***SEHEMU YA THELATHINI NA TANO***
(MSIMU WA 02)
Ilipita wiki moja, Vitalis akaruhusiwa kurudi nyumbani. Baada tu ya siku moja kikao kiliitishwa kati ya Vitalis, Kaguta, Miraji, Jombi, Bernadetha, Sandra na Bakari. Katika kikao Vitalis akatoa jibu lake kwamba ameridhia kurudi katika uwanja wa mapambano. Ila akatoa usia:
“Itatakiwa tutumie njia za kisasa zaidi kwa sasa.”
Kutimiza hilo, siku iliyofuata vifaa vilinunuliwa; vinyago, gloves, darubini, nguo nyeusi, mikasi, visu, kamba, vinasa sauti, radio call, tracker, mabuti na hata ramani kubwa ya Tanzania. Pia vikainishwa vipaumbele vya mapambano:
Kwenda kisiwani kukata mzizi wa fitna
Kutafuta na kuwakamata maaskari wanaoshirikiana na kundi la Mr Kim.
Kutafuta mawakala wote wa Kim. Wakianza na Isaac Makongo.
Kuwabana mawakala waeleze Kim alipo.
Kuwatafuta wanaume mapacha watatu.
Kukamata simu na vifaa vyovyote vya mawasiliano vya maadui kwa ajili ya kuwapa taarifa wazitakazo. Mtendaji akiwa Bakari.
Kumaliza na kufunga kila jengo linalotoa mafunzo ya kumtumikia bwana Kim.
Baada ya hapo kundi likapewa jina la THE GUESTS, yani kumaanisha ‘wageni.’
*** NDANI YA MDOMO WA MAUTI ***
Ilichukua juma moja kufuzu mafunzo ya kufyatua na kulenga risasi kwa wasio weza, Sandra na Bernadetha. Baada ya hapo, ikachukua tena majuma mawili kuwekana sawa kwa mazoezi mbalimbali kama vile kukimbia, kuruka, na hata kubana pumzi ndani ya maji, Vitalis na Kaguta wakiongoza wenzao. Walipomaliza hapo, sasa ikachukua tena juma moja kuelekezana jinsi ya kutumia kisu kama dhana pekee iliyo mkononi.
Kurusha kisu kwenye miti, kukata na kufunga na kuchimba kwa kutumia kisu. Hapo sasa ikawa imechukua mwezi mmoja rasmi kumaliza hayo. Siku iliyofuata wakiwa ndani, Bakari aliwafungia vifaa vya umeme mwilini kwa ajili ya mawasiliano. Kila mtu aliwekewa track na kupewa kisafirisha sauti kwa ajili ya kuwasiliana na wenzake.
Walivaa nguo nyeusi za kubana miili, gloves mikononi, na kofia za kufunika vichwa vyao, miguu yao ikaezekwa na viatu vikubwa vilivyobanwa vyema na kamba. Mabegi yao madogo yakajazwa kamba, risasi, mikasi, darubini, na chakula kidogo kilichofungwa kwenye kikontena kidogo cha kubana. Mikanda yao ikabebelea vifuko vya visu vikubwa. Kisha wakajiweka kwenye gari la Kaguta na kuanza safari ya kuelekea bwagamoyo.
Bakari pekee ndiye alibaki, alikaa na tanakilishi yake akiitumikisha satelaiti impe madadavuo ya maeneo yote ambayo wenzake wanakatiza, na hata kuwaelekeza pale panapohitajika. Kisafirisha sauti chake kilikuwa mdomoni, na pembeni yake aliweka kikombe cha kahawa alichokuwa anakipeleka mdomoni mwake kumpasha joto na kumfanya mchangamfu.
Kwakuwa gar aliendesha Kaguta, ndani ya muda mfupi ‘wageni’ walikanyaga ufukwe wa bwagamoyo. Walikodi boti ikawapeleka kisiwani na kuondoka zake. Hakukuwa na maajabu ya boti kupotea wala kuondoka yenyewe, labda kwakuwa jitu halikuwa na taarifa. Kabla ya kuenenda ndani ya kisiwa, Vitalis aliwasogeza wenzake karibu wakapeana maneno mawili matatu.
“Tunaweza tukapoteana humo ndani, hakikisha unawasiliana na wenzako kadiri inavyowezekana. Sawa?”
“Sawa!”
“Na pale utakapopotea, wasiliana na Bakari. Sisi tunamsikia lakini yeye anatuona pia. I know we can make it. Hii ndiyo hatua yetu ya kwanza, hatutakiwi kuipoteza kwa gharama yoyote.”
Waliweka mikono yao katikati wakigusana viganja. Wote wakasema:
“Sisi ni wageni wasio na mualiko. Mwenyeji umejiandaa?”
Walipeana matabasamu wakaifuata njia nyembamba iingiayo ndani. Baada ya hatua kadhaa, upepo ulitokea kusipojulikana ukawazoa na kumsambaratisha kila mtu sehemu yake. Baada ya kudondokea sehemu mpya, Vitalis alituma sauti yake kuuliza hali ya kila mmoja, wote wakasema wako sawa.
“Hakikisha unashikilia bunduki yako vyema. Focus!” Vitalis alisema kwa kujiamini. Wote wakafuata maelekezo. Macho yalitoka na mkono ukashikilia dhana kwanguvu.
“Kila mtu aende upande wake wa kaskazini, mtakutana baada ya kilometa mbili.” Taarifa ilitoka kwa Bakari, wote wakaipata na kuanza kuifuata.
Sandra alikuwa wa kwanza kujaribiwa. Akiwa anatembea kwa umakini, masikio yake yalimpa taarifa kuna kitu kinasogea. Alituma kichwa chake kila upande lakini hakuona kitu zaidi tu ya miti, miongoni mwao ukiwa wa mchungwa.
Basi akaendelea kutembea mbele akielekea kaskazini, ila hakupita muda mrefu, akasikia tena sauti na alipogeuka kutizama hakuona kitu, ila kuna jambo aligundua, mti wa mchungwa ulikuwa umesogea, haukuwepo pale alipouona mara ya kwanza. Kama vile hakugundua hilo, Sandra akaendelea kujongea kwenda mbele.
Punde sauti ya kitu kusogea iliita tena. Sandra aligeuka haraka kutizama na kuelekeza bunduki yake kwenye mti wa mchungwa, kabla hajafyatua risasi, mzizi wa mchungwa ulitambaa haraka ukakamata miguu ya Sandra na kuivuta, Sandra akadondoka, bunduki ikarukia kando. Mzizi ukaanza kumvuta Sandra karibu na mti. Sandra alitoa kisu haraka kiunoni mwake, akakata mzizi unaomvuta kisha akataarifu wenzake hali aliyopo.
“Hold on, nakuja muda si mrefu!” Sauti ya Kaguta ilimwambia Sandra.
Mzizi mwingine ulikuja haraka ukamchapa kibao Sandra na kumchana shavu. Ulimshika mkono wenye kisu ukaugongesha kwenye mti, Sandra akaachia kisu. Mzizi mwingine ukaja haraka ukakamata mguu wa Sandra na kuanza kumvuta tena kusogelea mti, wakati Sandra anavutwa alinyoosha mkono atwae bunduki yake iliyokuwa chini hatua kadhaa, mzizi mwingine ukasukumiza bunduki mbali.
Sandra akasogezwa karibu na mti, mizizi mingine ikachipuka na kumviringita kisha ikamnyanyua juu na kumtupia kwenye mti mwingine, Sandra akafikia mgongo na kudondoka kama mzigo. Alitoa sauti kali ya maumivu huku akiukunja mgongo wake.
“Nakuja Sandra, nipo karibu!” Sauti ya Kaguta ilisikika masikioni mwa Sandra.
“Kaguta fanya haraka!” Sauti ya Vitalis nayo ikasikika.
“Umekaribia kumfikia. Kimbilia upande huo huo.” Bakari naye alisikika akitoa maelezo.
Wakati Sandra akiwa anaugulia mgongo chini ya mti alikotupiwa, mzizi wa mchungwa ulikuja kwa kasi kama mkuki ukifuata kichwa chake, alikwepa mzizi ukachoma mti. Alitaka kunyanyuka, mzizi mwingine ukakamata mguu wake na kumdondosha kisha ukaanza kumburuza tena kufuata mti.
Wakati anasogezwa Sandra alipitishwa juu ya kisu chake, alikichukua kwa siri akaficha mkono nyuma, mzizi ulipomsogeza karibu na mti kama awali mizizi mingine ikaamka na kuanza kumpanda Sandra kuanzia miguuni huku ikimbinya kwanguvu. Ilipofika kiunoni, Sandra alipiga kelele kali ya maumivu, kabla ya mizizi kummalizia kumfunga tumboni na kifuani ilimsogeza karibu zaidi, Sandra akaona macho ya mti huo.
Yalikuwa makubwa na ya kijani mfumo wake ukiwa wa kenge.Hapo hapo Sandra akatoa kisu chake na kukikita kwenye macho hayo kwanguvu. Maji ya kijani yakaruka kama mafataki. Mti ukalalamika kwa kuyumba yumba huku na huko. Mizizi ikafunguka na kumuacha Sandra akadondoka chini, Sandra akiwa amebung’aa hapo, mti wa mchungwa ulidondoka na kumfunika. Alijitahidi achomoke lakini haikuwezekana, alibanwa.
Aliishia kupiga makelele ya kuomba msaada. Bahati njema Kaguta akawasili. Alimvuta akamchoropoa toka chini ya mti.
“Upo sawa?”
“Yah! Nipo okei.”
Kaguta aliutizama mti wa mchungwa kisha akamtizama Sandra.
“Upo vizuri, mama.”
“Ahsante.”
Sandra alichomoa kisu chake akakirejesha kiuoni. Mara sauti ya kelele ikawafikia masikioni kupitia earphone zao. Ilikuwa ni sauti ya Miraji ikiomba msaada. Ikafuatiwa na sauti ya Bakari.
“Miraji amebebwa. Anapelekwa upande wenu wa magharibi kwenu Bernadetha, Vitalis na Jombi, na kwa Kaguta na Sandra ni upande wa kaskazini magharibi. Fanyeni haraka!”
Haraka wote wakaanza kukimbia kuelekea kule walipoelekezwa.
Miraji alikuwa hewani akiwa amebebwa na ndege wa ajabu, alikuwa ni mweusi ti mwenye mdomo mrefu kama chuchunge. Mabawa yake yalikuwa mapana na yenye nguvu ingali macho yake ni mekundu yenye muundowa paka. Miraji hakuweza kufurukuta kwa ndege huyo aliyekuwa kamkamata mkono wake wa kuume na kucha zake zikiwa zimemtoboa.
Alijaribu kuutuma mkono wake wa kushoto kwenda kwenye mfuko wa suruali uliokaa upande wa kulia ili atoe kisu, lakini akashindwa. Upepo ulikuwa mkali na alihisi kupata maumivu zaidi. Hakukata tamaa, alijaribu tena akafanikiwa.
Alikata mguu wa ndege, ndege akamuachia akadondoka chini. Alifikia ubavu akalalamika kwa maumivu makali begani na kiunoni. Alitizama juu kumtizama ndege, ajabu akaona ndege watatu wakiwa wamefanana kama yule aliyembeba. Na mara wale ndege wakaanza kushuka kwa kasi wakimfuata Miraji. Miraji alinyanyuka akaanza kukimbia. Aliweka mkono wake sikioni akamuuliza Bakari:
“Nipo wapi?”
“Unaelekea kusini.” Bakari alijibu. “Nenda upande wako wa mashariki, wenzako wapo upande huo!”
Miraji aligeuza akaanza kuelekea upande wake wa mashariki. Hakufika mbali ndege mmoja alimsukuma na miguu akadondoka chini. Miraji kunyanyuka akakuta kazungukwa na ndege watatu.
Alivua begi lake akataka kuingiza mkono, ndege mmoja akatuma bawa lake likamzaba Miraji na kusogeza begi kando, kisha akamrukia Miraji na kumdonyoa shingoni kwanguvu huku miguu yake ikiwa juu ya kifua cha Miraji. Miraji alifurukuta kumtoa ndege juu yake lakini haikuwa rahisi kwani ndege aliweza kujibalansi na mbawa zake huku akimdonyoa maeneo mbalimbali.
Ilimchukua muda Miraji kuweka kisu chake vizuri mkononi na kukisokomeza kifuani mwa ndege aliyekuwa anamshambulia. Ndege akapiga kelele kali za kulalamikia maumivu aliyoyapata, Miraji akanyanyua mguu wake na kumsukumizia pembeni kisha akanyanyuka na kuanza kukimbia mbio za sakafuni ambazo hazimkufikisha mbali. Ndege wawili waliobakia walimuangusha chini, mmoja akakanyaga mikono ya Miraji na mwingine miguu, Miraji akabakia pasipo ujanja.
Ndege mmoja alipiga kelele za nguvu kwenye uso wa Miraji. Mate yalimtoka na kuingia mdomoni mwa Miraji aliyekuwa ameachama kwa mduwazo. Japokuwa Miraji alitema, lakini alikuwa kachelewa. Ndege alinyanyua shingo yake kwanguvu ammalize mhanga wake, ila mara sauti ya mlio wa bunduki ikavuma, kufumba na kufumbua ndege wote wakamdondokea Miraji wakiwa wafu.
****
☆Steve