Uzembe unavyoweka rehani maisha ya vichanga

Kikwajuni One

JF-Expert Member
Mar 18, 2013
13,142
6,947
Geita. Licha ya umuhimu wake kwa wajawazito, baadhi hawatumii dawa ya folic asidi, hivyo kuhatarisha afya za watoto walio tumboni.

Dawa hii, kwa majina mengine folate au vitamini B9 ambayo hutolewa bure na Serikali, husaidia mjamzito kujifungua mtoto mwenye afya njema ya ubongo na uti wa mgongo.
Kwa mujibu wa wataalamu, hupatikana zaidi kwenye mboga za kijani na matunda yenye uchachu kama limau na chungwa, lakini inaweza kutengenezwa maabara.

Matumizi hafifu ya dawa hii ni miongoni mwa sababu zinazochangia watoto kuzaliwa na tatizo la mgongo wazi na vichwa vikubwa. Nyingine zinazotajwa kuchangia ni imani potofu, lishe duni na uelewa mdogo wa aina ya vyakula wanavyopaswa kula wajawazito.

Kwa nini matumizi hafifu?
Maelezo ya kinamama wanne mkoani Geita, ni sehemu ya sababu za kwa nini baadhi ya wajawazito nchini hawatumii ipasavyo dawa hii licha ya umuhimu wake.

Maria Godad, mama wa watoto watatu ambaye kwa sasa ni mjamzito, anasema ameanza kliniki mimba ikiwa na miezi sita na hajawahi kutumia folic asidi kwa kuwa akimeza anapata kichefuchefu.

Naye, Monica Silas, ambaye ni mjamzito akiwa na watoto wengine saba, anasema hatumii dawa hizo kwa sababu zinamsumbua kwa kumsababishia kizunguzungu kila anapotumia. Pia anasema hajui faida au hasara ya kutumia dawa hizo.

Kwa upande wake, Salome Musa, mjamzito kwa mara ya kwanza, anasema mimba ina miezi mitano na ndiyo kwanza anahudhuria kituo cha afya.

Anaeleza hajui umuhimu wa dawa hizo, lakini amekuwa akisikia kutoka kwa kinamama wenzake kwamba zinachangia mjamzito kuchelewa kujifungua.

“Unakuta unatakiwa kujifungua mwezi wa tisa, lakini ukitumia dawa hizi wanasema unaweza kufika hadi mwezi wa 10, ndiyo maana hata nyumbani unaambiwa usimeze hivi vidonge,” anaeleza.

Hali ni tofauti kwa Neema Ramadhan, mama wa watoto watano akiwa na ujauzito wa sita, anayesema hutumia dawa hizo lakini kwa kuchelewa, kwa kuwa huanza kliniki mimba ikiwa na kati ya miezi sita au saba.
Sababu ya kuchelewa anasema ni kutokana na mimba kutomsumbua, hivyo haoni haja ya kuacha shughuli zake na kuwahi kliniki.

Maelezo ya daktari
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Waja iliyopo mjini Geita, Ernest Celestine, anasema ni kweli baadhi ya wajawazito hupata kichefuchefu kutokana na hali waliyo nayo.
Anasema wenye tatizo hilo hushauriwa kumeza dawa hizo usiku wakati wa kulala.

"Wengi wanatumia kichefuchefu kama kisingizio, lakini ukweli si sababu za wao kutapika kwa kuwa hata asipomeza dawa bado atatapika, hayo ni mabadiliko ya mwili tu. Wengine wamesikia tu mtaani na kuamini. Ukweli ni kuwa, dawa hizi ni muhimu kwa mwanamke anayetarajia kupata mtoto, bila kujali karaha ndogondogo zitokanazo na ujauzito," anasema.

Anasema mjamzito anapaswa kutumia microgramu 400 hadi 800 za folic asidi kila siku.
“Uti wa mgongo wa mtoto hutengenezwa na kukamilika katika wiki tatu au nne za mwanzo za ujauzito; kwa kipindi hicho unapaswa uwe umefunga ndiyo maana tunashauri anayetarajia kubeba ujauzito, ameze folic asidi miezi mitatu kabla na aendelee nazo hata baada ya kupata ujauzito,” anasema.

Dk Celestine anasema mbali na mtoto anayezaliwa na tatizo la mgongo wazi, ukosefu wa folic asidi husababisha pia watoto kuzaliwa ubongo ukiwa haujakua hivyo kutokuwa na fuvu.
Hali hiyo anasema husababisha mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo tofauti na umbile la kawaida, huku wengine wakizaliwa kikiwa kikubwa.

Marietha Ntwale, muuguzi katika Kituo cha Afya Nyankumbu, anasema licha ya dawa hizo kutolewa bure, kinamama wengi hufika kliniki wakiwa wamechelewa na hata wakipewa hawazitumii, wakiamini zitasababisha wachelewe kujifungua.

“Kwa siku nahudumia wajawazito 100, mwamko wa wao kutumia fefo (folic asidi) ni mdogo; wengi hawatumii wanaamini inachelewesha kuzaa hata ukiwalazimisha wachukue wakitoka wanazitupa njiani ukitoka unakutana nazo,” amesema Ntwale.

Anaeleza baadhi husema wakitumia dawa hizo huzimia au kupata kichefuchefu, jambo analosema si la kweli.
Ntwale anasema wajawazito wengi hufika kliniki kwa mara ya kwanza mimba ikiwa na wiki kati ya 34 na 36, kipindi ambacho mtoto amekamilika akisubiri kuzaliwa.

“Hapa tunapata watoto wenye midomo wazi, mgongo wazi, vichwa vikubwa, wengine tumbo wazi, wanakuwa na nundu karibu na makalio. Huwa tunapiga picha na kuzitumia kufundishia kinamama wengine,” anasema.

Hali ilivyo Geita
Takwimu mkoani Geita zinaonyesha katika kipindi cha kati ya Februari na Agosti mwaka huu, watoto zaidi ya wanane wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando baada ya kuzaliwa na matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Tanzania inatajwa kuwa ya tatu miongoni mwa nchi tano barani Afrika zenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na tatizo la mgongo wazi na vichwa vikubwa, ikitanguliwa na Algeria na Ethiopia.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Ndinisu Daniel, anasema hilo huchangiwa na wajawazito kutotumia dawa hizo hivyo kusababisha baadhi ya pingili za mgongo wa mtoto wakati akitengenezwa tumboni kwa mama kutofunga.

“Kinamama wakitumia dawa hii kabla ya kubeba ujauzito na kwa wale wanaobeba bila kutarajia wakawahi kliniki baada ya kujigundua ni wajawazito, tutapunguza tatizo hili kama si kulimaliza,” anasema.

Utambuzi wa tatizo
Dk Daniel anasema zipo aina mbili za kubaini endapo mtoto ana tatizo hilo, mojawapo ni kuzaliwa sehemu ya uti wa mgongo ikiwa imefunikwa na ngozi lakini pingili zinazotakiwa kufunika uti wa mgongo zinakuwa wazi.
Anasema aina hii kwa nje mtu hawezi kuona ila zipo dalili zinazoonyesha kama pingili haijafunga kwa ndani, baadhi huwa na nywele kidogo chini ya uti wa mgongo au tundu kama kipele au alama kwenye eneo hilo.
Anaeleza aina nyingine ni wanaozaliwa mgongo wazi na ngozi kuwa wazi, huku sehemu ya uti wa mgongo ikionekana kwa nje.

Matibabu
Wataalamu wanasema watoto wanaozaliwa uti wa mgongo haujaunga huishi na hupatiwa matibabu, lakini wanaozaliwa na changamoto ya ubongo au kutokuwapo fuvu, hufariki dunia muda mfupi au siku chache baada ya kuzaliwa.

Dk Daniel anasema zipo dawa kwa ajili ya kuzuia maambukizi ili bakteria wasiingie kwenye mfumo wa fahamu wakati mtoto akisubiri huduma ya upasuaji inayofanywa na madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu.
Anasema huduma ya upasuaji hupatikana kwenye hospitali za kanda pekee, kutokana na uchache wa madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu.

Takwimu kitaifa
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo, anasema takwimu zinaonyesha watoto tisa kwa kila 10,000 waliozaliwa hai wanakuwa na tatizo la kichwa kikubwa.
“Wizara inasimamia wilaya tano za ufuatiliaji wa kasoro za kuzaliwa, ikiwamo Ifakara, Kilosa, Kahama, Mbeya na Mbulu. Takwimu zimekusanywa tangu mwaka 2013 na ni ufuatiliaji wa idadi ya watu ndani ya wilaya. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, tulikuwa na watoto 4,800 wanaozaliwa na tatizo hilo kila mwaka,” anasema.

Profesa Lugajjo anasema ni gharama kubwa kuwahudumia watoto hao na hasa matibabu hospitalini, huku wengi wakifikishwa kwa kuchelewa wakiwa tayari na matatizo mengine ya utapiamlo, nimonia, kupooza kwa ubongo na kifafa; hivyo kukaa hospitalini kwa muda mrefu.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mkuu wa kitengo cha upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ambaye pia ni daktari bingwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Lemery Mchome, anayesema changamoto kubwa ni kuwa watoto hufika hospitali wakiwa wamechelewa, hivyo gharama ya matibabu kuwa kubwa.

Profesa Lugajjo anataja gharama za matibabu kuwa vipandikizi (Vp shunt) inakadiriwa kuwa Sh900,000.
“Katika ufuatiliaji wa miaka miwili kwa kila mtoto mmoja anayetibiwa hutumia ‘shunt’ mpaka tatu, hivyo kufanya gharama ya Sh2.7 milioni. Hapo hatujahesabu gharama za dawa, eneo la mazoezi na michezo, uchunguzi, matibabu ya kubadilisha na lishe,” anasema na kuongeza, kwa wastani matibabu hutumia wiki moja.

Profesa Lugajjo anasema baadhi ya kinamama wenye watoto wagonjwa hupewa talaka, hunyanyapaliwa na kutengwa na jamii.

Pia watoto wengi wamekuwa wakifichwa na kunyimwa matunzo, huku wengine wakifariki dunia pasipo kufikishwa vituo vya kutolea huduma, hivyo kuwapo vifo visivyorekodiwa.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya, imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kukuza mtandao wa matunzo kwa watoto hao kwa kushirikiana na harakati za wazazi.

“Tumekuwa tukihakikisha kinamama wanapata dawa za folic asidi na madini chuma. Tafiti zinaendelea kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),” anasema.

Profesa Lugajjo anasema kwa usaidizi kutoka taasisi za Cure International na Child Help International, MOI imetoa mafunzo kwa madaktari wa upasuaji kwa teknolojia ya ETV.
Anasema wamefanya kampeni za uhamasishaji nchi nzima kupitia kambi za upasuaji, mikutano na mafunzo ya mtandaoni.

Pia utoaji huduma endelevu na vifaa kwa ajili ya upasuaji ambavyo husambazwa katika hospitali zinazotoa huduma hiyo za KCMC, Bugando, ALMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Benjamin Mkapa.
“Tunafuatilia mafunzo kusaidia wafanyakazi, wakiwamo wauguzi wanaotoa mazoezi kwa watoto hao, timu ya ustawi wa jamii na tiba ya mwili,” anasema.

Profesa Lugajjo anasema wazazi huchangia kupitia taasisi ya watu wenye ulemavu wa mgongo wazi na kichwa kikubwa Tanzania (ASBAHT) iliyosajiliwa nchini mwaka 2006 ambayo ina matawi katika mikoa 12 ya Bara.
“Matawi haya yameunganishwa na hospitali za mikoa zinazolingana chini ya mganga mfawidhi na wanahudhuria mikutano ya kamati ya usimamizi wa afya bila malipo katika hospitali za rufaa husika,” anasema.

Profesa Lugajjo anasema bado hakuna takwimu maalumu za maeneo yanayoongoza kwa kuwa na watoto wenye changamoto hizo.

“Kwa mujibu wa takwimu za hospitali, mikoa inayoongoza ni Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma,” anasema.
Kwa upande wake, Dk Selestine anasema, “Mtu anapata madini ya folic asidi kwenye vyakula, matunda kama machungwa, zabibu, mboga kama spinachi, njegere, mayai lakini ni kiasi kidogo ambacho hakitoshelezi.”
Anasema utoaji wa elimu ya uzazi salama na umuhimu wa dawa hizo unahitajika na inapaswa kutolewa na wataalamu wa afya, viongozi wa jamii na wale wa Serikali.
 
Eeeeh kumbe Ina madhara makubwa Ivo isipotumiwa ........ngoja nikamsisitizie mama kija wangu aloo
 
Back
Top Bottom