Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

SURA YA KWANZA (MSIMU WA 02)

MAUAJI TENA!

Kichwa kimojawapo cha gazeti kilisomeka hivyo. Chini yake kulikuwa na picha tatu ambazo kama hutozitizama vema basi utaishia kusema ni maghofu ya miji ya kale. La hasha! Kumbe ni mabaki ya nyumba ya Mtemvu, ama tumuite marehemu Mtemvu kwa sasa – aliyekuwa afisa polisi kanda maalum Dar es Salaam.

Yeye pamoja na mkewe wote waliaga dunia ndani ya mlipuko mkubwa wa mabomu. Hakuna masalia yoyote ya miili yao

Mtemvu pamoja na mkewe walifariki ndani ya nyumba, pia nyumba yao kuteketea kwasababu ya kukawia kwa zimamoto. Zaidi ya hapo, watuhumiwa wa tukio walikuwa chini ya ulinzi hospitali wakipata matibabu.

Kwa upande wa Miraji hali yake haikuwa tenge kabisa, ni kama vile alikuwa wa kwenda ndani ya muda mchache ujao; risasi ya mgongo iliyotuama kwenye uti wake wa mgongo ilimweka katika hatari ya kupooza mwili. Kichwa kingine cha habari ilikuwa ni juu ya kuachiwa huru kwa bibie Bernadetha Kombo, yeye pamoja na binti yake, Marietta, ambaye alikuwa chini ya uangalizi maalum wa watoto.

Hakukuwa na gazeti, chaneli wala stesheni iliyokwepa habari hizo. Lakini swali kubwa lililotawala ni kwanini Miraji auwa washirika wa karibu wa babaye? Kutafuta majibu ya swali hilo, waandishi wa habari wakawa wanazonga hospitalikwa ajili ya Miraji na nyumbani kwa marehemu mzee Malale wakiwahitaji wahusika wawapatie majibu. Bahati mbaya Mama Miraji, Bernadetha, hakuwa tayari kuongea na waandishi wa habari kuhusu chochote na kwa Miraji bado hakuwa na afya ya kutosha kumfanya afungue kinywa.

Siku moja inspekta Vitalis akiwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa Jombi, alianza kudadisi kutaka kufahamu nini kinachoendelea nyuma ya pazia la mashambulizi. Aliamuru polisi na manesi wampe faragha, wakafanya hivyo na kumpa mwanya wa kuongea. Baada ya kujiridhisha yupo mwenyewe na mhusika wake, alianzisha soga;

“Uliniahidi kuniambia nini kipo nyuma ya yote haya. Sasa waweza kuniambia?” Alisema inspekta Vitalis katika sauti ya kuuliza. Jombi alishusha pumzi ndefu kisha akang’ata lips zake. Alinyanyua mkono wake usio na pingu akajikunia kichwa na kusema;

“Ndio, naweza.” Alijibu na kuongezea. “Mimi ni mtu tu niliyejitolea kumsaidia Miraji kutimiza adhma yake ya kulipiza kisasi, na si zaidi ya hapo hivyo sikuona kama nastahili adhabu ile ya kifo.”
“Kisasi?” Inspekta Vitalis alijita. “Kisasi kwa kina nani na kwanini?”
“Kisasi kwa wale wote ambao walishiriki kumuua baba yake.” Alijibu Jombi.
“Una uhakika kwamba baba yake aliuwawa?”
“Ndio. Miraji aliambiwa kila kitu na mama yake juu ya kifo cha baba yake.”
“Kwamba?”
“Baba yake aliuwawa na washirika wenzake baada ya dili ya magendo waliyoifanya kubumburuka. Hivyo wakamtoa sadaka kuficha identity na reputation zao mbele ya jamii.”
“Miraji alikuambia kuhusu hilo dili?”
“Kidogo. Aliniambia lilikuwa linahusu kusafirisha pembe za tembo kuelekea Italy, Rome. Na watu walioshiriki ni wale wote ambao tumewaua.”
“Una uhakika na unachokiongea?”
“Absolubtely. Nimekuambia kile chote nikijuacho.”

Inspekta alitulia kwanza kwa muda kama mtu anayefikiria jambo. Kisha akaendelea kuuliza;
“Wewe na Miraji mna mahusiano gani?”
“Ni rafiki yangu tokea zamani sana, tangu tupo kindergarten.” Jombi alijibu kwa kujiamini.
“Na kwa sasa wewe unafanya kazi gani?”
“Nafanya biashara tu.”
“Ipi?”
“Ya kuuza nguo. Nina duka langu la nguo maeneo ya Tandika.”
“Na kuhusu silaha na vifaa, mlikuwa mnavitolea wapi?”

Jombi alinyamaza kwa muda kidogo baada ya hilo swali. Ni kama vile alikuwa anafikiria cha kujibu. alimtazama kwa kumkazia macho, akatazama chini.

“Tulikuwa tunanunua.”
“Pesa mlikuwa mnapata wapi?”
“Tulikuwa tunakwapua pesa toka nyumbani kwa wakina Miraji.”
“Yote hiyo ya kununulia vifaa kama vile?”

Baada ya hilo swali, ghafla Jombi alishika kichwa na kulalama kinamuuma. Hakuweza kuongea tena zaidi alikuwa akilalamika na kugugumia kwa maumivu ya kichwa. Inspekta akampa muda wa kupumzika, ila wakati inspekta ananyanyuka apate kwenda, Jombi alijikakamua kuongea akamuomba simu inspekta kwa madai ya kuwasiliana na kuwajuza nduguze, bila hiyana, inspekta akampatia kisha akasonga pembeni. Jombi aliweka namba akapiga. Sauti yake aliishusha ikawa ya kunong’ona.

“Haloo boss…Jombi hapa…ndio, Jombi kijana wako…nipo Regency hospital kwa sasa, ila nipo chini ya ulinzi…naomba uniokoe boss wangu…kazi nimeshamaliza…Miraji bado, ila atakufa muda si mrefu sana hivyo sio wa kumuhofia kabisa…sawa sawa…ni ghorofa namba mbili, wodi ya tatu…sawa boss wangu…”

Alikata simu haraka baada ya kuona inspekta anakuja akiongozana na polisi. Inspekta aliposogea alitwaa simu yake na kuaga akiahidi kurudi baadae. Huku nyuma, Jombi alibakia akitabasamu na uso wake ulionyesha matumaini.

Usiku ulipoingia, macho ya Jombi yalikuwa yakipepesa pepesa huku na kule huku akipumua kwanguvu. Ni kama vile mtu aliyekuwa anategemea kitu muda si mwingi. Kushoto kwake alikuwa ameketi polisi aliyevalia bunduki, kulia kwake kulikuwa na vitanda vingine kadhaa vikiwa vimebebelea wagonjwa, na kitanda cha tatu toka cha kwake alikuwa amelala Miraji akiwa hana fahamu.

…moja…mbili…tatu…nne…tano…

Miraji alikuwa anahesabu kwa kunong’ona huku akipangua vidole vyake. Ilipofika kumi, mwanaume mrefu mweusi aliyekuwa kavalia nguo za daktari aliingia wodini. Macho yake yalitizama huku na kule kama mtu atafutaye ufunguo kwenye mchanga. Pap! Alikutana macho kwa macho na Jombi. Taratibu akaanza kusogea akimfuata Jombi. Tap! Tap! Tap! Viatu vyake viligonga sakafuni. Alipofika aliwasha tabasamu lake akamsalimia polisi kisha akamsalimia na Jombi.

“Unaendeleaje?” Alimtanabahi mgonjwa.
“Naendelea vizuri tu, dokta.”
“Sawa sawa. Sasa…” Dokta alisema kisha akakatisha ghafla na kumtizama polisi.
“Naomba utupishe kidogo, tuna maongezi ya siri na mgonjwa wangu.”

Polisi bila ya kuuliza akasonga nje ya wodi akasubiria mlangoni. Mwanaume yule aliyevalia kama daktari akamuuliza Jombi,

“Umemwambia yeyote kuhusu boss?”
“Hapana. Hakuna anayejua.” Jombi alijibu.

Mwanaume yule aliyevalia koti la daktari, aliingiza mkono wake kwenye mfuko akatoa sindano iliyobebelea kimiminika cha rangi ya njano. Ghafla, akamziba Jombi mdomo na kumshindilia sindano kwenye mguu wa kulia. Jombii alitapatapa kwa muda kidogo tu kisha akalegea kama mtu asiye na nguvu.

Haraka mwanaume yule akatoka wodini isijulikane wapi alielekea. Polisi aliporudi alimkuta Jombi anamimina povu,macho yamepanda juu huku akitikisa miguu kwa mbali kama mtu akataye roho.

Haraka polisi alitoka mbio akarudi na daktari.

***

Muendelezo soma hapa
 
SURA YA PILI
(MSIMU WA PILI)

Asubuhi iliwasili. Pamoja nayo, ilikuja na wingi wa shughuli kama kawaida katika mji wa Dar es Salaam. Magari na watu walikuwa wanapishana, hawa wakienda huku wengine walienda kule ilimradi tu pamekucha kila mtu aenda kutafuta ridhiki.

Baada ya mlango wa nyumba ya mama Miraji kufunguka, alitoka Marietta akiwa kavalia sare za shule na begi lake mgongoni. Hatua tatu tu mbele yake alikutana na inspekta Vitalis Byabata, akamsalimia.

“Mama yupo?”
“Ndio, yupo.” Alijibu Marietta kwa tabasamu pana.
“Haya, masomo mema mama eeh.”
“Ahsante.” AlisemaMarietta kisha akaendelea na safari yake. Inspekta alimtizama mpaka anaishia. Alitikisa kichwa chake na kutabasamu kama mtu akumbukaye jambo la kufurahisha. Akageuza na kuufuata mlango. Ngo! Ngo! Ngo!
“Hodiii!”
“Karibu!” Sauti iliitikia kwa ndani. Baada tu ya muda mchache, mama Miraji akawa tayari ameshafungua mlango.
“Karibu.”
“Ahsante. Naitwa inspekta Vitalis Byabata.” Inspekta alisema huku akionyeshea kitambulisho.
“Wewe ni mke wa marehemu Malale?”
“Ndio.”
“Nashukuru. Mimi ni supervisor wa kesi ya mwanao pamoja na mshirika wake. Naweza nikaingia ndani?”

Kabla ya kusema jambo, mama Miraji alimtizama inspekta na uso uliojikunja na macho ya mkazo.

“Karibu.”
Inspekta akaingia ndani na kuketi kwenye kiti.
“Nikusaidieje?”
“Nimekuja hapa kupata baadhi ya taarifa toka kwako…”
“Taarifa gani?”
“Kumhusu mwanao na kumhusu mumeo kidogo.”
“Unataka kujua nini? Si mumemkamata? Mnataka nini kingine, roho yangu?”
“Calm down, mama. Sipo hapa kwa ajili ya kugombana. Nina dhumuni la kuwasaidia.”
“Kutusaidia? Kamsaidie kwanza mwanangu uliyemlaza kitandani. Kawasaidia hao wezi na wauwaji unaowalinda, sio mimi!”
“Calm down, mama. Naomba utulize moyo wako. Naomba ushirikiano nipate kujua nini kinacoendelea.”
“Sitaki kuongea chochote. Naomba uende!” Mama Miraji alifoka huku akinyooshea kidole mlangoni. Haikujalisha inspekta aliongeaje, mama Miraji hakubadilisha msimamo wake. Alimtaka inspekta atoke nyumbani kwake. Inspekta hakuwa budi, aliaga na kuondoka zake.

Akiwa anatembea kuelekea barabarani, simu yake iliita akapokea akapewa taarifa juu ya kile kilichotukia hospitali usiku wa kuamkia siku hiyo.Upesi alidandia daladala akaelekea hospitalini. Alimkuta Jombi akiwa hana nguvu, mdomo wake umepauka, macho yake yakiwa mekundu mno na ngozi yake ikiwa imesinyaa. Maelezo ya daktari yakasema ameingiziwa sumu kali mno, kama wasingeliwahi kumuhudumia asingelikuwapo hai. Mtuhumiwa wa tendo hakujulikana. Kilichopatikana ni maelezo tu kuwa alivalia nguo za kitabibu.

Inspekta akapata maswali juu ya hilo jambo. Nani anataka kumuua Jombi, na kwanini? Alitamani kumuuliza Jombi lakini haikuwezekana, hali yake bado haikuruhusu. Ila tokea siku hiyo aliamua kuwalinda Miraji na Jombi yeye mwenyewe, hivyo akamtaka polisi apumzike kwa hilo.

Baada ya siku mbili kupita. Alikuja mwanamke mmoja mnene aliyevalia dera jekundu na njano. Alibebelea sahani, hotpot kubwa na chupa ya chai. Alijitambulisha anaitwa Miriam, ndugu yake Jombi, amekuja kumhudumia ndugu yake. Kabla ya kuruhusiwa kwenda ndani ya wodi, inspekta alimtaka afungue hotpot na aonje chakula alichokileta. Bila kusita, Miriam alionja chakula kumhakikishia inspekta kwamba kipo sawa. Kama hiyo haitoshi, inspekta alimsindikiza Miriam mpaka alipo Jombi ambaye walimkuta bado akiwa vilevile kama jana yake.

Japokuwa Miriam alimsalimia, Jombi hakusema kitu. Macho yake yalikuwa yamefumba, mdomo wake ukiwa wazi kama lango la mlanguzi. Hakuonyesha dalili yoyote ya kusikia aambiwacho. Miriam alimpa pole kisha akaanza kulia. Inspekta alimtaka anyamaze, naye akafanya hivyo. Alinyanyuka akaenendea hotpot alilokuja nalo akaanza kupakua. Ila kisiri na kwa utaratibu, aliupeleka mkono wake chini ya hotpot akaanza kufungua kitako. Wakati huo inspekta alikuwa ameketi juu ya kitanda na Jombi. Ghafla, Miriam aligeuka akiwa na kisu kidogo mkononi, alinyanyua mkono akitaka kumkita Jombi kifuani, haraka inspekta akauwahi mkono ule na kumtandika teke kali Miriam lililomrushia mbali.

Ajabu, mwanamke alisimama haraka. Alikunjia dera lake kiunoni akabakia na tight nyeusi. Akatoa mtandio wake shingoni na kuuhamishia mkononi. Upesi akarukia dirishani akipasua vioo, akiwa hewani alirushia mtandio wake dirishani ukanasa, akatua chini taratibu na kupotea eneo lile.

Inspekta akabaki na maswali. Nini wanamtafutia Jombi hivi? Alijiuliza asipate kabisa majibu. Baadae giza lilipoingia, alipokea ujumbe kwenye simu yake.

“Wakati unalinda mjinga wako, ulisahau familia yako. Sasa utamuacha mjinga wako kutafuta familia yako.”

Mdomo wa inspekta ukaachama.

“Oh my God!”

Haraka alitafuta namba ya mkewe kwenye simu akapiga. Simu iliita bila kupokelewa. Mwishowe inspekta alichoka akaamua aitupie simu mfukoni. Kwa dakika kama moja insekta akawa kama mtu aliyewehuka asijue cha kufanya. Alienda mbele na kurudi nyuma. Alitoka nje ya wodi kisha akarudi ndani. Alitoka akarudi tena, macho yakiwa yamemtoka kama tufe.

“Mungu wangu…what should I do now?” Alijisemesha mwenyewe. Ndani ya muda kidogo tena, alikurupuka na kutoa simu yake mfukoni. Alipiga simu polisi akawataka waje kuwalinda watuhumiwa yeye kapata dharura isiyokwepeka. Baada ya dakika tu chache, polisi walifika inspekta akang’oa nanga. Alikodisha pikipiki toka nje ya hospitali ikamuwahisha kwa kasi nyumbani kwake. Alipofika, kabla ya kuingia ndani, alianza kuita.

“Mama Joons!...Mama Jooons!...Jooons!”

Hakukuwa na majibu. Si mama wala mtoto aliyeitikia wito. Inspekta alifu gua mlango akaanza kupekua kila eneo la nyumba. Alipomaliza ndani alihamia nje ya nyumba lakini hakumuona mtu yeyote. Wakati anafanya hayo, macho yalianza kuwa mekundu kama mtu mwenye malengo ya kudondosha chozi.

“Mama Joons!...Mama Joons!”

Aliita kwa sauti hafifu isiyotosha hata kumshtua kuku anayedoea mchele. Baada ya kuzunguka bila ya mafanikio, aliamua kukaa chini akashika tama. Mara simu yake ikaita. Alishtuka akaitizama, ilikuwa ni namba ya mkewe. Haraka alipokea akaiweka sikioni.

“Haloo mama Jons!” Inspekta aliwahi kuongea. Hamaki sauti ya kiume ndiyo ikasikika sikioni kwake.
“Wewe nani? Mke wangu yupo wapi? Mtoto wangu yupo wapi?” Inspekta alifululiza maswali.
“Mke wako na mtoto wako tunao. Kama unataka kuwapata, tukabidhi mtu wetu haraka iwezekanavyo la sivyo utakosa familia yako muda si mrefu ujao.” Sauti toka simuni ilitishia.
“Mpo wapi sasa? Nitawaleteaje mtu wenu na sijui mlipo?”
“Ukiwa na mtu wetu tutaarifu, tutakwambia tulipo tukutane utupe mtu wetu tukupe wako. Na kaa ukijua hatuna muda wa kupoteza. Keshokutwa tunamuhitaji mtu wetu, la sivyo mtoto au mke wako atatangulia kuzimu.”
“Sasa jamani si mnajua siwezi tu kumtoa mtu ambaye yupo chini ya ulinzi kwa haraka hivyo?”
“Hilo ni juu yako, utachagua mwenyewe. Mtuhumiwa wako au familia yako. Na nikukumbushe tu, mwisho keshokutwa.” Simu ikakata.

Mithili ya kifaranga aliyemwagiwa maji, inspekta alinywea. Kama kuna muda tokea aanze kazi aliwahi kuwa katika njia panda, huu ndio ulikuwa wenyewe. Uso wake ulionyesha utupu. Macho yake yalichora simanzi na uso wake ulitambulisha ukosefu wa amani ndani ya nafsi.

Alinyanyuka akatembea kuelekea chumbani. Akiwa na viatu na nguoze, alijirushia kitandani akatizama dari kama mtu anayepanga mchoro. Alijigeuza kila upande wa kitanda. Alijigaragaza huku na kule, mwishowe usingizi ulimkwapua toka kwenye fahamu zake.

***
 
Steve usitufanyie hivi shusha mbili za mwisho
 
***SURA YA TATU***

(Msimu wa Pili)






Asubuhi ya mapema, muda ukiwa unaruhusu kwa wageni kutembelea wagonjwa, mama Miraji alikuwa tayari amekaa kandokando ya mwanaye asiye na ufahamu. Polisi pia alikuwa nao kwa kando zaidi. Macho ya mama Miraji yalikuwa mapole yakimtizama kinda lake. Mkono wake wa kuume alikuwa kauweka kichwani mwa mwanaye, kiganja chake alikuwa anakipeleka mbele na nyuma kama mfugaji ampetiye mbwa wake.




“Mwanangu, mama yako nipo hapa. Fungua basi macho baba upate kuniona.” Mama alinong’ona. Hakuweza kuvumilia, machozi yalianza kumchuruza. Alinyanyua khanga yake akajifuta. Lakini zaidi machozi yaliendelea kumtiririka na kumtiririka. Alishindwa kuyazuia. Alinyanyuka akashika korido akielekea nje ya wodi, mlangoni akapishana na inspekta akiingia ndani, ingawa inspekta alimsalimia, hakuitika.



Alielekea zake njeakaketi pembezoni mwa kuta ya sakafu akawa anatizama chini magari na watu wakiingia hospitalini. Aliacha macho yake mekundu yaangaze angaze huku na kule kutizama majengo. Angalau hapo macho yake yakakata machozi. Ingawa alikuwa anatembeza macho yake sehemu mbalimbali lakini hakuonekana kama mtu anayejali kile anachokitizama. Eidha mawazo yake hayakuwa pale ama hakuwa na muda wa kujadili kile anachokitazama. Akiwa hapo, inspekta aliungana naye akasimama pembeni yake wote wakawa wanatizama majengo na watu bila ya kusemeshana. Baada ya muda, inspekta alivunja ukimya akaongea kwa sauti ya chini.



“Wameteka familia yangu; mke na mtoto wangu. Wanataka niwakabidhi Jombi kwao ili waachie familia yangu huru. Wamenipa leo tu, kesho mwisho, bila ya hivyo watamuua mwanangu ama mke wangu.”
Mama Miraji taratibu aligeuza uso wake akamtazama inspekta.
“Wakina nani?” Aliuliza mama.
“Sijajua wakina nani.” Inspekta alijibu na kuongezea,“na sijui kwanini wanamtaka Jombi kwanguvu hivyo. Walijaribu kumuua mara mbili bila ya mafanikio, sasa wameona kuteka familia yangu ndio njia ya kutimiza malengo yao.”




Baada ya huo usemi, ukimya ulipuliza kati yao kwa muda kidogo wakaacha macho yao yaendelee kuzurura maeneo kadha wa kadha. Ukimya ulipovunjwa, alikuwa ni inspekta ndiye aliyekuwa na nyundo.




“Samahani sana, ndugu yangu. Najua mimi ndiye ninayehusika na kumlaza mwanao juu ya kitanda, ila tambua sikuwa na budi, nilikuwako kazini. Lakini kwa sasa nahisi kuna mambo mengi yaliyo nyuma ya pazia, na mengine nilikuwa nafichwa na mkuu wangu. Nimejaribu kupeleleza lakini sijafinikiwa, mtu pekee aliyetoa ushirikiano kwangu ni Jombi. Naye pia kuna ambayo amenificha. Kwa sasa yupo kitandani hajielewi, sina wa kumuuliza. Naomba unifungue macho, mama. Nataka kujua pumba kwenye mchele. Naomba unisaidie.” Inspekta aliongea kwa utaratibu huku akimtizama mama Miraji usoni kisha kimya kikatawala tena. Mama Miraji alisafisha koo lake kwanza akaongea,




“Mume wangu aliuwawa na wenzake kwa ajili ya kuficha siri. Miezi kadhaa iliyopita, walishiriki kufanya dili ya magendo. Japokuwa hakuwa na lengo, na mimi nilisimama kidete kupinga, umasikini na ufukara wetu ulimzidi nguvu. Nakumbuka aliniambia ‘mke wangu, nimefanya kazi kwa miaka yote hiyo lakini hali yetu haijabadilisha sare. Naomba nijaribu upande wa pili wa shilingi. Mara moja tu’. Masikini hakujua kama huo ndio utakuwa mwisho wake. Tokea apotee ulimwenguni, si rafiki yake wala nani niliyemuona tena. Maisha yamekuwa magumu zaidi.”




Mama Miraji alianza kumimina machozi upya. Inspekta alimtizama akatikisa kichwa kwa huzuni.




“Pole sana, mama. Hao washirika wake walikuwa ni wakina nani? Na je unaweza ukanambia walimuuaje mumeo?”




Mama Miraji alivuta kwanza vimakamasi vya kilio, akanena;




“Nakumbuka siku moja tukiwa nyumbani majambazi walituvamia wakiwa na bunduki. Hawakuchukua kitu hata kimoja. Walimpulizia mume wangu dawa kisha wakatokomea. Baada ya hapo tu mume wangu akaumwa hoi mno nusura kufa. Hata pale tulipompeleka hospitali, walimfuata tu na huko. Wakamuwekea sumu kwenye dripu yake na huo ndio ukawa mwisho wake.”



Inspekta alishusha pumzi ndefu akaguna.




“Vipi uliwahi sema hiki kitu popote pale labda?” Aliuliza.
“Hapana.” Mama Miraji alijibu. “Nilipanga kufanya hivyo lakini nguvu zilinisha pale dokta alipoamua kukengeuka na kusema uongo mbele ya wandishi wa habari. Alikana yale yote aliyoyasema akiwa na mimi. Badala yake alisema mume wangu kafa na ugonjwa tu, hakuna kiashiria chochote cha sumu ndani ya mwili wake, nani angeniamini mimi?”
“Pole sana mama. Huyo daktari anaitwa nani na anafanya kazi wapi?”
“Ni daktari fulani hivi mhindi, anaitwa Rajesh Deepti. Anafanya kazi Royal Hospital.”
“Sawa. Na vipi kuhusu Jombi, unamuelewaje wewe? Una kipi cha kumzungumzia?”
“Jombi ni rafiki wa mwanangu. Walianza urafiki kitambo lakini baadaye baba yake Miraji alikuja kugundua Jombi hakuwa mtu sahihi na mzuri. Aliwahi kushikiliwa na kesi ya madawa ya kulevya lakini baadae alikuja kutolewa, hatukujua kivipi. Basi kwakuwa urafiki wa Miraji na Jombi ulikuwa mgumu kukatika, baba yake Miraji aliamua kumsafirisha Miraji akasomee India. Bahati mbaya mume wangu alipofariki, ilibidi mtoto arudi nyumbani na hata shule hakuendelea tena na ndio hapo akakutana tena na Jombi.”
“Sawa sawa. Kwahiyo Jombi alikuwa anamsaidia rafikiye kulipiza kisasi? Sio?”
“Sijajua kwa kweli. Ila ndivyo inavyoonekana.”
“Na Jombi alinambia kwamba, pesa za vifaa na silaha walikuwa wanazikwapua toka nyumbani kwako, ni kweli?”
“Pesa za silaha?”
“Ndio. Kwa mujibu wa maelezo yake.”
“Hapana kwa kweli. Ndio pesa zilikuwa zinaibiwa lakini si za kutosha kununulia silaha. Kwa hilo si kweli.”
“Sawa, mama. Hapa kuna jambo linatia shaka. Kuna kundi au mtu yupo nyuma ya Jombi. Na ndiye atakuwa anahusika au wanahusika na kumpa silaha. Swali la kujiuliza ni kwamba, je watakuwa wanafaidika nini na mauaji hayo yaliyofanyika? Na je wanahusikaje na kutaka kumuua Jombi?”




Maswali hayo yaliwafanya inspekta na mama Miraji watulie kwa muda wakionyesha nyuso za mawazo. Hakuna yeyote aliyeonekana anaweza yajibu. Baada ya muda mchache, daktari alikuja.Inspekta na mama Miraji waliongozana naye kuwafuata wagonjwa wao. Daktari alianza na kitanda cha Jombi, mama Miraji na inspekta wakawa wapo pembeni kusikiliza. Baada ya daktari kumtizama na kumkagua Jombi kwa macho na kuperuzi taarifa zake alizokuja nazo alifungua mdomo kutema maneno;





“Mgonjwa anaendelea vizuri tu. Fahamu zake zitarejea taratibu taratibu natumai siku si nyingi atakuwa katika hali yake ya kawaida. Tuvute tu subira.” Daktari alitia nasibu, lakini pia hakusita kuongezea,
“Sumu aliyotiwa mwilini ni hatari mno. Imeathiri kwa kiasi kikubwa maini yake kwa kuayaunguza na figo yake pia ipo katika mushkeli, haifanyi kazi ipasavyo. Tumeona kuna uhitaji mkubwa wa kufanyiwa upasuaji hapo kesho.”
“Haina shida dokta.” Inspekta alimtoa daktari hofu. “Afanyiwe tu alimradi arudi katika hali yake ya kawaida.”
“Sawa.” Daktari aliitikia kisha akasonga kufuata kitanda alicholazwa Miraji, nyuma yake akifuatiwa na inspekta pamoja na mama mtoto. Daktari alifungua kadi yake akaitizama kwanza kisha akamtizama mgonjwa na kutikisa kichwa.
“Recovery yake ni ya taratibu mno. Kuna some nerves zimekuwa damaged na jeraha la risasi. Ingawa atapona, kuna hatari kubwa ya kupooza. Pia consciousness yake iko damaged, itahitaji muda pia kurecover. Kwa muda huu wote atakuwa anahitaji kula kwa mipira.”




Daktari alipomaliza tu kusema hayo maneno, machozi yalikuwa tayari yameshateremka kwenye uso wa mama Miraji. Kwikwi za hapa na pale nazo zilizuka zikiambatana na mafua.




“Pole sana, mama. Yatakwisha.” Daktari alihitimisha kisha akaondoka zake. Mama Miraji naye hakukaa sana, alimuaga inspekta anarudi nyumbani kumuandalia mwanaye, Marietta, chakula, atakuja baadae. Ila kabla ya kuondoka inspekta alimuomba namba ya simu, akampatia. Alipoondoka, Inspekta akabaki na polisi mwenzake sambamba na wagonjwa. Ingawa alikuwa na hiyo kampani, inspekta hakufungua tena mdomo wake kunena lolote. Alikuwa ameshika tama, uso wake ukitambuza fikira zinazomtambaa akilini.





Baada ya dakika kadhaa zisizopungua dakika thelathini wala kuzidi arobaini na tano, inspekta alikuwa tayari ametoka wodini. Alikuwa ameketi mgahawani akipata chakula cha mchana. Kwa taratibu mno, alikuwa anakula. Kijiko kilikuwa kinaenda mdomoni kila baada ya muda mrefu kidogo, na hata kutafuna kwake kulikuwa kumepooza. Alitoa simu yake mfukoni akawa anaitizama majina. Alipofika kwenye jina la mkewe, alijaribu kupiga lakini simu haikupatikana. Akaachana nayo na kuendelea kutazama majina mengine, alipofika kwenye namba aliyosevu ‘Mama Miraji’, alitulia akaitizama namba hiyo, kisha akapiga.





“Haloo…vipi umefika salama?...vipi nyumbani?...okay, samahani, naomba nikuulize kitu…unafahamu eneo alilokuwa anaishi Jombi?...enhe pembeni ya barabara…nyumba ya tatu…aaah sawa sawa nyumba nyeupe…kwa nje kuna uzio?...mweupe nao…sawa nimekuelewa…nashukuru sana, baadae!”





Alipomaliza kuongea na simu, aliongeza kasi ya kula akamaliza chakula na kupotea eneo lile. Moja kwa moja alielekea nyumbani kwa Jombi, alifungua mlango kwa waya maalum wa silva baada ya kudumbukiza kwenye kitundu kidogo kilichokuwepo kwenye kitasa. Aliingia na kutembea kwa tahadhari, mkono wake wa kuume haukuwa mbali na mfuko wa bunduki.





Alikagua sebule lakini hakuona kitu. Aligeuka kutaka kuelekea chumbani, hapo akatandikwa teke la nguvu mgongoni likitokea nyuma Kiiihh! Akarushiwa ukutani mithili ya karatasi puh! Alipogeuza shingo alikutana uso kwa uso na pande la mtu, mnene, mrefu akiwa kajazia misuli ya kutosha.





Inspekta alijaribu kuupeleka mkonowe kiunoni atekebunduki yake lakini upesi pande la mtu lilivuta stuli na mguu wake akamrushia inspekta. Kabla inspekta hajajipanga, jitu tayari lilikuwa lishamfikia likamkwida na kumnyanyua juu juu.




“Wewe nani?” Jitu liliuliza na sauti yake nzito ya kukwaruza. Inspekta hakujibu, badala yake alinyanyua mguu wake wa kulia kwanguvu akamtandika teke kali adui wake sehemu za siri. Jitu likapiga kelele kali za maumivu. Lilimwachia inspekta alafu likapiga magoti kusikilizia maumivu. Hapo inspekta akapata upenyo, alimtandika jitu teke kali kichwani, jitu likaangukia chini puh! Kama kiroba cha mchanga. Inspekta akatengenezea koti lake mwilini na kuelekea kwenye chumba cha kwanza, sasa mkononi akiwa kashikilia bunduki.





Alipiga teke mlango akaingia ndani. Alikuta silaha na vifaa kadhaa; kamba, mabomu, nguo, viatu, stendi za bunduki na bunduki zenyewe. Alipekuwa pekuwa kama kuna mtu anakitafuta, alipomaliza alienda chumba kingine mwendo ukawa ule ule wa kutafuta. Kwenye chumba cha mwisho, akaonekana kupata alichokuwa anataka. Alikuta karatasi kubwa ya nailoni imefunika kifaa kikubwa. Alipoivutia kando nailoni hiyo, alitabasamu na macho yake yakasema furaha.




“It is the time now bitches!”




Alisema inspekta huku akipiga ngumi hewani.




****


☆Steve
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom