Donatila
JF-Expert Member
- Oct 23, 2014
- 8,273
- 25,297
Arusha. Simba aliyefanyiwa upasuaji Novemba 8 mwaka huu baada ya kuugua ugonjwa wa henia na matatizo ya misuli ya tumbo hatimaye ametengwa na wenzake.
Sababu za kutengwa kwa Simba huyo anayeishi katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha zimedaiwa kwamba ni kutokana na harufu ya dawa alizopewa baada ya kufanyiwa upasuaji.
Pia sababu nyingine ya kutengwa kwa Simba huyo ni baada ya viungo vyake vya ndani ya tumbo kuwa nje tofauti na ilivyo kawaida.
Mtaalamu wa Tiba Afya ya Wanyama Pori kutoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorogoro Dk Atanas Nyaki amesema jaribio la kumrejesha simba huyo porini limeshindikana na kulazimu ahifadhiwe sehemu maalumu kwa usalama wake ili kuepuka hatari inayoweza kumpata.
“Tumetumia dawa zenye harufu kali inawafanya wenzake kusikia tofauti na walivyomzoea ndio sababu ya kumtenga,” amesema Dk Atanasi
Amesema pamoja na kufanyiwa upasuaji huo ambao ulikuwa mkubwa na si rahisi bado ataendelea kuwa na uvimbe ambao hautamuathiri na yuko chini ya uangalizi wa hali ya juu.
Aidha amesema wao kama madaktari wamejihakikishia kwamba anaweza kuchanganyika na wenzake ingawa wamemkataa hivyo wamejitahidi kuokoa maisha yake kwani wenzake walikuwa wakitaka kumuua.
Ameongeza kwamba Simba huyo anajengewa banda lake kama ilivyofanyika kwa Faru Fausta, na sasa wanasubiri uamuzi wa Serikali kujua wapi watampeleka kwani mnyama huyo ni mali ya Serikali.
Mwananchi