***SURA YA KUMI NA TISA***
(MSIMU WA 02)
Akiwa ameketi juu ya kiti kirefu mikono yake kaigemeza kwenye meza ya glocery, Kaguta alikuwa akipata kinywaji kigumu aina ya spirit tena kwa tarumbeta huku taratibu akitingiha tingisha kichwa chake kuonyesha kuvutiwa na muziki upigwao.
Baada ya kumaliza kinywaji chake akaagiza tena kingine kama kile kile akaendelea na starehe zake. Ila baada ya muda kama dakika tano tangu aagize kinywaji kipya, akamuita muhudumu na kumuuliza;
“Bhoke yupo wapi?”
Muhudumu akabinua mdomo na kurembua macho.
“Bhoke hayupo zamu leo, ila mimi nipo sema tu shida yako.”
Kaguta akatabasamu.
“Wewe utaniweza?”
“Kwanini nisikuweze? … Ngoma kubwa hii!”
Hapo Kaguta akacheka na kutikisa kichwa chake.
“Hapana! Hapana kwa kweli. Am sorry. Mi namtaka Bhoke, mtoto mashaalah sana yule, mie ndio type zangu zile!”
“Haya, ndio hayupo sasa!”
“Niitie basi, n’takutoa kidogo.”
“Shing’api?”
“Aaaah we niitie bwana hatuwezi shindwana.”
Mhudumu akampigia simu Bhoke. Baada ya dakika zisizozidi dakika kumi na tano Bhoke akaingizana eneoni na bodaboda. Alikuwa amevalia kimini kuntu chekundu akiacha mapaja yake makubwa rangi ya chocolate yabarizi. Kwa furaha walikumbatiana na Kaguta wakajuliana hali.
“Mbona umen’tupa hivyo, Benson?”
Bhoke alisema kwa tabasamu pana.
“Kazi zinanibana, Bhoke.”
“Kazi wapi wewe sema kama umepata uchi mwingine.”
“Aaaah Bhoke, nani kasema tena hayo?”
“Tatizo lako hata namba zako hukunipa nashindwa hata kukutafuta kwa njia yoyote ile.”
“Hata kama nikikupa namba yatakuwa yaleyale maana nabadili mara kwa mara. We tulia tu n’takuwa nakutafuta kama hivi.”
“Haya bana. Mie sina neno.”
“Nichum basi mtoto.”
Bhoke akambusu Kaguta shavuni.
“Utanibusuje shavuni bana kama mama yako?” Kaguta alilalamika. Bhoke akampa ulimi kabisa.
“Sasa je, mambo si ndio hayo. Kaa hapo unywe mrembo.”
Bhoke akaketi kwenye kiti cha pembezoni na Kaguta akaagiza safari, taratibu akaanza kuisuuza nafsi kwa kinywaji hiko huku wakipiga soga.
“Sasa mtoto, leo si unaenda kulala kwangu?”
“Unavyotaka wewe, mi sawa tu. Ila utanileta kazini kesho maana zamu yangu mchana.”
“Hilo tu, kuna kingine?”
“Walaah sema tu nimemis shoo zako za kibabe.”
Wakacheka na kugongeshana viganja. Kaguta akanyanyuka akalipia vinywaji na kumtoa muhudumu ngalawa kadhaa kisha wakaaga wakaondoka wakiwa wameshikana viuno. Wakati wanatoka kwenye geti la baa, wakapishana na Sandra. Kaguta hakuamini macho yake alidhani labda ni ulevi, alitikisa kichwa akatizama vizuri, akamuona kweli Sandra.
“Si unajua gari langu? Shika funguo, tangulia naja.” Kaguta alimpa maelekezo Bhoke.
“Unaenda wapi tena?”
“We tangulia, naja.”
Kaguta alisema kisha akashika njia kurudi ndani ya bar. Alimtizama Sandra anaelekea wapi, akamuona amemfuata mwanaume mmoja hivi mzee, yule aliyemtoa Robson polisi kipindi kile alivyokamatwa barabarani. Sandra akakumbatiana na huyo mzee na kupeana mabusu kisha wakaketi. Kaguta alitoa simu yake ya mkononi akaanza kuwarekodi kwa tahadhari asionekane.
Ali zoom na kuhakikisha amewajaza wahusika wake kwenye kioo barabara. Hapo akapoteza dakika kama tatu kabla ya honi ya gari haijamshtua na kukumbuka kuna mtu anamsubiria.
“Muda wote huo? Au ulikuwa na kademu kengine huko?”
“Wala! Kuna mtu nilipotezana naye muda sasa nikamuona leo, si unajua tena.”
Kaguta alijitetea, akawasha gari wakaondoka eneo lile.
Asubuhi palipokucha, Kaguta aliamka mapema akamuacha Bhoke kitandani amelala, akavaa nguoze za mazoezi na kutoka nje akaanza kupasha viungo vyake kwenye uwanja wa nyumba yake. Alipiga push up kadhaa, akaruka kamba. Alijog na kukimbia. Alipomaliza akarudi ndani na kumuamsha Bhoke waende kuoga.
Wakaenda kukoga na wakapata kifungua kinywa. Baadae Kaguta akampeleka Bhoke kazini kwake kisha yeye akaelekea Rosemath stationary. Alipaki gari lake upande wa pili wa barabara akawa anatizama eneo la stationary kwa mbali.
Muda ukayoyoma kama masaa mawili hivi likaja gari jeusi Suzuki Escudo likapaki nje ya stationary. Honi ilipigwa akatoka Sandra huku akiwapungia wenzake mkono wa kwaheri, akaingia ndani ya Escudo na gari likaondoka. Taratibu Kaguta akaanza kulifuatilia lile gari kwa nyuma.
Baada ya dakika kadhaa Escudo likapaki mbele ya duka kubwa la nguo maeneo ya Sinza, mzee akashuka na Sandra wakaingia ndani ya duka. Kaguta akawachukua video bila ya wao kujua. Baada ya kama lisaa yule mzee na Sandra wakatoka dukani na kurudi garini kisha Sandra akarejeshwa stationary na gari likaondoka.
Kaguta alipaki palepale alipokuwa amepaki awali. Alifungua video zake akawa anazitizama kwa makini. Alipomaliza aliweka simu yake kando, akalaza kiti na kutulia. Jioni iliposonga, stationary ikafungwa. Wadada wakatoka ofisini mwao na kutawanyika kwenda majumbani. Sandra akaja kuchukuliwa tena na gari lile lile, Escudo nyeusi, akapelekwa mpaka nyumbani kwake kisha gari likaondoka. Lilipotokomea, Kaguta akashuka na kuanza kuisogelea nyumba ya Sandra.
Akiwa ndani ya chumba chake, Sandra alivua nguo akavaa taulo jepesi kisha akaelekea bafuni kukoga. Alipotoka bafuni akamkuta Kaguta kajilaza kitandani. Akapigwa na butwaa.
“Wewe unafanya nini hapa?”
Kaguta akatabasamu.
“Vipi, kwani Roby anakuja?”
“Umeingiaje humu?”
“Kupitia mlangoni.”
“Mlango mbona nimefunga?”
“Haukufunga vya kutosha kunizuia nisiingie. Ila tuachane na hayo, njoo basi.”
“Wapi?”
“Aaah aah! Kwani kuna shida gani, Sandra?”
“Hujui? Mimi sina urafiki na maaskari.”
“Ndio mana ukanchoma siku zile ili bwana’ako afanye tukio?”
Kimya. Kaguta akasimama na kumsogelea Sandra akamshika kalio. Sandra akausukumizia pembeni mkono wa Kaguta.
“Usinishike!”
Kaguta akacheka kisha akawa serious ghafla.
“Kwanza mimi si askari. Si umeona hii?” Kaguta alionyeshea tattoo yake mkononi baada ya kukunja shati lake.
“Pili, siku zile ulinichomea na kunifanya nionekane mpumbavu, bwana’ako akafanya uhalifu. Leo ni zamu yako. Umeona hii?”
Kaguta akaanza kuonyeshea video za Sandra alizorekodi.
“Lazima zimfikie Roby. Kwahiyo jiandae.”
Kaguta alisema kisha akageuka na kuufuata mlango atoke. Ghafla Sandra akamshika mkono. Kaguta alipogeuka akamuona mwanamke kama alivyozaliwa.
“Tafadhali Kaguta, usifanye hivyo. Hujui ni kwa kiasi gani utafanya mambo yawe magumu kwangu na kwa Roby pia. Utasababisha vita kubwa. Please.”
Kaguta akatabasamu na kusema;
“Nitafanya utakavyo, endapo tu utanipa maelezo yote ninayoyahitaji. Upo tayari?”
Sandra alitizama chini na macho yaonyeshayo njia panda. Ni kama vile alikuwa ng’ombe mwembamba aliyelazimishwa ale majani ya shamba nzima ili kesho awe mnene mnadani. Mwishowe aliamua aketi kitandani na kumtizama Kaguta, akafungua mdomo kwa sauti iliyo karibu na mashaka;
“Unataka kujua nini toka kwangu?”
Kaguta akatabasamu. “Hayo ndio mambo sasa! … Kwanza, yule mzee uliyekuwa naye ni nani?”
“Anaitwa Isaac Makongo. Ni mkuu wetu.”
“Mkuu wenu kivipi?”
“Yeye ndiye coordinator. Kila kitu kutoka kwa mkuu hupitia kwake. Kuanzia pesa mpaka vifaa.”
“Kwahiyo ndio upo naye kimahusiano?”
Hapo Sandra alitulia kwanza na kupunguza kasi yake ya kujibu. Alitizama chini, Kaguta akarudia kuuliza swali.
“Si kwamba nipo naye kimahusiano.”
“Bali?”
“Ananitaka na sijui njia ya kumkatalia.”
“Hujui? Kwani wengine unawakataliaje?”
“Kumbuka nimekuambia yule ni mtu mkubwa. Kumkatalia maana yake ni kujiweka kwenye mazingira magumu mno hata kufa pia!”
“Kwahiyo kila mwanamke akitaka kuwa naye anampata, sio?”
“Nadhani.”
“Na vipi kumhusu Roby?”
“Kaguta, hakuna yeyote ninayempenda kati ya hao. Ni mazingira tu yananibana na kuniacha bila ya jinsi.”
“Na utakuwa mtumwa hivyo mpaka lini, Sandra?”
Sandra alidondosha chozi kusikia hilo swali. Alijifuta na vidole vyake vitatu lakini bado hakujibu, alikuwa anatizama tu chini mithili ya mtu anayejutia.
“Nani alikuingiza katika huu mtandao, Sandra?”
Kaguta aliuliza kwa sura ya huruma. Sandra hakujibu, bado alikuwa ameinamisha uso wake akitiririsha machozi. Baada ya dakika kama tano, Sandra ndipo akatia neno kwa sauti ya kukoroma tena huku akivuta makamasi ya kilio.
“Tokea nikiwa na miaka mitano, nilikuwa tayari nina chapa mwilini mwangu. Baba yangu alikuwa mtumishi mkubwa wa bwana Kim kiasi kwamba aliahidi familia yake yote kumtumikia mungu mtu huyo, Kim. Hata mama yangu pia akapigwa chapa na kuwa mfuasi, bahati mbaya yeye na mumewe hawakudumu. Waliuwawa wakiwa kazini na kuniacha yatima asiye na baba wala mama isipokuwa tu chapa niliyo nayo ya bwana Kim.”
Machozi yakawa kama mto kwenye mashavu ya Sandra. Alishindwa tena kuongea, akawa analia tu. Kaguta alimvuta na kumkumbata.
“Usilie, Sandra. Yatakwisha.”
“Hayawezi kwisha Kaguta, kamwe.” Sandra alisema kama mtu mwenye uhakika haswa na jambo analolitema. Kaguta alimbembeleza kama mwanaye, Sandra alipopoa ndio maelezo yakaendelea;
“Tokea hapo, nilichokuwa nakula, nakunywa na navaa ilikuwa ni juu ya taasisi ya bwana Kim. Nilikulia katika mikono hiyo mpaka leo hii najitambua japo siwezi kufanya lolote lile.”
“Hakuna jaribu lisilo na njia ya kutokea.”
“Hapana, Kaguta. Lipo na hili ni mojawapo. Ni ngumu mno kumshikia bwana Kim chini, nchi nzima ipo mikononi mwake. Serikali na mitaa yote ni ya kwake. Unaanzia wapi?”
“Amini mlango upo. Ila tu umepakwa rangi inayofanana na ukuta. Hatuna budi kuutafuta, kwa pamoja tutaweza.”
“Kwa pamoja?”
“Ndio, wewe na sisi.”
Sandra akatabasamu kidogo kisha akatikisa kichwa chake kwa mbali.
“Huwezi ukafanya lolote kwa sasa. Wewe ni mfuasi wa bwana Kim, hiyo chapa uliyo nayo haitokuruhusu ufanye jambo.”
“Hapana. Chapa hii itanizuia tu kutoa siri na si kufanya mengine.”
“Nani kakudanganya? … Ukishawekwa hiyo chapa, huyo aliyechorwa hapo mkononi mwako anaona kila unachokifanya. Kila hatua unayochukua. Kila utakachokuwa unakifanya atakutangulia kwa hatua tatu mbele. Weka hilo akilini mwako. Na hakuna lolote utakalofanya dhidi ya Mr Kim ukafanikiwa.”
Kaguta alitizama tattoo yake mkononi kwa uso wenye ndita. Aling’ta lips akashusha pumzi ndefu. Kwa muda kama wa kasoro dakika kukawa kimya. Kaguta alikumbuka yake yaliyokuwa yanatukia kule kisiwani akijaribu kulinganisha na kile akisemacho Sandra. Ni kweli walikuwa wanatanguliwa hatua tatu mbele? Alijiuliza hilo swali, sidhani kama alipata majibu, akamgeukia Sandra.
“Wapi naweza kumpata Isaac?”
“Wa nini, Kaguta? … Nimeshakuambia haiwezekani.”
“Nijibu maswali yangu.”
“Anaishi kurasini, nyumba namba 898.”
“Unaweza nambia anapendelea kitu gani, ama kutembelea maeneo gani … au ni mtu wa aina gani?”
“Anapenda sana mpira. Huwa hakosi kwenda kutizama mpira hasa Samaki Samaki ya maeneo ya Mbezi beach.”
“Ok.”
Kaguta akachukua simu toka mfukoni mwake akapakua application ya mpira na kuangalia ratiba ya mechi kubwa iliyo karibu, akaona mojawapo iliyopo kesho tena ikiwa ya ubingwa wa ulaya. Alitabasamu, akaenda kwenye reminder ya simu na kuweka tarehe ya mechi hiyo. Alipomaliza, alinyanyuka akamtizama Sandra na macho ya ahadi.
“Naomba niende nikuache upumzike. Tutaonana karibuni.”
“Okay. Take care.”
“You too!”
Kaguta akauendea mlango na kutoka nje. Sandra alivaa nguoze akajilaza kitandani. Hakuoneana yupo sawa. Si kingine itakuwa ni mawazo yalikuwa yanambana. Ila baada ya muda mafuriko ya usingizi yalimsomba na kumpeleka ng’ambo.
****
☆Steve