***SURA YA NANE***
(MSIMU WA 02)
Inspekta alitembea kwa taratibu akielekea nyumbani kwake. Hatua zake zilikuwa ni ndogo ndogo na vishindo vyake vya miguu ndivyo pekee vilikuwa vinasikika. Ilibakia hatua chache kumaliza safari yake fupi. Alitoa simu yake mfukoni baada ya kusikia inatetemeka, alikuwa ni mke wake anapiga. Alipokea kisha akaiweka sikioni.
“Nakuja mama, ndio nipo hapa kwa nje.”
Alisema inspekta kisha akakata. Ila ghafla wakati anarudisha simu yake mfukoni, alisikia sauti kama ya majani makavu yakikanyagwa.Alisimama akatizama nyuma lakini hakuona kitu. Alirudi hatua kadhaa chache nyuma huku akitizama lakini hakuna kilichoonekana. Alisonya akaendelea na safari yake ya kuelekea nyumbani.
Kwa nyuma, kulikuwa na mtu anamfuatilia inspekta. Alikuwa ni yule yule mwanaume aliyekuja na pikipiki akaongea na simu.Mwendo wake ulikuwa ni wataratibu akikanyaga chini kwa ustaarabu wa hali ya juu huku macho yake yakiwa yanatizama mbele alipokuwa anamuona inspekta akitembea.
Baada ya inspekta kuingia ndani ya nyumba yake, mwanaume yule aliyekuwa anamfuatilia alirudi pale alipomuacha mwenzake na pikipiki. Walipeana ishara ya dole gumba kisha wakapotea lile eneo.
***
Ni ndani ya nyumba kubwa kuukuu ya wazazi wake bwana Awadhi, mwanaume aliyepatikana na kitambulisho cha mpiga kura eneo la tukio, ndipo alipokuwepo inspekta akiwa ameketi kando kando na baba yake marehemualiyekuwa amejilaza juu ya kitanda duni. Baba alikuwa amevaa shuka alilolivuta mpaka kifuani. Hali yake haikuonyesha kuridhisha; alikuwa mwembamba kupindukia, mdomo wake ulikuwa kama uliopakwa chaki na uso wake ulikuwa ni wa kukomaa huku mifupa ya mashavu ikiwa imemsimama. Alitema mate mazito pembeni akamtizama inspekta na macho yake yaliyo hoi.
“Sikuwa na jinsi. Japokuwa nilimkana sana Awadhi kujihusisha na hilo kundi, sikufanikiwa kabisa. Bado alikuwa mbishi mno na hiki kifo chake ni kitu nilichokitegemea, ila sikudhani kama ingekuwa mapema hivi. Nilidhani ningelitangulia mimi kwanza.” Baba alisema kwa sauti ya chini. Alikohoa mara tatu akatema tena mate pembeni.
“Umeiona hiyo nyumba ndogo hapo nje?” Baba aliuliza.
“Ndio. Nimeiona mzee.”
“Hiyo nyumba ndiyo tulikuwa tunaishi mimi na familia yangu. Hii unayoiona kwa sasa, aliijenga Awadhi kwa pesa za biashara zake ambazo sikupata kufahamu ni zipi. Aliisusa hii nyumba bila kuimalizia kwasababu ya kuona napinga mambo ayafanyanyo na ndio maana unaona ipo hivi.”
“Na vipi kuhusu afya yako mzee. Nini hasa kinakusumbua?”
Baba alitulia kwa muda kidogo kama mtu anayewaza jambo. Alinyanyua mkono wake mwembamba akajikuna kichwa na kifua chake kigumu.
“Sijui naumwa nini. Napukutika, sina nguvu, sina hamu ya kula wala kunywa. Hali yangu inakuwa mbaya kila uchwao muda si mwingi nitamfuata mke wangu huko aliko.”
“Umewahi kwenda hospitali kujua nini shida?”
“Hapana. Hamna haja ya kwenda huko.”
“Kwanini?”
“Mimi na mke wangu tulikuwa na afya njema kama watu wengine. Shughuli yangu ya kuniingizia kipato ilikuwa ni uvuvi, japokuwa haikuwa inakidhi kila haja yangu, lakini hatukukosa cha kula wa kunywa. Mambo yalikuja kubadilika pale tu siku moja tulipojaribu kumzuia Awadhi asiende kwenye shughuli zake kama wazazi wake. Tulifunga milango na kumkalisha kitako. Lakini ajabu, palitokea na jitu kubwa jeusi.
Lilimnyanyua mke wangu na kumtupia hukoo! Nilipojaribu kumsogelea alininyanyua bila kunishika akanibamizia ukutani. Kabla hatujanyanyuka, alituonyeshea mikono yake vumbi jeusi likatoka na kutuvamia. Tulikohoa mno kwa kupaliwa. Sikuona kingine zaidi tu ya kusikia sauti ya Awadhi ikimtaka jitu lile liache anachokifanya. Pale macho yangu yalipokuja kuona, hakukuwa na mwingine zaidi ya Awadhi. Nilijitahidi kunyanyuka lakini sikuweza. Miguu haikuwa na nguvu kabisa. Mpaka leo sijawahi pata ahueni.”
Wakati baba anamaliza kuongea hayo machozi yalimtiririka. Inspekta alitikisa kichwa chake kwa huzuni akampa pole.
“Lakini mzee, unamjua ni nani anayehusika na kufadhili hawa wakina Awadhi?”
“Mmmh hapana, sifahamu kabisa. Nimejaribu sana kumpeleleza Awadhi lakini hakuwahi kusema hata mara moja nani ndiye mkuu wao. Aliishia tu kusema hayanihusu.”
“Na je ulishawahi kusikia kwa mtu mwingine yoyote labda kuhusu mtu anayewafadhili?”
“Hapana. Imekuwa ni siri sana. Sijawahi kusikia hata tetesi.”
Kabla ya inspekta hajaongeza neno lingine, simu yake iliita. Aliitoa simu yake mfukoni akaitizama na kuona ni mkewe ndiye anapiga. Alibofya kitufe akaweka simu sikioni.
“Haloo … eeh … wageni? … wageni gani? … wanasemaje? … haya nakuja … sawa nitawahi.” Inspekta alirudisha simu yake mfukoni na kumtizama baba Awadhi.
“Mzee naomba niende. Nitakuja siku nyingine. Nashukuru sana kwa ushirikiano wako.”
“Karibu sana, inspekta. Naomba ukitoka, hapo nje uniitie Swaumu, yule binti uliyenikuta naye.”
“Sawa, mzee.”
Inspekta aliaga akaondoka zake baada ya kutimiza kile alichoelekezwa na baba Awadhi. Alipanda daladala na aliposhuka alichukua pikipiki apate kuwahi. Alipofika kwenye uwanja wa nyumba yake alishuhudiaalama za tairi ya pikipiki kwenye mchanga. Aichuchuma akatizama vizuri alama zile ambazo kwa mbele kidogo zilionekana kuserereka. Alizipuuzia alama hizo akanyanyuka na kuuelekea mlango wa sebule.
Hapo napo alitulia kidogo akatizama viatu. Kulikuwa na viatu pea mbili tu; vya kike na vya mtoto wa kiume. Inspekta alionekana kama mtu mwenye shaka. Alifungua mlango akaingia ndani lakini hakukuta mtu yeyote. Alitizama chini sakafuni akaona matone ya damu. Macho yakamtoka ilihali na mdomo ukaachama kwa bumbuwazi.
“Mama Joons!”
Inspekta aliita. Haraka alikimbilia chumbani huko akakuta mwili wa mkewe pamoja na wa mtoto wake ikiwa imelala chini palipotapakaa damu, vichwa vikiwa vimekatwa na kuwekwa pembeni. Inspekta alihamaki akashika mdomo wake kwa kuduwaa. Alipiga magoti pembeni ya miili ya familia yake. Aliita na kuita lakini ilikuwa bure kwani watu walikuwa wafu.
Baada ya muda akiwa analia, inspekta alitazama pembeni akaona bahasha ya barua. Aliivuta akaitizama kwa kuigeuza akaona maandishi yakisomeka; To you, Inspekta Vitalis Byabata. Alichana bahasha ndani akakuta ujumbe;
Kwako, mpuuzi inspekta.
Barua hii haina kichwa cha habari. Ila kuja kwake imegharimu vichwa viwilivya familia yako.
Tunataka kukupasha habari kwamba, mbio unazozianza kushindana nasi hujui wapi zitakupeleka. Refa ni wa kwetu na barabara pia.
Kichwa kimoja baada ya kingine kitapotea kwa yeyote yule atakayekuwa karibu nawe. Kama unapenda marafiki na majamaa zako, acha mara moja kutufuatilia.
Wako mchinjaji.
Barua ikakomea hapo. Inspekta aliichana chana kwa hasira akatupia vipande huko na kuendelea kulia.
****
☆Steve