***SURA YA SITINI NA TATU***
(MSIMU WA 02)
Hamilton, Bermuda.
Walikusanyika wote kwenye uwanja wao kama walivyofanya hapo awali. Wanaume kama themanini kwa kuhesabu kwa macho wakiwa vifua wazi na wamevalia suruali za jeans nyeusi waliujaza uwanja. Mbele yao hakuwepo mtu yeyote bali viti viwili vikubwa ambavyo kimoja wacho kilijazwa dakika moja mbele na Kim Salvatore.
Alikuwa amevalia suti nyekundu na tai nyeusi. Mgongo wake ulikuwa umefunikwa na joho kubwa la manyoya lenye vidoti doti vyeusi. Kiatu chake cheusi kilikuwa kinameta meta kama nyota. Nywele zake za mchanganyiko wa mweupe na mweusi zilikuwa zinang’aa kwa kupakwa na kushiba mafuta. Ndevu zake zilichongwa vema huku nyusi zake zikiwekwa sawia na wanja.
Kwa mbali mdomo wake ulikuwa unameta mithili ya saa yake ya dhahabu aliyoivaa mkononi. Pete yake rangi ya fedha yenye kito cha almasi, aliivalia kidole cha mwisho. Alikuwa anatumia kidole hicho kugongea gongea mkono wa kiti taratibu kana kwamba anajaribisha kipaza sauti cha sherehe.
Kwa mazingira tu yaliyopo yalionyesha siku hiyo haikuwa ya kawaida. Sio tu uwepo wa viti viwili ulisema hivyo, bali hata mavazi na maandalizi. Uwanja mzima ulipambwa na bendera nyekundu zenye mchoro mweusi – mchoro wa mikono iliyopishana ikitengeneza umbo la ‘x’ – mchoro wa mikono ya chuma.
Kila nguzo ndani ya uwanja huo ulifunikwa na kitambaa chekundu kirefu, sakafu ikifunikwa na zulia jeusi.
Kim alitoa ishara kwa kuinamisha kichwa chake, wanaume wote wakaketi kana kwamba wapo masjid – mkao mmoja. Kulikuwa kimya, tuli. Kim akanyanyuka akatizama pande zote na kusema:
“Vema!”
Akatikisa kichwa kimakubaliano.
“Naona vyote vimekuwa vema. Na hivyo ndivyo inatakiwa iwe.”
Alitabasamu akatizama upande wake wa kushoto. Huko akatokea Rajul akibebelea kibakuli kidogo cha mbao. Alivalia nguo nyeupe ndefu ikimfunika miguu kabisa. Shingoni mwake alikuwa amevalia cheni yake ya madunguli ya mbao. Kichwa chake kisicho na nywele kilikuwa kimechorwa michoro miwili meupe zigzag.
Alitembea kwa umakini akifuata kiti kitupu. Aliketi akipakata kibakuli chake, akamtazama Kim na kumpa ishara ya kuinamisha kichwa. Kim akawatazama wafuasi wake.
“Leo ndio ile siku maalum. Siku adhimu kabisa. Leo ni siku ya kurudi utotoni. Leo ni siku ya kuzaliwa upya!”
Kim alisema kisha akaweka kituo. Akatabasamu.
“Nitakaowaita watakuja hapa mbele. Watakunywa damu ya kifalme, damu ya baraka, damu ya uongozi, damu ya nguvu. Punde tu damu hiyo itakapoingia kwenye mishipa yao, hawatokuwa binadamu tena bali simba kamili. Si panga wala risasi, si mikuki wala mishale zitawamaliza.”
Alipomaliza kusema hayo akaita majina ya wanaume watano. Kati ya wanaume hao watano, wanne walikuwa ni miongoni mwa wale wanaume watano waliotumwa Muscat, Oman, kuteka damu ya mfalme.
Mwenzao mmoja hakuitwa. Aliachwa akiwa ameketi, uso wake ukibeba ndita ametoa macho kana kwamba haamini. Alikunja ngumi yake akisaga meno. Alijikuta akinong’oneza akiwatizama wenzake wakinywa walichopewa kwenye kibakuli.
“Kwanini? … Kwanini?”
Alijaribu kukumbuka yote yaliyotukia Muscat, Oman. Jinsi alivyojituma akijifanya mwanamke. Jinsi alivyowaokoa wenzake kwa shuka la Wadhaab. Na jinsi alivyorusha mateke na ngumi za adabu kwa wanajeshi wa Oman.
Kote huko hakuona kosa alilolifanya. Kwanini hajaitwa na yeye? Aliwaza.
Mkutano ulidumu kwa dakika ishirini na tano kabla watu hawajatawanyika. Kim na Rajul waliongozana wakaelekea ofisini. Nyuso zao zilikuwa na furaha, zilipambwa na matabasamu. Waliketi wakawa wanapongezana kwa kupeana mikono na kutikisa vichwa vyao.
“Sasa yamekwisha, bwana Kim. Unaweza ukatawala ulimwengu tena kwa kuwasambaratisha maadui zako.” Alisema Rajul akitabasamu.
“Ahsante sana, Rajul. Nafikiria nikulipeje lakini nakosa majibu kabisa.”
“Hamna shida kabisa bwana Kim una …”
Mlango uligongwa.
“Nani?” Kim aliuliza kwa kupaza sauti.
“Stanis!”
Sauti ikamjibu toka mlangoni.
“Ingia!”
Mlango ulifunguliwa akaingia mtumishi wa Kim. Mtumishi aliyeona amenyiwa fursa ya kuitwa na kutunukiwa kama wenzake.
“Karibu, Stanis. Naweza kukusaidia?”
Kabla Stanis hajajibu, Rajul alisimama akamtizama Kim.
“Naomba niende. Nitakuja siku nyingine tuongee zaidi.”
Kim akampa ishara ya kuinamisha kichwa, Rajul akaondoka zake. Stanis akaketi alipokuwa amekaa Rajul.
“Nimekuja kuuliza, mkuu.”
“Kuuliza nini?”
“Kwanini umenibagua wakati nami nilitumia akili na nguvu zangu zote kukutumikia. Kwanini?”
Kim alitabasamu na shavu la upande mmoja. Aligonga meza yake mara mbili akaja mwanamke mrembo ndani ya sare nyeusi na nyeupe akibebelea chupa ya mvinyo na glasi. Alimmiminia Kim kinywaji kisha akaenda zake. Kim alikunywa mafundo mawili akimtizama Stanis. Aliweka glasi yake chini akauliza:
“Ulivyorudi toka Muscat, sikukupa mifuko miwili ya dhahabu?”
“Ulinipa.”
“Sikukupa wanawake watano warembo toka Brazil ukalale nao?”
“Ulinipa.”
“Sikukupatia nafasi ndani ya mamlaka yangu?”
“Ulinipa lakini …”
“Lakini nini? Unadhani yale niliyoyafanya pale yalikuwa ni zawadi tena?”
“Ni nini?”
“Stanis! … labda umesahau wewe ni nani na mimi ni nani. Naweza nikafanya lolote lile ninalolitaka, wewe ni nani uniulize na kutilia mashaka ninachokifanya? Wewe ni mtumishi tu. Huna haki yoyote ya kutaka mimi nifanye unavyotaka. Wewe ndio unafanya mimi ninavyotaka.”
Kim alisema kwa sauti ya chini yenye mkazo. Alijimiminia mvinyo kwenye glasi yake akanywa mafundo matatu.
Stanis alinyanyuka akataka kwenda. Kim akamuita.
“Unaenda wapi Stanis? … kaa hapo, bado tuna mengi ya kuongea.”
Stanis alirudi akaketi.
***
☆Steve