***SURA YA HAMSINI NA TISA***
(MSIMU WA 02)
Wakati adhana inalia kila upande wa jiji la Muscat, tayari magari yaliyombebelea Sultan pamoja na familia yake yalikuwa yapo barabarani kuelekea msikitini. Magari meusi. Magari ghali. Magari yasiyo na uwezo wa kupenyeza vyuma vya risasi. Barabara yote ilikuwa nyeupe kupisha msafara huo wa kiongozi mkubwa.
Wakati huo huo, watumishi watano wa Kim wakiwa na nyuso bandia waliwasili mbele ya jengo kubwa, Al Alam. Mmoja alibebelea begi mgongoni, wote wakibebelea kamera shingoni mwao. Walivalia kana kwamba ni watalii – bukta za timberland, nguo nyepesi za kurandana na joto, miwani ya kupambana na jua kali, raba na viatu vya wazi.
Walizunguka huku na kule wakitizama tizama jengo hilo na kulipiga picha. Walizidi kusogea zaidi na zaidi, mwishowe mlinzi akawafuata. Alikuwa amevalia kofia nyekundu yenye mkia mweusi mithili ya kaufagio. Nguo zake zilikuwa za kaki zikiwa zimenyooshwa vema na kupendeza. Usoni mwake alikuwa na mustachi mpana na macho yenye nyusi nyeusi zilizokoza.
“Hamruhusiwi kusogea zaidi, tafadhali.”
Alisema mlinzi akiunyoosha mkono wake.
Watalii hao feki wakaafiki maelezo. Waliendelea na safari yao wakizunguka jengo kubwa la Al Alam. Walipofika nyuma ya jengo hilo, huko kulipokuwa kimya na tulivu, walirudia tena zoezi lao la kusogelea jengo kwa karibu. Walinzi watatu waliwafuata wakiwakataza, hapo wakawakaba walinzi hao kwanguvu na kuwapokonyauhai. Haraka aliyebebelea begi akatoa kitambaa cha rangi ya dhahabu akawafunika walinzi waliouwawa. Kufumba na kufumbua walinzi hao wakapotea isijulikane wapi walielekea. Kilibakia tu kitambaa ambacho kilichukuliwa haraka kikarejeshwa begini wanaume wengine wakitwaa nguo za walinzi na kujivika.
Wanaume watatu waliovalia nguo za walinzi walisogelea jengo la Al Alam wenzao, wawili, wakienda kwa mbali kidogo kama watizamaji. Ila wote wakiwa wanawasiliana.
“Bado dakika tano Sultan atoke msikitini.” Alisema mtumishi mmoja wa Kim aliyekuwa nje ya jengo huku akitizama saa yake mkononi.
Ijumaa si tu kwamba ni siku maalum ya kuswali kwa waislamu ambao dhahiri ndio idadi kubwa ya wananchi wa Oman, bali pia ni siku ya mapumziko. Watu hawaendi kazini siku hiyo, wanakaa majumbani na familia zao. Baada ya kuswali, ijumaa huwa inashuhudia idadi kubwa ya watu wakiranda randa mitaani. Ni siku nzuri kwa kufanya tukio na kutoroka, labda ni sababu nyingine ya tukio hili la kutafuta damu ya Sultan kufanyika siku hii.
Zilikamilika dakika tano, magari ya msafara wa Sultan yakaanza kushika njia kurudi makaoni. Kama kawaida barabara ilikuwa nyeupe. Magari yalikuwa yanakimbia kwa kasi yakijipanga kwenye mpangilio wa moja. Gari la Sultan lilikuwa katikati likitanguliwa na kufuatiwa na magari ya walinzi.
Kuna walinzi waliovalia nguo za sare pia wakiwemo na wale waliovalia suti nyeusi pamoja na miwani. Hawa wa suti nyeusi, wanaume sita, ndio walikuwa karibu sana na Sultan. Walihusika kumfungulia Sultan milango ya gari na nyumba pia kuongozana naye kwa ukaribu.
Ndani ya jengo la Al Alam, mahali pa mfalme, kila eneo kuliwekwa kamera zikimulika huku na kule. Sehemu pekee palipokuwa hapana kamera ni vyumba vikubwa vya Sultan na familia yake. Sehemu zingine zote, kuanzia jiko kubwa lililopo ndani ya jumba hilo, korido pana safi za jengo hilo, sebule nene za jengo na sakafu zake zote palikuwa na kamera zilizokuwa zinaonekana na kusomwa ndani ya chumba cha teknishiani ambaye alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na walinzi wa jengo hilo.
Kama vile haitoshi, walinzi walitapakaa ndani ya jengo wakiwa wamesimama kama minara na silaha zao. Hata kama nzi angelikatiza mbele ya macho yao wasingelipepesuka kamwe. Walisimama kwa ukakamavu na utulivu kana kwamba wametiliwa gundi hapo.
Sultan pamoja na familia yake walikuta meza ya chakula ikiwa imejaa chakula na matunda ya kila aina. Wahudumu wa chakula walisimama pembeni wakingojea kupewa amri.
Familia hiyo iliketi wapate kula ila Sultan hakuwapo bali mkewe na wanawe wanne. Sultan alipoingia tu ndani alinyookea chumbani kwake na sasa ilipita dakika kadhaa hajaja mezani kupata chakula.
Mke wa Sultan baada ya kula matonge kadhaa, alimuita mlinzi kwa ishara akamuagiza aende kumtizama mume wake chumbani. Mlinzi alipokea amri hiyo akaenda kuitimiza. Aligonga mlango wa chumba cha Sultan pasipo majibu.
Alichungulia tundu la ufunguo akaona miguu ya Sultan ikiwa inatapatapa juu ya kitanda. Alivunja mlango akaingia ndani. Alimkuta Sultan akiwa anamimina damu ubavu wake wa kushoto kukiwa na tundu kubwa.
Sultan alinyanyua mkono akioneshea nyuma ya mlinzi. Mdomo wake ulikuwa unateta kitu ambacho hakikusikika vema. Mlinzi aligeuka kutizama nyuma akakutana na teke kali. Alidondoka chini akazirai.
Mwanaume aliyefanya hayo akatoka chumbani akiwa ameficha kitu ndani ya shati lake.
Teknishiani wa chumba cha kamera alimuona mwanaume huyo aliyeficha kitu akitoka ndani ya chumba akitembea haraka. Alipovuta picha yake kwa karibu, aliona mwanaume huyo ana damu mkononi. Haraka akatoa taarifa kwa walinzi wote juu ya mwanaume huyo.
Familia ya Sultan iliwekwa chini ya ulinzi kwa usalama. Walinzi wote waliokuwepo nje walikaa tenge kwa vita. Walinzi waliokuwepo ndani wakaanza kumfukuzia mwanaume aliyetokea chumba cha Sultan wakiongozwa na teknishiani wa chumba cha kamera.
Kutokana na jumba kuwa kubwa ilikuwa ngumu kwa mtuhumiwa kukamatwa kirahisi.
Kabla hajatiwa nguvuni, teknishiani alivamiwa ndani ya chumba chake akauwawa. Mwanaume mwingine, mtumishi wa Kim, akaanza kuwapoteza walinzi kwa kuwaelekeza muelekeo usio sahihi huku akiwasiliana na wenzake akiwataka wakutane chumba cha teknishiani.
Ndani ya muda usiofika dakika, wote watatu walifika ndani ya chumba cha teknishiani. Walijifunika na shuka lao rangi ya dhahabu, kufumba na kufumbua wakapotea. Walinzi walipokuja, walikuta tu shuka wavamizi wasionekane wapi wameenda, mlango upi wametokea.
Wanaume watatu wavamizi walitokea ufukweni mwa bahari. Walijikusanya wakiwasiliana na wenzao wakutane hotelini. Walivua nyuso zao za bandia wakazitupia baharini. Kando kando yao kidogo tu palikuwepo na maiti zile tatu za walinzi waliowaua.
Haraka walitoka eneo lile wakaelekea hotelini walipokutana na wenzao.
“Umefanikiwa?”
“Ndio! … hii hapa!” Mwanaume mwenye kibirika alioneshea.
“Sasa nini kinafuata?” Mmoja aliuliza.
“Tusiwe na haraka ya kuondoka.” Mmoja alijibu, mmojawapo wa wale walioachwa nje ya jengo. “Taarifa imeshatolewa mipaka yote ya jiji ifungwe asitoke mtu yeyote. Kila chombo pamoja na watu wake watakaguliwa kabla ya kutoka nje ya jiji.”
Mmoja alifungua dirisha akachungulia. Huko nje akaona magari ya wanajeshi yakizunguka zunguka huku na huko.
***
☆Steve