Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

**SURA YA AROBAINI NA MOJA**




(MSIMU WA 02)






Kesho yake ndani ya asubuhi Tahid akiwa amevaa suti yake nyeusi alikutana na bwana Isaac Makongo kwenye mgahawa mmoja uliokuwa na watu wachache. Walikuwa wanapata kifungua kinywa huku wakipeta soga. Kila walichokuwa wanakiongea kilikuwa kinasikika na Vitalis, Kaguta, Jombi na Miraji waliokuwa wapo ndani ya gari aina ya van iliyosimama umbali wa kama mita mbili toka eneo la mgahawa.
Uso wa Tahid haukuonyesha woga wala tafakuri tatanishi yoyote lakini mikono yake ilikuwa inatetemeka. Hakuweza kubeba kikombe cha chai, kila alipojaribu aliishia katikati na kukirejesha mezani. Isaac akagundua hilo.
“Vipi kuna tatizo?”
“Ndio.”
Tahid akatoa bunduki yake na kumuonyeshea Isaac huku akiwa ameificha na koti, akamuamuru afuate gari aina ya van iliyoko kando, Isaac akatii, wakasogea mpaka garini. Gari likafunguliwa Isaac akaingia ndani. Tahid akasema:
“Nimemaliza kazi yenu sasa, naomba video na remote ya bomu niende.”
Mara ghafla gari likatokea kwa nyuma, Tahid aligeuka kushangaa akakutana na risasi tatu zilizokita kifuani mwake, akadondoka chini kama gogo. Vitalis akafunga milango ya gari, mafuta yakakanyagwa kwanguvu. Barabarani ikawa mfukuzano, gari la wakina Vitalis mbele, nyuma yao wakiwa wanakimbizwa na Range rover nyeusi, risasi zikirushwa kama njugu. Magari yalipelekwa kwa kasi mno kama vile game. Kaguta aliyekamatia van alihakikisha habandui mguu wake sehemu ya kukanyagia mafuta, hata pale konani. Lakini hata waliokuwa wanawakimbiza walifanya vivyo hivyo.
Kaguta akatoka barabara kubwa ya njia nne, akaingia ya njia moja. Ila punde kwa mbele yakatokea magari mawili makubwa, yakaziba njia. Kaguta alipotaka kurudisha nyuma akashindwa, alibanwa na Range rover hatua kadhaa nyuma. Wanaume watano: mapacha watatu na wengine wawili wakashuka toka kwenye magari yao wakiwa wamebebelea bunduki wakawaamuru wote waliokuwepo ndani ya van washuke chini haraka kabla namba zinazohesabiwa hazijafika kumi.
Wakiwa katika mahesabu hayo, Vitalis akawaambia wenzake:
“Muda wa plan B sasa.”
Jombi akachomoa solo tape mfukoni akamfunika mdomo Isaac alafu wakashuka watu wanne tu: Vitalis, Kaguta, Jombi na Isaac. Miraji akabakizwa ndani. Mapacha wale watatu na wenzao wawili wote wakajongea sehemu moja, nyuma ya van, kumpokea Isaac. Vitalis na wenzake walikuwa wamenyoosha mikono juu, lakini muda huo huo wote walikuwa wanahesabu namba kwa kunong’oneza tokea wametoka ndani ya van. Ilipofika namba tano, wote wakarukia pembeni, ghafla van ikarudi nyuma haraka na kuwasukuma maadui wote kwanguvu wakarukia huko, wakina Vitalis wakawahi silaha za maadui na kuwaweka chini ya ulinzi. Wakawaamuru wote wapande ndani ya van. Wakapanda na kuondoka.
Wakiwa wametembea kwa dakika moja barabarani, mapacha watatu wakatizamana kwa macho yanayowasiliana. Mmoja akasema kwa kunong’oneza:
“Plan b.”
Wote wakapeleka mikono kwenye saa zao za mikononi na kuzibofya, moshi ukaanza kutoka taratibu. Wao wakabana pumzi huku wakiwatizama wengine ambao haikuchukua muda wakalewa na kulala. Baada ya lisaa limoja, macho ya Kaguta yakafunguka. Mapacha watatu, Isaac na wenzao wawili hawakuwepo, walibakia wahusika wanne wa kundi la WAGENI tu. Van ilikuwa imesimama kandokando ya barabara ikiwa wazi.
“Amkeni!” Kaguta aliwaamsha wenzake. Vitalis akapepesa macho kisha akauliza:
“Wapo wapi?”
“Hawapo. Wameondoka.” Kaguta alijibu huku akiwa amekunja sura. Vitalis akapiga ngumi gari.
“Shit! … Shit!”
Alishia tu kutikisa kichwa na kushika tama. Gari liliwashwa wakaondoka. Walipofika nyumbani, Bakari akawahabarisha.
“Nilifunga kamera ndani ya gari, nadhani inaweza kutusaidia kutupa baadhi ya taarifa.”
Wakaketi na kuanza kusoma matukio yote yaliyotukia ndani ya gari kwa kupitia tanakilishi ya Bakari. Wakaona jinsi mapacha wale watatu walivyopeana taarifa na kubofya saa zao. Wakaona pia jinsi walivyonusurika kufa baada ya jaribio la kupigwa risasi kushindikana pindi wakiwa wamelala kilevi baada ya mapacha wale watatu kukosa risasi za kufanyia tukio. Video ilipoisha, Kaguta akasema:
“Nadhani tulikosea target. Kumpata Isaac yatupasa kwanza kuwauwa hawa mbwa watatu. Wao ndio kila kitu. Na inawezekana Isaac ana chip ndani ya mwili wake, popote atakapokuwepo, hawa mbwa watatu watafahamu.”
“Kweli.” Vitalis akaunga mkono hoja.
“Ila kati ya hao watu watatu wanaofanana kuna ambaye anaongoza wenzake.” Miraji alichangia, “Wote hawa ni mtu mmoja tu ambaye amegawanywa, inaitwa Human Plurality Modification, ama HPM. Ukitizama vema video utaona kuna ambaye anatangulia kufanya kitu alafu wengine ndio wanafuata. Hata pale kwenye kunong’oneza huyo anayetangulia yeye ndiye aliyefanya hilo tukio, wengine wakafuata, huyo kiongozi anaitwa ‘the brain’ama ubongo. Kama tunataka kuwamaliza hawa watatu inabidi kwanza tumjue kiongozi wao, na huyo ndio awe primary target.”
“Miraji, Umejulia wapi haya mambo?” Kaguta aliuliza, Miraji akatabasamu kisha akamtizama Vitalis huku akitabasamu. Vitalis naye akarejesha tabasamu kisha akasema:
“Tuna bahati sana kuwa na wewe kwenye kundi letu. Sasa umetupa matumaini mapya. Naamini ukikaa na Bakari mnaweza mkafanya kazi nzuri tukakamilisha misheni yetu kwa ufanisi.”
Miraji akamtizama Bakari alafu wote wakatabasamu na kutikisa vichwa.
“Okay jamani. Naomba nitoe udhuru.” Kaguta akasema huku akisimama. “Leo nina mtoko na bibie Sandra usiku huu, naomba nikajiandae wandugu, si unajua tena?”
“Unaweza tu ukaenda, take care!” Vitalis akamsabahi rafiki yake. Kaguta akampa mkono kila mtu na kuwatakia kazi njema. Kaguta alipotoka ndani Miraji na Bakari wakamtizama Vitalis kwa macho yenye mshumbusi wa tafakuri.
“Vipi? … Mbona mnanitizama hivyo?” Vitalis aliuliza.
“Wewe hautoki na mwenzako?” Miraji akasema. Vitalis akaigiza.
“Nitoke na nani?”
“Kwani hujui nani?”
“Sijui nini mnaongelea.”
Bakari na Miraji wakatabasamu.
“Tunadhani na wewe ni muda muafaka wa kwenda mtoko na Miss Bernadetha.” Bakari akapasua jibu.
“Tafadhali mfanye mama yangu afurahi.” Miraji akashindilia msumari. Vitalis akakosa cha kusema, alibakia tu akitabasamu. Alinyanyuka akaenda chumbani kwake. Miraji na Bakari wakagongesha viganja vyao.
Baada mida ya saa mbili ya usiku gari la Kaguta likatua kwenye uwanja wa nyumba ya Vitalis. Ndani yake alikuwemo Kaguta na Sandra wakiwa wamependeza haswa. Honi ilipigwa na punde wakatoka Vitalis akiwa ameongozana na Bernadetha. Vitalis alivalia suti nyeusi wakati Bernadetha akiwa amevalia gauni refu jeupe lenye maua mekundu shingoni na mabegani. Walikuwa wanang’aa. Kaguta alitabasamu akamwambia Sandra:
“Yeyote aliyewapa hawa watu wazo la kufanya hivi, abarikiwe na mwenyezi Mungu mwenye enzi.”
Vitalis na Bernadetha wakapanda garini wakaondoka kwenda moja kwa moja KACHIKA BEACH HOTEL. Waliketi meza moja kila mtu akiwa karibu na mwenza wake. Vinywaji vikaletwa na kuchafua meza, mhudumu akamimina kinywaji kwenye kila glasi kisha akaondoka na kurudi na sahani zenye chakula laini.
Bakari na Miraji bado hawakuwa wamelala. Wote walikuwa wameketi karibu na tanakilishi wakiperuzi mambo. Miraji alishikilia usukani kwa kuweka vidole vyake juu ya vibofyeo akiweka maneno na kuyatafuta mtandaoni. Alama za fomula za kisayansi zilikuwa zinawekwa na kutafutwa mara kwa mara, mara zingine vitabu vya mambo ya uzalishaji na uzazi vikitafutwa na kusomwa na Miraji huku akiwa anaandika baadhi ya taarifa kando. Bakari alipiga mhayo akauliza:
“Uliyajulia wapi hayo mambo, Miraji?”
Miraji akaandika kwanza kitu kando alafu akamtizama Bakari aliyekuwa anarembua kiusingizi akamwambia:
“Haya ndiyo mambo niliyoyasomea India. Kabla sijaacha shule na kurudi nyumbani nilikuwa kwenye utafiti juu ya hii sayansi ya kugawanya watu na wakafanana vilevile.”
Bakari akapiga mhayo tena. Miraji akarejesha macho na vidole vyake kwenye tanakilishi akaendelea. Baada ya muda akasikia mtu anakoroma, aligeuza shingo kutizama akamkuta Bakari ameweka kichwa chake juu ya meza, amelala. Akanyanyuka akambeba akamlazia kwenye kochi kisha akarudi kuendelea na kazi yake.
Vicheko vilitawala meza ya wakina Vitalis. Nyuso za furaha zilitawala huku hakuna aliyeonekana kama anafikiria ulimwengu mwingine mbali na ule waliokuwemo. Kaguta na Vitalis walikuwa wanashindana kuimba huku wanawake wakiwa mahakimu kwa kutoa point. Kwakuwa hakuna aliyekuwa na sauti nzuri ya kuimba, basi lile tendo likawa kama mchezo wa futuhi, wote wakawa wanacheka na kusemana hapa na pale. Tafrija ilikuja kukatishwa pale alipokuja mwanamke mmoja akiwa kavalia nguo za wahudumu. Mwili wake ulikuwa umejaa kwa shepu ya kibantu, alitembea kwa madaha yote akasimama nyuma ya Kaguta kisha akainama na kumnong’oneza.
“Helo mpenzi!”
Kaguta akashtuka na kutizama sauti ilipotokea.
“Bhoke!” Kaguta akatahamaki. “Unafanya nini hapa?”
“Kwani vipi, hukutegemea kuniona, mpenzi?”
“Mpenzi wako nani? … Embu tafadhali nenda, hivi ndivyo mlivyofundishwa kuhudumia wateja?”
Bhoke akaguna.
“Leo unaniona takataka enh? Leo sina maana kwako, sio?”
“Kaguta, huyo nani?” Sandra akaingilia.
“Usihofu, mpenzi. Nitakuelezea.” Kaguta alijitetea.
“Utaeleza nini?” Bhoke akauliza, “Kumbe hata jina ulin’danganya ukanambia unaitwa Benson? Mwanaume wewe!”
Kaguta alinyanyuka akamtoa Bhoke lile eneo. Alimvutia mbali kabisa na eneo walilopo wenzake, akashusha pumzi ndefu na kutikisa kichwa chake.
“Unafanya nini, Bhoke? Tangu lini mimi na wewe tulikuwa wapenzi? Si tulikuwa tunamalizana tu kila mtu anaenda na zake?”
“Nilikudai pesa mara ngapi? Nilikudai pesa mara moja tu ile siku ya kwanza, siku zingine nilikuwa nakupa penzi bure kabisa. Unavyosema tulikuwa tunamalizana unamaanisha nini?”
Kaguta akatoa pochi yake mfukoni.
“Unanidai shilingi ngapi?”
Bhoke akasonya.
“Unadhani kama nilikuwa nataka pesa nisingekuambia muda wote huo? … Nakutaka wewe Benson, sijui Kaguta, vyovyote vile.”
“Unan’taka mimi?”
“Ndio. Nataka penzi ulilonipa liwe la kwangu tu.”
“Una wazimu wewe enh?”
“Ndio. Penzi lako lanipa wazimu.”
“Bhoke, tafadhali naomba uende. Unajua wale ni watu wa heshima sana. Unaniharibia picha yangu kwa kabisa.”
“Kwahiyo?”
“Nenda, tutayamaliza baadae.”
“Ole wako usinitafute.”
Bhoke akaondoka. Kaguta akashika kiuno.
“Aisee! Yani nimekimbia kule nije huku kumbe ndiyo nimeyakuta huku huku.”
Alitikisa kicha chake akang’ata lips.
“Kaja lini huku huyu mwanamke? … Mungu wangu!”
Aligeuza akawarudia wenzake akakuta kiti cha Sandra kitupu. Vitalis akamwambia:
“Ameondoka. Pole kwa maswahibu.” Kisha akatabasamu.
Hawakuchukua tena muda mrefu hapo, wakalipia bili na kuondoka zao. Kaguta aliwarudisha Vitalis na Bernadetha nyumbani yeye akaenda zake kwa madai ya kumfuata Sandra. Vitalis na Bernadetha wakaingia ndani wakawakuta Miraji amelala pembeni ya tanakilishi huku Bakari akiwa hajielewi usingizini kwenye kochi. Vitalis alimnyanyua mmoja mmoja akawapeleka chumbani na kuwafunika na shuka. Bernadetha alisimama mlangoni akimtizama Vitalis akiwafunika shuka wanausingizi. Vitalis alitoka chumban akamtizama Bernadetha kwa sekunde kadhaa, Bernadetha akasema:
“Una nguvu kweli. Umewabeba watu wazima hivyo.”
Vitalis akainama na kumnyanyua Bernadetha.
“Hata wewe naweza kukubeba.”
Alimpeleka chumbani akamlaza.
“Nakutakia usiku mwema. Nimefurahi sana kuwa na wewe usiku huu.” Kaguta alisema kisha akatoka chumbani. Bernadetha akavuta mto na kuukumbatia kwanguvu. Alitabasamu mwenyewe akajisemea:
“Ahsante kwa kurudisha furaha yangu.”
Masaa yakakimbia usiku ukakata. Asubuhi ya saa tatu, Miraji na Bakari walikuwa pamoja na Vitalis kwenye meza ya tanakilishi. Miraji akachukua karatasi yake aliyokuwa anaiandikia, akasema:
“Kuna habari nzuri na mbaya. Nianze na ipi?”
“Mbaya.” Vitalis akajibu.
“Habari mbaya ni kwamba, hatujapata njia ya kuwakamata mapacha watatu.”
“Na nzuri?”
“Habari nzuri, tumepata watu ambao kwa njia moja ama nyingine wanahusika na tendo hili la kisanyansi.”


***

☆Steve
 
Sandra kaenda wapi tena isije kuwa kaenda kufanya jaribio la kujiua tena, maana sijajua Sandra ni kabila gani isije ikawa ni kabila la mkoa flani mabingwa wa kujiua
 
Sandra kaenda wapi tena isije kuwa kaenda kufanya jaribio la kujiua tena, maana sijajua Sandra ni kabila gani isije ikawa ni kabila la mkoa flani mabingwa wa kujiua
Timu yao imepanda daraja msimu huu
 
**SURA YA AROBAINI NA MBILI**



(MSIMU WA 02)





“Wakina nani?”
“Tafiti hii imefanywa na watu wawili tu ulimwengu mzima: Profesa Kumar wa India na Profesa Hox wa Bermuda. Kama ningelifanikiwa basi nami ningekuwa wa tatu. Watafiti hao wawili ndio ambao wamefanikiwa kufikia tamati lakini kukiwa na utofauti mdogo, profesa Kumar wa India yeye alifanya practice yake kwenye mimea wakati profesa Hox yeye akifanya practice kwa wanyama akitumia panya. Wote walifanikiwa kwa kuunda vitu vipya vilivyofanana. Shida hatujui nani ndiye mhusika mkuu.”
“Ni profesa Hox.” Vitalis akajibu kwa kujiamini.
“Umejuaje?”
“Bermuda ni makao ya Mr Kim Slavatore. Ni lazima kutakuwa na mahusiano.”
“Kwahiyo?”
“Inabidi twende huko. Hakuna namna.”
Baada ya siku mbili ndege kubwa ya British Airways ikatua ndani ya uwanja wa kimataifa wa L.F. Wade, Vitals na Kaguta wakashuka. Walichukua taksi ikawapeleka hotelini wakapumzika kwa siku hiyo waliyofikia. Siku iliyofuata wakaanza msako wa kumtafuta profesa Hox kwa kwenda Bermuda College. Walitizama ratiba ya profesa huyo kwenye ubao wa matangazo, wakarejea siku ya maonano.
“My name is Vitalis, from Tanzania. And this fellow of mine, called Kaguta from the same country.”
“What can I help you?” Profesa Hox akauliza. Alikuwa ni mzee mwenye uwaraza na nywele zenye mvi. Macho yake yalikuwa yamefunikwa na miwani kubwa ya macho. Alikuwa na mustachi mweupe kwa mbali, alivalia shati lililojikunjakunja na suruali mpauko ya jeans.
“We are in need of your assistance and your cooperation, professor. There are some sensitive matters we want to discuss with you.”
“What matters?”
“Its about HPM: Huma Plurality Modification research.”
“What about it?”
“Can we discuss it further out of here?”
“No. And I’m not in the mood of talking about such matters. Just leave, please. Don’t ever come back here. Leave or I will call security.”
Vitalis akamtizama Kaguta.
“Tuondoke.”
Wakanyanyuka na kuondoka.
Wakati jioni imefika profesa Hox akafunga ofisi yake na kufuata gari lake. Alikwea akaondoka toka eneo la chuo, nyuma yake kuna gari likawasha taa na kuanza kumfuata profesa kwa umbali kidogo. Ikiwa ni kasoro lisaa, profesa akafika aelekeapo. Aliingia kwenye nyumba moja yenye ukubwa wa kati, geti likafungwa.
Siku iliyofuata na iliyofuata mchezo ukawa ndio huo huo wa profesa kufuatwa na gari nyuma yake pasipo kujua. Siku ya tatu, Kaguta akauliza:
“Kuna haja gani ya kufanya hivi, Vitalis? Huoni kama tunapoteza pesa kila siku kwa kukodi gari na kukaa hotelini?”
“Kaguta, inabidi tujue kwanza maeneo anayopenda kwenda huyu mlengwa wetu. Tujue kama huwa anafuatiliwa au anakutana na nani muda fulani ama mara kwa mara kabla ya kuchukua hatua yoyote. Kumbuka tupo kwenye makao ya adui. Kuwa mvumilivu.”
Siku ya nne baada ya Profesa kuingia ndani kwake akitokea kazini, Vitalis naye akaruka ukuta na kuingia ndani. Profesa akiwa sebuleni akasikia mbwa anabweka sana huko nje. Alitoka akiwa amebebela bunduki kubwa ‘gobore’ akatizama huku na kule pasipo kuona kitu.
“Shut up you dog!” Profesa alifoka. “I will kill you if I will hear your stupid barks again, fool!”
Akarudi ndani na kujilaza kwenye kochi ambapo napo hakukaa sana akaendea jokofu na kutoa chupa ya kilevi akawa anaigigidia mdomoni mithili ya kwamba yupo mashindanoni. Wakati anafanya yote hayo Vitalis akawa anamtizama kwa kumchungulia, baada ya muda mfupi Vitalis akatoka na kumrudia mwenzake aliyekuwa ameketi kwenye gari.
“Umepata nini?”
“Kuna kitu nimegundua. Profesa anaishi mwenyewe na ni mtu ambaye anasumbuliwa na msongo wa mawazo. Anakunywa na analala na picha kubwa iliyo ndani ya fremu.”
“Sasa hiyo itatusaidia nini, Vitalis?”
“Kaguta, inabidi tujue udhaifu wa profesa. Unadhani kila kitu kitaendeshwa na mdomo wa bunduki?”
Hawakuongea tena, gari lilitiwa moto wakahepa.
Siku iliyofuata Vitalis akafanya kile kile alichofanya siku iliyopita. Alizamia ndani ya nyumba ya profesa Hox akachungulia ndani. Akamuona profesa Hox anakunywa pombe huku akiwa anatizama picha kubwa akilia. Mara kadhaa alikuwa majina ya watu yakiambatana na vyeo vya mtoto na mke. Baada ya muda Vitalis akamrudia mwenzake, wakaondoka.
Siku iliyofuata Vitalis na Kaguta wote wakaingia ndani ya nyumba ya profesa punde tu baada mwenyeji kuingia, walimuweka profesa chini ya ulinzi na kumkalisha kitini. Kaguta akamnyooshea bunduki profesa.
“Tell us everything about HPM before I send you to hell.”
Profesa akatabasamu,
“Just kill me, unknown friend. Stop wasting you time.”
Vitalis akashusha mkono wa Kaguta.
“Si kila kitu kinaenda na risasi, Kaguta. Acha niseme naye.”
Vitalis akamtizama profesa machoni na kusema:
“I am sorry for all of our troubles. It is just we are in great need of your valuable explanations about HPM. Our country is in trouble because of it. Please help us.”
Profesa Hox alinyamaza kimya. Aliwatizama Kaguta na Vitalis kisha akatizama chini. Vitalis alishusha pumzi ndefu akamtazama tena profesa machoni.
“What about your family?”
Profesa akakunja sura yake.
“What do you know about my family?”
“Nothing.” Vitalis akajibu, “But what I know is that you are lonely and somehow you wish they could be here with you.”
Macho ya profesa yakaanza kubadilika rangi na kuwa mekundu. Vitalis akaendelea kuongea:
“There are many families in Tanzania that are in risk of becoming like yours because of HPM mis-use. Please help us, please save other families.”
Profesa hakuongea kitu, machozi yalimtiririka. Vitalis alinyanyuka akamuachia namba yake na kumtaka amtafute atakapokuwa tayari. Usiku huo wote mzima profesa akaumaliza kwa kulia.
Siku iliyofuata saa kumi na mbili jioni, profesa Hox akakutana na Vitalis pamoja na Kaguta maeneo ya ufukweni. Wakiwa wanakunywa vinywaji laini, profesa akaeleza yote anayoyajua kuhusu HPM. Haikuwa amri yake kupelekea matumizi mabaya ya teknolojia aliyoigundua bali ilikuwa ushawishi wa nguvu wa bwana Kim akiwa kateka familia yake na kuwapa madawa ya kuwaua kwa kumlaghai atawaponya pale tu atakapokabidhi tafiti yake nzima. Kwa kutumia teknolojia yake hiyo akatengeneza viumbe vyenye nguvu na uwezo wa ajabu baada ya kuchanganya vinasaba vya wanyama tofauti wa mazingira mbalimbali na wenye fiziki kubwa. Vinasaba hivyo vikawekwa kwenye miili ya wakina mama wajawazito na pindi walipojifungua wakatoka watoto mapacha. Ila miongoni mwao ni yule pekee aliyekuwa tumboni ndiye atakuwa na uwezo mkubwa wa kuliko wenzake. Na mara nyingine wenzake watakuwa wanafuatisha kile afanyacho. Atakapouwawa ama kujeruhiwa, wenzake wote watapata matokeo sawasawa na hayo.
Kaguta akataka kujua zaidi kuhusu udhaifu wao na kivipi wanaweza kuuwawa kwa wepesi. Profesa Hox akataka apewe muda zaidi arudi maabara kufanya utafiti.
“We don’t have time, professor. Please hurry up.” Vitalis akausia.
“I will try my level best.” Profesa akawapa moyo.
Zikapita siku tatu profesa Hox akiwa anashinda maabara usiku mzima. Siku ya nne akakutana na Kaguta na Vitalis akiwa amebebelea briefcase. Walikutania palepale walipokutana mara ya kwanza. Akiwa ameshikilia briefcase lake kwanguvu na mara zingine akitizama tizama usalama kwa kuangaza huku na huko, profesa akasema:
“Make sure you put this liquid inside of their body, it will either weak them up fast or kill them as well.”
Wakati profesa anatoa briefcase ikatokea gari moja jeusi Jaguar, lilikuwa latembea kwa kasi mno, mtu mmoja akachomoza ndani ya hilo gari na kurusha risasi nyingi mno kuwafuata wakina Vitalis. Profesa Hox akamiminiwa risasi za tumboni na kifuani. Briefcase nalo likachakazwa. Vitalis na Kaguta wakapona baada ya kulala chini upesi. Gari likatokomea haraka na kupotea machoni. Vitalis na Kaguta wakaharakisha kumtizama profesa Hox, wakamkuta ameshakufa, walipofungua na briefcase hawakukuta kitu, vyote vilivyokuwemo vilikuwa vimevunjika na kumwagika. Kaguta alishika kichwa chake kama mtu aliye msibani akapiga yowe:
“Uuuuuuuuuwiii!”
Alipiga magoti akamtizama Vitalis.

***

☆Steve
 
***SURA YA AROBAINI NA TATU**




(MSIMU WA 02)





“Sasa tumekuja kufanya nini huku, Vitalis? Dah!”
Vitalis akashika kiuno chake akashusha pumzi ndefu.
“Nyanyuka twende, Kaguta.”
Kaguta akanyanyuka wakaondoka. Wakaenda nyumbani kwa profesa Hox.
“Unadhani tutapata kitu huku?” Kaguta aliuliza.
“Ndio. Nina hisia hizo kabisa.”
Walizunguka nyumba ya profesa wakatokea maabara. Baada ya kupekuapekua wakaona kuna kamera, walizivunja zote kisha wakaendelea kutizama tizama. Punde Kaguta akaona karatasi moja kubwa jeupe likiwa limeandikwa fomula za kikemia. Akamuita Vitalis na kumuonyesha. Vitalis akatabasamu na kumkumbatia Kaguta.
“Tumeipata! … Hii ndo’ yenyewe.”
“Umejuaje?”
“Huoni ameandika hapa HPM demise formula?”
Haraka wakatoka ndani. Walikata tiketi ya ndege Siku ya pili kufuata wakawa tayari wapo ndani ya ndege kurudi nyumbani. Ila kuna watu walikuwa wanawafuatilia. Bahati nzuri waliwahi, kabla hawajakutwa ndege ilikuwa tayari ipo angani.
Baada ya siku moja wakawasili Julius. K. Nyerere Airport. Miraji na Bakari wakaja kuwapokea. Vitalis alimuonyesha ile karatasi Miraji, akamuulza:
“Unaelewa chochote hapo?”
Miraji akatizama karatasi kwa umakini alafu akajibu:
“Ndio.”
Vitalis akaangua kicheko. Walipofika nyumbani Miraji akamuonyesha karatasi mama yake, akaitizama kisha akamtikisia kichwa. Miraji akamuambia Vitalis:
“Tunaweza kutengeneza ila kuna mahitaji yanatakiwa yawepo.”
“Hakuna shida kuhusu hilo.” Vitalis akawatoa shaka. “Nitazitafuta na kuzileta, tajeni tu.”
Baada tu ya siku moja kazi ya kutengeneza dawa ikamalizika. Lakini bado ikawa haitoshi.
“Tutawapata wapi sasa?” Miraji aliuliza.
“Hiyo ni kazi yangu.” Bakari akajibu. Alivuta tanakilishi yake akacheza video iliyorekodiwa kwenye van. Ilipofikia sehemu gari la mapacha lilipoonekana likiingia, akasimamisha video. Akanakili plate number za hilo gari, akalichora na kuli-scan. Alifungua mtandao wa Dar city center akatuma gari alilochora na kulitafuta, punde taarifa zikaja.
“Lipo maeneo ya Kijitonyama kwa sasa pembeni ya Exim bank kwa mujibu wa kamera zilizo karibu.”
Kaguta, Vitalis na Miraji wakabebelea sindano za dawa wakapanda gari kuelekea Kijitonyama. Walipofika wakaliona gari lengwa ila wenye nalo hawakuonekana wapo upande upi wa dunia. Kaguta akapaki kando kwa lengo la kungojea.
Baada ya dakika moja lilitokea gari kubwa aina ya Scania likagonga gari walilomo wakina Kaguta kwanguvu upande wa nyuma na kulifanya nyang’anyang’a. Kabla wakina Kaguta hawajafanya lolote, gari likasukumwa kwanguvu kufuata ukuta mkubwa ulio mbele. Kaguta alijitahidi kukamata breki lakini haikusaidia kuwasimamisha wakazidi kusogelea ukuta kwa haraka. Kaguta aligeuka akapaza sauti:
“Tushuke upesi!”
Milango ya gari ikafunguliwa watu wakajirusha nje. Gari la Kaguta likaburuzwa na kwenda kubondwa ukutani likageuzwa chuma chakavu kufumba na kufumbua macho. Kaguta alishika kichwa chake, akalalama:
“Gari langu!”
Mapacha watatu wakashuka toka kwenye gari lao kubwa na kuanza kuchukua hatua kuwafuata WAGENI. Kaguta alishindwa kusubiria akawakimbilia mapacha adui akamvaa mmoja wao na kumbwagia chini, kabla mapacha wengine wawili hawajafanya kitu nao wakavamiwa na Vitalis pamoja na Miraji. Mapigano yakazuka lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa na uwezo wa kumshinda pacha aliye naye. Mapacha walikuwa na nguvu, wepesi na wenye kufikiria kwa haraka zaidi. Kabla Vitalis hajanyanyua ngumi yake na kuituisha kwenye uso wa pacha, tayari mkono ulikamatwa na kutenguliwa. Kabla Kaguta hajanyanyua teke mguu ulishapanguliwa na kurudishwa. Kabla Miraji hajatuma kichwa chake, pacha alishawahi na kupeleka kichwa chake haraka. WAGENI hawakupata hata muda wa kutoa sindano kwenye mikanda yao iliyobebelea vifuko. Walichakazwa ndani ya muda mchache, wakiwa wamelala chini kwa kuchoka, mapacha walisonga karibu yao wakawanyooshea midomo ya bunduki. Mmoja aliyekaa katikati akasema kwa kubinua mdomo:
“Sali sala zenu za mwisho.”
Kabla vidole vyao havijabinya vitufe ghafla likatokea gari aina ya defender rangi ya kijivu likiwa katika mwendo wa kasi sana. Mapacha wote waligeuza shingo zao kutizama hilo gari. Liliwasomba kama fyagio likawatupia mbali mithili ya mipira. Gari lilisimama wakachomoza Jombi, Bernadetha na Sandra wakiwa katika nguo za kazi.
“Mpo okay?”
Jombi aliuliza kwa sauti.
“Tupo sawa!” Vitalis akajibu, Kaguta akaongezea:
“Tupo fresh.” Huku akimpa mkono Miraji na kumnyanyua. Mara sauti ya Scania ikapasua ngoma zao za masikio. Walistaajabu kuona Scania linakuja kwa kasi kufuata gari walilokuja nalo wakina Jombi. Jombi aliondoa gari lao haraka kurudi nyuma. Bernadetha na Sandra walichomoza madirishani wakaanza kumwaga risasi wakilenga Scania. Baada ya muda mfupi Scania lilisukuma defender ikageuzwa upande unaoelekea Scania. Bernadetha aliendelea kumwaga risasi akapasua kioo cha pembeni na kumjeruhi pacha mmoja wapo begani. Jombi alishika usukani na mkono mmoja mwingine akatolea bunduki akapasua matairi ya Scania. Scania likasimama tuli. Jombi akasogeza gari na kulipaki mbele kidogo mwa Scania, yeye na wenzake wote wakaelekezea bunduki zao kwenye Scania wakingoja yeyote atakayetokea awe mali yao. Punde Kaguta na Miraji nao wakafika eneo la tukio. Macho yao yote yalielekezwa kwenye gari kubwa jekundu, Scania.
“Vitalis yupo wapi?” Bernadetha alimuuliza Kaguta. Kaguta aligeuza geuza shingo yake pasipo kumuona Vitalis, alistaajabu:
“Wote tulikuwa tunakuja hapa …. Sijui wapi ameelekea. Miraji umemuona Vitalis?”
“Hapana.”
Wakiwa kwenye bumbuwazi wakasikia sauti za watu wanaolia kwa maumivu ndani ya Scania. Mara wakaona damu zachafua kioo cha mbele cha gari hilo kubwa, ndani ya sekunde chache pacha mmoja akatupwa nje akiwa anavuja damu, amechanwa chanwa usoni na shingoni, punde tena akatupwa pacha mwingine na mwingine alafu kukabakia kimya kama vile hakuna kilichotokea. Kwa dakika nzima hakuna aliyefanya lolote zaidi ya kubung’aa. Bernadetha alishuka akakimbilia kwenye Scania. Alichungulia ndani akaona mwili wa binadamu umejikunyata mfumo wa coil u-uchi wa mnyama. Akaita kwa uso wenye wenye mushkeli:
“Vitalis!”
Mara yule mtu akatizama sauti inapotokea. Loh! Alikuwa ni Vitalis. Bernadetha akatabasamu kisha akawatizama wenzake waliokuwa wanajongea. Akasema kwa furaha:
“Vitalis! Vitalis yupo humu!”
Baadae giza likiwa limetawala na Vitalis akiwa amejipumzisha kitandani, Bernadetha akafungua mlango na kuingia ndani. Aliketi kitandani akamgusa bega Vitalis.
“Unaendeleaje?”
Vitalis alijinyoosha akajibu:
“Naendelea vizuri. Wewe je?”
“Nipo poa. Nini kilitokea, Vitalis?”
Vitalis alishusha pumzi ndefu kwa kutumia pua yake alafu akatikisa kichwa:
“Bernadetha.” Aliita, “Mimi sio binadamu tena.”
“Kwanini unasema hivyo, Vitalis?”
“Mimi ni mnyama sasa. Tena mnyama wa ajabu. Nimeshuhudia kwa macho yangu nabadilika, natokwa manyoya kama simba!”
“Usihofu, Vitalis. Pumzika kwa sasa. Tutaongea baadae, hakuna lisilowezekana.”
Bernadetha alisema huku akimfunika shuka Vitalis alafu akatoka na kwenda sebuleni alipowakuta wenzake wakiwa wanamsubiri.
“Anaendelea vizuri. Nimemtaka apumzike kwa sasa.” Bernadetha alisema kwa sura yenye uhakika. Kaguta akauliza:
“Amekuambia lolote kuhusu mabadiliko yake?”
Bernadetha akakuna nyusi kwanza alafu akajibu:
“Ameniambia kwamba aligeuka na kuwa mnyama. Yupo katika hali ya hofu ndio mana nikamtaka apumzike tuyapanga baadae.”
“Unadhani nini litakuwa tatizo kwenye mwili wake?” Miraji aliuliza. Jombi akawahi kujibu:
“Pasi na shaka ni wale mbwa mwitu wa kisiwani- walimng’ata mkono wake. Huwa nasikia mate yao si mazuri kwa kiumbe kama binadamu, yaweza pelekea akapata mabadiliko sometimes.”



***

☆Steve
 
***SURA YA AROBAINI NA NNE***





(MSIMU WA 02)






“Sasa tutafanya nini kama hayo anayoyaongea Jombi yakisadikika?” Sandra akauliza. Watu wakakaa kimya kwa dakika kadhaa, pumzi tu ndizo zikisikika. Hakuna aliyeonekana ana majibu, hata wenye nayo labda walihofia kuyasema mbele ya kadamnasi. Mwishowe waliamua kufunga kikao mpaka pale watakapolipatia ufumbuzi linalowatatiza.
Siku iliyofuata saa tano na dakika ishirini na tatu asubuhi, Bakari alisimama mbele ya wenzake wote wakiwa sebuleni. Mkononi mwake alikuwa kabebelea kafimbo kadogo keupe akiwa anakatumia kuonyeshea kilichoandikwa ama kuchorwa kwa kugusia ubao mweupe uliokuwa umesimama na miguu minne mbele yake. Juu ya ubao kulikuwa na tarakimu kadhaa pamoja na mchoro mkubwa wa nyoka aliyejiviringita kwenye mti na kusimamisha vichwa vyake vitatu juu. Bakari alisema akionyeshea mchoro wa nyoka:
“Huu ndio mchoro waliokuwa nao mapacha watatu kwenye migongo yao. Ni tofauti kabisa na michoro mingine tunayoifahamu. Bila shaka utakuwa na maana yake ambayo tunahitaji kuifanyia ufumbuzi.”
Kaguta akakohoa kidogo kukamata atensheni za watu alafu akasema:
“Bakari, huo mchoro si mara ya kwanza kwetu kuuona. Kama una kumbukumbu nzuri kwa mara ya kwanza tuliushuhudia ukutani mwa yule mzee wa Bwagamoyo.”
Vitalis akatikisa kichwa chake kama mtu anayekubali kilichosemwa.
“Ni kweli anachokiongea Kaguta, tuliuona huo mchoro huko. Utakuwa una maana gani? Kuna haja ya kuurejelea kwa bwana Alwatan Kombo?”
Sandra akaguna. Watu wote wakampa nyuso zao.
“Kwa bwana Kim hakuna kundi moja linaloweza kumlinda na kuhakikisha matakwa yake yanatimia. Ni lazima awe na mianya na fursa nyingi kufanya hayo. Je kwenye huo ukutwa wa bwana Kombo, mlipata kuona michoro mingapi?”
Kaguta na Vitalis walitazamana kama vile kila mtu anamngoja mwenzake aanze. Vitalis akajibu:
“Nadhani kama nakumbuka vema, ni michoro mitano.” Alafu akauliza, “Au sio Kaguta?”
Kaguta akatikisa kichwa. Sandra akaendelea kutema maneno:
“Basi tukae tukijua kwamba kuna makundi matano yanayomlinda Mr Kim. Kila kundi litakuwa na miiko yake pia wajibu wake, na vile vile viongozi. Kuna haja ya kung’amua hilo.”
“Ila hatuoni kama hapo tunajiingiza kwenye msoto mwingine mpya kabla hatujaumaliza huu uliopo?” Bernadetha aliuliza kisha akaongezea:
“Mi nadhani kuna haja kwanza ya kumalizana na hawa mawakala wanaobebelea mchoro wa jitu. Baada ya hapo tuhamie kwenye hilo kundi jingine. Kwa maono yangu naona kama vile haya makundi yanategemeana kwa njia moja ama nyingine, na yana hulka ya kusaidiana. Kundi hilo la nyoka limewasaidia wenzao eidha sababu wameombwa wafanye hivyo ama wameona wenzao wapo taabani.”
“Naunga mkono shauri.” Jombi alisema. “Tulinywe kwanza tulilolikoroga kabla ya kuomba kopo lingine la togwa.”
Wazo likapewa fursa. Bakari akaendelea na ubao wake, sasa akagusisha ki-fimbo chake kwenye tarakimu zilizoandikwa pembeni ya mchoro wa nyoka: 25119-20.
“Nyuma ya shingo ya pacha mmoja kuna nambari hizi. Kuna yeyote mwenye utambuzi kuhusu hili?”
“Naomba hilo liwe homework. Tuanze kupanga jinsi ya kuwakamata mawakala kwa kuanza na Isaack.” Kaguta alitoa wazo. Vitalis akatabasamu.
“Hapo ndio patamu sana. Hakuna sehemu napapenda kama hapo. Tuanze sasa.”
Bakari akafuta ubao na kuandika kichwa cha habari ‘THE PLAN’.
Ilikatiza siku moja baina yao. Siku iliyofuata ikiwa ni jioni Isaac alikuwa kwenye gari lake akirudi nyumbani. Alifika getini akapiga honi lakini hakuna aliyekuja kumpokea wala kumfungulia geti. Alikunja sura yake akalaani huku akishuka garini:
“Pumbavu sana huyu. Kaenda wapi muda huu?”
Alisogelea geti akajaribu kulisukumiza likafunguka.
“Yani hata geti kaacha wazi. Jinga kabisa! Naona amechoka kazi sasa.”
Aliingiza gari lake ndani, akarejea kwenye geti lake na kulifunga. Moja kwa moja akaenda ndani. Hakuona pembezoni mwa kibanda cha mlinzi kulikuwapo na matone ya damu yakielekea nyuma ya kibanda hiko. Labda angelijua angelisita kwenda ndani.
Mlango wa sebule ulifunguka pasipo kelele Isaack akaingia ndani. Kabla hajafanya lolote alinyoosha mkono wake akawasha taa. Uso kwa uso akakutana na njemba mbili zikiwa zimejaa kwenye kochi, nyuso zao zilikuwa zimevikwa vinyago vyeusi, macho tu yakiwa wazi. Isaack akakodoa macho.
“Wakina nani nyie?”
Njemba mmoja akatoa bunduki yake na kumnyooshea Isaack. Akamuamuru:
“Kaa chini!”
Isaac akatii.
“Sisi ni wageni wako wa leo.” Sauti ya Vitalis ilisikika toka kinywani mwa yule aliyebebelea bunduki.
“Mnataka nini kwangu?”
“Tunataka uhai wako. La sivyo utupe taarifa tunazozitaka.”
Isaack akatabasamu.
“Kumbe ni nyie. Bado hamjachoka kunifuatilia? … Labda tu niwasaidie kuokoa muda wenu kwa mara nyingine kwa kuwapa jibu la moja kwa moja – sitosema lolote, msitegemee kupata taarifa yoyote toka kwangu.”
Njemba aliyeshikilia bunduki akamtizama mwenzake na kumpa ishara ya kichwa. Mwenzake akanyanyuka na kwenda mbele kidogo akifuata chumba cha kulia chakula. Kilikuwa ni giza tupu hakuna kinachoonekana. Njemba yule akawasha taa tap! Mara ikaonekana miili mitatu mfu ya mapacha wakiwa na majeraha ya kina kirefu. Isaack akapigwa na butwaa. Alitaka kunyanyuka lakini akaamriwa na njemba mwenye bunduki:
“Tulia hapo hapo!”
Akatulia. Uso wake ulibebelea tambara la wasiwasi mkubwa.
“Najua ulikuwa unaleta kiburi kwasababu ulidhani watu wako wa kukusaidia wapo. Pole sana, najua umeshtushwa. Sasa vipi utatupatia majibu yetu?”
Isaack alikunja sura akaropoka:
“Laiti mngejua mnachohangaika nacho ni kikubwa kuliko nyie, msingediriki kuhatarisha maisha yenu kiasi hiki. Hamtofika popote, nawahakikishia. Hakuna atakayewatambua nyie kama mashujaa. Kwani mnataka shilingi ngapi? Semeni niwape. Mmenisababishia hasara kubwa sana. Mmekamata unga wangu wa pesa ndefu mkauharibu, bado hamjatosheka?”
Njemba mwenye bunduki hakusema kitu, alibinya kifyatulio taratibu risasi ikaenda kwa kasi na kutoboa goti la Isaack. Isaack akapiga kelele kali za maumivu.
“Nishakuambia nini nataka. Ulisikia nikisema pesa?” Njemba mwenye bunduki akauliza. “Sasa basi utanipa ninachokitaka au lah?”
Isaack aliendelea kulia na maumivu. Njemba mwenye bunduki akafyatua tena risasi kulenga ugoko wa mguu mwingine, Isaack akalia kama mtoto.
“Please stoop! … Please naumiaa!”
“Utakapokuwa tayari kusema utaniambia. La sivyo tutaendelea na zoezi letu hatua kwa hatua.” Alisema njemba mwenye bunduki kisha akalenga risasi kiatu cha Isaack. Isaack akaendelea kumwaga kilio. Jasho lilimvuja. Damu zilimtapakaa miguuni. Machozi nayo yalimtiririka. Hakujua ashike wapi aache wapi. Njemba mwenye bunduki akanyooshea bunduki kwenye ugoko wa mguu ulitobolewa goti. Isaack akanyoosha mkono mmoja akimpa ishara ya kumkataza.
“Nasema! … Nitawaambia mnachokitaka! Nakuomba usiendelee, nakuomba!”
Njemba mwenye bunduki akapumzisha mkono wake juu ya mapaja, akauliza:
“Umeanza biashara ya madawa ya kulevya kuanzia lini? Unauingizaje nchini? Na unapouleta, unampelekea nani?”
Isaack akameza kwa mate alafu akaongea akiwa anatetemeka.
“Nimeanza miaka mitano iliyopita. Nahonga vyombo vya usalama na wao ndio wanaonipitishia, bandarini au uwanja wa ndege.”
“Na soko?”
“Soko langu hasa hasa ni vijana. Pia napeleka kwa wale vijana ambao wapo kwenye kambi zetu za mafunzo.”
“Mr Kim Salvatore ni nani kwako?”
“Simjui.”
Njemba mwenye bunduki akanyanyua mkono wake uliobebelea silaha. Isaack akapayuka:
“Nasema! Nasema! Nakuomba usifyatue! Nasema!”
“Mr Kim Salvatore ni nani kwako?”
“Ni boss wangu. Yeye ndiye mkuu wetu.”
“Na wewe una nafasi gani kwake?”
“Mimi ni wakala. Nahusika kusajili wale wote wenye ngozi nyeusi Tanzania kujiunga na jeshi la Mr Kim.”
“Vipi kuhusu mtandao wenu hapa Tanzania, ni mpana kiasi gani?”
“Hakuna sekta ambayo hakuna mtu wetu. Zote zina mtu wetu kwa njia moja ama nyingine. Tafadhali naomba niende hospitali, nimepoteza damu nyingi mno.”


***

☆Steve
 
steve vp mzee muda ndio huu au leo zamu yako ya sungusungu

steve ukuje tym ndio hii

Utamu unakuja.
Utamu unakata.

Sandra kaenda wapi tena isije kuwa kaenda kufanya jaribio la kujiua tena, maana sijajua Sandra ni kabila gani isije ikawa ni kabila la mkoa flani mabingwa wa kujiua

Mambo yananoga tu

Mkuu ushatupa alosto ya kutosha tupia
Haya chap chap njoeni.



☆Steve
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom