***SURA YA HAMSINI NA TATU***
(MSIMU WA 02)
Hilo jambo lilimuumiza sana Vitalis. Alijihukumu kushiriki uzembe wa kumruhusu mshenzi kama yule atoroke mbele ya macho yake. Alijua fika uhai wa mamba ni vifo vya wasio na hatia. Hakuna yeyote anayejua ataenda kufanya nini baada ya jaribio lake la kuteka wanafunzi kushindikana. Ni lazima atiwe mikononi haraka! Afunzwe adabu! Mwili wake uvunjwe vunjwe na umeze risasi si chini ya tano! Aliwaza Vitalis mwenyewe akiwa amebinua mdomo wake na amekunja sura kama mtu aliyekunywa dawa chungu.
Sasa ni fursa ya kuvamia ofisi yao na kuisambaratisha. Tusimpe muda wa kupanga mambo yake zaidi.
****
Baada tu ya muda mchache baada ya tukio la utekaji wa wanafunzi kushindikana, Mamba alishakuwa mtu tofauti kwa kubadilisha mavazi na hata usafiri – haikuwa tena van wala mark X aliyokuwa anaendesha bali range rover nyekundu aliyoisogeza mpaka eneo la bar. Uso wake ulikuwa umebeadilika kwa kupachikwa ndevu za bandia na macho kufunikwa na miwani meusi.
Alishuka akatembea taratibu mpaka ndani ya bar, punde akatoka na Bhoke akiwa kamkamatia kiuno wakitabasamu na kuongea. Alimfungulia mwanamke huyo mlango akaingia ndani, gari likang’oa nanga.
Baadae mida ya saa kumi na moja jioni, Bhoke akakutwa akiwa mfu ndani ya Limpopo guest house, Sinza, kifua chake kikiwa kimetobolewa na risasi tatu. Mdomo wake umeachama na macho yapo wazi. Shuka limetapakaa damu. Si mapokezi wala yeyote aliyesikia milio ya risasi wala kelele zozote, zaidi maelezo yalisema mwanaume aliyeingia na marehemu aliondoka baada tu ya dakika chache walipoingia chumbani.
Habari hizo zilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii. Na hata zikachukua nafasi kwenye taarifa za habari. WAGENI walifahamu fika ni nani aliyefanya huo unyama. Kukaa kwao kimya kungeendeleza matukio hayo ya umwagaji damu. Siku inayofuata ilikuwa ni alhamis – siku adhimu kwa shambulizi la ofisi ya BEAST. Sandra akishirikiana na Kaguta na Vitalis walitega gari lao pembeni kidogo ya barabara umbali wa kilomita moja tokea ofisi za BEAST zilipo. Punde wakiwa hapo wakaona gari la kusambaza sigara laja, wakaliteka na kwenda nalo mpaka mbele ya uzio wa jengo hilo lenye ulinzi mkali. Wakiwa wamevalia nguo za wahudumu, ilikuwa ngumu kugundulikana. Walitumia bunduki zao zenye viwamba vya kumeza sauti wakawamaliza walinzi wote wa nje kisha wakagonga geti na kuingia ndani ya uzio kwa urahisi mno.
Ndani ya sekunde kumi tu, walinzi wote wakawa wamelala chini wakivuja damu waliokuwemo ndani wasijue kinachoendelea huko nje. Vitalis na wenzake wakajigawa mmoja akaenda upande wa kushoto, mwingine kulia na mmoja katikati. Ufahamu wao juu ya hilo eneo kwa kutumia teknolojia ya google map uliwasaidia kunyambua mazingira vema. Mikono yao mepesi iliyokomaa kwa mazoezi na mateke yao mazito yenye nguvu yalirahisisha sana kazi – haikuonekana ngumu hata kidogo ukilinganisha na mazoezi yao wanayoyafanya kila uchwao. Mpaka wanaingia kwenye chumba cha mkuu, hawakuwa hata na mchubuko. Walisimama wima mbele ya mwanaume wa kilatini aliyelaza nywele zake nyuma kwa ustadi mkubwa, mdomoni mwake akiwa ana sigara kubwa. Macho yalikuwa yamemtoka kwa butwaa – wazi hakutegemea watu kuvamia ngome yake na kuingia kwa urahisi hivyo, tena bila hata ya kutambua.
“Who are you?” Mlatini aliuliza kwa uso uliokuwa unajitahidi kufichama hofu. Alitoa sigara yake akailaza kisosini.
“We are your angels of death.” Vitalis alijibu kwa kebehi kisha akamuamuru mlengwa wake asimame upesi kabla hajammwaga ubongo. Mlatini akawa mkaidi kidogo, alijaribu kufungua droo yake atwae bunduki, kabla droo haijasogea risasi ikapiga kando yake na kumshtua.
“Don’t even dare to try!” Kaguta alisema na uso wa kazi ‘uso wa mbuzi’ kisha akamtwaa Mlatini huyo na kutangulia naye nje pamoja na Sandra, Vitalis akibakia kidogo ofisini macho yake yakitembea tembea huku na huko.
Juu ya ukuta mdogo wa ubao wa matangazo, Vitalis aliona picha kadhaa za mifuko ya mbolea na matangazo ya biashara hiyo. Aliposogea na kutizama kwa ukaribu picha hizo za mbolea, chini yake akaona tarehe 8/8/2014 – Ilikuwa siku ya nanenane! Siku ya wakulima! Bila shaka BEAST walikuwepo kwenye maadhimisho ya sherehe hiyo wakitangaza bidhaa yao. Na pasipo kujua wakulima wakanunua bidhaa zao – mabaki ya binadamu wenzao waliouwawa na kuzikwa kimakundi kisha kuchanganywa na kemikali mbalimbali.
Bila shaka BEAST watakuwepo tena kwenye maadhimisho ya sherehe hiyo karibuni. Vitalis aliwaza. Bado wiki moja tu sikukuu ya nanenane ifikie kilele. Huo ndio muda muafaka sasa wa kuwatia wadhalimu hawa mikononi na kumsaidia Mungu kuwahukumu.
***
Hali ya utulivu na pilikapilika za hapa na kule zilimeza jiji la Dar es Salaam. Maduka yalifurika watu wakikatiza kule na kule katika mitaa ya Kariakoo. Kama kawaida kila mtu alikuwa ameshika yake, ukitizama kwa juu unaweza ukasema ni sisimizi wamemwagwa eneo hilo, kumbe ni watu! Katikati ya watu hao alikuwemo mwanaume mmoja aliyevalia suti nyeusi mkononi amebebelea briefcase. Alikuwa yu nadhifu mno. Kichwa chake kilikingwa jua na kofia safi nyeusi yenye ufito mwekundu. Macho yalizibwa na miwani nyeusi huku mdomo ukiwa umezungukwa na ndevu nyingi. Hakuwa mwingine, bali Mamba. Lakini kumfahamu ilihitaji uchambuzi wa hali ya juu. Dhahiri shairi alikuwa ana tukio la kufanya eneoni hapo. Laiti kama wananchi wangelikuwa wanafahamu wangelikimbia kuokoa pumzi zao.
Alitembea kwa wima pasi na hofu. Alikata mitaa akiwa anapiga mluzi taratibu kama njiwa pori. Kichwani kwake alikuwa amelaza ramani nzima ya tukio analotaka kulifanya – kulipua soko kuu! Alizama ndani ya jengo hilo mpaka chini kabisa kana kwamba ni mteja. Akiwa anatembea tembea na kutizama tizama hali ya usalama, mwanaume mmoja alimsimamisha, alikuwa ni mlinzi. Mamba alipata shaka lakini hakuruhusu hilo jambo liteke uso wake. Alitabasamu akauliza:
“Kuna shida afande?”
Huku mkono wake ukiwa tayari umeshakakamaa kufanya tukio lolote litakaloamuliwa na akili yake iliyokuwa inachemka.
“Vipi, wewe ni mgeni humu?” Mlinzi aliuliza. Mamba akatabasamu, alijua mlinzi alimuona wakati anayasoma mazingira. Japokuwa yeye ni mwenyeji huwezi mdanganya lolote kuhusu Dar, aliamua kujifanya mjinga.
“Ndio, mimi ni mgeni.” Alisema na sauti yenye mkandamizo wa kisukuma kwa mbali. Hilo likatosha kumfanya mlinzi ajue ni mtu toka kijijini.
“Nimekuja natafauta mbolea nzuri ya mahindi yangu.”
“Oooh! Nenda mbele kidogo alafu ukunje kushoto, utaona duka la mbolea na madawa ya shambani. Sawa mzee?”
“Sawa. Nashukuru gete!” Alisema Mamba kasha akafuatisha ushauri aliopewa. Alinyookea dukani hapo akajifanya mteja anayeulizia bidhaa. Aliweka mkoba wake chini kisha akaondoka kama mtu anayejinasibu kuusahau mzigo huo. Alitembea kwa kasi mno akielekea kutoka nje. Mlinzi aliyemuelekeza duka la mbolea alimuona mtu wake huyo akitembea haraka huku mkononi akiwa mtupu – akapata shaka. Eidha ameibiwa na watoto wa mjini – aliwaza. Haraka alianza kumfukuzia Mamba huku akijaribu kumuita. Mamba alizidi kusonga asigeuke nyuma kabisa ingawa alisikia sauti ya mlinzi ikimuita. Alipoacha jengo la soko nyuma kwa hatua kadhaa mlipuko mkubwa ukamrusha mbele akadondokea kwenye gari. Jengo lote la soko lilikuwa linawaka moto kama vile tanuru. Taharuki ilikamata watu wakakimbia huku na huko. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa ndani ya soko akatoka mzima. Mlinzi pekee aliyekuwa anamkimbiza Mamba ndiye aliyepona. Aliamka akarusha uso wake kwa mbali akamuona Mamba akiyoyoma katikati ya umati wa watu unaokimbia. Alinyanyuka akamkimbilia lakini hakumuona abadani. Mamba alikuwa tayari ameshavua na kutupa kofia yake na ndevu zake bandia zilikuwa tayari zimeshatupwa kando. Ilikuwa ni ngumu tena kudhani kama ni yuleyule aliyekuwa amebeba mkoba awali. Alikuwa ni mtu mwingine akiwa tayari ameshawateketeza watu 250 ndani ya dakika, sasa akiwa tayari yupo ndani ya taksi akisepa. Huo ulikuwa ni ujumbe maridhawa sana kwa WAGENI. Wameuwa watu wake watatu na kumteka mkuu wake, sasa yeye ameua watu 250. Nani zaidi? Alijikuta akitabasamu.
***
Zilipita siku tatu za vuguvugu la tukio la ugaidi Dar es Salaam, Kariakoo. Bado watu wa Dar hawakuwa na amani, maongezi yao yalitawaliwa sana na hilo tukio la kutisha mno kuwahi kutokea katika nchi ya Tanzania. Japokuwa jeshi la polisi lilitoa tamko lake likijinasibu kufuatilia na kumtia mikononi mhalifu aliyeshiriki, bado haikutosha kuondoa ukakasi wa hofu uliowaganda wananchi waliokuwa kwenye maombolezo. Mbona siku zazidi kuyoyoma na mtuhumiwa hajakamatwa? Hilo swali lilihukumu kazi ya polisi.
Kando kando ya bahari ya hindi iliyokuwa inapuliza kwa mawimbi madogomadogo, Vitalis aliketi akiwa ana mawazo. Kwa mara ya kwanza alijihisi hana mchango wowote kwa wananchi wa Tanzania. Kama watu 250 wanakufa na yeye yupo hai, ana faida gani sasa? Alijiuliza. Alijihisi si lolote si chochote. Alijiona ngoma yake ya kitoto haswa.
Mawazo yake yalitambaa juu ya maji ya bahari. Upepo mkali uliokuwa unampuliza haukusaidia chochote kuondoa zigo la tafakuri alilonalo kichwani. Alijikuta akisaga meno yake huku akikunja ngumi kakamavu. Alitamani Mamba atokee ili apate kumtia adabu na kumvunja vunja bila huruma. Aliishia tu kutamani na kutamani, hakujua wapi atampata adui wake huyo – hawezi akakaa tena na kule kiwandani – anajua yupo mtaani kuonyesha umwamba wake dhidi ya mapacha watatu, ila haswa ni wapi aende ili amkamate baradhuli huyo amuonjeshe kifo? Alibaki anawaza mpaka pale aliposhtuliwa na mkono begani.
“Usiwaze sana, Vitalis.” Sauti ya Bernadetha ilimkarimu. Alinyanyua uso wake akamtizama mwanamke huyo mwenye sura tamu. Akajikuta anatabasamu kwa mbali. Bernadetha aliketi karibu na Vitalis, akamshika mkono.
“Unadhani huyu muuaji ndiye Yule aliyemuua Waziri?” Bernadetha aliuliza.
“Bila shaka ndiye yeye akiwa ametumwa na mkuu wake tuliyemkamata.” Vitalis akajibu kisha akaongezea: “Kwa mujibu wa maelezo ya mlinzi wa soko, kimo cha mtuhumiwa na sifa za mwili wake ni sawa na zile za yule aliyemuua waziri kutokana na maelezo ya mtoto wa marehemu. Ametusakizia kifo cha waziri na sasa anachokifanya ni kuzidi kuwafanya wananchi waamini kile walichokianzisha, uongo. Pia kututaabisha.”
Bernadetha alitizama maji ya bahari akisema:
“Ndiye yeye pia aliyemuua Bhoke … Ila si ulisema umepata nafasi nzuri ya kuwakamata?”
“Ndio, sikukuu ya nanenane, ila naona mbali. Mpaka pale siku hiyo itakapowasili atakuwa kaua wananchi wangapi wasio na hatia?”
Walinyamaza kwa muda, Bernadetha akasema:
“Labda nina wazo.”
***
☆Steve