Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,999
21.-(1) A police officer or other person shall not, in the course of
arresting a person, use more force or subject the person to greater indignity
than is necessary to make the arrest or to prevent the escape of the person
after he has been arrested.
(2) Without limiting the application of subsection (1), a police
officer shall not, in the course of arresting a person, do an act likely to
cause the death of that person, unless the police officer believes on
reasonable grounds that the doing of that act is necessary to protect life or
to prevent serious injury to some other person.
Kama nilivyosema kwenye uzi mwingine ninaamini Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Bw. Michael Kamuhanda anastahili kutiwa pingu na kufikishwa mahakamani akiunganishwa na mtuhumiwa nambari moja wa mauaji ya Daud Mwangosi siku kadhaa zilizopita. Ninaamini - na ushahidi uko upande wangu - Kamanda Kamuhanda alipaswa kusimamishwa kazi mara moja, kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi na kuvuliwa vyeo vyake ili aweze kuunganishwa na watuhumiwa wengine (wale waliompiga Mwangosi wanatakiwa pia wawemo).
Hata hivyo ninaamini kuna sababu kubwa mbili za kwanini kumchelewesha kumchukulia hatua Kamanda Kamuhanda kumetoa nafasi ya kuchezea ushahidi (tampering with evidence), kutishia mashahidi (intimidation of witnesses) na kwa namna yoyote kupindisha mwenendo wa uchunguzi na hivyo kuharibu mchakato wa kupata haki (obstruction of justice). Kwenye nchi ambayo inaheshimu utawala wa sheria kwa vile Kamanda Kamuhanda alikuwa ni shuhuda wa tukio (material witness) hakupaswa kuwa sehemu ya uchunguzi na kwa hakika hakupaswa kuendelea na wadhifa wake wakati uchunguzi wa mauaji yaliyotokea mbele yake na kwa sababu yake unafanyika. Kumwacha aendelee na nafasi yake ni mojawapo ya uvunjaji mkubwa wa haki ambao serikali imeruhusu na wanasiasa wetu wanavumilia.
Sababu za kwanini Kamuhanda asimamishwe kazi na kufunguliwa mashtaka (asili ya mashtaka sitaki kuhisi sana lakini itakuwa ni kati ya matumizi mbaya ya madaraka hadi mauaji) ni hizi zifuatazo.
a. Hakuwa na sababu ya kuvunja shughuli ya Chadema ambayo ilikuwa inafanyika kwa mujibu wa sheria. Kwa wale walioona video ya mazungumzo yaliyotangulia vurumai kati ya Kamuhanda na Waandishi hoja kubwa ilikuwa kama mkutano wa CDM ulikuwa ni "mkutano wa ndani" (internal meeting) au ulikuwa ni mkutano uliokatazwa. Waandishi - hasa marehemu Mwangosi - walisikika wakimpa nafasi nyingi Kamuhanda kubadilisha njia. Kwamba maana ya "internal meeting" siyo sawasawa na "inside meeting". Kwa maana ya kawaida ya lugha ya Kiingereza mkutano unaweza kuwani "internal" bila kuwa "inside".
Kwa kauli yake mwenyewe kamanda Kamuhanda alifanya makusa zaidi pale alipodai kuwa yeye ana haki ya kutafsiri sheria zote na siyo kipengele kimoja. Kwa kweli yeye si mtafsiri wa sheria na kama angekuwa na hekima (na ushahidi unaonesha kuwa hana) alipaswa kuuliza mwanasheria wa serikali au mwanasheria mwingine kama mkutano ule ambao ulikuwa ni "internal meeting" unalindwa na haukuwa sehemu ya mikutano iliyopigwa marufuku.
Kwa kutoa agizo la kuuvunja mkutano ule Kamanda Kamuhanda - japo inaweza kuwa ni katika bona fide - alivunja na kuingilia kati shughuli halali ya chama cha siasa kikifanya mambo yake ya ndani. Hakuwa na mamlaka, wala sababu ya kuingilia mkutano wa ndani na alikuwa na nafasi ya kutosha kuweza kujihakikishia kuwa agizo lake lilikuwa halali. Kinyume na watu wengine ambao wanataka kuwa CDM walipaswa kutii amri ya polisi binafsi naamini hawakutakiwa kutii amri hiyo ya kuwataka waondoke kwa sababu haikuwa amri halali, haikuwahusu na kwa hakika ilitolewa na mtu ambaye alitumia madaraka yake vibaya.
b. Wakati tukio la kuanza kumpiga mwandishi Mwangosi limeanza Kamanda Kamuhanda alikuwa na haki na uwezo wa kuhakikisha haki za raia zinalindwa. Polisi wote wanajifunza sheria hii ambayo nimeweka hapo juu ambayo inaelekeza wazi kuwa polisi wanapomkamata mtu au kumzuia mtu asiwatoroke hawapaswi kutumia nguvu zaidi ya inayohitajika. Yeye kama Kamanda wa POlisi wa Mkoa aliona jinsi nguvu ya jeshi la polisi iliyokuwepo pale na kwa hakika hakukuwa na mtu hata mmoja ambaye alikuwa ni tishio kwa jeshi hilo.
Lakini zaidi ni kuwa walipomkamata Daud Mwangosi hakuwa na kitu kingine chochote cha kutishia polisi zaidi ya kamera na laptop yake. Wingi wa polisi waliomzunguka - picha na video zinashuhudia - unathibitisha pasipo shaka kuwa kama polisi waliamini (kwa sababu yoyote ile) kuwa Mwangosi amefanya kosa na anastahili kuwekwa chini ya ulinzi, polisi walikuwa na uwezo na nguvu ya kuweza kumdhibiti bila kumpiga. Lakini kwa polisi kumkamata, kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda wa POlisi wa Mkoa inathibitisha tu kuwa kamanda huyu hafai kuongoza hata chipukizi! Alitakiwa avuliwe vyeo vyake na kuwekwa kizuizini mara baada ya mauaji yale ya Songea ambayo nayo yalitokea katika mazingira ya kutatanisha.
Je atafikishwa mahakamani?
Kwa jinsi polisi walivyochukulia hili na zaidi wanasiasa wetu (wa chama tawala) walivyokubali hili ni wazi kuwa Kamuhanda zaidi atakachofanywa ni kuhamishwa na kupelekwa mkoa mwingine (ningependa binafsi aletwe Dar kuchukua nafasi ya Kova). Kumshtaki mtu mkubwa kama huyu ambaye ushahidi dhidi yake ni mkubwa kuliko ule wa Zomba na kesi ya wauza madini utatikisa jeshhi la polisi. Na kwa vile jeshi hili ni la kulindana (IGP Mwema ndiye aliyemwamisha kutoka Ruvuma!) ni wazi kuwa njia pekee ya kuja kumshughulikia ni uongozi wa CDM kuweka rekodi ya watendaji hawa ili watakapoingia madarakani iwe ni watu wa kwanza kushughulikiwa. Ikumbukwe mauaji hayana muda wa kukoma kuchunguzwa.
SWALI LA UCHOCHEZI:
Polisi wamekuwa wakiendesha kampeni ya kuwataka raia watii sheria bila "shurti". Je, ni nani atawafanya polisi wawe wa kwanza kutii sheria bila kushurtishwa? Au wao polisi hawafikirii kuwa wanatakiwa kuwa ni mfano wa kwanza wa kutii sheria bila shurti?