****SURA YA NNE****
(MSIMU WA 02)
Pembezoni mwa bahari, upepo ukiwa unavuma kwa kasi, kulikuwa kumepakiwa magari mawili, prado nyeusi. Vioo vyake vilikuwa tinted, na wanaume watatu wenye miili mikubwa wakiwa wamevalia miwani meusi na nguo zinazobana misuli yao walikuwa wameegemea magari hayo, mikononi walikuwa na bunduki.
Baada ya muda kidogo, gari ndogo ya kijivu aina ya Toyota Altezza ilifika eneo hilo tulivu ambalo watu hawakuwapo zaidi tu ya wale wanaume watatu. Gari hilo liliposimama, kioo cha nyuma kilishuka akaonekana Jombi, alivalia miwani akiegemea kochi. Baada ya hapo, kioo kilipandishwa na kufunga. Sauti ya inspekta ikasikika tokea kwenye radio call waliyokuwa wamebebelea wanaume wale wa shoka.
“Nami naomba nione familia yangu.”
Mwanaume mmoja aliyekuwa na bunduki akaligonga gari kama ishara, kioo kikashushwa mke na mtoto wa inspekta wakaonekana. Walikuwa na sura zenye hofu. Sauti ya inspekta ikaendelea kusema;
“Nipo peke yangu, mpo watatu tena wenye silaha, mtanipaje uhakika na uhai wangu na wa familia yangu endapo nikiwapa mtu wenu?”
Mwanaume aliyeshikilia radio call akamjibu,
“Hatuna shida na wewe wala familia yako, tunamtaka mtu wetu tu.”
“Okay. Nitahesabu mpaka tatu, utaachia familia yangu, nami nitamuachia mtu wenu. Sawa?”
“Sawa!”
“Moja…mbili…tatu!”
Milango ya magari ikafunguka. Mke na mtoto wa inspekta wakatoka kuifuata Altezza, Jombi naye akatoka akawa anaifuata prado huku akitembea kwa shida kama vile mtu mwenye mpango wa kudondokea kwa mbele. Wakati wanapishana, Jombi alinong’ona akamuambia mke wa inspekta;
“Ukiingia tu ndani endesha, potea.”
Kwa kuwa mwendo wa Jombi ulikuwa ni wa kusua sua alikawia kidogo kuwasili. Alipowafikia tu wanaume wale mabaunsa, Altezza ikawashwa na kuanza kuondolewa. Hapo hapo Jombi akamkamata Baunsa aliyekuwa karibu naye akampiga na kiwiko usoni. Pale tu mabaunsa wengine waliponyanyua silaha zao, ghafla, milio ya bunduki ilisikika, kufumba na kufumbua wote wakawa chini! Punde mwanaume mmoja akiwa amebebelea bunduki, akatoka majini. Alipovua mask yake akaonekana ni inspekta akiwa anatabasamu huku akimtizama Jombi.
Loh! Mara naye yule mwanaume aliyekuwa na sura ya Jombi akajishika shingoni na kuvuta kwanguvu ngozi yake, sura ya Jombi ikabanduka kama nyoka ajivuae gamba. Kumbe alikuwa ni mwanaume mwingine, kwa jina alikuwa anaitwa Kaguta, almaarufu kama “The red bullet”.
“Kazi nzuri sana, broh!” Inspekta alimpongeza mwenzie kwa kumkumbatia. “Naona sasa umerudi rasmi kazini.”
“Ahsante, Vitalis. Nilimiss sana hizi mishe. Natumai utanipa sehemu mujarabu za kutumia ujuzi wangu niliojifunza.”
“Ha ha ha na huko Cuba wamekuharibu kweli. Usikonde kazi zipo nyingi sana. Kuna mlima mkubwa upo mbele yetu unasubiri kusogezwa.”
“Mlima tu. Hata kama ni kukausha bahari am jus ready! Sema nini, sasa ninachokimiss ni warembo wa Cuba. Nawakumbuka kweli!”
“Ha ha ha umeanza Kaguta! Utaacha lini mambo yako?”
“Bado kidogo tu. Wewe si umeoa bwana!”
“Wewe nani kakukataza kuoa? Si hutaki.”
“Najua siwezi kutulia na bucha moja japo nyama ile ile. Vipi, tusepe, au?”
“Ngoja kwanza kidogo.” Inspekta alisema kisha akafuata miili ya watu waliowashambulia na kuanza kuipekua mifukoni huku akikusanya silaha zao. Kwenye mwili wa mmoja akakuta kitambulisho cha mpiga kura, na kwenye miili ya wengine akatohoa simu za mkononi.
“Sasa tunaweza tukaondoka.” Inspekta alimwambia mwenzake wakapanda gari moja wapo la majambazi wakaondoka eneo lile. Wakiwa njiani wakatoa taarifa polisi, ndani ya muda finyu polisi wakiongozana na magari ya kubebea majeruhi walifika sehemu ilipofanyikia tukio.
Jua likazama.
Ndani ya bar pana iliyoezekwa na makuti makavu watu wakiwa wamefurika na meza zikiwa zimechafuka na vilevi, kwenye upande mmoja wa ndanikidogo, alikuwa ameketi Inspekta na Kaguta. Bia kadhaa zilikuwa zimejaa mezani kwao. Kaguta alikuwa akipiga tarumbeta kama wasemavyo wanywaji, akiweka mdomo wa chupa kinywani na kumiminia humo, kwa upande wa inspekta alikuwa anatumia glasi kubwa akiwa anaijazia bia humo pomoni.
“Kama nilivyokuambia ndugu yangu, stori nzimandio hiyo. Nategemea kesho ama kesho kutwa nianze kufuatilia kile kitambulisho labda kinaweza nisaidia kujua hiyo gang inapatikana wapi na ipo chini ya nani.”
“Nakutakia kazi njema. Utakapohitaji msaada wangu, usisite kun’taarifu.” Kaguta alitia neno likafuatiwa na mafundo kadhaa ya bia.“Ila mwanangu kwa jinsi ulivyonambia, inabidi uwe makini. Inaonyesha jamaa wako very well equipped.”
“Hilo kweli, wako vizuri. Wanazo hadi mashine za kutengenezea sura bandia, Fake the face make up!”
“Ila kama isingekuwa yule mama, tusingeweza kufanya ile make-up vizuri.”
“Mama Miraji?”
“Huyo huyo. Yuko vizuri sana.”
“Ni kweli. Msaada wake umetusaidia sana.”
“Namuonea huruma hana mwanaume wa kumliwaza, lazima atakuwa mpweke sana.”
“Nani kasema? Au mawazo yako tu?”
“Kwani hilo nalo mpaka lisemwe? Hujui wimbo wa Yvonne Chakachaka ‘Every woman needs a man?” Aliuliza Kaguta kisha akaanza kuimba wimbo huo kwa sauti akiigiza kama mtu anayetumbuiza jukwaani. Inspekta akamzuia.
“Acha bana, huoni watu wote wanatutizama?”
“Aaaah!...unaogopa watu?”
“Zishapanda kichwani eenh?”
“Waaapi…bado sana, yani hapa wala sisikii. Sijui ni juice hizi au bia? Pombe Cuba bwana.”
“Kila kitu Cuba. Khaa!”
Kaguta akacheka baada ya kusikia hiyo kauli. Waliendelea kupiga soga hapo bar, giza likizidi kuwa nene. Lakini kinyume na muda, kadiri ulivyokuwa unasonga watu wakawa bado wanafurika eneo hilo kustarehe. Pale saa ya inspekta iliposema ni saa nane ya usiku, ndipo mabwana hao wawili waliponyanyuka na kuacha bar nyuma ya migongo yao kwenda kupanda gari la Kaguta, Toyota Mark 2.
“Utaweza ku-drive kweli, Kaguta?”
“Kwanini nisiweze?”
“Ah-ah! Umekunywa sana bwana, lete ufunguo niendeshe.”
“Vitalis, nipo sawa. Mbona muoga sana wewe.”
“Nina familia ndugu yangu.”
“We twende, nimekuambia nakuua mie.”
Walipanda kwenye gari, Kaguta akawa dereva. Kabla ya kuondoka, inspekta alihakikisha kafunga mkanda kwa usalama wake. Gari liliondolewa kwa kasi likawekwa kwenye barabara ya lami, mwendo ukawa wa ku-overtake. Ndani mziki mkubwa ukitema sauti ya Samba Mapangala na kibao chake maridhawa ‘Dunia tunapita’.
.Wakiwa wapo barabarani tayari wameshaacha bar kwa maili zisizopungua tatu, kwa mbali kidogo mbele yao upande waliokuwemo walishuhudia lori lililobebelea mifuko ya saruji, lilikuwa linatembea kwa mwendo wa taratibu huku mara kwa mara taa zake nyekundu za nyuma zikiwa zinawaka. Inspekta alitizama lile lori kwa makini na kwa sura ya woga;
“Angalia usiparamie ilo lori ndugu yangu.” Alitoa nasaha. Kaguta huku akiwa ametabasamu, alipindisha tairi ghafula akahamia upande wake wa kushoto toka upande lilipo lori, kisha akaongeza kasi kwa malengo ya kuliweka nyuma lori lile ili arudi upande aliokuwemo, wa kulia.
Gari la Kaguta lilipofika katikati ya lori, ghafula lori lilianza kusogea upande wao kwa kasi. Kaguta alipiga honi kutahadharisha lakini ilikuwa kazi bure. Lori lilizidi kuja! Upesi Kaguta alipunguza mwendokasi, bahati mbaya ama nzuri akakwangua taa za nyuma za lori za upande wa kushoto.
“We mshenzi wewe! Pita basi mbwa wewe!” Kaguta aliwaka kama moto wa kifuu.
Lori lilizidi kuja upande wao, ila kabla halijakaa vizuri kwenye mstari wa barabara waliopo wakina inspekta, lilikunja kona kali kurudi lilipotokea. Hapo sasa shughuli ikawa kubwa. Wakati kichwa cha lori kikirudi upande wake, mkia wake ulifuata gari la wakina inspekta kwa kasi ukabamiza kwa ubapa … buuh! Gari likapoteza dira, kama tamthilia kwenye runinga, lilipinduka likabiringita mara tatu! Bumbum!…bumbum!..bumbum!
Lori lililofanya tendo likapunguza mwendo na kusimama. Walishuka wanaume watatu waliobebelea bunduki kubwa ‘SMG’ mikononi mwao, wakalifuata gari la wakina inspekta na kuanza kulimiminia risasi za haja.
Tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!
Gari likawa nyambu nyambu kwa matundu, baada tu ya dakika moja likalipuka boooom! Moto mkubwa ukalitekeza ndani ya muda mchache. Wanaume wale baada ya kushuhudia hayo, walipeana tano za kupongezana kisha wakalirejea lori lao. Walipolifikia, mmoja wao alidanda akitaka kufungua mlango. Mara puh! Mlango ulisukumwa kwanguvu na teke kali tokea ndani ukawasomba na kuwaangusha wanaume wawili waliotoka kushambulia. Papo kwa papo, mwanaume mmoja akatoka kwenye lori kwa kasi akiruka kama ngedere akamvamia mwanaume aliyebakia amesimama kwa teke kali la kifuana kwenda naye mpaka chini akampokonya bunduki.
Hamaki, yule mwanaume alikuwa ni Kaguta! Wanaume wale wawili waliodondoshwa na mlangowalijikusanya na kushikilia bunduki wakiwa huko huko chini wakamnyooshea Kaguta. Katika hali ya wepesi, Kaguta alimgeuza mwanaume aliyedondokea naye chini akajiziba naye. Risasi zikamkosa wakati zikimiminika kwa mtu aliyemfanya ngao yake.
Haikuchukua muda sana, risasi zikakata, ni wazi nyingi ziliishia kwenye kulipua gari. Hapo ndio Kaguta kwa nguvu zake zote akamrusha mwanaume aliyemtumia kama ngao ya risasi kwa wenzake. Wenzake wakafanya kosa kwa kumtizama na kufungua mikono yao kumdaka mwenzao aliyerushwa, Kaguta akatumia mwanya huo mujarabu, haraka aliubeba mwili wake na mikono akaruhusu miguu yake iambae na kuwabetua wanaume wale wawili waliokuwa wamempokea mwenzao, kisha akawaweka chini ya ulinzi.
“Tulia hapo hapo. Sogeza hata kope muone!” Kaguta alitoa tisho kwa macho makali mithili ya mbwa mkali aliye mawindoni. Alipiga mluzi, mlango wa lori ukafunguliwa akatoka inspekta.
“Umemaliza?”
“Yap! Kazi ndogo sana hii?”
“Sasa tutatumia gari gani na wameshalipua letu?”
“Tutatumia lori lao. Tutafanyaje sasa?”
Inspekta alisogea vizuri akaanza kuwapekuwa wale wanaume, ambao ni wawili kati yao ndio walikuwa wazima. Mmoja alikuwa kitambo ameshafariki.
“Kwahiyo mlikuwa mnatufatilia, sio?” Aliuliza Kaguta kwa sauti kali.
“Ndio.”
“Hongereni sana. Bahati mbaya hamtokuwa na second chanceningewaelekeza kazi kama zile mnafanyaje.” Kaguta alimwaga maneno.“Ila labda mnaweza pata nafasi nyingine, ya Mungu mengi. Siku nyingine mkiwa mnataka kupindua gari hakikisheni mnaotaka kuwapindua wapo ndani ya gari. Nilikwangua taa za nyuma za gari lenu, ila hamkujali. Giza lililokuwepo lilitufanya sisi kuhamia kwenye trela bila nyie kufahamu. Mkapindua gari na kwenda kuliteketeza bila kuhakikisha tena kama kuna watu, kosa la pili. Kosa la tatu, hamkumuacha mtu kwenye lori. Poleni.” Alihitimisha Kaguta.
****
☆ Steve