***SURA YA SITINI NA SITA***
(MSIMU WA 02)
Hamilton, Bermuda.
Mawimbi ya bahari yalichapa fukwe taratibu yakisukumwa na upepo.
Siku hiyo maji yalikuwa machache, kwa kuyatizama tu ungaligundua hilo. Yalisonga mbali tofauti na kawaida yake. Hiyo ikawa fursa nzuri kwa watoto kuchezea maji na hata pia kwa watu kutembea tembea fukweni wakanyage mchanga ambao huwa unamezwa na maji mara nyingi.
Miongoni mwa watu hao, alikuwapo Stanis. Suruali yake ya jeans aliyoivaa aliikunja vema mpaka magotini akivalia shati jeupe jepesi lililokuwa linapeperushwa na upepo wa bahari.
Asionekane na furaha aliranda randa huku na kule akiyapiga maji teke. Ila mara kadhaa alitizama kushoto na kulia kama anatafuta kitu kisha akaendelea na shughuli yake ya kuzurura.
Baada ya dakika kama nne mbele simu yake ilitetemeka mfukoni. Aliitoa akaitizama. Alitabasamu akajongea kutoka eneo la bahari akielekea upande wake wa kushoto.
Huko akakutana na mwanaume chotara ya mweupe na mweusi mwenye nywele ndefu nyeusi ti. Walikumbatiana wakasonga mbali zaidi wakiteta;
"Yuko wapi Fraud?" Stanis aliuliza.
"Wote wameshafika, wanakungoja." Alijibu mwanaume yule mwenye nywele ndefu, Gog.
Walifika mahali fulani palipoezekwa makuti mepesi, wakajumuika na wanaume wengine watatu, jumla wakawa watano: Stanis, Gog,Fraud, Nun na Adrian.
Baada ya kutizama kushoto na kulia, Stanis akasema:
"Nimewaita hapa kwasababu najua ninyi ni marafiki zangu, watu wangu ninaowaamini, na ninatumai hamtoniangusha kamwe."
Alitizama tena kushoto na kulia kisha akaendelea:
"Bila shaka wote mnakumbuka jinsi nilivyowaunganisha kwa Kim baada ya kuhangaika sana. Nisingependa tujadili sana mambo ya nyuma, ila nadhani sasa ni muda wa kunigawia kidogo fadhila. Si tu kwasababu ya urafiki, bali pia fadhila hiyo yenu itawarejeshea fadhila kubwa sana."
"Kipi unataka tufanye Stanis?" Nun aliuliza wakimkodolea macho Stanis kwa makini.
"Nataka tuchukue huu ufalme!" Stanis alisema akitumbua macho.
"Nataka tuukwapue, tuuweke mikononi mwetu!"
"Kivipi?" Fraud aliuliza na kuongezea, "Sidhani kama hilo jambo ni rahisi hivyo."
"Si rahisi ila inawezekana!" Stanis alijibu kimkazo. Akaongezea:
"Nina mipango yote. Kila kitu nimeshakianisha, ni utekelezaji tu ndio unaotakiwa."
Akanyamaza akiwatizama wenzake kwa macho ya ufahamu.
"Nani atakuwa na mimi?" Aliuliza.
"Tupo pamoja." Gog akajibu akitikisa kichwa.
"Na mimi pia." Fraud akadakia akimaliziwa na wengine wawili.
Stanis akatabasamu.
"Ahsanteni sana." Alisema kisha akachuchumaa chini, akachora ardhi na kidole.
"Tizameni hapa mniambie ..."
***
Hakukuwa salama tena kisiwani. Boti ilishatua karibu na fukwe Vitalis na wenzake wakijipakia wapate kuyeya.
Walifanya hivyo baada ya kutoa heshima zao za mwisho kwenye makaburi ya wenzao waliotangulia mbele za haki. Baada ya kila mmoja kusali kwa imani yake, walibeba walichokiona cha muhimu wakatia moto boti mpaka walipokutana na kisiwa ambacho hata jina hawakukifahamu.
Hakikuwa kikubwa kama cha hapo mwanzo. Kilifungwa na misitu mingi kikitengeneza giza hata wakati wa mchana.
Kwa kutizama haraka haraka, hakukuwepo na dalili yoyote ya viumbe kuishi hapo. Palikuwa kimya, kimya mno. Hata milio ya ndege haikuwepo. Labda tu sauti ya mawimbi yakichapa fukwe.
Kabla basi ya jua kuzama, wanaume wakachakarika kukata miti, kusafisha vichaka watengeneze mahali pa kupumzikia.
Kwa ugumu wa kazi, mpaka jua lazama hawakuwa wamefanikiwa. Ila walipiga angalau hatua. Walishapata eneo safi ambalo walichopeka mistimu ya miti hapo na paa la majani majani kuvutia muda.
Kupambana na giza na ubaridi wakawasha moto wakiketi kwa kuuzunguka.
"Nini kinachofuata sasa?" Sandra aliuliza. Kana kwamba wamepanga, wote wakajikuta wakimtazama Vitalis.
"Kuna wengine wapo nchini, itabidi tuwamalize mapema. Bahati nzuri kwa upatikanaji wa simu ya mmojawao kutatusaidia kuwatambua wapi walipo. Hatuna muda mwingi, lakini pia hatupo mbali sana na mkuu wao, Kim." Alisema Vitalis. Akaendelea kuhutubia:
"Tumepewa sababu nyingine ya kupambana - kuwapumzisha wenzetu mahali salama. Kama tusipofanikiwa basi hawatokuwa na amani huko walipo. Tumebakiza michoro miwili tu, mmoja kati yao tumeshaanza kuhangaika nao. Hatutakiwi kuchoka bali kuongeza nguvu zaidi. Tuwe waangalifu sana tunapotoka nje ya hili eneo kwasababu yoyote ile, iwe ni kwaajili ya kufuata vifaa vyetu vya umeme ama kufuata mahitaji. Keshokutwa tutatoka huku mafichoni twende bara. Na hatutorudi mpaka pale tutakapohakikisha hakuna yeyote kati yao anayevuta pumzi tena.
"Kwanini keshokutwa si kesho?" Bernadetha aliuliza.
"Kwasababu kesho tuna kazi kubwa ya kufanya hapa." Kaguta alimsaidia Vitalis kujibu kisha akaongeza:
"Vipi tukienda huko bara, tutapata vinywaji? Nina kiu sana aisee! Sijaonja kitambo."
Sandra akamzaba Kaguta kofi dogo mgongoni.
"Umeanza. Hakuna kunywa tena!"
"Kidogo tu nisafishe koo." Kaguta alijitetea wakaendelea kuzozana na Sandra kiutani.
Giza lilisonga mwishowe wakapitiwa na usingizi. Moto ulivuma mpaka ukatika pakawa giza kamili ambalo lilishinda mwanga wa mwezi kwa kishindo kikuu.
***
☆Steve