JOTO LA MOTO
JF-Expert Member
- Apr 11, 2018
- 766
- 561
SCRIPT ZA IMA
KUTOKA:KWA MSANII JOTO LA MOTO.
SEHEMU YA KWANZA.
NYUMBANI KWA MR BEN-SEBULENI-USIKU.
Mama Esta, Mama,30, na Mr Beni, bwana, 35, wameketi sofani wakipata chakula huku wakipeana michapo ya hapa na pale, upande mwingine kwenye meza ya chakula wapo Meki, kijana barubaru, miaka 17, Esta, binti, miaka 7, na Sia, mdada, miaka 18 nao wakipata chakula, chini ya meza Meki ananyoosha mguu wake na kumgusa Sia, Sia anageuka na kumkata Meki jicho na kumnyooshea kidole huku akitoa tabasamu, na Meki anarudisha tabasamu pamoja na ishara zinazomsababisha Sia kucheka huku akijizuia sauti isitoke, Mr Beni na Mama Esta bado wakiendelea na michapo yao.
NYUMBANI KWA MR BENI-JIKONI-BAADAE.
Sia yupo kwenye sinki anaosha vyombo, “nikusaidie” Sia anashtushwa na sauti ya Meki nyuma yake, Sia anageuka kumuangalia Meki na kutabasamu kisha anasogea pembeni, Meki anasogea kwenye sinki na kuanza kuosha vile vyombo, “shauri yako Meki Mama yako akikukuta hapa tena leo mimi sipo” anasema Sia, “wamesha lala” anasema Meki, “wewe sema tu hivyo na unakumbuka juzi alikuja sebuleni saa tano” anaongeza Sia, “akija nitamwambia tu ukweli” anasema Meki, “ukweli gani?" anauliza Sia, “kwamba nakusaidia” anasema Meki, “mmh” anaguna Sia, kinapita kimya kifupi “kalale utachelewa shule kesho..shauri yako” anasema Sia, “sichelewi” anasema Meki huku akiendelea kuosha vile vyombo, kinapita kimya kifupi “Meki una roho nzuri” anasema Sia, Meki anageuka na kumuangalia Sia huku wote wakiachia tabasamu usoni.
NYUMBANI KWA MR BENI-MIEZI KADHAA BAADAE
Nyuma ya nyumba, Sia ameketi kwenye jiwe, akiwa amejiinamia, mlangoni anatoka Mama Esta na kwenda pale alipoketi Sia, “bado unajisikia vibaya?” anauliza Mama Esta, Sia anashtuka na kuinua kichwa, “kidogo afadhali dada” anasema Sia kwa sauti ya kichovu, “kesho asubuhi tunaenda hospitali ukapimwe” anasema Mama Esta huku Sia akibaki anatoa macho.
Kwenye kona anakuja Meki akiwa amevaa sare za shule, anasimama na kuwaangalia Sia na Mama Esta wakiongea, Mama Esta anaondoka, Meki anakwenda pale alipoketi Sia, “umemwambia?” Meki anamuuliza Sia kwa sauti yenye hofu, “sijamwambia” anajibu Sia, Meki anashusha pumzi kama Mtu aliyepata ahueni ya jambo “kuna Nesi rafiki yangu nimeongea nae..amesema kesho nikupeleke” anasema Meki, Sia anageuka kumuangalia Meki kwa jicho kali, “hivi niongee lugha gani uelewe Meki” anasema Sia kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo, “sitoi” anasema Sia, Meki anashusha pumzi, “sawa” anasema Meki kwa sauti ya chini huku anainuka, “sasa unitaje uone nitakachokufanya” anasema Meki, “utanifanya nini?” anasema Sia kwa sauti ya chini lakini yenye shari, “wewe niharibie tu uone” anasema Meki, “na usifikiri nacheza” anaongeza Meki kwa sauti iliyojaa vitisho huku akiondoka kuelekea ndani ya nyumba,na Sia akimsindikiza na jicho kali.
NYUMBANI KWA MR BEN-SIKU ILIYOFUATA-SEBULENI
Mama Esta ameketi kochini, “Sia” anaita Mama Esta, “bee” inasikika sauti ya Sia, sekunde chache baadae Sia anafika, “hebu keti hapo” Sia anaketi, Mama Esta anashusha pumzi nyepesi, “enhe..majibu yako nadhani umeyaona?” anasema Mama Esta, “sasa naomba uniambie ni nani muhusika” anasema Mama Esta kwa sauti ya chini na ya msisitizo, Sia anabaki kimya, Mama Esta anamuangalia Sia, “nasubiri jibu Sia?” anasema Mama Esta, Sia bado anabaki kimya akiangalia chini, inasikika honi ya gari, Mama Esta anashusha pumzi, “kesho nikitoka kazini nataka jibu” anasema Mama Esta, “andika hata kwenye karatasi unipe kama kuongea huwezi” anasema Mama Esta, Sia anabaki kimya, “hebu niondokee hapa”, Mama Esta anamkaripia Sia, Sia anainuka na kuondoka, mlango unafunguka, anaingia Mr Beni, “pole” Mama Esta anamwambia Mr Beni huku Mr Beni akiweka funguo za gari mezani na kuketi kwenye kochi.