***SURA YA THELATHINI NA NANE***
(MSIMU WA 02)
Saa tano na robo usiku.
Vitalis alikuwa juu ya kitanda akiwa amefunga macho kama mtu aliyelala. Alikuwa amevaa kaptula fupi huku kifua chake kikiwa wazi. Ni kama vile kuna kitu kilikuwa kinamsumbua kwani alikuwa akijigeuzia huku na huko huku akiwa amekunja sura yake. Baada ya muda mfupi akiwa anajibiduabidua Vitalis alianza kutota mno. Jasho lilimvuja na kulowanisha kitanda. Kama hilo halitoshi alianza kugugumia lakini ajabu sauti aliyokuwa anaitoa haikuwa iliyozoeleka, bali ya kunguruma kama simba. Jeraha lake la meno ya mbwa mwitu mkononi nalo lilianza kuvuja likitoa ute mzito wa maji maji, na wakati yote hayo yanafanyika macho ya Vitalis yalikuwa yamefumba.
Zilichukua dakika tano zoezi likiwa ni hilo hilo lajirudia. Vitalis alikuja shtuka akawa anahema kwanguvu. Alitizama viganja vyake na miguu, mishipa ilikuwa imedinda. Alijishika shingo kama vile anaugulia. Alinyoosha viungo vya mwili huku akiwa amekunja sura. Akajiuliza,
“Nini kimetokea?” huku akitizama vinyweleo vyake vilivyokuwa vimesimama dede.
Saa moja na nusu asubuhi.
Bakari alikuwa anapiga mswaki huku akiwa anatizama tanakilishi yake iliyokuwa inamuonyesha ndani ya nyumba ya OCD. Baada ya punde alimuona OCD akiwa anamkaribisha mtu ndani kwake. Bakari alivuta karibu picha ya kamera, akamuona bwana Isaac Makongo akiingia ndani na kuketi kwenye kochi akifuatiwa na OCD aliyeketi kando naye. Hapo Bakari akaamua kufuta picha za kamera zingine kwenye kioo cha tanakilishi yake na kukuza picha ya kamera moja tu ambayo ilikuwa karibu na wahusika wake. Alipofanya hivyo, alitoa mswaki mdomoni mwake akapaza sauti kumuita Vitalis, Vitalis akaja punde.
“Rekodi, haraka!” Vitalis alimuagiza Bakari, haraka zoezi hilo likaruhusiwa kisha wote macho yao yakawa yanatizama.
“Naomba mnipatie ulinzi ndugu zanguni nipo hatarini.” Sauti ya OCD ilivuma ikimuambia Isaac.
“Usihofu, tupo na wewe mwanzo mpaka mwisho. Fadhila zako kwetu si za kusahaulika. Umetusaidia sana kukamata hii nchi na tunakuahidi kukulinda.”
“Ahsante sana, Isaac. Ila unadhani ni nani aliye nyuma ya mpango huu wa kuniua?”
“OCD, Mr Kim ni mtu mkubwa sana ulimwengu mzima. Ni mtu mwenye mafanikio na kama unavyojua biashara zake, hawezi akakosa maadui. Maadui hao ndio wanaokutafuta kwakuwa wanajua mchango wako kwa bwana Kim. Ila ondoa hofu ushanipa taarifa.”
“Sawa. Nakuamini.”
“Mengineyo?”
“Hakuna lingine, mkuu. Labda tu niliulizie fungu langu, umepita mwezi sasa.”
“Lingine?”
“Hakuna.”
“Ok. Pesa yako itakuja kesho, kuna kijana wangu atakuletea ofisini kwako. Ila kumbuka kuna mzigo unakuja ukitokea Brazil, hakikisha unapita airport pasipo na shaka. Ni mzigo wa milioni mia tano, unga wa high class.”
“Niachie hiyo kazi, mkuu. Unajua huwa sikuangushi.”
Baada ya maongezi hayo walinyanyuka wakapeana mkono kisha wakatoka ndani. Bakari alimtizama Vitalis wote wakajikuta wanatabasamu.
Siku iliyofuata saa kumi na moja na dakika tano jioni, mlango wa OCD uligongwa. OCD alpofungua alimkuta mlinzi wake akiwa amebebelea kasha la CD. Mlinzi akamkabidhi kasha hilo na kumuambia:
“Kuna mtu amepitisha nje, amesema ni mzigo wako.”
“Nani?” OCD aliuliza.
“Simjui.” Mlinzi akajibu.
“Unaruhusuje mtu usiyemjua akupe kitu na ulete kwangu? Kama bomu je?”
“Hapana, mkuu. Nimekikagua nikaona ni CD tu.”
OCD alichukua ule mzigo akauweka ndani ya DVD player alafuakaketi pembeni ya runinga yake. Baada ya CD kucheza machozi yalianza kumtoka OCD. Aliona kila kitu ambacho alikifanya na kuongea na Isaac. Picha ya CD ilipokwisha, maandishi yalijionyesha yakisomeka: TUBU MAOVU YAKO KABLA HATUJASAMBAZA KANDA HII KWENYE VITUO VYA HABARI.
Uso wa OCD ukabadilika ghafla na kuwa mweusi zaidi. Alidondosha runinga yake akaipasua. Akatafuta kamera zote zilizopachikwa ndani kwake akazitoa na kuzipasua. Ujumbe ukaingia kwenye simu yake;
“It is too late.”
Nayo simu akairushia ukutani na kuipasua. Akapiga yowe kali la hasira. Jasho la hamaki na woga likamtoka. Machozi yakazidi kumbubujika, mwishowe akakaa kwenye kiti na kushika tama uso wake ukiwa na mikanganyiko ya hofu na hasira. Hakika ndege alikuwa tunduni sasa. Tena tundu bovu.
Baada ya masaa kumi na mbili, chaneli za runinga zikaanza kurusha matangazo ya moja kwa moja. Kanda ya OCD ilisambazwa kwenye kila kituo cha chaneli za runinga. Kwenye kila kioo cha runinga picha ya OCD na Isaac Makongo ikatapakaa, wananchi wakaona kwa macho yao. Haikuchukua muda mrefu, magari ya polisi yakaongozana kwenda kwa OCD. Walikuta mwili tu, OCD akiwa tayari ameshajimaliza kwa kunywa madawa. Ni msiba ndio ukafuata baada ya hapo, watu wengi wakahudhuria ikiwemo waliokuwa wafanyakazi wenzake na OCD, lakini wengiwao walikuwa wananchi wa kawaida ambao waliguswa na taarifa za OCD na eidha walitaka kumuona mtu huyo kwa sura kabla hajamezwa na udongo wa dunia.
Vitalis Byabata alikuwa ni miongoni mwa wahudhuriaji wa msiba. Alikuwa amevaa nguo nyeusi na miwani yenye vioo vya kahawia. Kidogo alikaa mbali na wenzake, alikuwa ametulia tuli akitikisa kichwa chake. Kulikuwa na makelele mengi watu wakiruruma huku na kule, ila kuna sauti fulani iliteka masikio Vitalis.
“Hili jambo linatutisha sasa, nani atakayefuata baada ya mkuu wetu? … Inabidi sasa tujitizame vizuri ndugu yangu bila hivyo tutakwisha.”
Vitalis akageuza shingo yake kutafuta makazi ya hiyo sauti. Kwa mbali toka kwake akaona watu wawili wananong’onezana. Kabla ya kujiuliza kwanini wale watu wanaongelea yale mambo, Vitalis alishangaa amesikiaje sauti toka mbali vile, tena ya watu wanaonong’onezana? Haikuwa kawaida. Badala ya kushughulikia wale watu Vitalis akaanza kukumbuka usiku ule aliokuwa anahangaika kitandani, je una mahusiano na yale mabadiliko yake? Mwishowe akaamua kupuuzia na kuweka akili yake kwa wale watu wawili ambao muda mfupi baada ya kuaga mwili wa marehemu waliagana na kuondoka. Mmoja wao aliyekuwa mfupi, jina Morgan, akiwa amevalia shati jeusi na suruali ya jeans alifuata gari lake Harrier akaingia ndani. Kabla hajaipa moto gari, alikabwakwanguvu na mtu tokea viti vya nyuma. Akaulizwa;
“Wewe ni nani? Na OCD na Bwana Kim ni nani zako?”
Morgan akaleta ngumu kusema kitu. Alikabwa kwanguvu zaidi, akaamua kusema;
“Naitwa Morgan, ofisa wa polisi.”
“OCD na Kim ni nani zako?”
“Mabosi wangu … Ni mabosi wangu.”
“Sawa sawa. Sasa basi, tunakupa nafasi ya kutubu ili uwe hai. La sivyo uhai wako utakuwa haki yetu.”
Baada ya hicho kitisho, mkabaji alishuka gari likaondoka. Kumbe alikuwa ni Vitalis Byabata, alitoa simu yake mfukoni akampigia Bakari.
“Nimepachika kifaa kwenye mojawapo ya gari, unaweza ukakiona hapo kwenye mashine yako? … Hakikisha unaifuatilia hiyo gari, naamini baada ya kumtishia atafanya move itakayotusaidia kuwapata wote.”
Simu ikarudishwa mfukoni. Kaguta akaondoka kurudi nyumbani, alimkuta Bernadetha akiwa chumbani pamoja na Kaguta. Walikuwa wamevaa gloves nyeupe. Juu ya meza kulikuwapo na sindano nyingi, madawa yaliyokuwa yamepondwa na kabeseni ka maji. Kaguta alikuwa anatwanga madawa, wakati Bernadetha akichukua madawa na kuyaweka kwenye maji kisha anayafyonza na sindano na kuziweka pembeni. Vitalis akawapa pole kwa kazi. Alivua miwani yake akasema;
“Kuna mambo nahisi hayapo sawa mwilini mwangu.”
Kaguta na Bernadetha wakaacha kazi yao na kumtizama Vitalis.
“Mambo yapi?” Bernadetha akauliza.
“Usiku nimekuwa nahangaika sana, natota jasho. Alafu ajabu, nimekua na uwezo mkubwa wa kusikia. Sijui imekuaje?”
“Vipi jeraha lako limepona?” Bernadetha akauliza, kabla Kaguta hajajibu, Bernadetha akanyanyua mkono wa Vitalis na kuutizama. Jeraha halikuwapo. Lilikuwa limekauka pasijulikane hata kama kuna kitu kilitokea. Bernadetha alimtizama Vitalis kwa uso wa butwaa. Akauliza;
“Imekuaje jeraha limepotea haraka hivyo?”
Mara sauti ya Bakari ikaingilia ikiwaita. Wote walitoka wakaenda sebuleni.
“Lile gari limeelekea msitu wa Pande!” Bakari alitoa taarifa. “Kutakuwa kuna kitu kinafanyika huko.”
Vitalis akamuita Jombi na Miraji akawataka wajiandae waende kazini.
Huko ndani ya msitu wa pande, Morgan akiwa na wenzake wanne walitoka kwenye gari wakatembea hatua kadhaa. Kisha wakaanza kujadili. Waliona msituni ni salama kuliko ndani ya nyumba kutokana na yale yaliyomkuta OCD. Ila baada tu ya muda mfupi, WAGENI wakawa tayari wamewasili eneo la tukio. Vitalis alisafisha koo lake, wakina Morgan wakageuka na kuwakuta wanaume wawili ndani ya vinyago; Kaguta na Vitalis. Morgan akatabasamu.
“Hatimaye mpo kwenye mikono yetu. Mlidhani sisi wajinga, sio? Kuja huku msituni huku mkiwa mmepachikatracker kwenye gari letu?Poleni sana. Kwa taarifa yenu tuliona mlichokiweka kwenye gari, na tumewavuta huku ili muwe historia. Tutawaua na kuwazika huku huku, hakuna atakayewajua.”
Vitalis akatikisa kichwa naye akasema:
“Unadhani hilo linawafanya msiwe wajinga? Bado nyie ni wajinga kwasababu, moja; mmesahau kwamba mmeacha alama za matairi ya magari matatu manne, alafu mkaacha moja hapo ili ionekane mpo wenyewe wakati mmekuja wengi, matokeo yake tumeshaharibu magari hayo. Pili, mmesahau kufuta nyayo zenu zilizoingia humu msituni, inaonekana mpo watu hamsini tano na hapo mnajidanganya kwa kutuonyesha mpo watano. Sasa unadhani na sisi ni wajinga kiasi cha kuja kupambana na watu hamsini na tano kwa wawili?”
Morgan alitizama wenzake, alafu akapiga mluzi. Mara wakatokea watu hamsini tokea gizani waliobebelea bunduki. Wote wakanyooshea bunduki kwa Vitalis na Kaguta. Vitalis naye akapiga mluzi, mara taa za gari zikawaka na kuwamulika wakina Morgan na kuwafanya vipofu kwa muda. Milio ya risasi ikavuma. Taa zilipozima, watu wote hamsini waliobebelea bunduki wakawa wapo chini wamekufa. Walibakia Morgan na wenzake wanne tu. Walipepesa macho yao huku na huko, waliposikia kishindo wakaelekezea bunduki zao huko na kufyatua risasi. Mara taa za gari zikawamulika tena usoni na kuwafanya vipofu, zilipozima wote wakawa wameuwawa kasoro Morgan ambaye alichomekwa sindano ya dawa shingoni na kupokonywa bunduki.
“Sasa sikia.” Kaguta alimwambia Morgan. “Dawa uliyowekwa mwilini itakumaliza pole pole. Bahati nzuri dawa ya kukuponya tunayo. Ila ili uipate, nenda katubu maovu yako mbele ya kadamnasi, la sivyo uhai wako utakuwa mali yetu.”
Baada ya hapo, Vitalis na Kaguta wakapotea.
Kwa siku mbili Morgan akawa mtu wa kukakamaa na kutema mapovu macho yakiwa yamemtoka na jasho likimchuruza. Siku ya tatu akaita vyombo vya habari akaeleza ushiriki wake na OCD na bwana Kim. Baadae mzigo wa boksi ukatumwa nyumbani kwake ukiwa umeandikwa ‘antidote’ kwa juu. Ndani yake alikuta kichupa kidogo chenye kinywaji rangi nyekundu. Akanywa.
“Mmmh … Mbona kama Fanta?”
Alipotizama kwa makini akakuta ujumbe kwenye kikaratasi cha chupa … HUNA HAKI YA UHAI. Polisi walipokuja kumkamata Morgan walimkuta tayari yu mfu. Alikuwa chini amekakamaa kama gogo kavu.
***
☆Steve