***SURA YA KUMI NA SABA***
(MSIMU WA 02)
Inspekta, huku akiwa amekinga uso wake dhidi ya mwanga mkali ummulikao, akajibu;
“Tumekuja kuonana na Mzee Kombo!”
“Mna miadi naye?”
“Hapana!”
“Basi nyie ni wavamizi. Je, hamkupata kusikia yale yaongelewayo kuhusu hii mahali?”
“Tumesikia ila tuna shida?”
“Shida isiyo ambatana na miadi kwetu ni ukaidi. Poteeni kwenye hiki kisiwa. Tafuteni njia mtokomee la sivyo kila baada ya dakika kumi na tatu, mtapata jaribu mpaka pale mtakapokwisha kabisa!”
“Basi tunaomba utuonyeshe njia!” Jombi akasema huku akitizama chini, uso wake ameukunja na kauziba na kiganja.
“Kama mlivyokuja, ndivyo mtakavyotoka. Hamkupewa mualiko kuingia na hamtosindikizwa mkitoka. Kumbuka, ni kila baada ya dakika kumi na tatu, hesabu tokea sasa!”
Paap! Mwanga ukapotea. Taratibu mawingu yakaanza kufunguka na kukawa mchana kama awali. Inspekta akanyanyua mkono wake wa kushoto kutizama saa, akaona ni saa nane na nusu. Akawaambia wenzake hayo majira.
“Sasa tunafanyaje? Tunatokea wapi?” Jombi aliuliza.
“Mi nadhani tutumie akili zetu tu.” Inspekta alipendekeza, “mi ninavyojua, mto huwa unamwagia maji baharini. Tuufuatishe mto huu mpaka pale unapomwagia maji yake.”
Kaguta na Jombi wakaafiki. Hao wakaungana na inspekta kuanza kufuatilia maji ya mto yaendako. Huku wakiruka viunzi kama mawe na mabanzi ya miti wakasonga. Baada ya dakika kadhaa, saa ya mkononi ya inspekta ikapiga alarm … ti! ti! Inspekta akaitizama. Akaona sasa ni saa nane na dakika arobaini na tatu. Kabla hajafungua mdomo kulonga lolote, Jombi alipaza sauti huku akionyeshea upande wa pili wa mto;
“Bakari! Bakari yulee!”
Inspekta na Kaguta wakatizama upesi. Wakaona mwili wa mtu ukiwa umejilaza pembezoni mwa mto, nguo na hata umbo likiwa la Bakari.
“Atakuwa amekufa nini?” Kaguta aliuliza.
“Labda. Twendeni tukamtizame, hatuwezi tukamtelekeza.” Jombi alitoa wazo. Haoo, yeye na Kaguta wakaanza kuongozana wakiruka juu ya mawe waende upande wa pili. Inspekta yeye akasita. Jombi na Kaguta walipovuka mto, wakamtizama.
“Njoo bana! Kumbuka huyu jamaa alijitolea kutuleta hapa!” Kaguta alieleza. Inspekta akaamua avuke na kuungana nao wakausogelea mwili wa Bakari uliokuwa umelala kifudifudi.
“Kuna kitu kitakuwa kimemkuta.” Jombi alisema kwa uhakika. Alichuchumaa akataka kumgeuza Bakari alale chali. Upesi, inspekta akamkataza kufanya hilo baada ya kuona kucha ndefu kwenye vidole wa Bakari. Kufumba na kufumbua, Bakari akaamka na kumkwaruza Jombi kifuani! Macho yake yalikuwa mekundu mno kama bendera, meno yake yalikuwa kama ya popo na kuchaze zikiwa ndefu mno. Jombi akasogea haraka huku akimtizama Bakari wa ajabu.
“Bakari, vipi?” Jombi alitahamaki. Kifua chake kilikuwa kinachuruza damu toka kwenye mikwaruzo.
“Huyo si Bakari!” Inspekta aling’aka. “Hilo ni jaribu, dakika ya kumi na tatu imeshatimia.”
Kauli hiyo ilipokoma, Bakari wa ajabu akamrukia inspekta na kwenda naye chini. Bakari yule wa ajabu akanyanyua mkono wake wa kuume amrarue inspekta, Inspekta akauzuia mkono huo na kumtupa Bakari mbali kwa teke. Bakari akanyanyuka haraka, ila kabla hajamrukia tena inspekta, Kaguta akakabiliana naye kwa kwa kumrushia teke, Bakari akalidaka na kumtupia Kaguta pembeni kama karatasi. Jombi akasogea na kurusha ngumi, Bakari akadaka mkono na kuuviringita kisha akampa teke matata Jombi, Jombi akarukia kando.
Inspekta aliokota gongo akalirusha kwa Bakari wa ajabu, Bakari akalidaka. Inspekta akarusha teke, nalo likadakwa kisha Bakari akafunguka kumpa teke la kifua inspekta,inspekta akarushwa kando! Haraka Kaguta alinyanyuka akamsogelea Bakari wa ajabu, Jombi naye akajongea, wakamuweka Bakari kati. Kaguta alirusha ngumi, Bakari akakwepa. Jombi alirusha teke, Bakari akainama kisha ghafla akaruka na kujizungusha hewani akifungua miguu yake ambayo iliwanasiibu vizuri Kaguta na Jombi kwenye mapaji yao ya uso, wakadondokea kando!
Upesi inspekta akanyanyuka na kumrudia Bakari. Alirusha ngumi yake ya kulia, Bakari akaipangua. Alirusha ngumi yake ya kushoto, Bakari akaitoa. Alirusha tena ya kulia, Bakari akaidaka na kumzungusha inspekta kama mtu achezaye blues kisha akamtupia huko kwa teke kali. Sasa wanaume wote watatu; Kaguta, inspekta na Jombi wakawa wapo chini wakigugumia maumivu.
Bakari wa ajabu akacheka sana. Kisha akauliza kwa kebehi;
“Hiko ndicho mlicho nacho?”
Kaguta akakunja sura kwa hasira. Akataka kunyanyuka ila inspekta akamshika mkono na kumuambia;
“Hiyo si suluhishi. Kwa mmoja mmoja hatutoweza, twende kwa pamoja ila kwa akili nguvu na zaidi.”
Kaguta akatikisa kichwa kukubali. Wakanyanyuka na kumfuata Bakari wa ajabu, inspekta akakaa kwa mbele, Kaguta akakaa nyuma yake. Inspekta akatishia kurusha ngumi, Bakari akasogea kidogo. Inspekta akanyanyua mguu wake wa kushoto akitishia kurusha teke, Bakari akajiandaa kulipokea, haraka inspekta akabadili maamuzi, aliruka juu akiwa amekunja goti lake kumshambulia Bakari, Bakari akawahi kujikinga kichwa, na hapo ndipo Kaguta akatelezesha mguu wake kumkata mtama Bakari. Wakati Bakari anaanguka alifungua mikono yake iliyokuwa imemkinga kichwa, huo ukawa upenyo kwa inspekta akampatia goti la meno na kumvujisha damu.
“Pumbavu!” Bakari aling’aka baada ya kutema damu pembeni. Aliwatizama wakina inspekta akawaona wamejipanga vile vile, inspekta mbele Kaguta nyuma. Alipotizama kando, akamuona Jombi, alikuwa ameketi kitako kama mtu atizamaye sinema.
Bakari akaguna huku akibinua mdomowe. Haraka akatumia mikono yake kujifyatua na kusimama. Akakunja ngumi na kuwapa ishara wakina inspekta washambulie. Inspekta bila kulaza damu akakunja goti na kurusha teke, Baraka akalidaka, ila kabla hajafanya lolote na mguu alioudaka, Inspekta akautumia huo mguu kujinyanyulia juu na kurusha teke lingine lililombamiza Bakari usoni na kumpeleka chini. Baraka akanyanyuka tena kwa hasira, alirusha ngumi inspekta akaikwepa Kaguta akaidaka.
Alipotaka kunyanyua mguu arushe teke, inspekta akazuia mguu kisha akampiga Bakari ngumi ya tumbo, wakati Bakari wa ajabu akiguguma na maumivu ya tumbo, mkono wake uliorusha ngumi ulivutwa na Kaguta kisha akapewa ngumi kubwa ya uso akadondokea mti, ukampenya kifuani na kutokea mbele, huo ukawa mwisho wa Bakari wa ajabu.
Inspekta, Kaguta na Jombi wakapongezana. Inspekta akatizama saa yake ya mkononi akaona ni saa nane na dakika hamsini na tatu. Zilisalia dakika tatu tu kutimia dakika kumi na tatu ya pili. Inspekta akawashika wenzake mkono na kuwavuta.
“Tuna dakika tatu tu kabla ya jaribu lingine kuja!”
Kama upepo wakaanza kukimbia kwa haraka mno kuufuata mto. Baada ya muda kidogo, mto ulikata kona wakina inspekta wakashangaa kuona shimo kubwa mno mbele yao. Ndani ya shimo hilo kubwa, ndipo maji yote ya mto yakawa yanamiminikia humo.
“Duh! Sasa tunafanyaje?” Inspekta akauliza huku akihema. Kaguta akainama akashika magoti yake. Jombi akashika kiuno huku akitota jasho. Hawakusema kitu chochote zaidi ya kujitahidi kuvuta pumzi walizoziteketeza mbioni. Ila zoezi lao hilo kabla halijakamilika, lilikatishwa na mlio wa saa ya inspekta. Ilikuwa ni saa nane na dakika hamsini na sita! Inspekta aliwaambia wenzake wakaanza kupepesa macho yao pande zote nane za dunia.
Ajabu hawakuona kitu. Ila baada ya sekunde kadhaa, kwa mbali upande wa kusini wakaanza kushuhudia tukio la ajabu. Miti ilikuwa inadondoka kwa kasi. Ndege walikuwa wanaruka na kukimbia ila hakikuonekana ni kitu gani chafanya hayo!Hapo, inspekta akashauri warukie shimoni mule maji ya mto yaendako. Kaguta na Jombi wakachungulia shimo wasipate kuona kikomo chake. Kidogo wakatia ashki.
“Hakuna njia nyingine, guys. Mmekiona hiko kinachokuja?” Inspekta alionyeshea kidole anapopaongelea.
“Ila unajuaje kama humo shimoni ni salama kuliko hiko kijacho?” Jombi aliuliza.
“Ukiona maji yanaingia mahali, ujue kuna sehemu yanatokea. Simple geography.” Inspekta alisema lakini muda huu hakungoja tena maswali, alishika mikono ya Kaguta na Jombi akajirushia shimoni. Walikuwa hewani kwa takribani dakika tano kabla hawajafika chini walipozama na kuibukia baharini. Walipotizama nyuma yao, wakakiona kisiwa kwa mbaali, kikiwa na udogo wake ule ule.
Walivuka mtihani. Ila sasa tabu ikawa je, watafikaje nchi kavu na hawana chombo chochote? Waliulizana pasipo kupata majibu. Bahati jema, kwa mbali kidogo inspekta akaona mtumbwi wa Bakari. Wakaufuata na kupanda. Huku wakitumia mikono yao kama mapakuo ya maji, wakasogea taratibu taratibu mpaka wakafika nchi kavu.Waliposhuka tu, wavuvi wakawazingira.
“Mwenzetu yupo wapi?”
Inspekta akatizamana na wenzie. Hakuna aliyejibu, wote walitoa tu macho. Wavuvi wakarudia swali;
“Bakari yupo wapi, au mmeshamtoa kafara?”
“Hapana. Kusema ukweli hatujui alipo.” Inspekta alijbu.
“Hamjui alipo? Si mmeondoka naye hapa!” Mvuvi mmoja aliuliza kwa jazba.
“Ndio, tumeondoka naye. Lakini tulipofika kule kisiwani akatupotea. Hatujajua atakuwa wapi.” Kaguta alieleleza. Wavuvi wakatizamana, mvuvi mmoja akawaonyeshea ishara wenzie kwa kupandisha nyusi moja, ghafla wavuvi wakawavamia wakina inspekta na kuanza kuparangana.
Bahati mbaya hawakufua dafu, wakagaragazwa na kufanywa mahututi kwa mateke na ngumi za haja. Inspekta akawaomba radhi kwa usumbufu kisha akashika njia yeye na wenzake waondoke zao. Walipopiga hatua sita mbele, sauti ikawafikia;
“Majambaaaziii!”
****
☆Steve