu swali Belinda alianza kulia akiwa amemkumbatia mtoto wake Alicia mikononi, alitamani amwambie ukweli lakini aliogopa!Alijua ungemuumiza sana kwani siku zote alionekana kutishwa sana na ugonjwa huo.
“Mama usilie tafadhali niambie ukweli na kama ni Ukimwi mimi niliutoa wapi mbona bado mdogo? Nani aliniambukiza? Au ni wewe mama?” Alicia aliendelea kuuliza maswali mfululizo.
Belinda aliendelea kulia hakuwa na jibu la kumwambia mtoto wake, ilikuwa ni siku mbaya sana kwake, siku aliyotakiwa kueleza ukweli ambao aliuficha kwa muda mrefu.
Belinda aliendelea
kutokwa na machozi
mbele ya mtoto wake, hakuwa na kitu cha kumweleza Alicia aliyetaka kuufahamu ukweli kuhusu afya yake baada ya kuugua na kuteseka kwa muda mrefu.
Hakuwa tayari kuitoboa siri ya ugonjwa wa mwanae alijua wazi alikuwa mgonjwa na ugonjwa uliomsumbua ulikuwa ni Ukimwi uliompata yeye kutoka kwa mume wake naye akaufikisha kwa mtoto wao.
Alikuwa na uhakika asilimia mia moja hata yeye na mume wake walikuwa wagonjwa wa ugonjwa huo wakisubiri kifo! Lakini kwa upande wao aliona walistahili kwa sababu walishiriki tendo la ndoa! Alicia hakuwa na sababu yoyote ya kufa kwa kosa ambalo hakulifanya kifo chake kilikuwa cha damu isiyo na hatia.
“This is a death of an innocent blood!”(Hiki ni kifo cha damu isiyo na hatia!) Belinda alijikuta akitamka maneno hayo huku akilia machozi, Alicia alipoyasikia alishtuka.
“Mama unasemaje?”
“Nimesema hiki ni kifo cha damu isiyo na hatia, lakini si makosa yangu mwanangu ni makosa ya baba yako!”
“Nini mama mbona sikuelewi!?” Alicia aliuliza kwa mshangao, alishindwa kuvumilia kumwona mama yake akilia naye machozi yalianza kumtoka.
“Mama hakuna sababu ya kulia tafadhali niambie ni kosa gani baba alifanya?” Alicia aliendelea kudadisi.
Kabla Belinda hajafungua mdomo kujibu swali hilo mlango ulifunguliwa na Prosper akaingia, alishangazwa na hali aliyoikuta sebuleni!
Mke wake na mtoto walikuwa wamekumbatiana wakilia na kwa jinsi mwili wa Alicia ulivyokuwa umekondeana uliishia katika mikono ya mama yake.
“Belinda vipi tena?”
Aliuliza Prosper lakini hakuna jibu lililipatikana na aliendelea kuuliza tena na tena lakini bado Belinda hakujibu kitu chochote zaidi ya kumwaga machozi.
“Nini kimetokea mke wangu?”
“Alicia anataka kuufahamu ukweli!”
“Ukweli gani?” Prosper aliuliza.
“Juu ya afya yake, mimi nimeshindwa kumtobolea ukweli huo ni bora umweleze mwenyewe!” Alisema Belinda.
“Baba nielezeni ukweli nimeteseka sana na ugonjwa huu, ni miaka mingi naumwa lakini hamjawahi kunieleza naumwa nini lakini leo nataka kujua au ni Ukimwi nini? Nielezeni tu msiogope ili nikisubiri kifo changu vizuri!” Alicia aliongea kama mtu mzima, siku hiyo wazazi wake walimshangaa sana.
Prosper alitetemeshwa na swali la Alicia, alishindwa kuelewa ni jibu gani angempa mtoto wake, ingawa alielewa wazi ni kitu gani mtoto wake alitaka kufahamu! Ni yeye ndiye alikuwa na wajibu wa matatizo yote ndani ya familia yake na ni yeye ndiye aliyeuingiza Ukimwi ndani ya nyumba yake kwa sababu ya tabia ya kishoga aliyojifunza gerezani.
“Mwanangu Alicia!”
“Naam baba!”
“Ni mimi mwanangu ni mimi ninayekutesa!”
“Kwani ulifanya nini baba?”
“Ni mimi ninayekuua mwanangu!” Alisema Prosper na baadaye kuangua kilio.
“Ninahitaji kusamehewa sana Alicia na si wewe tu bali hata mke wangu anisamehe ninajua sote tutakufa kwa sababu ya uzembe wangu mimi!”
“Kwanini unasema hivyo baba?”
“Sikiliza Alicia, nilikutana na mama yako miaka mingi iliyopita tukiwa shuleni na tukapendana,lakini nilipata bahati mbaya ya kufungwa kwa kosa ambako sikulifanya, muda wote uliokuja kule nilikokuwa nikiishi nilikuwa gerezani lakini hatukukuambia ukweli ni huko gerezani ndiko nilikoambukizwa Ukimwi ambao mimi niliupitisha hadi kwa mama yako na kutoka kwa mama yako ndiyo ulifika kwako nisamahe mwanangu!”
“Kwa hiyo mimi naumwa Ukimwi baba?Kwahiyo nitakufa?” Aliuliza Alicia huku akilia machozi.
“Huo ndio ukweli mwanangu si wewe tu utakayekufa bali mimi pia na tutakufa sababu ya baba yako lakini hakuna sababu ya kumlaumu tumekwishachelewa hivyo ni vyema kumsamehe kwani maji yakimwagika hayawezi kuzoleka, sawa mwanangu Alicia?” Aliuliza Belinda akitegemea mtoto wake angetoa msamaha lakini alishangaa kuona Alicia akiendelea kulia kwa uchungu na kuwalaumu wazazi wake kwa kila kitu.
“Siwezi kuwasamahe kwani sikustahili kufa kwa sababu ya makosa yenu! Ee Mungu kwanini uliruhusu jambo hili linitokee mimi?”
Alicia aliendelea kulia machozi! Maneno mengi aliyoyasema hayakuwa ya mtoto wa umri wake!
“Nisamehe mwanangu!” Alisema Prosper huku akimbeba Alicia na kumweka miguuni pake.
“Kwanini nikusamehe baba?”
“Nisamehe ni makosa yangu ndiyo yanayokutesa!” Aliendelea kusema Prosper.
Alicia aliendelea kulia na kuongea maneno ya kuwalaumu wazazi wake kwa kitendo walichokifanya kusababisha yeye asiifaidi dunia na kuyafupisha maisha yake, aliwalaumu zaidi kwa kitendo cha kutomwambia ukweli kwa kipindi kirefu na kutojali afya ake ili aishi maisha marefu zaidi.
*Je, nini kitaendelea?*