***SURA YA SABINI NA TISA***
(MSIMU WA 02)
MTUNZI: Stevie Mollel
No: 0685 758 123
Kwenye majira ya saa kumi jioni uwanja mkubwa wa ndege wa Bermuda ulipokea ndege mbili kubwa: Emirates Airways na British Airlines. Toka ndani ya ndege kubwa nyeupe yenye rangi ya kijani na nyekundu mkiani, Emirates Airways, Vitalis akiongozana na wanakundi wenzake: Kaguta, Miraji, Bakari na Bernadetha walishuka wakiwa wamebebelea mabegi ya kukidhi juhudi za mikono yao.
Waliongozana mpaka nje ya uwanja wakajiweka ndani ya taksi iliyokomea kwenye mojawapo ya hoteli ya hadhi ya kati, huko wakachukua vyumba viwili tu wakikukabaliana kujigawa watatu kwa wawili, Vitalis akiangukia kukaa na Bernadetha chumba kimoja baada ya majibizano ya sekunde kadhaa.
Hawakulenga kufanya lolote kwa hiyo siku zaidi ya kupumzika waondoe uchovu wa safari iliyowagharimu siku mbili njiani. Bernadetha akiwa amejilaza kwenye kitanda kikubwa ameshapotelea usingizini, Vitalis alikuwa ameketi sofani miguu yake imepandia mezani kwa kunyooshwa. Ilikuwa ni saa mbili sasa ya usiku. Televisheni kubwa iliyobandikwa ukutani ilikuwa inaonyesha matukio kadhaa ya siku hiyo iliyokuwa inaelekea kuisha. Angalau kwa kuikodolea macho, Vitalis alijipata akiwa na kitu cha kumsogezea muda baada ya kukosa kabisa usingizi.
Aliendea jokofu akatoa kinywaji cha rangi nyekundu iliyoiva kikiwa kimewekwa kwenye chupa ya kioo mithili ya bilauri. Aliitizama chupa hiyo akabinua mdomo, itakuwa tu ni kiywaji hawawezi kutia sumu ndani ya jokofu la wageni. Aliweka chupa hiyo juu ya meza ndogo ya kioo iliyokaa karibu na sofa akaendelea kukodolea televisheni akinywa kinywaji hicho mafundo ya mbalimbali. Isimchukue muda mrefu akaona habari iliyokamata muda wake – kifo cha watu wawili: mtu na mkewe, siku moja maeneo tofauti.
Taarifa hiyo ilionyesha miili ya marehemu hao huku washuhudiaji wakieleza yale waliyopata kuyaona ama kuyasikia. Mwanaume alitapanywa kifua huku mkewe akishindiliwa risasi zisizo na idadi.
“Tuliwaona wanaume watano majira ya asubuhi. Hatukujua nini walifanya humo ndani ila tokea walivyoondoka hatukumuona tena Johnny mpaka sasa tulipopata taarifa amekufa.” Alisema shuhuda mmoja.
“Asubuhi ya mapema wakati mimi na mke wangu tunajiandaa kwa ajili ya kwenda shambani, tulimuona Kelly akitoka na wanaume wawili ndani ya nyumba yake. Walikuwa wanatembea kwa kujikongoja wakielekea upande wa baharini, hatokumuona tena mpaka pale tulipokuja kuambiwa ameuwawa.” Alisema shuhuda mwingine.
“Japokuwa niliwaona hao wanaume kwa mbali majira hayo ya asubuhi, ila nina uhakika ndio wale wanaotangazwa kwenye Tv kama watuhumiwa wa mauaji.” Alisema shuhuda mwingine.
Vitalis alifuatilia habari hiyo kwa makini. Alijikuta akiamini kuna jambo ambalo ataling’amua na likawa na umuhimu kwenye kile walichokuja kukifanya ndani ya nchi hiyo. Hii ni nchi ndogo yenye jiji dogo, kila la uhalifu linalojiri humu basi lazima litakuwa na mkono wa mtu mkubwa, aliamini. Na mtu huyo mkubwa anaweza kuwa Kim.
Kwa usiku wote hata pale taarifa ya habari ilipokoma, aliendelea kuwaza na kuwazua juu ya kile alichokiona. Nani wale waliouwawa? Kwanini wameuwawa? Nani kawaua? Wakina nani wanaotafutwa kwa kesi ya mauaji? Mbona wanatafutwa kinyemela? Maswali hayo yalisindikiza usiku wake barabara mpaka asubuhi alipoamka na kwenda kutwaa mojawapo ya gazeti apate habari kwa undani.
Kitu kipya alichokipata gazetini ni kuhabarishwa kuwa mmojawapo wa wanaume wale wanaotafutwa kwa kutangaziwa kesi ya mauaji kwenye televisheni, aliwahi kuwa mfanyakazi wa Kim Salvatore – Stanis Laughen. Hapo Vitalis akapata walakini zaidi na msukumo wa kufuatilia hilo. Alipata maswali zaidi ambayo aliona jukumu la kuyatafutia majibu.
“Nataka utafute chochote unachoweza kupata juu ya watu hao wanaotafutwa kwa kesi ya mauaji pia matukio yote ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni ndani ya jiji.” Vitalis alimuagiza Bakari.
Pasipo kukawia, Bakari alivalia njuga swala hilo kwa kuanza kuperuzi mitandaoni. Kwa msaada mkubwa wa mtandao wa Youtube, alipata video za taarifa za nyuma akapakua video hizo na kuzitunza kisha akaziwasilisha kwa Vitalis.
“Sioni haja ya kujivuta, Vitalis!” Kaguta alifoka. “Muda unaenda na hatuna muda wa kupoteza zaidi. Tunafahamu mahali alipo Kim, tunangoja nini kumfuata?”
Uso wa Kaguta ulikuwa umejazwa nondo za hasira, hata matendo yake aliyokuwa anayaonyesha wakati akiongea yalisema hayo. Aliona ni upotezaji wa muda, ya nini kuperuzi na mnajua chaka la adui yenu? Huko si kuuzunguka mbuyu? Aliwatizama wenzake akawaona waoga.
“Kaguta, si kila jambo latibiwa na hasira, mengine yahitaji akili.” Vitalis alihasa. “Huwezi kwenda tu kumvamia Kim kwakuwa unafahamu anapokaa, la hasha! Unajua amejipangaje? Unajua udhaifu wake? Unajua wapi umpige akaumia?”
Kaguta aliutupa mkono wake wa kuume kwa kupuuza.
“Unadhani itatuchukua muda gani kuyajua yote hayo? Tutakaa tungoje?”
“Haitochukua muda mrefu. Tunajua hatuna muda mrefu wa kukaa hapa. Hata pesa tuliyonayo ni haba.”
“Nanyi wote mnaaminii hilo?” Kaguta aliuliza akiwatizama wengineo: Bernadetha, Miraji na Bakari. Hawakujibu lakini sura zao zilionyesha wapo pamoja na Vitalis. Kaguta alitikisa kichwa akisaga meno, alitoka ndani akaubamiza mlango kwanguvu. Vitalis alishusha pumzi ndefu akawatizama wenzake.
“Najua wote hapa tumepoteza watu wetu tunaowapenda kwasababu ya huyu mdhalimu, Kim. Lakini kama tukiacha hasira zikashika uwezo wetu wa kufikiri, basi nasi tutaishia huko walipoishia waliotutangulia.”
Alifuatilia video zote alizokabidhiwa na Bakari, akapata yale aliyokuwa anayataka. Hakusita kuwashirikisha wenzake.
“Kuna wanaume wawili wanatafutwa na polisi kwa kesi ya mauaji, ila nachelea kusema wanaume hao wanatafutwa na Kim kwasababu ambayo bado hatujaijua. Kwanini nasema hivyo na kwanini hili jambo ni muhimu kwetu? Kwa mujibu wa taarifa ya habari ya jana usiku, mwanaume mmoja aliyeshutumiwa kuwapokea wanaume hao wawili wanaotafutwa, aliuwawa kwa kuvunja mbavu nyang’anyang’a. Pigo hilo la kuvunjwa mbavu liliwahi kujiri hapo awali kwenye Temple mojawapo hapa jijini ambapo ndipo mmojawapo wa wanaume anayetafutwa alikuwa anaishi. Kwahiyo mtu aliyefanya mauaji hayo huko temple ndiye aliyefanya mauaji hayo huko kijijini, lengo likiwa ni lile lile la kumtafuta mtu wao. Hili jambo la polisi kuwatafuta ni ghelesha tu, kwani kwenye matukio yote hayo hakuna tukio hata moja polisi walipohusika zaidi ya wanaume watano wanaotajwa, na hapa ndipo ninanapopata uhakika wa kusema ni Kim anahusika kwasababu ya nguvu yake ya kutawala vyombo vya dola. Kim anatumia ushawishi wa polisi kuwapata anaowatafuta. Swali la kujiuliza ni kwamba, mtumishi wa Kim kwanini yupo na huyo mtu wanayetafutwa naye? Na kwanini Kim anawatafuta kwa hali na mali?”
Miraji alisafisha koo lake akauliza:
“Kwahiyo unaona kuna umuhimu wa kuwatafuta watu hao?”
“Hakika!” Vitalis alijibu. “Kim hatafuti watu ambao sio hatari kwake. Hatafuti watu ambao hawana umuhimu kwake. Kuna jambo ambalo hawa watu wawili wanalo, laweza likaturahishia kazi zaidi.”
“Sasa tutawapatia wapi hao watu?” Bernadetha aliuliza.
“Popote pale.” Vitalis akajibu. Alimtizama Bakari akamwambia:
“Nahitaji picha za hao watu zikiwa manipulated. Wakiwa wana ndevu, wakiwa na nywele ndefu, wakiwa hawana nywele kabisa, wakiwa wamevaa kofia, wakiwa wamesuka, na kadhalika. Nataka nipate picha zao wakiwa kwenye mazingira yoyote ambayo wanaweza wakajivika.”
Bakari akatabasamu.
“Hilo tayari lishakwisha.” Alisema kwa kujiamini.
***
☆Steve