Kwakuwa Nilisha sema na kuandika Mawazo yangu juu ya Muundo Wa Muungano wetu Mara kadha na hasa kuhusu dhana ya utanganyika.
ninaomba kuweka Hapa Sehemu Kati ya yale aliyo ya sema Prof. Idea Shivji wakati wa kongamano la vijana hivi majuzi. Msisitizo Zaidi Hasa kwenye Suala la UTANGANYIKA!!
Nanukuu,
"Juu ya hilo la Utanganyika, ningependa kuongeza maneno machache hasa kwa faida ya vijana wetu. Nimeshangaa kidogo kwamba hata mzee na mwanazuoni mwenzangu Prof. Mpangala ametumia msamiati wa Utaifa wa Tanganyika bila kudadisi kihistoria Utaifa wa Tanganyika.
Kwa muhtasari tu, kabla ya vita vya kwanza, hatukuwa na Tanganyika. Tulikuwa na German East Africa ambayo eneo lake lilijumuisha Burundi, Rwanda na eneo hilo la Tanganyika chini ya himaya ya ubeberu wa Wajerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika vita, Rwanda na Burundi ziligawiwa kwa Ubelgiji na Tanganyika kwa Uingereza. Waingereza ndipo wakaunda neno hili Tanganyika na iliitwa Tanganyika Territory, yaani, bustani ya wakoloni, siyo taifa.Mababu zetu waliopigania uhuru walijikita kwenye dhana ya Utaifa wa Kiafrika, kama alivyoeleza vizuri tu Profesa Mpangala. Vyama vya wananchi, kutoka TAA (Tanganyika African Association) mpaka TANU (Tanganyika African National Union), viliweka msisitizo kwenye African, Uafrika wao. Iliwabidi kuweka neno Tanganyika kwa sababu tu ndilo lililokuwa eneo la utawala wa wakoloni.Tulipopata uhuru mnamo Desemba 1961, hatukuwa taifa kwa sababu mkuu wa nchi bado alikuwa Malkia. Mwezi wa Novemba 1962 ndipo tukawa Jamhuri ya Tanganyika wakati Mwalimu alipochaguliwa kuwa Rais. Na Mwalimu tangu mwanzo alisistiza kwamba sisi hatukuwa taifa bali mkusanyiko wa makabila na lilikuwa jukumu la serikali huru kujenga utaifa (nation-building).
Lakini Mwalimu hakupata muda wa kutosha kujenga utaifa wa Tanganyika kwa sababu mwezi Aprili 1964, yaani baada ya miezi 14 tu, tukaungana na Zanzibar kuwa Tanzania. Na kwa takriban nusu karne tumekuwa tunajenga Utaifa wa Tanzania.
Sasa hii dhana ya Utaifa wa Tanganyika, au Utanganyika, unatoka wapi? Na mantiki na historia yake ni ipi?Ningependa kujua hapa tulipo ni vijana wangapi kati yenu mlizaliwa kama Watanganyika. Nyoosheni mikono juu. Nyinyi wote mlizaliwa mkiwa Watanzania, utaifa wenu ni Utanzania; utambulisho wenu ni Utanzania; mnajitambua kama Watanzania na mnatambuliwa na wengine kama Watanzania.Ukweli ni kwamba mkingangania Utanganyika wenu, ambao wala hamjui kama mtakuwa mnavunja taifa, mtakuwa mnatumikia maslahi na matakwa ya mabeberu na wanasiasa wachache wenye uchu wa madaraka. Na Utanganyika wenu hautadumu kwa sababu mtaanza kudai sasa Jamhuri ya Makonde na Jamhuri ya Sukuma! Mtakuwa vipande vipande. Hivi siyo vitisho; kuna mifano hai mbele yetu. Somalia imesambaratika, Libya pia, Sudan, Afrika ya Kati, na nchi nyingine nje ya Afrika Afghanistan, Pakistan, Syria, Iraq bila kutaja nchi za Ulaya"
- Prof. Issa Shivji 2014.
Comrades, maneno haya ya mwanazuoni huyu nikama ameyasikia kutoka kwangu ama kuyasoma katika kuta zangu katika mitandao mbali mbali,. Sijilinganishi naye., hapana hata kidogo. Ila ninachosema nikwamba mtu yeyote mwenye nia njema na fikira tulivu anaweza kung'amua nia hasa ya wale wanaotupandikiza hisia za utanganyika na uzanzibari. Walafi wamadaraka!!
Nilisha sema na ninasema tena hapa Tanganyika Siijui, na wala Siihitaji.!!
Comrades ninashukuru sana.