Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

***SURA YA HAMSINI NA NNE***





(MSIMU WA 02)







Vitalis akamuazima masikio yake.
“Kesho kuna mkutano mkubwa wa polisi, wadau na wananchi kujadili swala la usalama kutokana na matukio ya hapa karibuni. Nadhani lazima mtuhumiwa wetu afike hilo eneo. Unaonaje?”
Vitalis alitulia kwa muda kidogo akatikisa kichwa chake.
“Wazo zuri sana. Lazima awepo hilo eneo. Ni muhimu sana kuwepo hapo.”
Baada ya muda mfupi Bakari alisonga karibu akiwa amevalia bukta na shati jepesi lililokuwa linarushwa na upepo wa bahari mithili ya tiara. Mkononi mwake alikuwa ameshikilia simu yenye kioo kikubwa na juu ya kioo hiko palikuwepo na picha ya mwanaume mzungu mwenye masharubu marefu.
“Samahani kwa kuingilia maongezi yenu.” Bakari alijitambulisha kwa hiyo kauli kisha akaendelea:
“Nimefanikisha ile kazi mkuu.”
“Sawa sawa. Niambie ambacho umekipata.” Vitalis alisema akijitengenezea.
“Mtu huyo ambaye tumemteka ni moja kati ya washiriki wa lililokuwa kundi maarufu la uhalifu huko Venezuela. Kundi hilo lilikuwa linahusiana na usambazaji wa madawa ya kulevya lakini pia likihusika na mauaji ya watu wasiopungua mia tatu kwa sababu mbalimbali. Kwa pamoja, serikali ya Venezuela ikishirikiana na ya Marekani walifanikiwa kuliangamiza kundi hili kwenye miaka ya 2004. Wahusika kadhaa walikamatwa na wengine wakafungwa kifungo cha maisha. Ila viongozi wa hilo kundi ambao walikuwa ni watatu, walitoroka na mpaka leo haijulikani walipo. Wanatafutwa kwa udi na uvumba na zawadi nono kupatikana kwa atakayefanikisha hilo.”
Bakari alimuonyesha Vitalis picha iliyokuwepo kwenye kioo cha simu, akasema:
“Huyo ndiye tuliyemkamata.”
Vitalis akasataajabu: “Mbona hafananii?”
“Mtizame macho yake vizuri. Wanafahamu ya kwamba wanatafutwa hivyo amebadilisha kabisa mionekano yao iwe ngumu kutambulika. Amepunguza nywele zake, amenyoa masharubu na kukuza ndevu za kidevuni kwa wingi. Ila yeye hakuwa kiongozi wa hilo kundi, bali hawa hapa.”
Bakari akafagia simu yake zikaja picha zingine tatu.
“Huu ndio muonekano wao wa awali, hatujajua kwa sasa watakuwa wanaonekanaje. Na watakuwa wanatumia majina gani.”
“Print hizo picha zote unikabidhi. Tutazihitaji sana, hasa tarehe nane.”
“Sawa, mkuu.”

***

Washikadau pamoja na waandishi wa habari mbalimbali walikuwa tayari wamefurika kwenye uwanja wa jengo la LAPF Tower wakati muda ukiwa unajongea kabisa kuelekea kwenye mkutano wa hadhara uliotishwa na mamlaka ya usalama. Kamera zilikuwa zi tayari, na baadhi ya waandishi wa habari walikuwa wanawahoji watu waliokuwepo hapo kabla ya uongozi wa usalama kuwasili muda mfupi ujao.
Katika hali hiyo hiyo ya zaga zaga na zogo zogo, mwanaume mmoja aliyevalia koti jepesi refu la kaki, kofia pamoja na miwani nyeusi ya jua alipenya akaingia ndani ya uwanja wa mkutano ambamo alikuta watu wachache tu. Aliketi kwenye kiti cha nyuma kabisa akaanza kupepesa macho yake huku na huko ayasome mazingira.
Mwanaume huyo alipovua kofia yake hapo ndipo taswira ya Mamba ikaonekana kwa kujitosheleza – uso na kichwa chake visivyovutia ambavyo havikupoozwa na ndevu za bandia alizokuwa amejivika.
Alikunja nne akitizama saa yake kisha akabinua mdomo kana kwamba analaumu kutozingatiwa kwa muda. Alipotizama saa yake mara ya nne akasikia ving’ora huko nje na mara watu wakaanza kuingia ndani wakiongozana na viongozi wa usalama. Ndani ya dakika kumi na tano mbele mhadhara ukaanza kwa kutambulishwa kwa viongozi kisha kupewa nafasi kwa mkuu wa jeshi la polisi kutoa maneno.
Eneo zima la mhadhara lilikuwa limezingirwa na maafisa usalama wakiwa wametulia ndani ya sare za polisi na wengine ndani ya nguo za kiraia. Kwa haraka haraka Mamba aliwahesabu maafisa hao akapata idadi ya watu ishirini. Alisonya akichezea chezea ndevu zake bandia alafu akarusha macho yake kwa mkuu wa jeshi la polisi aliyekuwa anaendelea kubwabwaja kwa hisia za ukali na huruma juu ya usalama wa nchi, mkono wake wa kushoto akiwa ameshikilia kitambaa cha kujikaushia jasho.
Mamba alimtizama mkuu huyo wa jeshi la polisi kana kwamba anatizama katuni. Alididimiza mkono ndani ya koti akagusa bunduki yake na kifaa kidogo cheusi chenye umbo la mraba ambacho alikibonyeza na kutoa mkono mfukoni haraka, kifaa hicho kikaanza kuhesabu kuanzia dakika thelathini kushuka chini. Mamba akatabasamu alafu akaanza kuwatizama watu waliokuwa wamejaa humo kwa macho ya huruma. Moyoni alijua anawateketeza watu hao ndani ya muda mfupi tu ujao kama vile alivyofanya kwenye soko kuu, Kariakoo, na hii itaendelea kuwa salamu tamu kabisa kwa wale waliomteka mkubwa wake. Na hatoacha kufanya mauaji hayo mpaka pale wanaojiita WAGENI watajisalimisha.
Kwahiyo wakati dakika za kifaa cha mraba zaendelea kuyoyoma kushuka chini, Mamba alikuwa akifuatisha dakika hizo kwa kuzihesabu mdomoni akisubiria zibakie dakika chache tu apate kuyoyoma na kuwaachia wahanga msala.

****

Dakika za kwenye saa ya Vitalis zilikuwa zinaenda kwa kasi kwa mujibu wake. Aliona anachelewa kuwepo eneo la tukio kiasi kwamba akaona gari linanyata wakati alikuwa anaendesha kwa kasi yote. Mithili ya mtu anayeendesha gemu, Vitalis alikwepa magari mengine barabarani na kuyavuka. Alikuja kukanyaga breki kali mbele ya uwanja wa hoteli ya LAPF Tower, kabla hajashuka akapachika mustachi wa bandia na kujiveka miwani meusi ya jua.
Alitembea kwa kasi akaingia ndani ya jengo la hoteli lakini akapanda ghorofa la juu hivyo akawa anatizama mkutano ukiendelea kwa chini. Macho yake hayakutulia kwa kutizama. Alikuwa anamtafuta Mamba amekaa upanda gani ili apate kumshughulikia. Kwa dakika tatu alitafuta bila ya mafanikio, baadae macho yake yakatuama kwa mwanaume aliyekuwa amevaa koti na kofia.
Alimtilia shaka.
Alimchambua kwa macho yake makini akajidhihirishia kuwa ndiye mlengwa wake, Mamba, lakini akiwa katika muonekano tofauti. Alipomtizama zaidi akagundua ya kwamba Mamba alikuwa akinong’ona kana kwamba kuna kitu anasoma, na mkono wake wa kuume ulikuwa umetuama juu ya kitu fulani cha mraba.
Vitalis akazidi kupata shaka. Alihisi kabisa kile kitu ni bomu na vile anavyonong’ona Mamba basi atakuwa anahesabu muda. Lakini kabla hajafanya kitu, aliona Mamba akinyanyuka na kuondoka anaelekea chooni. Haraka Vitalis akashuka na kwenda huko.
Akiwa ananyata alirusha macho yake kumtafuta Mamba ameingia mlango gani wa choo. Alifungua mlango mmoja mmoja na kutizama asione kitu. Ulipobakia mlango mmoja tu, Vitalis akashusha pumzi kwanza kisha akaupiga teke mlango huo lakini namo hakukuta kitu, patupu!
Hapo hapo ghafla akahisi kitu cha baridi kisogoni kwake. Moja kwa moja akatambua ni mdomo wa bunduki. Mamba alikuwa amemzidi ujanja kwa kujibandika juu kisha akashuka taratibu nyuma yake.
“Ulidhani sikukuona?” Mamba aliuliza kwa dharau. “Kaa ukijua kwamba unapoishia wewe kufikiri ndipo mimi naanzia. Leo umejileta mwenyewe na nitakugeuza kuwa mshkaki pamoja na nyumbu zako wote waliopo humu ndani.”
Kisha akacheka kibabe.
“Kabla sijaondoa uhai wako, nakuahidi nitamaliza kikundi chako chote tena ndani ya juma moja tu.”
Wakati Mamba anahororoja Vitalis alinyanyua macho yake kutizama juu akaona bomu limepachikwa na lasoma dakika kumi na tano. Ni dakika chache mno kabla eneo hilo lote halijageuzwa kuwa tanuru. Hakukuwa na muda wa kupoteza kabisa, Vitalis aliwaza.
Kwa wepesi wa ajabu akageuka na kupangua mkono wa Mamba uliobebea bunduki kisha akafyatua mateke mawili makali yaliyomsomba Mamba na kumtupa chini huku bunduki ikirukia pembeni. Alirukia bomu na kulibandua kisha akaanza kuhangaika nalo alizime. Mamba akiwa amejawa na hasira akanyanyuka kwa pupa akikunja ngumi. Alirusha mateke mazito Vitalis akayakwepa huku akiendelea kuhangaika kuzima bomu. Alirusha ngumi mbili za mfululizo, moja ikamkosa Vitalis lakini nyingine ikatua tumboni na kumfanya Vitalis augulie vikali huku akimpa nafasi nzuri Mamba kumzabua tena na teke zito la mguu wake wa kulia. Vitalis akatupwa kando bomu likiruka upande wake wa kushoto.
“Huwezi kupambana na mimi wewe. Mbona hauna kitu kabisa!” Mamba alisema kwa kebehi. Sekunde moja tu mbele alijikuta yupo hewani baada ya kulambwa mtama mkali na Vitalis, kabla hajatua chini aliongezewa teke kali la mbavu likamcheusha damu na kumuacha akiugulia kwa maumivu makali. Vitalis akaendelea na shughuli yake ya kulizima bomu.


***

☆Steve
 
***SURA YA HAMSINI NA TANO***






(MSIMU WA 02)







Baada ya dakika moja Mamba akanyanyuka tena apambane. Mara hii alitaka kuifuata bunduki yake ili amalize kazi kwa wepesi, ila kabla hajaifikia Vitalis aliilenga bunduki hiyo kwa bomu, bunduki ikaenda mbali zaidi. Ile Mamba kumtizama Vitalis akashangaa mtu yupo hewani kufumba na kufumbua akazawadiwa mateke mawili kwa pigo la kisigino, chali akaachwa hoi, mdomo wazi. Vitalis akaokota bomu na kuendelea kushughulika nalo sasa muda ukiwa umebakia dakika tano tu lilipuke na kugeuza eneo lote bahari ya moto.
Kwa uangalifu mkubwa, Vitalis akafukunyua bomu hilo na kukuta waya tatu zenye rangi tofauti tofauti. Aligusa kila waya na kusikilizia kwa muda kama inapitisha moto. Baada ya muda vidole vyake vikawa vimebakia na waya rangi ya njano tu baada ya akili yake kutambua kwamba ndio waya wa kuukata ili bomu likome.
Sasa ilikuwa ni kupata ama kukosa.
Kama atakuwa amelikosea bomu litafyatuka na kutekeza wote. Kama atakuwa amefanya mahesabu yake vyema, atakuwa ameokoa watu lukuki waliomo ndani ya jengo hilo.
Alishusha kwanza pumzi ndefu alafu akafunga macho. Kwanguvu zake zote akauvuta na kuukata waya huo wa njano. Bomu likaacha kuhesabu muda. Vitalis akatabasamu kwa kujipogeza. Akaikota bunduki na kumnyooshea Mamba apate kummaliza. Ila kabla uamuazi huo haujapita, akasikia vishindo vya watu vikija.
Wanaume watatu, maafisa wa usalama, walikuwa wanaongozana wakielekea maliwatoni wakiteta. Walipokamata korido ya uchaguzi wa vyoo wakashangaa kumkuta mwanaume, Mamba, amelala chini pembeni yake kukiwa na bomu na bunduki. Walitoa bunduki zao wakapekua pekua wasimuone mtu mwingine yeyote. Walimuweka Mamba chini ya ulinzi wakamtwaa na kumpeleka kituoni.
Kukutwa na ndevu bandia, bomu na bunduki kulimweka Mamba hatiani. Taarifa za habari ziliporushwa kutangaza hatia hiyo, ushahidi wa mlinzi wa soko kuu na mtoto wa marehemu waziri akisaidiana na Sandra ukazidi kukazia kamba kwenye hukumu ya Mamba.
Hakuwa na nafasi yoyote ya kuwa huru tena.

*****

Asubuhi hiyo bahari ilikuwa na mawimbi makubwa yenye hasira yaliyochapa fukwe kwa fujo na kutengeneza sauti ya nguvu. Jua lilikuwa kali pamoja pia na upepo wa bahari.
Ilikuwa ngumu kuamini kama kuna watu ndani ya maji ya bahari yaliyoonekana tu kwa macho kwamba ni marefu na yenye nguvu mpaka pale wanaume wawili: Vitalis na Kaguta, walipotoka kwenye maji hayo baada ya nusu saa wakiwa wamevalia nguo zilizobana miili yao barabara.
Walitembea kwa ukakamavu wakielekea kwenye makazi yao huku wakichonga maneno kuhusu siku ya nanenane. Walipofika ndani walimkuta mtoto tu, Marietta, akiwa amelala, wengine wote walikuwa upande wa pili wa fukwe wakifanya mazoezi mbalimbali ya kutengeneza pumzi na kujenga stamina.
Baada ya lisaa limoja wote walikutana mezani kupata kifungua kinywa, wakawa wanaongea na kupanga yale ya kutendeka ndani ya mkoa wa Dodoma, mkoa utakaoshuhudia sherehe ya nanenane kwa mwaka huo. Tageti yao kubwa ikiwa ni kuwakamata waamerika kusini watatu: Emilio, Cruz na Santanna.
“Tunafahamu fika kutakuwepo na pacha tatu mbili kwenye hiyo shughuli. Tunatakiwa tuwe wepesi zaidi wa kufanya maamuzi kuliko kawaida. Wote hapa tunajua jinsi mapacha walivyo haraka na wenye nguvu. Inahitajika matumizi ya akili zaidi. Hakikisha unatumia vyema sindano zenye dawa kuwafanya wawe dhaifu. Hakikisha pia unakuwa kwenye mawasiliano na wenzako. Na pia hakikisha watu hawa watatu wanakufa kwa gharama yeyote ile.” Vitalis alihutubia akiwatizama wenzake machoni. Wote wakaridhia na kufanya maongezi yawe mafupi zaidi kabla ya kumaliza kula, kupumzika na kisha kwenda kufanyia mazoezi walichopanga siku hiyo ya nanenane wakitumia miti iliyochongwa kama watu.
Zilipopita siku tatu ndipo ikawadia siku ya tukio – siku ya kufa ama kupona – tarehe nane mwezi wa nane. Vitalis akiwa amevalia suti nyeusi isiyo na tai aliongozana na wenzake: Kaguta, Jombi, Sandra, Bakari na Miraji wote wakiwa ndani ya suti nyeusi wakaingia ndani ya uwanja wa sherehe na kuketi juu kabisa.
Bakari alifungua tanakilishi akajaza mtandao. Alipobonyeza vitufe mara tatu akajiona alipo na wenzake kwenye ramani. Akatikisa kichwa na kuweka earphone.
“Tayari, nawaona wote sasa. Embu jaribu na sauti.”
Sandra aligeukia upande wake wa kushoto alafu akaongea maneno kadhaa, yote yakasikika kwa Bakari. Bakari akatikisa kichwa.
“Tayari na sauti pia. Mnaweza mkaenda sasa.”
Baada tu ya hayo maneno wote wakatawanyika wakimuacha Bakari peke yake na tanakilishi yake wakawa wanawasiliana kila mtu akiwa kwenye pande yake.
Baada ya muda mfupi:
“Kuna watu watatu wanaingia ukumbini sasa hivi, nadhani ndio watu tunaowatafuta.”
Sauti ya Vitalis ilifika masikioni mwa Bakari. Punde ikaambatana na picha kwenye tanakilishi.
“Umeziona hizo picha?”
“Ndio.” Bakari alijibu.
“Embu zitizame kama ni wenyewe.”
Bakari alifananisha picha hizo alizotumiwa na zile alizozipakua kwenye mtandao kuhusu kundi la kijambazi, majibu yakaja ni zenyewe baada ya macho kufanyiwa upembuzi.
“Ndio wenyewe.”
“Sawa sawa.”
Vitalis akawasiliana na wenzake kuwataarifu upande ambao mlengwa wao yupo ili wahakikishe hawawapotezi kisha taratibu akawa anatizama saa yake kana kwamba kuna jambo analingoja litokee muda si mrefu.
Uwanja ulikuwa umejaa watu pomoni. Vikundi mbalimbali vya wakulima na washikadau wa kilimo walikuwa tayari wameshajipanga kwa ajili ya maonyesho. Kila kitu kilikuwa kimeshajipanga kwa mujibu ya ratiba, ni waziri tu wa kilimo ndiye alikuwa anangojewa ili tafrija ipate anza.
“Sandra, Miraji, muda umewadia. Fanyeni kazi yenu sasa kabla waziri hajaingia!” Vitalis aliagiza. Baada tu ya hilo agizo mlipuko mkubwa ulitokea upande wa juu kabisa ambapo hamna watu. Watu wakaanza kukimbia huku na huko wakigombania milango ya kutokea nje.
Baada tu ya dakika chache, uwanja wote ulikuwa mweupe kasoro watu wachache mno. Vitalis pamoja na wenzake, pia Emilio, Santanna na Cruz wakiwa pamoja na kundi lao lenye watu kumi na nne – mapacha ndani. Milango yote ya uwanja ikafungwa na Miraji. Alafu sauti ya Bakari ikasema kwenye kipaza:
“Leo ni mwisho wenu, wapendwa.”
Kundi lote linalowalinda waamerika kusini likakusanyika na kuwaweka wakuu wao katikati. Lakini bado hawakujua wala kuona wanaopambana nao. Uwanja mzima walijiona wenyewe tu. Si Vitalis wala wenzake walikuwa wanaonekana wapi walipojificha.
Ni ghafla mlio wa kitu kama kamshale ukavuma. Kutizama, Pacha mmoja alikuwa amedungwa sindano mkono wake wa kuume. Punde tu, pacha huyo akalegea na kudondoka chini kama mzigo.
“Upande ulee!”
Mwanaume mmoja alielekezea kidole chake ilipotokea sindano – upande wa kulia. Wanaume watano wakaanza kukimbilia huko kabla ya sindano nyingine mbili kuruka tokea upande wa kushoto, zikawachoma mapacha wengine wawili na kuwaacha chini wamelegea.
“Upande huu!”
Mwanaume mwingine akaonyeshea kidole chake upande wa kushoto. Ila kabla hawajakimbilia huko, pacha mmoja akawaonyeshea ishara ya kuwakataza kisha akawaelekeza wajigawanye kwa kila upande. Wakafanya hivyo.
Sindano zingine tatu zilirushwa, mapacha waliobakia wakazidaka kwa mikono yao kabla hazijawakuta, wakazivunja na kuzitupilia mbali. Kisha wakakimbia haraka kufuata sehemu ambapo sindano hizo zimetokea. Huko wakakutana na Miraji upande wa kulia na Jombi upande wa kushoto wakiwa wameshikilia pinde zenye sindano.
Kabla mpambano haujajiri, taa zikazima kukawa giza. Zilipowaka zikawaka kwa fujo mno na kuwapiga usoni mapacha hao ambao walishindwa kuhimili – Vinasaba vya wanyama walivyonavyo mwilini haviwezi kustahimili mwanga mkali machoni. Kabla hawajakaa vyema walishashindiliwa sindano kwenye miili yao wakaachwa hoi hawajiwezi kwa lolote kwa chochote. Mapacha wote wakawa historia. Sasa wakabakia binadamu nane wa kawaida ambao hawakuwaumiza kichwa WAGENI kupambana nao.
Vitalis alichukua wanaume wawili, vile vile Jombi, Kaguta na Miraji. Waliwasulubu wanaume hao kwa mateke na ngumi takatifu zilizowaacha wakilowea kwenye ulimwengu mchungu wa maumivu huku hakuna yeyote miongoni mwao aliyethubutu kurusha ngumi ama teke lolote lililofanikiwa kumgusa Vitalis au wenzake.
Baada ya hapo hakukuwepo tena na kizingiti kilichosimama mbele ya WAGENI. Hakuna mwanaume yeyote aliyekuwa mbele yao isipokuwa tu wale waliowafuata: Cruz, Santanna na Emilio tena wakiwa wamevaa nyuso za hofu baada ya kuona jinsi watumishi wao walivyosambaratishwa.
“What do you want from us?”



****

☆Steve
 
***SURA YA HAMSINI NA SITA***





(MSIMU WA 02)







Emilio, mwanaume mrefu kuliko wenzake aliuliza akijitahidi kuonyesha hana hofu yoyote.
“We want your life.” Kaguta alijibu moja kwa moja kwa ufupi.
Sauti za ving’ora vya polisi zilisikika nje ya uwanja. Magari kadhaa ya polisi yalifika mengine yakiwa njiani kuja na mapolisi lukuki. Sauti hizo za ving’ora ziliwapa matumaini wakina Emilio, kwa namna moja ama nyingine wakajihisi wanaweza wakawa salama. Labda Mungu anaweza tia mkono, eidha waliwaza.
“Do you hear that? … Police are here. They are going to catch you!” Santanna alitishia. Bakari akamjibu akitabasamu:
“So you think you are going to escape just like how you did in Venezuela?”
Emilio na wenzake wakatizamana. Hawakuwahi kudhani kama kuna mtu yeyote anafahamu juu ya matukio yao huko Venezuela. Walipigwa na butwaa.
“Who are you people?” Cruz aliuliza, Vitalis akajibu:
“We are the guests – the guests who have no invitation.”
“Please, don’t kill us. Don’t uncover our identity. We will give you money. How much do you want? Enh?” Emilio alijikomba.
Jibu alilopata lilikuwa ni vyuma vya risasi kupenya kichwani mwake pamoja na mwa wenzake. Hawakupata hata muda wa kuugulia maumivu. Tiketi zao za kwenda jehanamu zilikuwa VIP.
WAGENI isijulikane wapi wamepitia, waliyoyoma wakiwaachia polisi maiti zikitapakaa ndani ya uwanja. Siku iliyofuata picha za marehemu Emilio na wenzake zikatumwa kwenye tovuti rasmi ya usalama wa taifa zikiambatana na maelezo yaliyojitosheleza.
Kama vile haitoshi, makabrasha hayo yalitumwa Interpol. Ndani ya siku tatu mbele, taarifa za magaidi hao zikaanikwa na kurusha kwenye vyombo vikubwa vya habari kama vile CNN, BBC na Al Jazeera huku waziri wa mambo ya ndani akiwa na mengi ya kujieleza juu ya uwepo wa watu hao nchini pasipo kuwa na taarifa.

****





Hamilton, Bermuda.

Uso wa Kim Salvatore, mwanaume chotara wa kizungu na kiafrika, ulikuwa mwekundu mkono wake ukitetemeka na kumwaga kahawa aliyojaziwa kikombeni.
Ilikuwa ngumu kwake kuamini anachokiona kwenye televisheni – taarifa ya habari ya CNN ikionyesha miili ya Emilio, Cruz na Santanna – Wanaume aliokutana nao miaka mitano nyuma kipindi alipokwenda Venezuela kwa biashara ya madawa kulevya kabla ya miaka miwili mbele wanaume hao kumtaka awasitiri kwa miaka kadhaa mpaka pale nyuso zao zitakaposahaulika wakiahidi kumlipa fadhila wasimuache mikono mitupu.
Kim alitupa kikombe chake cha kahawa chini akibinua mdomo. Nyuma yake walisimama wanaume wawili wazungu wakivalia suti. Punde alitokea binti mrembo akiwa ndani ya sare nyeusi na nyeupe akasafisha eneo lililotapakaa vipande vya chupa na kahawa alafu akaondoka upesi. Alirudi ndani ya muda mfupi akibebelea kikombe kingine cha kahawa akaweka mezani.
Kim alizima televisheni akawatizama wanaume wawili walionyuma yake. Hakusema kitu bali aliwapa ishara kwa kuonyesha kidole kwenye televisheni kisha akachinja shingo yake na mkono. Wanaume wale wakaitikia kwa kutikisa kichwa. Kim akapiga ngumi kiganjani mwake akisaga meno. Alinyooshea kidole nje akikunja sura, upesi wanaume wale wakatoka nje pasipo kuaga.
Kim alishusha pumzi ndefu akachezea sharubu zake kwa muda. Alinyoosha mkono akateka simu pana nyeusi iliyoketi kushoto kwake. Hapo mkono wake wa kushoto ukaonekana mchoro mkubwa wa kisu kikichuruza damu. Mchoro huo ulifunikwa na koti la suti pale Kim alipoweka simu yake sikioni, akateta kwa ufupi:
“Njoo nyumbani kwangu upesi.”
Sauti yake nzito iliyoenda moja kwa moja ilitosha kumtisha mtu yeyote.
Asiwe mpweke kwa muda mrefu, akafika mwanaume mzee mwenye asili ya India. Alivalia joho rangi ya kahawia na nyeusi. Kichwa chake ambacho hakikuwa na nywele kilikuwa kimechorwa mistari miwili meupe kuanzia nyuma ya shingo ikiishia kwenye paji la uso kwa kutengeneza kaduara kadogo chekundu. Macho ya mwanaume huyo yalipakawa wanja mweusi, shingoni akivalia kamba iliyobebelea madunguli rangi ya kijivu yenye ukubwa sawa.
Rajul – mwanaume huyo aliitwa Rajul.
“Wito wako wa ghafula, mheshimiwa. Vipi kuna tatizo?”
Aliuliza Rajul akiketi.
Tangu aje, Kim hakumtizama kabisa, alikuwa anatizama televisheni yake aliyoizima kana kwamba kuna jambo nyeti anafuatilia.
“Nahitaji msaada wako wa hali na mali” Alisema Kim bado akitizama televisheni yake.
“Mambo yangu yanakuwa mabaya kadiri siku zinavyoenda mbele. Najiuliza ni wapi nilikosea hatua lakini nakosa majibu kabisa.”
Rajul alijitengenezea vizuri akisikiliza kwa makini.
“Mambo yangu yanapanguliwa kila siku huko upande wangu wa pili wa dunia. Watu wangu wanatishiwa, wanakamatwa, wanauwawa. Sasa imekuwa ngumu hata kuingia ubia na baadhi ya viongozi kwasababu tu wanahofia usalama wao. Pesa yangu imekuwa dhaifu, dhaifu, dhaifu.” Kim aliweka kituo akamtazama Rajul.
“Kuna shida gani? Wapi nimekosea? Tafadhali unaweza ukaniambia?”
Rajul alitikisa kichwa chake akakumbatisha viganjavye.
“Mr Kim, unajua kabisa ya kwamba tokea mwanzoni nilikusaidia kwa uwezo wangu wote pasipo kufinya wala kubana jambo. Nilikupa michoro iliyo hai, michoro mitakatifu, michoro inayoweza kuadhibu. Unafahamu ni jinsi gani michakato ile ilivyotafuna watu, muda na pesa. Ilipelekea mpaka nikafukuzwa kwa kukiuka maadili na miongozo ya matumizi ya nguvu zetu. Sasa nini wataka tena toka kwangu? Unadhani nawezaje tena kukusaidia?”
“Rajul!” Kim alipaza sauti yake. “Unajivunia michoro uliyonipa? Ajabu kweli!”
Akatikisa kichwa.
“Unafahamu kabisa michoro yako ilikuwa ni kwaajili tu ya kuwaongoza wafuasi wangu. Haiwezi kutambua adui na kumteketeza bali inawateketeza watu wangu tu pale wanapokiuka masharti …”
“Bwana Kim kwani kipi ulitaka?” Rajul alikatiza kauli ya Kim. “Wakati unanifuata uliniambia wazi kabisa lengo lako la kwanza ni kuhakikisha watu wako wanakuwa na maadili ya kazi. Wanatii miiko yao. Wanatii amri yako. Wanaficha siri za oganaizesheni kwa njia yoyote ile. Si ndio nikakupatia hiyo michoro na viapo vyake?”
Kim kimya.
“Uliniambia endapo tu watu wako watatii maadili na maagizo, mengine yatamalizwa na pesa zako. Nami nikafanya hivyo. Leo unaiona michoro haina mana? … na nilikuweka wazi, wazi kabisa. – michoro ni kinga lakini pia inaweza kuwa silaha hatari ya kuwaangamiza maadui wako pale utakapomwaga damu ya mtoto wako wa kiume kisha ukanuwia unachotaka. Hukufanya hivyo kwa mtumishi mweusi? Lawama zinatoka wapi tena mheshimiwa?”
Kim kimya. Alikuna sharubu zake akifikiria anayoambiwa. Yalikuwa ni ukweli mtupu na hakuwa na lolote la kumsukuma kutema cheche. Aligonga meza yake mara tatu akaja mwanamke mrembo ndani ya sare akimletea maji ya kunywa kwenye glasi kubwa. Aliyaweka mezani akatokomea.
Kim alinyanyua glasi ya maji akanywa mafundo matatu kupoza nafsi. Alinyamaza kwa sekunde kadhaa alafu akashusha pumzi na kusema kwa sauti ya upole:
“Sawa, Rajul, nimekuelewa. Unakumbuka niliweza kumtumikisha mtumishi mweusi baada tu ya mwanangu pekee wa kiume kupata ajali na kuwa kwenye hali mbaya. Nilishindwa kumuona akiteseka vile hospitali. Niliamua kumuua na hapo ndio nikateka damu yake nitimize adhma. Sasa sina mtoto yeyote kwahiyo unaniambia hakuna nafasi yoyote ya mimi kufufua na kuipa nguvu michoro tena?”
“Unayo.” Rajul alijibu na kuongezea: “Ila nafasi hiyo ni finyu mno na yenye kuhitaji juhudi za dhati. Lakini kabla sijaendelea yanipasa kutizama kwenye ramli zangu umebakiza michoro mingapi kwa sasa ambayo twaweza kuipa nguvu zaidi.”
Kim alitikisa kichwa kuafiki. Rajul alinyanyuka akatoka, baada ya dakika mbili alirudi ndani akishikilia chungu kidogo kilichojengwa na malighafi ya mbao. Alimtaka Kim avue viatu aketi kitako chini. Kim akatii.
Rajul akiwa amesimama alitoa kiwembe pasipojulikana akakata nywele za Kim na kuzitia ndani ya kichungu. Alichanja mgongo wa kiganja cha mkono wa Kim wa kushoto akakinga damu. Aliweka kichungu juu ya kichwa cha Kim alafu akakifunika na kiganja chake kipana akifumba macho na kuteta maneno kadhaa yasiyoeleweka.
Alitoa kiganja chake akaona michoro miwili ndani ya chungu: Simba na mistari mitatu ya mawimbi kuwakilisha maji.
Aliketi kitako akimtizama Kim, akamwambia:
“Una michoro miwili tu iliyobaki: simba na maji. Unaweza ukaipa nguvu tena ikakulinda na kutekeza maadui zako kufumba na kufumbua.”
“Niambie cha kufanya.” Kim alisema kwa kujiamini.
“Mbadala pekee wa damu ya mtoto wa kiume, ni damu ya familia ya kifalme, royal blood.” Rajul alieleza.
“Damu ya familia ya kifalme? Kivipi?” Kim aliuliza.
“Unatakiwa utafute damu ya familia ya kifalme. Familia yoyote ambayo inatoa viongozi wanaotawala, namaanisha sio kama Uingereza na Spania ambazo zina wafalme na malkia lakini hawana nguvu za kisiasa kama mawaziri wao wakuu. Inatakiwa damu ya familia zinazotawala kisiasa, kijamii na kiuchumi.”
Kim alinyamaza kwa muda akitizama chini. Rajul akamuuliza:
“Utaweza ama tuache?”
Kim akanyanyua uso wake akiukunja.
“Hakuna lisilowezekana, Rajul. Niitafanya hivyo.”
Rajul akatabasamu.
“Nilitegemea hilo jibu. Kim ninayemjua mimi hapendi kushindwa … haina shida, utakapopata hiyo damu, unajua wapi pa kunitafuta.”
Rajul alijikusanya akaondoka zake. Kim aliketi kitini akifikiria. Mtihani uliosimama mbele yake haukuwa wa kitoto hata kidogo. Kijasho chembamba kilimchuruza lakini bado alijikuta akitabasamu alipogundua bado ana mwanya mwingine wa kuweka mambo yake mujarab.

***


☆Steve
 
Asante sana kwa hii kituAsante sana kwa hii kitu na kesho kama kawaida ya tunamalizia weekend au vp
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom