Simulizi: Dada wa kazi

Simulizi: Dada wa kazi

SCRIPT ZA IMA.
DADA WA KAZI.
SEHEMU YA PILI
.
GENGENI-SIKU INAYOFUATA.
Sia anafika gengeni, “karibu switii” anasema Obo, kijana muuza genge, miaka 22, “vipi bebii wangu” anaongeza Obo kwa sauti ya bashasha huku akitoka gengeni na kuja upande alipo Sia, “naomba usinisumbue..nipe mboga mimi nirudi nyumbani” anasema Sia kwa sauti isiyo na mzaha, “mh” Obo anaguna na kurudi gengeni, “unataka nini leo maana naona upo vibaya” anasema Obo, “nipe nyanya za mia tano na karoti za mia mbili” anasema Sia, “alafu jibu langu utanipa lini Siaa?” anauliza Obo huku akimpatia Sia Nyanya na karoti, “jibu gani?” anauliza Sia kwa ukali, “acha kunizengua basi Siaa” anasema Obo, “unataka nianze tena upya?” anasema Obo, “kumbuka na mimi nina moyo eti Sia” anaendelea Obo, “achana na mimi bana” anasema Sia kwa ukali huku akimpatia Obo sarafu ya shilingi mia tano na ya mia mbili, “hiyo ya kwako” anasema Obo, Sia anabaki anamuangalia Obo kwa ukali kwa sekunde kadhaa kisha anaweka zile pesa pale mezani na kugeuka kuondoka “nasubiri jibu” anapayuka Obo huku Sia akitokomea.

NYUMBANI KWA MR BEN-JIONI.
Sia na Esta wameketi kochini wakiangalia TV, anaingia Meki akiwa kwenye sare za shule, Meki anaona Sia akiwa amefumbata kipande cha limao mkononi, anaketi na kushusha pumzi, “dingi na mama wako wapi?” anauliza Meki, “wameenda kanisani” anajibu Esta, Meki anamuangalia Sia kwa muda, Sia naye anageuka kumuangalia Meki, “siamini kama ungekuja kuwa katili hivi Meki?” anasema Sia, “ukatili gani?” anauliza Meki, Sia anashusha pumzi, “Mungu akusaidie tu huko uendako” anasema Sia, “wewe sema chochote tu unachojisikia..ila ujue sitaki mazoea” anasema Meki, “mazoea ya nini?” anauliza Esta, “wewe hayakuhusu angalia TV kule” Meki anambwatukia Esta, “usifikiri sina stori za Mpare Muuza genge” Meki anamwambia Sia, Sia anageuka kumuangalia Meki kwa mshangao, wanabaki wanaangaliana, Sia anashusha pumzi na kugeuka kuangalia kwenye TV, inasikika honi ya gari, “Daddy” anapayuka Esta huku yeye na Sia wakiinuka na kutoka,Meki anabaki ameketi akibofya bofya remote ya TV.

GENGENI KWA OBO-MCHANA.
Sia anafika gengeni, “karibu bebii” anasema Obo kwa bashasha huku akitoka gengeni na kuja alipo Sia, “upo tayari tukachukue zawadi yako?” anasema Obo, “kuichukua wapi?” anauliza Sia huku ameukunja uso, “si nyumbani?” anasema Obo, “ungetaka kunipa ungenipa wala usinisumbue mimi” anasema Sia, “ushaniona mimi ni wa kwenda kwenye nyumba za watu hovyo” anaongeza Sia, “nipe biringanya mbili nasubiriwa kupika” anasema Sia, Obo anarudi gengeni, anakuja Kibo, kijana wa miaka 21, anasimama pembeni, Obo anachukua biriganya mbili na kumpatia Sia, Sia anatoa noti ya shilingi elfu moja, Obo anatikisa mabega kuashiria hataki kuipokea, Sia anageuka na kuondoka, Kibo anasogea gengeni, “huyu Demu bado anakuzengua tu?” anauliza Kibo, “mambo mazuri hayataki haraka Kibo” anasema Obo.
Ndiyo maana wauza genge wanachelewaga sana kuinuka... mtaji wenyewe mdogo bado wanahonga honga...


Cc: mahondaw
 
"DADA WA KAZI"
SEHEMU YA MWISHO.


NYUMBANI KWA OBO-CHUMBANI-MCHANA.
Sia ameketi juu ya kitanda, kwenye chumba kidogo kilichosongamana vitu, kitanda, stuli, jiko la mchina, kiti cha plastiki na vikorokoro vingine kadhaa, Sia ametulia akiangalia huku na kule, mlango unafunguka, anaingia Obo akiwa na chupa ya soda na mfuko mdogo mweusi, “yaani leo siamini umekuja..mpaka nahisi kuchanganyikiwa” anasema Obo kwa bashasha huku akiwa amesimama na chupa ya soda na mfuko wake mkononi akimshangaa Sia, Obo anaweka chupa na ule mfuko juu ya stuli, “sasa pale gengeni umemuacha nani?” anauliza Sia, “yupo yule rafiki yangu Kibo” anasema Obo huku akiifungua ile soda, “karibu” anasema Obo huku anaketi kwenye kiti, “siku ya leo nitaiandika kwenye kitabu changu” anasema Obo, Sia anamuangalia Obo akimshangaa, “kwa nini?” anauliza Sia, Obo anashusha pumzi, “hujui tu furaha niliyonayo moyoni kwa wewe kufika hapa Sia” anasema Obo kisha anaufungua mfuko ule aliokuja nao wenye Kuku na chips.

NYUMBANI KWA MR BENI-MCHANA
Sia yupo uwani anaanika nguo, Meki anatoka ndani na kusimama barazani, "nasikia unaondoka..safari lini?” anauliza Meki, Sia anabaki kimya na kumkata Meki jicho, Sia anamalizia kuanika nguo, anachukua ndoo na kuingia ndani.

NYUMBANI KWA MR BENI-SEBULENI-NDANI
Sia anaingia na ndoo mkononi, Esta yupo mezani anakula, “dada Sia nitakumisi” anasema Esta, Sia anaiweka ndoo chini na kwenda kwa Esta na kuketi pembeni, “usijali Esta mdogo wangu..ipo siku tutakutana tu” anasema Sia, “sisi ni binaadamu..milima ndio huwa haikutani” anaongeza Sia huku amemshika Esta begani.

NYUMBANI KWA OBO-CHUMBANI-MCHANA.
Obo ameketi juu ya kitanda, Sia ameketi kwenye kiti amejiinamia, “ulisema kuna kitu muhimu unataka kuniambia” anasema Obo, Sia anabaki anaangalia chini kwa muda kisha anainua kichwa na kushusha pumzi “nahisi nina dalili za mimba” anasema Sia kwa sauti ya chini yenye mawimbi ya uoga kisha anageuza macho na kuangalia pembeni, Obo anabaki na butwaa bila kuongea neno, zinapita sekunde kadhaa, Sia anageuka na kumuangalia tena Obo ambaye bado amebaki na butwaa, "upo serious?" anauliza Obo kwa mshangao, "tangu nimetoka hapa siku ile sijaona siku zangu", Obo anabaki ametoa macho,“ila Sia..tumekutana mara moja tu?” anasema Obo, “unaijua biology Obo?” Sia anamuuliza Obo, “siijui..lakini inanishangaza” anasema Obo, “ndio hivyo..hata mara moja mimba inaweza kutunga Obo” anasema Sia, “na sina mtu zaidi yako Obo” anasema Sia, Obo anashusha pumzi, wanakuwa kimya kwa sekunde kadhaa,"na ukithibitisha ni mimba umepanga kufanya nini Sia", Sia anabaki anaangalia chini,"nitakusikiliza wewe", anasema Sia kisha wote wanabaki kimya, Sia akiangalia chini, na Obo anamuangalia Sia, “najua hii ni habari nzito sana kwako Obo” anasema Sia huku bado anaangalia chini, “ngoja nikuache upate muda wa kutafakari” anaongeza Sia,Obo anashusha pumzi nzito, “nitakabiliana na matokeo yoyote Sia” anasema Obo, “mimi ngoja nirudi nyumbani” anasema Sia huku anainuka, Obo naye anainuka, “Sia", Obo anaita na kusita, "kama ndivyo itakavyokuwa..kwa nini usihamie tu hapa tuishi wote?” anasema Obo, Sia anashusha pumzi na kuangalia juu, kisha anaangalia pembeni, “sio rahisi hivyo kama unavyofikiri Obo..ngoja nikafikirie” anasema Sia huku akiufungua mlango na kutoka, Obo naye anatoka.

MIAKA KUMI NA TANO BAADAE

UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA KILIMANJARO-MCHANA.
Meki, kijana wa miaka 32, anatokea sehemu ya abiria wanaowasili, anafika kwa Mr Beni mwenye miaka 50, Mama Esta, miaka,45 na Esta, miaka 22, wanakumbatiana huku wote wakiwa wenye furaha na bashasha za hali ya juu, baada ya shamra shamra zile fupi za mapokezi wanaelekea lilipo gari, wanaingiza mabegi na kisha wote wanaingia garini na kuondoka.

NYUMBANI KWA MR BENI-SEBULENI-MCHANA-
Meki, Esta, Mama Esta, Ben, Mr Chuo, Masawe na Mama keni wameketi wakiwa na vinywaji na vyakula vya aina mbalimbali, “karibu tena Tanzania Meki” anasema Mr Chuo, “nashukuru sana Anko” anasema Meki, “miaka kumi Ulaya mzee..mpaka tumekusahau” anasema Mr Chuo, “ni tisa na nusu sio kumi” anasema Meki, “kwa nini umeamua kurudi..na niliambiwa una kazi nzuri sana London” anasema Mama Keni, Meki anashusha pumzi, “kwanza siku zote nyumbani ni nyumbani Mama mdogo..pili nilichoacha kule ni kazi tu..lakini elimu iliyo kichwani nimekuja nayo” anaongeza Meki, “kwa hiyo utafungua ofisi hapa Arusha?” anasema Masawe, “Mzee alishaweka mipango yote sawa..Mungu akipenda wiki ijayo naanza kazi Anko” anasema Meki, "hongera sana Meki" anasema Mama Keni, wanabaki kimya kwa muda kidogo, “kuna wakati maisha mazuri sio kila kitu..Mtu unahitaji familia yako” anasema Meki, “tuliambiwa umeoa na unaishi na Mkeo ila naona umekuja mwenyewe” anasema Masawe, “ni kweli ila Mama yule wa kizungu tulishindwana tukaachana tangu miaka miwili iliyopita”, “kwa hiyo Watoto umemuachia” anauliza Mr Chuo, “imebidi” anasema Meki huku wote wakiendelea kupata vyakula na vinywaji.

NYUMBANI KWA MR BENI-BAADAE USIKU.
Meki na Mr Lao, Mzee wa miaka 68 hivi, wameketi kwenye sofa, “kwa hiyo utaalamu wote ule wa Ulaya bado ikashindikana?” anauliza Mr Lao, “Mjomba..wale Watoto wawili tuliokuwa tunaishi nao wote nilimkuta nao yule Mwenzangu” anasema Meki, Mr Lao anashusha pumzi, “nakumbuka holiday moja nilienda Russia..nikaenda kucheza mchezo wa kuteleza kwenye barafu..nikapata ajali mbaya sana nikateguka kiuno” anasema Meki, “kumbe sikujua baada ya miezi mitatu ya matibabu ningeishia kubaki bila uwezo wa kuzalisha tena mbegu za uzazi” anasema Meki kwa hisia, Mr Lao anashusha pumzi, “Meki kijana wangu..haupo peke yako kwenye tatizo kama hilo” anasema Mr Lao, “wapo wengi tu hawajabahatika kupata Watoto na bado wanaishi raha mustarehe”, “kwangu ni tofauti Mjomba Lao” anadakia Meki, “mimi nina mtoto” anasema Meki, Mr Lao anashtuka, anakuja Mama Esta na kuketi kwenye sofa, “Mama yako ana hiyo taarifa?” anauliza Mr Lao, “taarifa gani?” anauliza Mama Esta, “Meki anasema kumbe aliacha Mtoto Tanzania kabla hajaenda Ulaya” anasema Mr Lao, Mama Esta anabaki anatoa macho, “eti unasemaje Meki?", “unamkumbuka Sia..ile mimba aliyoondoka nayo ilikuwa ni yangu” anasema Meki, Mama Esta anabaki kimya kwa muda kisha anashusha pumzi, “jamani..sasa yule si tayari ana maisha yake huko?” anasema Mama Esta, “hata kama..mimi nahitaji damu yangu..na hicho ndio kilichonirudisha Tanzania Mama” anasema Meki kwa hisia, “Ulaya kule nilikuwa na kila kitu” anasema Meki, “kule nagombewa kwa utaalamu wangu wa computer” anaongeza Meki, “lakini imenibidi niache kila kitu nirudi Tanzania kwa ajili ya damu yangu” anasema Meki huku akishusha pumzi nzito, Mr Lao na Mama Esta wote wamebaki wakimuangalia Meki vile anavyoongea kwa hisia kali, Mama Esta na Mr Lao wanaangaliana, “sasa unamtafutia wapi huyo Sia Mwanangu..maana hata hatujui alipo”, “kuna mtu nilishampa kazi tangu nikiwa nipo London” anasema Meki, Mr Lao na Mama Esta wanabaki kimya wakimuangalia Meki.

SHULE YA MSINGI MERU.
Gari aina ya RAV 4 nyeupe imepaki pembeni ya uwanja wa shule, ndani yupo Meki na Duso, Watoto kadhaa wanatoka shuleni, Duso anashtuka, “ndio yule” anasema Duso na kumshtua Meki, Meki anamuangalia Bremi, kijana mdogo, miaka 14, akipita, Meki anafungua mlango na kutoka kwenye Gari, anamfuata Bremi na kumfikia, “dogo hujambo?” Meki anamsalimia Bremi, Bremi anashtuka na kugeuka kwa Meki, “shikamoo” anasalimu Bremi, “marahaba” anaitikia Meki huku akitoa seti mpya ya kompasi na kumpa Bremi, Bremi anasita kisha anapokea, “mimi naitwa Mwalimu Maiko” anasema Meki, “nataka nikufundishe tuition ya hisabati” anaongeza Meki huku Bremi bado amebaki na butwaa, “hutaki kuwa mtaalamu wa computer?" Meki anamuuliza Bremi, Bremi anabaki kimya, “unaishi wapi?” anauliza Meki, “Sekei”, “unaishi na Mama yako?” anauliza Meki, “naishi na Mama na baba”, “ukifika msalimie sana Mama..mwambie Mwalimu Maiko anamsalimia..ila nitakuja siku moja kumsalimia” anasema Meki na kuondoka kurudi garini, “hatua kwa hatua” anasema Duso baada ya Meki kuufungua mlango na kuingia garini, “ukishazoeana nae kazi inakuwa rahisi kama kumsukuma mlevi” anaendelea Duso huku Meki akiwasha gari na kuondoka.

NYUMBANI KWA BREMI-USIKU.
Sia na Bremi wameketi, Sia akiangalia lile kompasi, “umesema anaitwa Mwalimu nani?” anauliza Sia, “Mwalimu Maiko” anasema Bremi, “ulishawahi kukutane nae kabla?” anauliza Sia, “hapana” anajibu Bremi, Sia anabaki mwenye butwaa, “amesema niwasalimie..naye atakuja kuwasalimia” anasema Bremi, Sia anshusha pumzi, “jamani..mbona hata hilo jina halinijii kichwani” anasema Sia.

MTAA WA SEKEI-MCHANA.
Toyota RAV 4 inafika na kusimama, ndani yupo Duso, Meki na Bremi, “mwambie Mama Mwalimu Maiko kaja kumsalimia” anasema Meki, Bremi anateremka na kuondoka, dakika chache baadae wanakuja Sia na Bremi, Duso na Meki wameketi kwenye baraza ya Mgahawa jirani na gari yao, “yule pale” Bremi anamwambia Sia huku akionyesha walipoketi Duso na Meki, Sia anasogea akiwa na mshangao, anafika walipoketi Duso na Meki, “Sia” Meki anaita huku anainuka, Sia anashtuka, “Meki” anaita Sia kwa mshtuko na bashasha, wanakumbatiana kwa furaha, “umekuwa libaba” anasema Sia, “na wewe umekuwa mmama” anasema Meki, “karibu ukae” anasema Meki, “hapana siwezi kukaa huku..naomba ukaribie nyumbani sio mbali na hapa Meki” anasema Sia, “nyumbani nitakaribia tu Sia..ila kwanza kuna jambo nataka kukuuliza” Meki anamwambia Sia, “jambo gani?” anauliza Sia kwa mshangao na kubaki kimya kwa muda, “ndio umsikilize tu mara moja Mama Bremi” anasema Duso huku akimshika Bremi mkono, “sisi tukae pale Mama aongee na Mwalimu” Duso anamwambia Bremi huku wakielekea kwenye meza iliyopo pembeni na kuketi, Sia na Meki wanaketi, “utakunywa nini?” anauliza Meki, “hapana sitokaa hapa zaidi ya dakika tano” anasema Sia, “tena ni heshima tu kwa kuwa ni wewe Meki sikaagi huku mimi” anasema Sia, “ni hivi Sia” anasema Meki, “alafu hilo jina lilishakufa zamani Meki” anasema Sia, “niite Pendo au Mama Bremi” anasema Sia, “sawa” anasema Meki na kushusha pumzi, “nilitaka tuongee kuhusu Mtoto” anasema Meki, Sia anashtuka, “amefanyaje tena Mungu wangu?” anauliza Sia kwa mshtuko, “ni hivi Sia..sorry Pendo..nadhani unakumbuka vizuri kuwa uliondoka kwetu na mimba yangu” anasema Meki, sia anabaki akimtolea Meki macho, “unasemaje Meki?” anauliza Sia kama vile hakusikia kabisa kilichosemwa na Meki, “uliondoka ukiwa na uja uzito wangu sidhani kama umesahau” anasema Meki, “wee” anasema Sia kwa mshtuko huku anainuka, “sikuondoka kwenu na mimba mimi” anasema Sia, “na naomba usinifuate kuanzia leo Meki” Sia anaondoka, anamfuata Bremi pale pembeni mezani, “twende” Sia anamwambia Bremi huku anamuinua na wanaondoka.

NYUMBANI KWA KINA BREMI-SIKU KADHAA BAADAE-MCHANA.
Bremi na Gumbo,kijana, 23, wanafika nyumbani, Sia yupo sebuleni akichagua mchele kwenye ungo, “shikamoo Mama” anasalimu Bremi, “marahaba Mwanangu..umeonana na Mwalimu Kesi?” Sia anamuuliza Bremi, "hapana ila Mjombaa alienda ofisini", "nimeenda kwa Mwalimu Mkuu” anasema Gumbo, “ila wanasema mpaka sasa bado huyo bwana hajaonekana tena pale shuleni..na wameshaandaa mtego” anaongeza Gumbo, “ila kuna hii barua Bremi amepewa” anasema Gumbo huku akimpatia Sia bahasha ndogo ya kaki, “Mtu gani?” anauliza Sia, “Magembe” anasema Bremi, “Magembe ni nani? Anauliza Sia, “tupo naye darasani”, huku Sia akifungua ile bahasha, “yeye ameipata wapi?” anauliza Sia, “anasema kuna Mtu kampa” anasema Bremi huku Sia akiitoa karatasi kwenye ile bahasha na kuanza kuisoma, “nina uhakika wa asilimia mia moja kuwa huyo Bremi ni mwanangu Sia..sijali utasema nini ila nitafanya kila niwezalo damu yangu haitopotea” Sia anasoma kilichoandikwa kwenye barua ile huku akionekana kushikwa butwaa na kuwa kama mtu aliyeishiwa nguvu baada ya kumaliza kuisoma, anashusha pumzi na kujiegemeza pale kochini.

OFISINI KWA MEKI-DAY
Meki ameketi kwenye kiti kikubwa, pembeni ameketi Mazo, kijana, 33, na Duso, “nafanya hivi kwa sababu yule Mama amekataa kuonyesha ushirikiano Mr Mazo” anasema Meki huku Mazo akiandika kwenye kijitabu, “labda anapata ugumu kwa kuwa mume anayeishi naye kwa sasa hajui hilo?” anasema Mazo, “hiyo sio shida yangu Mr Mazo” anasema Meki, “nadhani kwanza tungejaribu kuonana na mume wake kabla ya kwenda huku kwenye sheria Mr Meki” anasema Mazo, “mumewe anafanya shughuli gani?” anauliza Mazo, “kwa sasa ni pastor” anasema Duso, “na tayari wana Watoto wengine watatu” anaongeza Duso, wanabaki kimya kwa muda huku Mazo akiandika kwenye kijitabu chake, “nadhani kwanza tumtafute huyo Pastor” anasema Mazo, “ushauri mzuri” anasema Duso, “tusipoteze muda wazee” anasema Meki, “wala hatupotezi muda Mr Meki” anasema Mazo.

NYUMBANI KWA KINA BREMI-DAY
Sia, Obo na Mzee Mude, baba wa makamo,68, wameketi, Obo amejiinamia huku mikono yote miwili ikiwa kaiegesha kwenye kichwa chake kama Mtu aliyezidiwa na mawazo, na Sia ametulia akiangalia chini, “ulipaswa kuniambia ukweli kuhusu Bremi tangu siku ya kwanza Sia” anasema Obo huku bado amejiinamia,"Pastor..nadhani Mama Bremi amejieleza vizuri hali iliyokuwa wakati ule" anasema Mzee Mude, wanabaki kimya kwa muda “na kumbuka lolote utakaloamua hapa Pastor liwe ni kwa muongozo wa Mwenyeenzi Mungu” anaongeza Mzee Mude, Obo anabaki ameinama, kisha anainua kichwa na kumuangalia Sia, “Mke wangu” anasema Obo, Sia anainua kichwa kumuangalia Obo, “tumetoka mbali na tumepitia mengi” anasema Obo, “yaliyotokea yametokea” anaongeza Obo na kubaki kimya kwa muda, “nitafanya kila linalowezekana..Mwanetu Bremi abaki hapa ndani” anasema Obo, Sia anasogea na kumkumbatia Obo huku akibubujikwa na machozi, “umeongea vizuri sana Pastor” anasema Mzee Mude, "nisamehe kwa yote Mume wangu" anasema Sia huku anabubujikwa machozi, "nimeshakusamehe Mama Bremi" anasema Obo..

OFISINI KWA MEKI-MCHANA.
Meki ameketi akitumia computer iliyopo mezani, Simu ya mezani inaita, anaipokea, “unasemaje Leila?..mwambie aingie” anasema Meki kwenye simu kisha anairudisha simu mezani, sekunde chache baadae mlango unafunguliwa na Leila akimruhusu Mzee Mude aingie, “heshima yako Mzee” anasalimu Meki, “nashukuru kijana wangu” anajibu Mzee Mude, “karibu” anasema Meki huku akimuelekeza kiti kilichopo pale mbele, Mzee Mude anaketi, “mimi ndiye tuliongea jana kwenye simu” anasema Mzee Mude, Meki anashusha pumzi, “Mzee sitobadili msimamo kwa hiyo msipoteze muda” anasema Meki, “tusubiri tu haki ipatikane mahakamani” anasema Meki, “sikatai kijana wangu” anasema Mzee Mude, “tumekaa mezani na mmekataa kunipa Mwanangu” anasema Meki, “ni hivi kijana” anasema Mzee Mude, “yule kijana maisha yake yote ameishi pale na wenzake..na Wazazi wake” anasema Mzee Mude, “hata kama Mahakama itakupa hiyo haki bado hutokuwa na baraka ya Mama wa Mtoto..baraka ya Baba aliyemlea tangu akiwa na siku moja mpaka leo ana miaka kumi na nne” anasema Mzee Mude, Meki anashusha pumzi na kubaki kimya, “hata kama ukifanikiwa hicho unachotaka..unadhani Bremi ataridhia kuja kwako na kuacha familia aliyoizoea?” anaongeza Mzee Mude “Mzee” anasema Meki na kutulia kwa muda, “wala sikutegemea utakuja na jipya” anasema Meki, “tumeshafungua shauri mahakamani..tuache sheria ichukue mkondo wake” anasema Meki, Mzee Mude anashusha pumzi, “sawa Mwanangu..mimi ngoja nikuache..nilikuja niongee hayo tu” anasema Mzee Mude huku anainuka na kutoka, Meki anabaki ametulia akiwa amejiegemeza kwenye kiti kama Mtu anayetafakari jambo, zinapita dakika kadhaa, mlango unagongwa, "ingia" anasema Meki, mlango unafunguka anaingia Muze akiwa na faili na kitabu kidogo mkononi, “mipango yote ipo tayari Kaka” anasema Muze huku akiketi, “muda si mrefu tutapangiwa siku ya kuanza kusikiliza shauri” anasema Muze huku bado Meki akiwa amekaa kimya, Meki anashusha pumzi huku akibaki anamuangalia Muze, "nimekuelewa kaka" anasema Meki.

WIKI KADHAA BAADAE-NYUMBANI KWA MR BENI.
Meki ameketi kochini, anakuja Mama Esta akiwa na thermos, anaifungua na kumimina chai kwenye kikombe kilichopo pale mezani, kisha anaketi, “kwa hiyo sasa umeamuaje Mwanangu?” anauliza Mama Esta, “maana hata sisi hatukutegemea mambo bado yangekuwa magumu hivyo hata baada ya majibu ya DNA” anasema Mama Esta, Meki anashusha pumzi, “bado hata sijajua la kufanya Mama” anasema Meki kwa sauti ya kukata tamaa, “sikujua kama hata Bremi naye angenigomea mbele ya uso wangu” anaongeza Meki huku akilengwa machozi, Mama Esta anashusha pumzi, wanabaki kimya kila mmoja akionekana kuwaza la kwake.

MIEZI MIWILI BAADAE-MTAA WA KIJENGE JUU.
Duso amesimama nje ya ukuta wa nyumba akiwa na simu sikioni, “sasa hapo ulizieni tu ofisi ya mtendaji..mimi mtanikuta hapa nawasubiri” anasema Duso kisha anaitoa simu sikioni na kubaki amesimama pale pale, dakika kadhaa baadae inafika gari, ndani yupo Mr Beni, Mama Esta na Esta, Duso anakwenda lilipo gari, Mr Beni, Esta na Mama Esta wanateremka na kusalimiana na Duso huku wakishikana mikono mmoja baada ya mwingine, kisha Duso anawaongoza Mr Beni, Esta na Mama Esta kuelekea vichochoro vya pale uswahilini, “ndio unaishi huku Mwanangu?” Mama Esta anamuuliza Duso, “ndio Mama yangu” anajibu Duso, wanakatiza nyumba baada ya nyumba huku wakivuka mitaro na marundo ya taka taka kabla ya kufika ilipo nyumba moja kuukuu, “karibuni..hapa ndio geto” anasema Duso huku akisukuma mlango, wanaingia, wanamkuta Meki amelala kwenye kochi bovu, chini kukiwa na chupa kadhaa za pombe kali na vichungi vingi vya sigara, nywele zake zikiwa timtim, nguo alizovaa ni chafu, akionekana Mtu ambaye ajakutana na maji kwa siku kadhaa,“hoya” anasema Duso huku akimsogelea Meki pale kochini na kumgusa mgongoni, Meki anashtuka na kufungua macho huku akionekana mchovu sana, “Wazazi wako wamekuja kukuona” Duso anamwambia Meki, huku Mama Esta na Esta wanalengwa machozi, “Wazee naombeni mniache” anasema Meki kwa sauti dhaifu, “Meki” anaita Mr Beni na kubaki kimya kwa muda, “jana tumekutana na Sia na Pastor” anasema Mr Beni kisha anamuangalia Mama Esta na kumpa ishara aongee, “Meki Mwanangu Sia na Pastor wamekubali Bremi awe anaonana na wewe” anasema Mama Esta, “utakuwa naye kisha baadae ndio atarudi kwao” anasema Mama Esta huku akitumia leso kujifuta machozi, Meki anabaki kimya pale kochini, “inuka twende nyumbani” anasema Mama Esta, “hoya..inuka mani” anasema Duso, “Wazazi hao hapo wanakujali ndio maana wamekuja hapa Meki” anasema Duso huku Mr Beni akisogea, Duso na Mr Beni wanamuinua Meki pale kochini, “mimi mngeniacha tu” anasema Meki huku Mr Beni na Duso wanamuinua Meki na kumsimamisha, “mimi sina tena thamani hapa duniani” anasema Meki, “usimkufuru Mungu Meki” anasema Mama Esta, Mr Beni na Duso wanamkokota na kutoka naye nje.

SIKU KADHAA BAADAE-SEKEI.
Gari ya Meki Toyota RAV 4, inafika, wanateremka Meki, Bremi na Mama Esta, Bremi akiwa na boksi lenye zawadi mbalimbali, Bremi, Meki na Mama Esta wanaenda na kufika waliposimama Sia na Pastor Obo, huku wakionyesha tabasamu, “twashukuru kwa yote” anasema Mama Esta, “tunawashukuru sana kwa ushirikiano wenu” anasema Meki, “na kesho pia tungeomba Bremi aje ashinde nasi” anasema Mama Esta, “hapana” anasema Sia, “nadhani tumeshakubaliana ni kila jumamosi moja ya mwezi” anasema Pastor, “na si tumeandikishiana jamani” anasema Pastor Obo, Meki anashusha pumzi, “au wewe unasemaje Bremi” Sia anamuuliza Bremi, “mimi nawasikiliza nyie Baba na Mama” Bremi anamwambia Sia, “jamani Sia mdogo wangu” anasema Mama Esta huku akipiga magoti mbele ya Sia, Sia anamuinua Mama Esta, “Dada mbona tulikubaliana vizuri tu” anasema Sia, “ni kweli ila Meki bado anahitaji uhuru na huyu Mtoto” anasema Mama Esta, Sia na Obo wanaangaliana, “Dada..hebu ngoja tukaongee alafu tuone ni kipi cha kufanya kisha tutawajulisha” anasema Sia, “msichukue muda mrefu basi jamani” anasema Esta, “tutajitahidi wiki hii hii tuwape jibu” anasema Obo, kisha wanageuka na kuondoka, Meki na Mama Esta wanarudi kwenye gari yao na kuondoka.

SIKU KADHAA BAADAE-OFISINI KWA MEKI-MCHANA.
Leila, dada, 25, anaingia ofisini, Meki amelala kwenye kiti kama Mtu aliyezidiwa na kinywaji kikali, Leila anashtuka, “bosi” Leila anaita huku akimsogelea Meki, Leila anashtuka kuona kichupa cha dawa kikiwa pale mezani na chupa ndogo ya maji iliyonywewa robo na povu likimtoka Meki mdomoni, Leila anashtuka na kupiga ukunga.

HOSPITALI-BAADAE.
Mr Ben, Mama Esta, Esta na Leila wameketi kwenye benchi, anakuja Dokta Toye, anamnong’oneza Mr Beni, Mr Beni anainuka na wanasogea hadi pembeni kwenye kona, Dokta Toye anashusha pumzi kisha anaivua miwani yake, “Meki alishapotea kabla ya kufikishwa hapa hospitali” anasema Dr Toye, “oh my God” anasema Mr Beni na kushusha pumzi huku akisogelea ukuta na kujiegemeza kama Mtu aliyechoka sana, Dokta Toye anatoa karatasi mfukoni na kumpa Mr Beni, “ilikuwa kwenye mfuko wa shati la Meki” anasema Dr Toye, “nimepoteza thamani Duniani..nimekosa thamani hata kwa Mwanangu wa kumzaa mwenyewe..sioni haja ya kuishi” inasomeka ile karatasi, Mr Beni anashusha pumzi nzito.

MWISHO
Chapter closed...


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom