Simulizi: Chumba cha Misukule (Sehemu ya 01)

Simulizi: Chumba cha Misukule (Sehemu ya 01)

Shunie

JF-Expert Member
Joined
Aug 14, 2016
Posts
157,400
Reaction score
465,165
Mtunzi Juma Hiza

Sehemu ya 01.

Huu ni mkasa ambao sitoweza kuusahau katika maisha yangu mpaka siku nitakayokufa.
Kwa jina naitwa Stella ni mtoto wa pili na mwisho kuzaliwa katika familia yetu. Kwa sasa ninapokusimulia mkasa huu nina umri wa miaka ishirini na saba.

Nakumbuka siku ya kwanza nilipoanza kuishi maisha yangu ya kujitegemea ilikuwa ni pale nilipohitimu elimu yangu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam na kufanikiwa kupata kazi katika kampuni moja hapa mjini ambayo ilikuwa ikinilipa mshahara mzuri uliokidhi mahitaji yangu.

Katika kipindi hicho nilinunua vitu vyote vya umuhimu ambavyo vilihitajika wakati wa kuanza maisha. Nilipoona nimekamilisha kila kitu ndipo hapo nilipoanza kutafuta chumba.
Nilijitahidi kutafuta chumba sehemu tofauti tofauti bila mafanikio yoyote, nilipoona nimeshindwa ndipo hapo nilipoamua kumtafuta dalali mzoefu wa kazi hiyo aliyekuwa akiitwa Mbegu.

Nilipompata na kumwelezea shida yangu kwamba nilihitaji chumba cha aina gani aliweza kunielewa na haraka alianza mchakato wa kunitafutia chumba hicho.

Hazikupita siku nyingi hatimaye alifanikiwa kupata chumba hicho.
Nakumbuka siku hiyo nilikuwa ofisini nikiendelea kufanya kazi zangu kama ilivyokuwa kawaida. Ghafla! simu yangu ilianza kuita, nilipoangalia kwenye kioo cha simu na kuliona jina la dalali, Mbegu haraka sana nilipokea.

“Vipi Stella za kazi?” sauti ya dalali Mbegu ilinipokea simuni kwa kunisalimu.
“Nzuri tu sijui wewe,” nilimjibu.
“Kwangu pia ni nzuri.”

“Enhe niambie, umefikia wapi?”
“Nimefanikiwa kupata chumba.”
“Kipo maeneo gani?”
“Kulekule Sinza kwa Remi uliponiambia.”
“Ni kizuri?”

“Ndiyo naamini utakipenda sana, kimeendana na uzuri wako pia.”
“Hahaha! Sawa basi jioni nikitoka kazini nitakupitia hapo kijiweni ili niende nikakione.”
“Hakuna tatizo bosi wangu.”
“Sawa,” nilimwambia kisha nikakata simu.

Je nini kitaendelea.
20210610_171216.jpg
 
Sehemu ya 02.

Jioni ya siku hiyo nilipotoka kazini nilimpitia Mbegu kisha nikaongozana naye moja kwa moja mpaka katika chumba hicho kilichokuwepo maeneo ya Sinza kwa Remi.
Nilipofika na kukiona kiukweli nilikipenda sana, kama nilivyokuwa nikihitaji kupanga chumba katika mazingira ambayo hakukuwa kuna wapangaji wengi kuhofia uswahili ndivyo ambavyo nyumba hiyo ilivyokuwa.

Ukiachana na nyumba kubwa ya mama mwenye nyumba ambaye alikuwa akiishi hapo, nje kulikuwa kuna chumba kimoja ambacho ndicho alikuwa akikipangisha kwa wakati huo.

“Vipi unakionaje lakini?” aliniuliza Mbegu muda huo nilikuwa nikiendelea kukikagua chumba hicho ambacho kilikuwa kina choo pamoja na bafu ndani kwa ndani.

“Kipo vizuri sana, nimekipenda kiukweli,” nilimjibu Mbegu, nikamwona akitabasamu.
Sikutaka kupoteza muda, kwa kuwa kweli nilihitaji kupanga chumba hicho haraka sana nilifuata taratibu zote za kuandikishiana mkataba na mama mwenye nyumba huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la mama Siwema.

Nilipokamilisha kila kitu sanjari na kumlipa kodi yake ya miezi sita hatimaye nilifanikiwa kuhamia katika chumba hicho ambacho leo hii ndicho kilichonifanya nikusimulie mkasa huu wa kusisimua.

***
Nilianza kuishi maisha mapya katika chumba hicho. Awali sikuona tatizo lolote lile, niliishi vizuri huku kila siku nilikuwa nikienda ofisini kutekeleza majukumu yangu.
Ilikuwa hivyo lakini baada ya kupita mwezi mmoja ndipo hapo nilipoanza kuona vitu vya ajabu katika chumba hicho.

Nakumbuka siku moja majira ya usiku wa manane nilipokuwa nimelala nilishtuka baada ya kuisikia sauti ya mtu ambaye alikuwa akiniita.

Baada ya kuamka nilihisi labda nilikuwa naota lakini kitu cha kushangaza muda huo nilipokuwa nimeshtuka kutoka usingizini sauti ya mtu huyo aliyekuwa akiniita iliendelea kuniita na ilikuwa ikisikika kutokea chooni.

Kiukweli nilishangaa sana, hapo nilikuwa nikiishi peke yangu na hakukuwa kuna mtu aliyekuwa akinifahamu kwa jina zaidi ya mama mwenye nyumba tu.
*
*

Je, nini kiliendelea baada ya Stella kuisikia sauti ya mtu aliyekuwa akimuita?

Itaendelea…
 
Sehemu ya 03.

Sasa ni nani huyo ambaye alikuwa akiniita na ilikuwaje akaingia chooni ilihali mlango wa chumba changu nilikuwa nimeufunga?
Nafikiri mpaka kufikia hapo utaweza kufahamu ni hofu kiasi gani ambayo ilikuwa imeniingia kwa wakati huo.

Kutokana na hofu hiyo ilinibidi nitoke kitandani, nikaenda kufungua mlango wa chooni na kuangalia kama kulikuwa kuna mtu lakini kitu cha kushangaza hakukuwa kuna mtu yeyote. Nilishangaa mno!
Nilichokifanya nilipuuzia, nikarudi tena kitandani kulala huku hofu ikiwa bado imenitawala moyoni mwangu.

Sekunde chache baadaye nikasikia tena sauti ya mtu huyo ikiniita.
“Stella! Stella!”
Safari hii sauti yake ilisikika mara mbili masikioni mwangu kama vile sauti ya mwang’wi.

“Wewe ni nani?” kwa sauti iliyojaa hofu nilimuuliza lakini sikujibiwa. Nilipokelewa na ukimya uliozidi kunitisha vibaya mno.
Usiku huo ulikuwa mrefu kwangu, japokuwa nilipitiwa na usingizi lakini ulikuwa ni ule wa maruweruwe.
***
Siku iliyofuata niliamka, nikajiandaa kama kawaida yangu. Wakati nilipokuwa nikiondoka kuelekea ofisini ndipo hapo kuna mama mmoja alinisimamisha barabarani. Sikumfahamu mama huyo hata hivyo situtaka kumpuuzia, ilibidi nisimame ili nimsikilize shida yake.

“Shikamoo,” nilimsalimia.
“Marahaba binti hujambo?” aliitikia huku akinisalimu.
“Sijambo,” nilimwambia.
“Unaonekana ni msichana mgeni mtaa huu?”

“Ndiyo ni kweli mama.”
“Unaishi wapi?”
“Hapo tu sio mbali.”
“Umepanga?”
“Ndiyo.”
“Kwa nani?”
“Kwa mama mmoja anaitwa mama Siwema sijui unamfahamu?” nilimwambia huku nikimuuliza. Nikashangaa kumwona mama huyo akitabasamu baada ya kumtajia jina la mama mwenye nyumba wangu.

“Ni nani ambaye hamjui huyo mama ni maarufu sana mtaa huu hasa kwa mambo yake ya usiku. Kumbe ndiyo umeenda kupanga kwake?”
“Ndiyo.”

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 04.

Nilipomjibu hivyo ndipo hapo akaanza kuniambia kwamba nifanye mpango nihame katika nyumba hiyo kwa sababu mama mwenye nyumba wangu alikuwa ni mchawi.
“Kivipi?” nilimuuliza huku nikiwa siamini kile alichokuwa akiniambia kwa wakati huo.

“Nimekwambia kama unayapenda maisha yako fanya mpango uhame lakini kama huyapendi endelea kuishi hapo na unachokitafuta utakipata,” aliniambia maneno ambayo yalizidi kunitisha.

Baada ya kunieleza hayo mama huyo aliondoka zake. Nikabaki njia panda nisijue ni nini ambacho nilitakuwa kuamua muda huo.
***

Kiukweli nilichanganyikiwa mno, kila nilipokuwa nikiyakumbuka maneno ya yule mama yalizidi kunifanya niingiwe na uoga usiokuwa na kifani.

Hapa ngoja nikwambie kitu, katika maisha yangu hakukuwa kuna kitu ambacho nilikuwa nikikiogopa kama uchawi, kitendo cha kuambiwa kwamba nilitakiwa kuhama katika nyumba niliopanga kwa sababu mama mwenye nyumba wangu alikuwa ni mchawi na angeweza kuniroga hilo lilinifanya nizidi kuogopa mno.

Huo haukuwa mwisho bali ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuanza kuambiwa na majirani waliokuwa wakiishi mtaa huo kuhusu tabia za mama mwenye nyumba wangu ambaye alikuwa akijihusisha na uchawi.

“Dada una moyo kweli,” aliniambia jamaa mmoja.
“Kivipi?” nilimuuliza.

“Huogopi, unaishi na mchawi nyumba moja.”
“Naishi na mchawi?”
“Ndiyo, ina maana hufahamu kwamba mama mwenye nyumba wako ni mchawi?” aliniambia.

Huyo hakuwa ni mtu wa kwanza kuniambia hivyo, japokuwa kuna wakati nilihisi labda walikuwa wakimzushia mama mwenye nyumba wangu vibaya lakini kadri idadi ya watu waliokuwa wakiongezeka kuniambia kuhusu jambo hilo hilo moja nilianza kuona kuna ukweli ndani yake.

Siku ziliendelea kukatika huku nikiendelea kuishi katika nyumba hiyo ambayo kila mtu alikuwa akiinyooshea kidole.

Baada ya kupita siku kadhaa ndipo hapo uvumilivu ulinishinda, kwa yale niliokuwa nikiyasikia huko nje yalinitisha mno, ikabidi nichukue uamuzi wa kutaka kuhama katika nyumba hiyo.

*
*

Je, nini kiliendelea? Stella atafanikiwa kweli kuhama katika nyumba hiyo?
Itaendelea…
 
Sehemu ya 05.

Kabla sijamwambia mama mwenye nyumba kwanza nilimtafuta dalali, Mbegu nikamwambia kwamba nilitaka kuhama hivyo anitafutie nyumba nyingine.

Nilipomwambia hivyo alishangaa sana.
“Kwa nini unataka kuhama mapema kiasi hicho au mama mwenye nyumba tayari ameshaanza mdomo?” aliniuliza.
“Hapana,” nilimjibu.
“Tatizo nini?”

“Nimeamua tu kubadilisha mazingira.”
“Haiwezekani lazima kutakuwa na sababu tu,” aliniambia kisha akaendelea kunidadisi ili kutaka kujua kulitokea nini ambacho kilisababisha mpaka nitake kuhama katika nyumba hiyo ambayo nilikaa kwa muda wa miezi mitatu tu.

Sikutaka kumficha kitu, ilibidi nimweleze kila kitu kilichotokea.
“Nimeshindwa kuendelea kuishi kwenye nyumba hii inayonyooshewa kidole na kila mtu,” nilimwambia huku nikionyesha kuchoka.

“Stella hebu kuwa kama msomi basi. Usipende kuamini kila neno unaloambiwa huko mtaani.”

“Mbegu unasema hivyo kwa sababu sio wewe unayeishi katika ile nyumba, laiti kama ungekuwa unaishi wewe usingethubutu kuzungumza maneno hayo. Ile nyumba inatisha”
“Inatisha kivipi?”

“Kwanza nikilala usiku nasikia sauti za ajabu ajabu, mara nisikie kama naitwa na mtu chooni nikienda kuangalia sioni mtu yeyote, yaani naona mauzauza tu,” nilimwambia lakini kitu cha kushangaza Mbegu alianza kunicheka, akaniambia kwamba yote hayo yalisababishwa na uoga wangu.
“Itabidi utafute mtu wa kulala naye kama unaogopa,” aliniambia huku akinipa ushauri huo.

“Nani sasa?” nilimuuliza.
“Hata mpenzi wako kwani huna mpenzi?”
“Mbegu tatizo lako unafanya utani wakati nipo kwenye matatizo.”

“Stella hebu acha kuogopa, yule mama mimi namfahamu vizuri ni mtu poa kabisa hana mambo hayo ya kichawi watu wanamzushia tu,” aliniambia huku akimtetea mama mwenye nyumba wangu.

Japokuwa nilipanga kuhama katika nyumba hiyo lakini Mbegu alinizuia kufanya hivyo, alizidi kuniaminisha kwamba hapo nilipopanga nilikuwa sehemu salama na wala sikutakiwa kuhama.

Kutokana na ushawishi mkubwa alionao ndiyo uliosababisha nisihame, hata sijui ni nini kilitokea, nilijikuta nikibadilisha mawazo yangu nikaendelea kuishi kwenye nyumba hiyo japokuwa kuna wakati nilikuwa nikiogopa.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 06.

Siku zilizidi kusonga mbele huku nikiendelea kufanya kazi kama kawaida. Ukumbuke mpaka kufikia hapo nilikuwa nimetimiza miezi mitatu tangu nilipohamia katika chumba hicho.

Katika kipindi hicho nilianza kuyaona mabadiliko fulani, ile sauti ya mtu ambaye alikuwa akiniita usiku naweza kusema kwa wakati huo sikuweza kuisikia tena.
Hali hiyo ilinifanya nianze kuamini labda kweli uoga wangu ndiyo uliokuwa ukisababisha nihisi kama kuna mtu aliyekuwa akiniita ilihali si kweli.

Baada ya kupita mwezi mmoja ndipo hapo mauzauza mengine yalipoanza kunitokea. Kipindi hicho sikuwa nikiitwa usiku kama vile mwanzo la, isipokuwa kila siku nilipokuwa nikienda ofisini, niliporudi jioni niliona kuna vitu ambavyo havikuwa sawa chumbani kwangu.

Hapa ngoja nikwambie kitu, nilikuwa nikipenda sana kununua vitu kwa bei ya jumla na kuviweka ndani. Ukiachana na hilo kwa kuwa nilikuwa nina jokofu dogo hivyo lilinirahisishia hata vyakula mbalimbali nilivyokuwa nikivinunua na vingine kuvibakiza vyote nilivihifadhi huko.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa, katika kipindi hicho kila siku majira ya jioni nilipokuwa nikirudi kutoka ofisini nilishangaa kuona baadhi ya vitu havipo sawa, mfano kama vyakula nilivyokuwa nimevihifadhi ndani ya jokofu vyote nilivikuta vimeliwa.

Hilo lilinishangaza sana, hapo ndani nilikuwa nikiishi peke yangu. Sasa ni nani mwingine ambaye alikuwa akiingia wakati sipo na kuanza kula?

Akili yangu ilinituma labda ni mama mwenye nyumba wangu ndiye alikuwa akiingia wakati mimi sipo na kunifanyia mchezo huo.
Siku hiyo sikutaka kupoteza muda hata kidogo, ilibidi nitoke katika chumba changu nikaenda kumgongea mlango mama mwenye nyumba wangu. Haikuchukua sekunde nyingi akafungua mlango.
*
*

Je, nini kiliendelea? Nini hatma ya Stella na mama mwenye nyumba wake?
Itaendelea…
 
Sehemu ya 07.

“Shikamoo mama,” nilimsalimia huku nikiwa na jazba.
“Marahaba mwanangu vipi mbona hivyo, kuna usalama kweli?” aliniuliza.
“Usalama upo ila kuna vitu sivielewi mama.”
“Vitu gani tena mwanangu?”

“Mama samahani hivi kila siku nikitoka kwenda ofisini huwa unaingia ndani kwangu?” nilimuuliza swali hilo badala ya kunijibu nikashangaa kumwona akinitolea macho kama vile mtu aliyekabwa na kibaka uchochoroni.
“Mimi naingia ndani kwako?” aliniuliza baada ya kimya kifupi.

“Nimekuuliza lakini.”
“Hapana, sijawahi hata mara moja kuingia na siwezi kuingia bila ridhaa yako.”
“Sasa ni nani atakuwa na tabia ya kuingia kila siku ndani kwangu?”
“Kwani kuna nini mwanangu? Umeibiwa?”
“Ni bora ningeibiwa ningejua naenda polisi kushtaki lakini sio kwa haya mauzauza yanayonitokea.”

“Mwanangu mbona sikuelewi kwani kuna nini kimetokea hebu niambie.”
“Ni siku ya tatu leo kila ninaporudi ndani kwangu nashangaa kuona vyakula nilivyovihifadhi vyote vimeliwa na sijui ni nani anayeingia na kuvila.”
“Vimeliwa?”
“Ndiyo.”
“Mungu wangu! Sasa ni nani huyo atayekuwa anaingia ndani kwako.”

“Mimi sijui.”
“Au utakuta labda ni panya ndiyo wanaokula.”
“Panya?”
“Ndiyo.”
“Mama panya wafungue friji waingie na kuanza kula kweli?”

“Sasa kama sio panya ni nani ambaye atakuwa ameingia huko ndani kwako na mimi kama unavyonijua kutwa nashinda ndani kwangu.”
“Basi sawa mama nilitaka kujua tu ndiyo maana nikakuuliza.”

“Haya mwanangu pole sana.”
“Ahsante,” nilimwambia.
Mpaka kufikia hapo unaweza ukaona ni kwa jinsi gani ambavyo mama mwenye nyumba wangu alionyesha kutofahamu kitu chochote kile.

Japokuwa yeye ndiye mtu pekee niliyekuwa nikimuhisi kwamba atakuwa ameingia ndani kwangu lakini kwa wakati huo alikataa.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 08.

“Sasa ni nani ambaye atakuwa na tabia ya kuingia ndani kwangu wakati sipo na kuanza kula?” Hilo lilikuwa ni swali ambalo lilikosa mtu wa kunijibu kwa wakati huo.

Nilichanganyikiwa, wakati mwingine sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikiona, nilihisi labda nipo ndotoni na muda wowote ningeweza kuamka lakini haikuwa hivyo, kile nilichokuwa nikikiona kilikuwa ni ukweli mtupu ambao nilitakiwa kukubaliana nao.
Siku hiyo ilipita huku kichwani mwangu nikijiuliza maswali mengi ambayo yalikosa majibu,

Siku iliyofuata kama kawaida niliamka mapema nikajiandaa kwa ajili ya kulekea kazini. Siku hiyo sikutaka kuondoka hivi hivi, nilichokifanya niliweka sumu ya panya kwenye chakula ambacho nilikibakiza usiku wa kuamkia siku hiyo halafu nikakiweka kwenye friji.

Lengo langu la kufanya hivyo nilitaka kumjua mbaya wangu, yaani kama ni panya ama kuna binadamu yeyote ambaye ndiye aliyekuwa akinifanyia michezo hiyo basi siku hiyo ndiyo uwe mwisho wa maisha yake.
Baada ya kukiweka chakula hicho kwenye friji, niliondoka zangu nikaelekea kazini ambapo nilipofika nilifanya kazi zangu kama kawaida.

Jioni ya siku hiyo niliporudi katika chumba changu, nilipofungua friji sikutaka kuamini kile nilichokiona kwa wakati huo.

Nilikuta chakula chote kikiwa kimeliwa tena kama haitoshi nikakuta vyombo vyangu vikiwa vimepanguliwa panguliwa hovyo. Yaani kwa jinsi chumba changu kilivyokuwa kikionekana muda huo ni kama vile ndani humo waliingia watu ambao walikuwa wakigombana na mwisho wa siku kuanza kurushiana vyombo.

Nilipigwa na butwaa, hapa hata kama ungekuwa ni wewe lazima ungechanganyikiwa tu!

Kwa wakati huo nilihisi labda ni panya ndiyo waliofanya vurugu hizo, kwa kuamini labda ndiyo waliokula chakula chenye sumu lakini nilipokagua chumba kizima mpaka uvunguni mwa kitandani sikuona cha panya wala chochote.

“Haiwezekani hapa lazima kutakuwa na kitu tu,” nilijisemea moyoni mwangu kwa ghadhabu huku nikiwa nimechoshwa na mauzauza hayo.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 09.

Sikutaka kuendelea kuwemo ndani humo, nilichokifanya nilitoka nikaenda kwa mama mwenye nyumba wangu. Nilimkuta akiwa nje anapika.

Aliponiona tu! aliniita huku akijishtukia, nakumbuka sikumsalimia lakini cha kushangaza aliitikia salamu.
“Mama unajua sielewi kuna kitu gani ndani kwangu kinachoendelea?” nilimwambia huku nikimuuliza.

“Kivipi tena mwanangu?” aliniuliza huku akionyesha kutofahamu kitu chochote kama kawaida yake.
“Mimi sielewi kila nikirudi nakuta vitu vyangu havipo sawa.”

“Sasa mwanangu hilo ni swali la kuniuliza mimi kweli? Kwani tunaishi wote?”
“Lakini mama nitamuuliza nani mwingine na wakati humu ndani tunaishi wawili tu na hakuna mpangaji mwingine.”

“Hata kama mwanangu lakini unanikosea sana ina maana unataka kusema kuwa mimi ndiye ninayeingia ndani kwako kila siku?”
“Sina maana hiyo mama.”

“Kama huna maana hiyo utakuwa na maana gani nyingine kwa sababu sasa kama tunaishi wawili humu ndani basi mimi ndiye nitakuwa na tabia ya kuingia ndani kwako.”
“Mbona sielewi lakini naona kama unanichanganya.”

“Hebu kumbuka vizuri au labda una rafiki yako yeyote huwa ana tabia ya kuja wakati wewe ukiwa haupo.”

“Sina rafiki mwenye tabia hiyo na funguo yangu muda wote nipo nayo.”
“Sasa atakuwa ni nani mwenye tabia hiyo?” aliniuliza.

Kiukweli nilizidi kuchanganyikiwa vibaya mno, swali hilo ambalo aliniuliza mama mwenye nyumba wangu ndilo hilo hilo ambalo na mimi nilijiuliza kichwani mwangu bila kupata jibu lolote.

Nikwambie tu huo ulikuwa ni muendelezo wa mauzauza hayo yaliokuwa yakinitokea katika chumba hicho.

Wakati mwingine nilianza kuamini yale maneno ya watu ambao walikuwa wakiniambia kwamba nilikosea njia nikaenda kupanga kwa mchawi.
Japokuwa sikuwaamini hata kidogo lakini maneno yao nilianza kuona yakitimia hasa kutokana na mauzauza mfululizo yaliokuwa yakinitokea kila siku.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 10.

Kiukweli kama ni kuvumilia nilivumilia vya kutosha na katika kipindi hicho sikutaka tena kuendelea kuishi katika nyumba hiyo.
Nilichokifanya nilimwambia mama mwenye nyumba wangu kwamba mwezi huo nilitaka kuhama.
“Unataka kuhama?” aliniuliza huku akinishangaa.

“Ndiyo nataka kuhama,” nilimwambia.
“Kwa sababu gani?”
“Mama nimechoka kuishi kwenye hii nyumba yako isiyoisha mauzauza kila siku, yaani ni bora nihame nikatafute maisha kwingine kuliko kuendelea kuishi humu ndani.”
“Unafikiri utaweza kuhama?”
“Kwa nini nisiweze na wakati najilipia kodi mwenyewe.”

“Humu huwezi kuhama kirahisi.”
“Siwezi kuhama?”
“Ndiyo na kama utakuwa mkaidi utaenda kuungana na wenzako waliokuwa na kiburi kama wewe,” aliniambia kisha akanisonya. Nikashangaa!

Kiukweli maneno ambayo aliniambia kwa wakati huo yalinishangaza mno. Sikujua alimaanisha nini, ikabidi nimuulize.
“Nimekwambia huwezi kuhama humu ndani,” alirudi kuniambia huku akinikazia macho kwa ukali.

“Kivipi?” nilimuuliza huku nikizidi kuwa katika hali ya sintofahamu.
Ni hapa ambapo alianza kuniambia kama angeniruhusu niondoke katika nyumba hiyo basi nienda kutangaza siri zake jambo ambalo hakutaka kuona likitokea.

Hakuishia hapo tu, aliendelea kuniambia kwamba hata wapangaji wengine ambao waliwahi kupanga katika chumba hicho kabla yangu baada ya kugundua siri zake walipotaka kuhama kilazima aliamua kuwapeleka katika ulimwengu mwingine tofauti na huu ambao tunaishi binadamu.

“Ndugu zao wanajua wamekufa lakini mimi ndiye ninayejua wako wapi na yote kiburi chao ndicho kilichowaponza,” aliniambia huku akinipigwa mkwara.

Niliogopa mno, mpaka kufikia hapo wala sikuhitaji tena mtu wa kuniambia kwamba mama mwenye nyumba wangu alikuwa ni mchawi, isipokuwa maneno yake yalitosha kuniaminisha kwamba alikuwa ni mchawi tena alikuwa akiwageuza wapangaji misukule.

“Ila sikulazimishi kama na wewe unataka kuungana na wapangaji wenzako sawa hama mimi nitakupeleka ila kama hutaki basi endelea kuishi humu ndani na siri zote zibaki kuwa za humuhumu nje zisitoke,” aliniambia huku akinipa uhuru wa kuchagua.
*
*

Je, nini kitaendelea? Nini hatma ya Stella na mama mwenye nyumba wake?
Itaendelea...
 
Sehemu ya 11.

Kiukweli nilihisi kuishiwa nguvu za mwili, japokuwa alinipa uhuru wa kuchagua jambo moja kati ya mawili ambayo alinipa lakini kitendo cha kuendelea kuishi katika nyumba hiyo ilikuwa ni sawa sawa na mtu aliyeingia shimoni ilihali hajui ni kwa vipi angeweza kutoka na kitendo cha kuhama katika nyumba hiyo nilikuwa nikijihatarishia usalama wa maisha yangu, yaani kama ningethubutu kuhama basi muda wowote ningeenda kuungana na wapangaji wenzangu ambao waligeuzwa misukule.

Sijui nikwambie nilikuwa katika hali gani muda huo ili upate picha halisi jinsi nilivyokuwa.

Nilichanganyikiwa vibaya mno na kila wazo la msaada ambalo lilinijia kichwani mwangu nilihisi sio msaada sahihi kwangu hivyo niliachana nalo.

Kwa wakati huo hofu niliomuonyesha mama mwenye nyumba wangu naweza kusema kuwa ndiyo ambayo aliitumia kama silaha ya kuniangamiza.

“Unakumbuka ulikuwa ukiniambia kwamba kila ukirudi ndani kwako unakuta vitu vyako havipo sawa?” aliniuliza.
“Ndiyo,” nilimjibu.
“Sasa unajua ni akina nani ambao walikuwa wakiifanya kazi hiyo?”

“Hapana.”
“Hao ni wapangaji ambao nimewageuza misukule na mule ndani ndipo ninapowafugia,” aliniambia, nilishtuka sana baada ya kusikia hivyo.

“Usishtuke mbona ulikuwa ukiishia nao siku zote,” aliniambia huku akitabasamu kana kwamba alikuwa akinieleza taarifa nzuri za kufaulu mtihani wa taifa wa kidato cha nne.
“Nilikuwa naishi na misukule?” nilimuuliza kwa mshangao!
“Ndiyo.”

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 12.

“Mungu wangu!” nilijikuta nikisema huku nisiamini kama kweli siku zote hizo nilikuwa nikiishi na misukule ndani ya chumba kimoja.

Huo ndiyo ulikuwa ukweli ambao nilitakiwa kukubaliana nao kwa wakati huo. Japokuwa niliogopa sana lakini mama mwenye nyumba wangu aliendelea kunisisitiza kwamba kama ningeendelea kuishi katika nyumba yake basi nilitakiwa kuishi na misukule hiyo.
Hapa hata kama ungekuwa na moyo wa ujasiri kiasi gani nafikiri usingeweza kuishi na misukule hiyo.

Aliponiambia hivyo nilishtuka.
“Hutakiwi kuogopa Stella, kama uliweza kuishi nayo siku zote hizo leo utashindwa vipi?” aliniuliza.

“Mama laki…” nilimuita lakini kabla sijamalizia sentensi yangu alinikata kauli.
“Lakini nini Stella? Kipi unachokiogopa?”
“Mama niishi na misukule ndani?”
“Ndiyo utaishi nayo mpaka siku Mungu atakapokuchukua,” alinijibu huku akimaanisha kwamba sikutakiwa kuhama ndani humo mpaka pale siku nitakayokufa.

Kiukweli nilizidi kuchanganyikiwa vibaya mno, naweza kusema huo ndiyo ulikuwa mwanzo wangu mwingine wa kuishi maisha mfano wa mfungwa aliyekuwepo gerezani akitumikia kifungo chake cha maisha.
***

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 13.

Niliendelea kuishi katika chumba hicho ambacho kilikuwa kikifugiwa misukule na mama mwenye nyumba wangu.
Kila ilipofika majira ya usiku kiukweli sikuweza kulala. Ningeweza vipi kulala hali ya kuwa nilijua fika ndani humo kulikuwa na misukule?

Muda wote nilikuwa macho huku hofu ikiwa imenitawala moyoni mwangu. Ama kweli kuishi na misukule ndani ya chumba kimoja ilitaka moyo.

Siku ziliendelea kukatika huku nikivumilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu.

Ilikuwa hivyo lakini taratibu utofauti wangu ulianza kuonekana ofisini. Nakumbuka mtu wa kwanza ambaye ndiye aliyegundua utofauti wangu alikuwa ni mfanyakazi mwenzangu ambaye aliitwa Glory.

Kila siku ofisini alikuwa akiniona ni mtu ambaye nimetawaliwa sana na mawazo. Hakujua ni sababu gani iliyonifanya mpaka nikawa katika hali hiyo, siku moja alichokifanya akaamua kuniuliza ili ajue sababu.
“Hakuna kitu mbona nipo sawa tu,” nilimwambia huku nikimficha.

“Sio kweli Stella, ninakufahamu umebadilika sana siku hizi nini shida?” aliniuliza.
“Glory kweli hakuna kitu, huniamini?”
“Nakuamini sana ila kuna kitu unajaribu kunificha.”
“Kitu gani?”

“Sikijui na sijui kwa nini unanificha.”
“Glory kweli hakuna kitu, siwezi kukuficha kama kungekuwa na tatizo ningekwambia.”
“Sawa kama kweli hakuna kitu, tuendelee kufanya kazi,” aliniambia.
*
*

Je, Stella atamwambia Glory ukweli?
Itaendelea...
 
Sehemu ya 14.

Japokuwa nilimficha lakini moyoni mwangu niliumia sana, nilitamani kumwambia ukweli wa kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu lakini nilipoyakumbuka yale maneno ya mama mwenye nyumba wangu pamoja na vitisho alivyonipa niliogopa kumwambia. Ukweli nikabaki nao moyoni mwangu japokuwa ulinitesa mno!

***
Maisha yaliendelea huku kila siku Glory akiendelea kunidadisi ili kujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu. Sikutaka kumwambia ukweli ingawa nafsi yangu ilinisuta.

Siku moja niliporudi nyumbani nilishangaa kumkuta mama mwenye nyumba wangu akiwa amesimama mlangoni kwangu, nilishangaa, nikamsalimia lakini cha kushangaza hakuitikia salamu yangu.
“Stella kama unataka na wewe nikugeuze msukule thubutu kumwambia ukweli rafiki yako Glory,” aliniambia huku akininyooshea kidole cha shahada.

Nilibaki nimepigwa na butwaa huku nisijue nilitakiwa kumwambia nini kwa wakati huo. Nilishangazwa zaidi na jinsi alivyomfahamu Glory.

“Huwezi kunidanganya, kila kitu unachokifanya nakiona na huyo rafiki yako Glory mwambie awe makini,” aliniambia huku akinitahadharisha.

“Sawa mama sitamwambia chochote,” nilimwambia kwa sauti iliyojaa uoga.
“Nimekukumbusha tu maana sisi binadamu tuna desturi ya kusahau.”
“Hapana mama siwezi kusahau.”
“Na ukumbuke kuwa siku ukitoa siri za humu ndani nakugeuza msukule.”

“Sitothubutu mama kumwambia mtu yeyote siri za humu ndani.”
“Sawa kuwa makini,” aliniambia kisha akaondoka kuelekea ndani kwake.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 15.

Kiukweli nilizidi kuchanganyikiwa vibaya mno, kama kuna maisha ambayo mtu anaweza kuyachoka hapa duniani basi mimi ndiye nilikuwa huyo mtu. Katika kipindi hicho nilichoka kuishi maisha hayo ya kupewa vitisho kila siku.

Baada ya kupita siku kadhaa hatimaye kodi ya chumba changu ikawa imeisha, nikajisemea moyoni mwangu kama mama mwenye nyumba angekuja kunidai kodi yake ningemwambia kwamba sina ili hiyo ndiyo iwe sababu ya kunifukuza lakini huwezi kuamini kilichotokea.

Tangu kodi yangu ilipoisha muda wake sikudaiwa chochote, niliendelea kuishi bure kama nyumbani kwetu na huduma zote muhimu kama vile maji, umeme nilikuwa nikipata bila tatizo lolote.

***
“Nitaendelea kuishi kwa hofu na vitisho hivi mpaka lini?” siku moja nilijiuliza bila kupata jibu, ndipo hapo ambapo niliamua kumwambia ukweli Glory huku moyoni mwangu nikijisemea ‘liwalo na liwe’ kwa sababu nilishachoka kuishi maisha hayo.

“Glory nina matatizo makubwa sana,” nilimwambia, nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni majira ya mchana, tulikuwa kwenye mgahawa mmoja tukila chakula.

“Matatizo gani hayo?” aliniuliza huku akinitazama kwa macho ya kutaka kufahamu kilichokuwa kimetokea.

“Ni kuhusu pale ninapoishi.”
“Pamefanyaje?”
“Yaani kuna mambo yanayoendelea kiukweli yanazidi kunichanganya akili yangu.”
“Yanakuchanganya kivipi? Hebu nieleze.”
“Hivi nikikwambia kwamba naishi na misukule utaamini.”

“Unaishi na misukule?”
“Ndiyo.”
“Kivipi?”
“Naishi nayo chumba kimoja.”
“Wee Stella wewe misukule utaweza vipi kuishi nayo?”

“Yule mama mwenye nyumba wangu ni mchawi na ndiye anayeifuga.”
“Makubwa kwa hiyo wewe umejuaje?”

Je nini kitaendelea?
 
Du ingekuwa mimi ningemchinja huyo mama na kwenda kuishi jela
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom