***SURA YA KUMI NA MBILI***
(MSIMU WA 02)
****
Pipiiii!
Kaguta alipiga honi nje ya nyumba ya inspekta. Alishuka akiwa na furaha mkononi kabebelea flash yake. Huku akipiga mluzi alitembea kwa kudunda mpaka mlangoni. alifungua mlango akamkuta inspekta pamoja na mama Miraji. Tabasamu la uongo likajaa usoni mwake.
“Habari zenu jamani?”
“Njema tu. Karibu.” Mama Miraji alisema kwa tabasamu wakati inspekta akiwa kimya anamtizama tu Kaguta.
“Ahsante … Ahsante sana, mama.” Alisema Kaguta bila hata ya kuingia ndani. Alimrushia inspekta flash kisha akamkonyeza.
“Mie wala siingii. Nilikuja tu kuleta mzigo huo, baadae!” Alisema Kaguta, kabla hata hajajibiwa alishafunga mlango na kushika njia.
“Mbona hujamkaribisha mwenzio?” Mama Miraji alimuuliza inspekta. Inspekta alitikisa kichwa akaguna.
“Ana yake huyo. Si mgeni wa kukaribishwa.”
Mama Miraji alitabasamu na kucheka kidogo; “Haya bana, waarabu wa pemba mwajuana kwa viremba.”
Walicheka kwa pamoja kisha wakatizamana kama watu wasio na maneno mapya ya kuongea.
“Sasa … acha basi nikuandalie chakula mgeni wangu upate kula.” Inspekta alinyanyuka.
“Hapana bana. Usijichoshe bure.”
“Bure? … si bure kukupikia. Nisingependa mgeni utoke hapa bila ya kutia chochote mdomoni maana hata kinywaji umekataa.”
“Hamna shida bwana, inspekta. Mie nipo sawa tu.”
“Tia hata sunna basi.”
“Mila zetu haziruhusu mwanamke kukaa alafu mwanaume aingie jikoni. Naomba basi nikusaidie kupika.”
“Jamani, mgeni tena?”
“Kwani kuna shida?”
“Hapana. Haya twende nikuelekeze. “
Mama Miraji alisimama na kuongozana na inspekta mpaka jikoni. Wakati akiwa anapika, inspekta alileta tanakilishi mpakato yake sebuleni akachomeka flash na kuanza kuperuzi kilichowekwa humo na Kaguta.
Baada ya muda si mrefu, chakula kilikuwa tayari juu ya meza.
Inspekta akishirikiana na mama Miraji waliweka sahani mezani, maji ya kunywa na kunawa pamoja na matunda kadhaa. Chakula kilikuwa wali njegere ukiwa na nyama ndani yake.
Inspekta alimnawisha mikono mama Miraji, mama Miraji naye akafanya vivo hivyo. Wakaanza kula.
“Kwahiyo kwa sasa unajishughulisha nini, mama?”
“Nabangaiza na vibiashara vyangu. Nauza vitenge na madela kwa kupitisha pitisha majumbani.”
“Hongera sana.”
“Kwa lipi?”
“Kutafuta pesa. Familia inakula hapo.”
“Nashukuru Mungu, anajaalia.”
“Mtoto wako anaendeleaje?”
“Marietta anaendelea vizuri. Muda si mrefu sana atarudi toka shule. Alafu nimekumbuka, nimepitia hospitali wakati nakuja huku. Jombi ameanza kuongea japokuwa kwa shida.”
“Kweli?”
“Ndio. Daktari amesema muda si mrefu atarudi katika hali yake ya kawaida. Ila kuna kitu nimegundua, hii hospitali waliyopo sasa wanahudumiwa vizuri kuliko kule.”
“Yap. Ile hospitali ni ghali kuliko ile ya mwanzo.”
Walimaliza kula wakakaa kwa muda kidogo Mama Miraji akaaga anaenda nyumbani kumuwahi mwana. Inspekta alimsindikiza mpaka barabarani akamkodishia mwanamama pikipiki. Walihaidiana kuonana tena kesho hospitalini.
Baada ya masaa kadhaa jua likiwa tayari limeshazama, Kaguta alirudi nyumbani kwa inspekta. Akiwa na tabasamu pana, alimkumbatia mwenzake kwanguvu;
“We jembe! … Jembe haswaa? … Vipi anasemaje?”
“Nani?”
“Aaah … Hujui namuongelea nani banaa? … Si mama Miraji!”
“Tumepiga naye tu story, ameshaondoka. Picha ya mke wangu bado imeng’ang’ania ubongo wangu, Kila nikikaa na mama Miraji namkumbuka mke wangu.” Inspekta alisema kwa sauti ya upole. Kaguta akamshika bega.
“Najua jinsi unavyojisikia. Lakini huwezi ukaishi hivi milele, Vitalis? Inabidi ufungue moyo wako upate angalau faraja.”
“Sijui. Labda huko mbele. Embu kaa kwanza tufanye kazi kuna vtu nimeviona kwenye ile flash.”
“Wee nani akae sasa hivi? … Tutafanya baadae bwana saa hizi nina miadi na mtoto mzuri tunaenda kupata dinner.”
“Duh! … nani tena?”
“Sandra. Anafanya kazi kule Rosemath stationary.”
“Haya dinner njema.”
“Baade kaka.”
“Poa, take care.”
Kaguta alitoka nje akakwea garini na kupotea eneo lile. Ni baada ya dakika kama thelathini tu alikuwa tayari ameshafika eneo la miadi. Haikuchukua muda, mrembo Sandra naye akatokea.
Alikuwa amenoga mno kwa gauni lake refu jeusi la kumeta-meta. Gauni lilimbana vizuri na kumchora umbo lake kuntu namba nane. Lips zake zilitiwa nakshi ya lipstick kwa mbali na sura yenye make-up kwa wastani.
Kaguta alinyanyuka akampa mwanamke kumbato. Alisogeza kiti akamkaribisha malkia. Mhudumu alisogea na menyu, wahusika wakaagiza chakula na vinywaji wavitakavyo.
Wakiwa wanapata chakula, kwa nje ya hoteli. Pikipiki ilijisogeza eneo la kupaki ikiwa na mtu mmoja tu aliyevua kofia yake ngumu nyeusi akaiweka juu ya usukani. Loh! Alikuwa ni Robson. Alinyofoa ufunguo wa pikipiki na kuingia ndani ya hoteli. Moja kwa moja alienda kukaa sehemu aliyokuwa anawachora Kaguta na Sandra kwa mbali.
“You really look very beautiful. Sitosheki kukutazama.” Kaguta alinong’oneza huku akitizama macho ya Sandra.
“Ahsante. Usin’sifie sana n’tashindwa kula mwenzio.” Sandra alisema kwa tabasamu jembamba macho yakielekea chini.
“Kizuri kipe sifa yake, mama. Mimi si wale wasemayo ya moyoni mtu angali maiti.”
“Nashukuru, Al Kareem. Kama jina lako lilivyo, wewe ni mkarimu sana.”
“Kweli?”
“Haswaa!”
“Nafurahi kusikia hayo toka katika kinywa chako kitamu. Natumai yametoka katika moyo wako uliolemewa na upendo.”
Sandra alitabasamu akachoma kipande cha chips na uma akapeleka mdomoni.
“Una maneno wewe, Kareem. Kama vile unanishushia mashairi.”
“Hamna bana, mie na ughani wa mashairi wapi na wapi. Sema tu nasema kile kilichopo moyoni. Heri kufa macho, Sandra, kuliko moyo.”
“Ni kweli.”
Kaguta alikunya fundo moja la mvinyo, akakata kipande cha kuku na kukiweka mdomoni. Alipotafuna na kukimeza, alilonga;
“Una muda gani pale kazini kwako?”
“Miaka miwili na nusu sasa.” Sandra alijibu.
“Upo tayari kuacha kazi yako?”
“Mmmh … Hapana. Hata kama nitakuwa tayari sitaweza.”
“Kwanini? … Wanakulazimisha?”
“Hapana. Ni mkataba wangu tu ndivyo usemavyo.”
“Kwamba hakuna kuacha kazi?”
Sandra alipeleka kwanza glasi yake ya mvinyo mdomoni akanywa mafundo mawili;
“Huwezi kuelewa, Kareem. Tuachane tu na hayo maongezi.”
Kaguta hakuongeza tena neno. Alimaliza mvivyo wake kwenye glasi akawa anamtazama tu Sandra.
“Umekasirika?”
“Hapana. Sidhani kama naweza kupata sababu ya kumkasirikia mrembo kama wewe.” Alisema Kaguta huku akilazimisha tabasamu. Sandra alitabasamu na kutikisa kichwa bila kusema kitu, aliacha mikono na mdomo wake vifanye kazi ya kujaza tumbo kwa chakula na kinywaji. Alipomaliza, alijifuta mdomo wake na tishu akamtazama Kaguta na jicho lililosikia mvinyo.
“Ahsante sana. Umefanya siku yangu ya leo iwe very special.”
“Usihofu, malkia. Wastahili haya.” Alisema Kaguta kwa pambe. Alinyanyua tishu yake akaondoa kajipande ka chakula kalichobakia shavuni mwa Sandra.
“Ahsante.”
“Karibu sana.”
Kaguta alimuita muhudumu akalipia chakula kisha wakanyanyuka yeye na Sandra wakiwa wameshikana mikono wakalifuata gari. Kaguta alimfungulia mwanamke mlango, ndipo na yeye akaingia na kuwasha chombo.
Tofauti kabisa na siku zingine, Kaguta aliendesha kwa mwendo wa kawaida usio na papara. Aliwasha radio yake ya gari na kuchomeka flash iliyokuwa imeketi juu ya dashboard, muziki ukaanza kufanya kazi yake ya kuwakonga nyoyo huku wakipashana habari za hapa na pale. Ni baada ya muda kidogo, Kaguta aligundua kuna pikipiki inawafuatilia nyuma. Aliongeza kidogo mwendokasi akamwambia Sandra;
“Itabidi ukalale kwangu leo.”
“Kwanini?”
“Kwa usalama wako.”
“Usalama wangu? … Kivipi?”
“Tizama hapo kwenye kioo.” Kaguta alionyeshea kioo cha gari kilichojishikiza darini. “Umeona hiyo pikipiki, inatufuatilia.”
Sandra alitzama kwa umakini kiooni. Uso wake ulianza kujenga hofu akawa anatizama tizama nyuma kila muda.
“Usihofu, funga mkanda.”
Upesi, Sandra alifunga mkanda akamtizama Kaguta; “Tayari!”
“Mbona una woga hivyo, unamjua huyo anayetufuata?”
“Ndio. Ni Roby … Robinson!”
“Unamuogopa enh?”
“Si mtu mzuri, Kareem. Kaa naye mbali sana.”
“Kwanini?”
“Huwa hajiulizi mara mbili kumuua mtu. Ni muuaji!”
“Kwanini atufuatilie? … Anataka nini kwetu?”
“Sijui!”
“Hapana, Sandra. Kuna kitu unanificha. Hawezi akatufuatilia hivi hivi. Au unataka kuniua, Sandra?”
“Hapana!”
“Bali?”
“Kusema ukweli nilikuongopea. Mimi na Robinson tuna mahusiano, ni mchumba wangu. Atakuwa amenifuatilia toka nyumbani. Ni mtu mwenye wivu sana, mkali na asiyeelewa.”
“Unakaa naye?”
“Hapana. Ila huwa anakuja kunitembelea mara kwa mara. Si mtu wa kukaa sana, huwa anabanwa sana na kazi.”
“Ulinambia ni mfanyakazi mwenzako, uongo kweli?”
“Kweli. Ni mfanyakazi mwenzangu.”
“Anafanya kazi wapi? … Stationary?”
“Hapana. Tuko kampuni moja tu, ila vitengo tofauti. Yeye husimamia usalama pamoja na usiri wa kampuni.”
“Kampuni yenu inaitwaje?”
“Mikmath Company Limited.”
“Makao yake makuu yapo wapi?”
“Barmuda. Ila kwa hapa Tanzania yapo Posta mpya.”
Kaguta hakuuliza tena swali jingine. Aliacha barabara kuu ya lami akashika ya vumbi.
“Acha nikuonyesha shoo.” Kaguta alimwambia Sandra kwa sura ya tabasamu. Alizima taa za gari na kuburuta matairi kwenye vumbi kwanguvu huku gari likiwa haendi popote. Vumbi lilitapakaa kama wingu kisionekane cha mbele. Robinson alipunguza mwendo akapita kwa uangalifu ndani ya vumbi lile nene.
Alipochomoza upande wa pili, hakuona kitu. Hakukuwa na ishara yoyote ya gari mbele yake wala mbali yake. Alisimama kwa muda kutazama apate jua cha kufanya. Ghafla … Taa za gari zilimmulika usoni! Gari lilichomoza toka kwenye eneo lenye mifungamano ya miti na kuifuata pikipiki kwa haraka na kuigonga tairi la mbele kabla Robinson hajachukua hatua yoyote.
Pikipiki ilirukia kando ya barabara dereva wake akirushwa mbali. Tairi lake la mbele lilipinda na kutengeneza umbo la zigzag. Kaguta alirudisha gari lake nyuma na kuliondoa kwa kasi kufuata barabara ya lami. Ndani ya muda mfupi akawa tayari ameshafika nyumbani kwake. Alishuka akamfungulia Sandra mlango na kuingia ndani.
“Umeinjoy show yangu?” Kaguta alimuuliza Sandra kwa sauti ya kebehi. Sandra alifungua mikono yake akamkumbatia Kaguta na kumbusu.
“Leo umekuwa shujaa wangu.”
Kaguta alipeleka mdomo wake kwenye mdomo wa Sandra wakaanza kunyonyana ndimi. Hawakukomea hapo, mikono yao ilifanya kazi ya kupapasana huku na kule kwa papara. Ni Sandra ndiye aliyekatisha hilo zoezi kwa kusema;
“Twende tukaoge kwanza.”
Hao walielekea chumbani. Kaguta alivua nguo zake kisha akahamia kwa mwanadada, Sandra. Kwa taratibu na kwa madaha, Kaguta alifungua zipu ya gauni la Sandra na kuishusha chini, Sandra akabakia na sidiria na tight nyeupe.
Kaguta aliondoa sidiria akahamia kwenye tight nayo akaishusha chini. Mwanamke akabakia na bikini nyeupe, sasa hapo Kaguta akapata kuona tattoo kubwa pajani mwa Sandra. Tattoo ya mtu kivuli. Tattoo ya mtu mteketezaji. Kaguta alipigwa na butwaa kutazama mchoro huo. Sandra akiwa na macho ya kilevi, aliuliza;
“Vipi, kuna lolote baya?”
“Hapana!” Kaguta aliwahi kusema. “Nilikuwa nashangaa tu hii tattoo.”
“Umeipenda?”
“Inatisha. Sema tu ipo kwenye paja lako, ingekuwa kwenye paja la mwingine ningezirai.” Alitania Kaguta huku akishusha nguo ya mwanadada iliyobakia. Walienda kukoga, walipojilaza kitandani waliacha tamaa za miili yao ziongee, wakatimiziana haja.
****
☆Steve