***SURA YA AROBAINI NA NANE***
(MSIMU WA 02)
Saa tatu na nusu usiku:
Sandra alimkabidhi simu Bakari, akamwambia:
“Hiyo ni simu ya marehemu. Kuna mtu aliwasiliana naye kabla ya tukio, unaweza ukatizama.”
Bakari alipokea simu akaiweka mezani kisha naye akalonga kuwaambia wenzake:
“Tumepata mtu ambaye tunahisi ndiye mlengwa wetu.” Alimeza mate alafu akaendelea:
“Kati ya wale watu wawili, kuna mmoja ambaye ndani ya uzio wa nyumba yake kuna magari mawili yenye tarakimu sawa sawa na zile ambazo zilikuwa ubavuni mwa gari linalohusika na tukio la mauaji – 251 19-20.”
“Maeneo gani?” Kaguta aliuliza.
“Kijitonyama.” Bakari akajibu.
“Tupo pazuri sasa.” Vitalis akasema, “Ila kwanza track hiyo namba ya mwisho kuongea na waziri. Nataka kufahamu inapatikana maeneo gani. Endapo ikirandana na hilo eneo basi huyo ndiye mlengwa wetu. Kama sio, basi sio yeye, itakuwa tu ni watu wengine wanaoshabihiana nao kidhalimu.”
“Naomba nifanye hiyo kazi sasa.”
“Sawa, hakuna shida.”
“Kuna yeyote mwenye uelewa kuhusu tarakimu hizo zilizo kwenye gari na miili ya hawa watu?” Vitalis aliuliza. Hakuna aliyejibu.
“Inabidi tujue. Kuna kitu kitakuwa kimejificha nyuma ya hizo tarakimu.” Vitalis alisema kisha soga zingine zikachukua nafasi huku Bakari akiperuzi kwenye tanakilishi yake. Baada ya muda Bakari akapiga ngumi hewani.
“Zina-match!” Alipayuka. Vitalis akasogea karibu.
“Namba ya simu inarandana na hilo eneo!” Bakari alisema kwa furaha, “Patakuwa ndio penyewe!”
Vitalis akatikisa kichwa.
“Sasa tunavamia ama?” Kaguta aliuliza.
“Hapana.” Vitalis aliwahi kujibu. “Inabidi kwanza tusome hilo eneo kwa muda kama wa wiki, tujue nani anaingia nani anatoka, wapo wangapi, ulinzi upoje, na wapi tunaweza tukapatumia kuingilia.”
“Tutafanyeje sasa kufanya yote hayo?” Bernadetha aliuliza.
“Kwa kupeana shift ya kutembelea eneo hilo. Eidha kwa njia ya kufanya mazoezi, ama mpita njia, ama mkazi jirani.” Vitalis alijibu.
Kuanzia siku iliyofuata vikaanza kutekelezwa vilivyopangwa - Sandra na Bernadetha wakawa wanapita kila siku asubuhi wakifanya mazoezi. Bakari, Jombi, Miraji na Kaguta wakawa wanagawana majukumu, leo ikiwa mpita njia kesho utakaa kando kusoma gazeti, ama kufanya mzozano wa mpira ama tamthilia kando kando ya nyumba. Wiki moja ilipopita wakapeana taarifa.
“Eneo lina ulinzi. Walinzi wawili mpaka watatu wanalinda geti kwa siku na wanapeana zamu kila asubuhi.” Bernadetha alisema.
“Magari yanayoingia hapo ndani ni Mark X nyeusi tu, ikiwemo lile linalohusika na mauaji.” Kaguta alitoa taarifa.
“Ila ndani ya juma kuna siku mbili ambapo gari la kuleta sigara laja. Kama tunataka kuingia ndani huo ndio mwanya mzuri.” Miraji alichangia.
“Hapana, bado hatuwezi kuvamia hilo eneo.” Vitalis alitoa angalizo, “Yatupasa turudi kwa Alwatan Kombo. Yatupasa tufahamu nini kinachounda huyu mnyama, nyoka, kama vile tulivyofanya kwa lile jitu. Tusipofanya hivyo, hatuwezi kufanikiwa abadani.”
“Wazo zuri. Lini tunaenda?” Kaguta alichombeza.
“Kesho.” Vitalis akajibu.
Saa sita na dakika mbili mchana siku iliyofuata:
Kaguta na Vitalis aliyekuwa amevalia kofia kubwa ‘cowboy’ walikuwa wapo eneo la nyumba ya Alwatan Kombo. Milango yote ilikuwa umefungwa na kufuli kubwa. Hata ndani kulikuwa kweupe pe! Kaguta alipopaza sauti yake kuita dirishani alijibiwa na mwangwi mkavu.
Walisogea nyuma ya nyumba kwenda kufuata kijumba cha kazi cha Alwatan Kombo, wakakuta nacho kimefungwa. Majani yalikuwa yameota mpaka mlangoni. Walivunja mlango wakaingia ndani, wakakuta kumejazwa na majani, hata ukuta ukiwa umefifia na michoro haionekani. Walipangusa pangusa ukuta kwa mbali wakaona mchoro wa nyoka.
“Huu hapa!” Vitalis aliropoka. Waliutizama vyema mchoro wakaona kwa mbali kuna visu tisa juu ya kichwa cha nyoka huyo mwenye vichwa vitatu. Ila ghafla wakasikia sauti za watu huko nje.
Wanaume watano waliovalia suti walikuwa wamebebelea bunduki mikononi wakirusha macho yao huku na huko. Waligawana wawili wakaelekea kushoto na watatu wakaelekea kulia. Wote walikuja kukutana kwenye kijumba, walipoingia ndani hawakukuta mtu. Walipekua pekua huku na huko ila hawakuona yeyote.
Saa nane mchana:
Kaguta na Vitalis walifika nyumbani wakamkuta Bakari akiwa ameketi kwenye tanakilishi yake. Vitalis alivua kofia akairushia kwenye kochi, wakamjulia hali Bakari.
“Kuna ujumbe umeingia kwenye simu yangu.” Bakari aliwaambia huku akimkabidhi simu Vitalis.
“Aliyetuma huo ujumbe ni yule yule tuliyem-track!” Vitalis alijazishia habari. Kaguta na Vitalis wakausoma ujumbe … WE ARE IN THE WAR: HUNT OR BE HUNTED. Vitalis alishusha pumzi ndefu, Kaguta akamuuliza Bakari:
“Unaweza ukaniambia huyu jamaa yupo wapi kwa sasa?”
“Ndio. Yupo nyumbani kwake.”
“Gari la sigara huwa linapita kila lini hapo nyumbani kwake?”
“Jumanne na Alhamisi.”
“Tunaenda kuvamia!”
“Hapana!” Vitalis akadakia. “Hatutakiwi tuwe na haraka kiasi hiko, Kaguta. Tuwe na plan kwanza!”
“Tukichelewa wataanza wao ku-hit!” Kaguta alitoa angalizo.
“Na tukiwahi bila ya plan tutaishia wapi?” Vitalis aliuliza, Kaguta akabakia kimya.
“Kwanza tunatakiwa kujua, maana vichwa vitatu vya nyoka ni nini? Na maana ya visu tisa pia. Na zile tarakimu pia. Tukifahamu hivyo, tutakuwa tuna nafasi kubwa ya ushindi.”
“Sawa.” Kaguta akaitikia.
Siku iliyofuata mshale wa saa kumi na mbili asubuhi:
Kaguta na Vitalis wakiwa wamevalia traksuit na makoti ya hood walikuwa wanafanya mazoezi ya kukimbia. Vitalis alikuwa amevalia kofia ya koti uso wake ukiwa chini huku Kaguta akiweka kichwa chake wazi na akitizama mbele. Haikuchukua muda mrefu lilitokea gari aina ya van kwa kasi likasimama mbele wakashuka wanaume watano waliobebelea bunduki, wakawateka Kaguta na Vitalis, gari likatokomea.
Zilipita siku mbilia Vitalis na Kaguta hawakuonekana wala kujulikana walipo. Bakari pamoja na wenzake wakamezwa na maswali.
“Sasa tunafanyaje?” Bernadetha aliuliza.
“Tatizo ni kwamba hatujui tunawatafutia wapi!” Sandra alijibu kwa kuduwaa.
“Inabidi tuitafute ile namba. Ni wao pekee ndio watakuwa wanahusika, hakuna mwingine. Mnakumbuka ule ujumbe niliowaonyesha?” Bakari aliuliza alafu akaendelea:
“Ama twende tukavamie nyumba yao.”
“Una uhakika gani watakuwa wamewaweka humo?” Jombi aliuliza. Wote wakawa kimya kwa muda kabla Bakari hajatizama vibonyezeo vya simu yake Nokia tochi kwa sekunde kadhaa kisha akachukua peni haraka na kuanza kuandika kitu kwenye karatasi. Aliandika: ‘BEAST’ alafu akawaonyeshea wenzake.
“Ndio nini?” Jombi aliuliza.
“Maana ya tarakimu: 251 19-20.” Vitalis akajibu. “Hizo namba walizoziweka hapo zina maana ya BEAST, yani mnyama. Badala ya kuandika herufi, wao wakatumia namba za herufi. A = 1, B = 2, C = 3 na kuendelea. 2 maana yake B, 5 maana yake E, 1 maana yake A, 19 maana yake S, na 20 maana yake T.”
“Sasa itatusaidiaje kuwapata wenzetu.” Jombi aliuliza. Sandra akalipuka:
“Najua! Najua walipo!”
“Wapi?”
“Kuna jengo! … Kuna jengo kubwa njiani kuelekea Arusha. Nakumbuka Isaac alishawahi kunionyesha kwa mbali. Limeandikwa BEAST kwenye paa. Isaac aliniambia ni sehemu ya mateso na mateka, ila yeye mwenyewe hawezi kufika huko!”
“Na ni kwasababu hakuwa kwenye kundi la nyoka!” Bakari alidakia.
“Twendeni!” Miraji akapaza sauti.
Jengo la BEAST lilikuwa maili kama thelathini toka ulipo mkoa wa Dar Es Salaam. Lilikuwa ni jengo pweke lisilo na jirani isipokuwa tu uwanda wa msitu na vichaka. Ukuta mkubwa na mrefu ulikuwa umelizunguka jengo hilo pamoja na geti refu jekundu. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anafahamu nini kinachoendelea ndani ya jengo hilo isipokuwa tu wahusika. Hakuna unyama ambao uliachwa kutendeka ndani ya jengo hilo ambalo halikuwahi kushuhudia mateka yeyote akitoka na pumzi yake aliyoingia nayo. Kilikuwa ni kiwanda cha kupokonya uhai wa watu na kuwageuza wafu waliofukiwa kwenye mashimo kadhaa yalikuwa umbali mdogo tu na jengo hilo. Baada ya muda mashimo hayo yalifukuliwa na kutoa mbolea ambayo ilichanganywa na madawa kisha kusafirishwa nje ya nchi. Ni ngumu kuyafahamu yote hayo kutokana na ulinzi mkali unaobana eneo hilo. Ni jengo pekee tena likiwa limekaa mbali na barabara hivyo kufanya usalama kuwa imara tangu kunawapa fursa walinzi kutizama pande zote za jengo na kugundua hatari mapema iwezekanavyo.
***
☆Steve