mmh! aisee nimeguswa, siyo na kisa ila na jinsi dada mwenye mume alivyoelezea. Bibie pole sana. Uko kwenye wakati mgumu sana lakini utapita, wakati huwa unaponya majeraha. Tafuta muda wa kutosha utafakari, kama kulia ulie sana, ila katika kutafakari huko usije ukatafuta namna ya kujihusisha kwenye hilo saga kwamba wewe ulichangia vipi mumeo kukusaliti. Huna mchango wowote maana uamuzi alifanya yeye (haijalishi sababu).
Pia katika tafakuri yako usijaribu kufanya uamuzi kwa kuzingatia nafasi ya huyu mama kwenye ndoa yako - kwamba ukiachana na mumeo utampa huyu mama ushindi, na ukimrudia utamuaibisha. Huyu mama bila kujali nia yake ( ya tukose wote) amecheza nafasi ya kukuonyesha ubazazi/udhaifu wa mume wako. Mama mwenyewe anajitetea kuwa mumeo alimwambia yuko single, kwa hiyo akajua kapata kijana wa kumtuliza masahibu yake. Si ajabu kagharamika hapo, halafu eti leo kidume kinaleta habari ya kuwa na ndoa. Sitaki kumbebesha lawama mama maana kama ndoa yake imevunjika si ajabu naye alifanya desparate move kuamua kujiliwaza kwa mwanaume aliyeonyesha kumjali. Yeye alihitaji faraja tu - umri ni namba - after all hahitaji ndoa, kwa nini ajali umri? Mama kawekeza hisia na labda hela zake hapo. Halafu labda ndoa yake imevunjika kutokana na usaliti wa mumewe, kwa hiyo haoni umuhimu wa kujali ndoa za wenzie wakati wenzie hawakujali ya kwake. Kisaikolojia inawezekana huyo mama anamuadhibu mumewe kwa kukomesha mwanaume yeyote atakayekatiza anga zake. Hapa najaribu kukwambia uache kujiuliza ni kwa nini huyu mama na mume wako wamekuwa wakatili kiasi hicho kwako.
Ndo hivyo, dunia haina huruma na mtu, yenyewe inazunguka tu na kanuni zake. We ndo unatakiwa usimame kwenye nafasi yako, ujihoji wewe ni nani, kwa nini unaishi, unataka kufanya nini, na kitakusaidieaje kuwa kitu unachotaka kuwa.
Wewe ndo mchezaji kwenye hii mechi ya maisha. Mume wako, huyo mama na sisi wanajamvi ni washabiki tu. Mchezaji akiwa uwanjani kunakuwa na wazomeaji, washangiliaji, wasikitiaji n.k. Lakini mchezaji mahiri hababaishwi na washabiki, anacheza kufikia lengo lake - si kwa mechi ile tu bali kwa maisha yake yote.
Kwa hiyo uamuzi wowote utakaochukua maadam utauchukua ukiwa umetulia - huna hasira wala uchungu, utakuwa ni uamuzi sahihi. Kwa hiyo unaweza kusamehe na kuendelea na ndoa, au wa kusamehe na kuvunja ndoa, au kuendelea na ndoa bila kusamehe, ni wewe tu, hatukujui imani wala mtazamo wako wa maisha.